*ROHO YAKE INADAI --- 20*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
.
.
Brian akajaribu kutazama kile akitazamacho Olivia. Ilikuwa ni kwenye pindo la mfuko wa joho la padri. Hapo alipotazama vema, akaona kitu kama damu kwa ndani ya mfuko. Akapata shaka.
.
.
Akiwa kwenye hilo ombwe, mara mlango ukagongwa. Na sauti kavu ya kizee ikasema, “Hodi!”
.
.
ENDELEA
.
.
Brian akatoa macho kwa mshangao. Aliogopa. Alihisi hiyo hodi haitomtendea jema.
.
.
“Brian, kafungue mlango,” mama akamwamuru. Brian akasita. Alimtazama mama yake kwa sekunde chache kisha akanyanyuka. Hata mama alihisi Brian hayupo sawa. Aliufungua mlango na uso kwa uso akakutana na Brewster!
.
.
Mzee huyo alikuwa amekodoa macho haswa. Kwenye paji lake la uso upande wa kulia alikuwa amevilia damu. Brian akamsalimu. Alikuwa anaogopa kwa namna ambavyo Brewster alivyokuwa anamtazama.
.
.
“Mama yako yupo?”
.
.
“Ndio, yupo. Karibu.”
.
.
Brewster aliingia ndani, akasalimu kila mtu. Kwakuwa kulikuwa na watu wengi humo, akaomba kuonana na mama Brian faragha. Basi Mama Brian akaomba radhi na kisha akaelekea nje pamoja na Brewster.
.
.
Huko wakakaa kwa muda wa kama dakika tano. Waliteta wakiwa hawasikiki na hata mmoja wa walioko ndani. Walipomaliza, Brewster hakurudi tena ndani hata kuaga, akaenda zake, Mama Brian akarudi ndani peke yake.
.
.
“Samahani kwa usumbufu.”
.
.
“Usijali,” akasem Padri Alfonso kisha akauliza Mama Brian akiwa anaketi kitini. “Unamjua yule mzee?”
.
.
“Aaahmm … ndio! Kiasi chake.”
.
.
Padri Alfonso akatikisa kichwa na kunyamaza asitie neno. Mama Brian akauliza, “Vipi kuna shida yoyote?”
.
.
“Ndio, ipo.”
.
.
“Ipi hiyo?”
.
.
“Watu wanasema si mtu mzuri. Hana marafiki wala mtu wa karibu. Ni mtu anayependa upweke. Mara kadhaa nimekuwa nikiletewa mashataka yake kanisani.”
.
.
“Umejuana naye lini?” Dada Magdalena akamuuliza mama Brian.
.
.
“Si muda mrefu sana.”
.
.
“Na tangu ulipojuana naye umemwona ni mtu wa namna gani? … Anakuletea habari gani?” Dada Magdalena akaendelea kuuliza. Kidogo Mama Brian akasita. Akamtazama Padri Alfonso na Dada Magdalena kisha na kusema, “Habari za kawaida tu. Hamna cha zaidi.”
.
.
“Hamna shida. Tulikuwa tuna hofu kutokana na historia yake. Nadhani sasa tunaweza kuendelea na huduma yetu,” akasema Padri Alfonso. Basi wote wakanyanyuka na kisha taa zikazimwa na kuwashwa mishumaa kwa maelekezo ya Padri.
.
.
Dada Magdalena akafukiza, na kumwagia maji maeneo mbalimbali ya nyumba. Maji ya baraka. Kisha wakafunga macho na sala ikaanza baada ya kuimba na kusema kwa pamoja vifungu kadhaa.
.
.
Wakasali kwa dakika sita mfululizo pasi na kukoma. Kwenye dakika ya saba, Brian akavutwa mkono wake wa kuume. Upesi akafungua macho na kutazama. Akamwona Olivia akiwa amejawa na hofu usoni. Macho yake yanatiririsha machozi.
.
.
“Nini, Olivia?” Brian akauliza kwa kunong’ona akitumia haswa uso wake kufikisha ujumbe. Olivia akaonyeshea koridoni. Brian kutazama hakuona kitu. “Kuna nini?” akauliza tena kwa mtindo uleule.
.
.
Olivia akatikisa kichwa. Kwa sura na mkono wake, akaonyeshea kulikuwa na kitu. Brian akamhimiza afunge macho, asitazame popote pale. Olivia akatazama tena kule koridoni kwa mashaka, kisha akafunga macho yake, Brian akafuatia.
.
.
Sala ikawa inaendelea. Baada tena ya dakika mbili, Olivia akamvuta Brian mkono. Brian akafungua macho yake kumtazama. Lakini kabla hajasema kitu, akaona mtu anaishia koridoni upesi. Olivia akanyooshea kule koridoni na kumwambia Brian kwa ishara ya kinywa, “Kuna mtu kule!” sasa hivi Brian hakuwa na haja ya kubisha kwani kwa macho yake alishuhudia.
.
.
Alikuwa nani yule?
.
.
“Kuna mtu kule!” Olivia alisema akiwa anachuruza machozi. Sauti yake ilikuwa inasikika kwa chini maana alikuwa ananong’ona. Basi Brian akatoka pale eneo la sala na kwenda koridoni kutazama. Alirusha macho yake, hakuona kitu! Ila mlango wa chumba chake ulikuwa wazi. Ulikuwa unachezacheza kuashiria umeguswa.
.
.
Akawaza. Mtu yule amekimbilia chumbani mwake? Basi akaanza kuchukua hatua kwenda huko kutazama. Olivia alikuwa anamtazama kwa hofu, ni kama vile alikuwa anataka kumzuia asifanye hilo.
.
.
Brian akasonga. Kulikuwa ni giza, ila kwakuwa nyumba za jirani na huko nje taa zilikuwa zinawaka, basi akaweza kuona akanyagapo. Taratibu akasonga na kusonga. Alipofikia mlangoni, akatazama ndani ya chumba chake. Hakuwa anaona jambo.
.
.
Akasonga kuzama ndani. Alikuwa ana hofu. Alikuwa anatembea kwa tahadhari macho yake akiyatupa kule na kule. Alipodumbukia kabisa ndani ya chumba, akasikia sauti ya kishindo cha mguu. Akapatwa na woga. Kutazama mlangoni alikuwa ni Olivia.
.
.
“Olivia, rudi sebuleni!” Brian akamwambia kwa kunong’ona. Olivia akatikisa kichwa na kusema, “yupo kule!”
.
.
“Wapi?” Brian akauliza.
.
.
“Jikoni!” Olivia akajibu akionyeshea kidole. Basi Brian, upesi, akatoka na kwenda jikoni akiongozana na Olivia. Walipofika huko hawakukuta kitu.
.
.
“Hamna kitu, Olivia.”
.
.
“Nilimwona! Alinichungulia na kisha akakimbilia huko!”
.
.
Brian akashusha pumzi ndefu. “Olivia, huyo mtu hataki tuwepo kwenye sala. Anatusumbua tusishiriki huduma. Turudi kwenye maombi na sasa tusitazame wala kuhangaika naye.”
.
.
Olivia akajibu kwa kumeza mate. Brian akautwaa mkono wake na kumrudisha sebuleni lakini binti huyo akitazamatazama huko nyuma, pembeni na kule aelekeapo.
.
.
Wakajiunga na sala. Wakafunga macho yao kwanguvu wakitulia. Kheri wale waliowaacha hawakutambua kama waliondoka. Au labda walitambua wakanyamaza.
.
.
Sala, kama walivyoiacha, ikaendelea. Sasa hivi wakadumu kwa dakika moja tu, na mara Brian akaanza kuhisi upepo kana kwamba wapo nje ya jengo. Akakunja uso wake kwa maulizo, ila hakufungua macho yake. Punde, sauti ya sala ikakoma!
.
.
Brian akiwa amefumba macho yake, yu gizani, akajitahidi kuskiza asisikie kitu. Muda kidogo akasikia sauti ya Olivia ikimwita! Akafungua macho kutazama, akamwona Olivia akiwa kando yake. Ila hawakuwa ndani bali nje! Kiza. Kimya.
.
.
“Olivia tuko wapi hapa?” Brian akauliza akitazama kila pande yake. Wote walikuwa wamejawa na hofu. Olivia alikuwa anachuruza machozi lukuki hata kunena hawezi.
.
.
Kutazama vema, wakagundua eneo walilopo ni la kanisa. Hapo palikuwa ni uwanjani. Hatua kama ishirini na nne mbele upande wao wa kaskazini kulikuwa na jengo kubwa la kanisa la Boston!
.
.
Wamefikaje hapa?
.
.
“Brian!” Olivia akaita. Akanyooshea kidole chake upande wa mashariki, huko, kwa mbali, Brian akamwona mtu akiwa amevalia nguo nyeupe. Mrefu, amesimama wima. Na kando ya mtu huyo, akamwona mwingine kama kivuli, ila kichwa chenye kiremba cheupe!
.
.
Punde watu hao wakaanza kuwasogelea! Mwendo wao ulikuwa ni kana kwamba watu wasio na maungio ama wamevunjika mifupa lakini wakitaka tu kutembea! Waliogofya. Na japo walikuwa mbali, macho yalikuwa yanang’aa kama taa ama paka awapo gizani.
.
.
“Kimbia!” Brian akaropoka. Upesi wakaanza kukimbia na Olivia kuelekea kule kanisani. Hawakuwa wanaona majengo mengine yoyote zaidi ya kanisa. Mbali na jengo hilo kulikuwa na misitu tu ikiwa imewazingira!
.
.
Wakakimbia kwa kasi na kukomea kwenye lango la kanisa. Wakajaribu kulifungua, haikuwezekana. Lilikuwa limetiwa ‘lock’, basi haraka wakaachana nalo na kuuendea mlango mwingine mdogo. Wakaujaribu, huo ukafunguka.
.
.
Wakazama ndani upesi na kuurejeshea. Wakiwa wanahema kwa pupa, macho yamewatoka, wakapata tulizo ya kuwa huenda sasa wakawa salama. Ila punde wakapata hisia tofauti! Ni kama baada ya sekunde sita tangu kuingia humo. Walihisi hawakuwa wenyewe, kuna watu wengine zaidi ya wao ndani ya jengo.
.
.
Kutazama kwenye ukumbi wa kanisa, vitini, kulikuwa na watu wameketi. Na walipotazama madhabauni, kulikuwa na padri, Padri Alfonso, akiongoza misa.
.
.
Nyuso za watu wote hawa hazikuwa za watu wa kawaida. Zilikuwa ni nyuso nyeupe zilizojawa na michirizi meusi kana kwamba vijito vya mito. Midomo meusi. Macho ya njano na nyekundu yaliyokuwa yanawatazama watu walioharibu misa yao, Brian na Olivia!
.
.
Kwa muda kidogo Brian akakosa la kufanya. Olivia akalia kwa hofu. Waliona huo ndiyo mwisho wa maisha yao. Waumini wote wakasimama na wakiongozwa na Padri Alfonso na Dada Magdalena wakawasogelea Brian na Olivia ambao hawakuwa na mahali pengine pa kukimbilia. Walijaribu kufungua mlango pasipo mafanikio.
.
.
Waliwapowasogelea kabisa, wakasimama wote na kusema kwa pamoja, “Unaona nini Brian?” kisha wakanyoosha mikono yao kuwadaka.
.
.
Brian na Olivia wakapiga kelele kali. Wakawashtua watu wote waliokuwepo kwenye sala. Wote wakakoma kusali na kuwatazama kwa mshangao.
.
.
“Brian! Olivia! Mmekumbwa na nini?” mama Brian akauliza. Brian kabla hajajibu kitu, akarusha macho yake kwa Padri Alfonso na Dada Magdalena. Dada Magdalena akatabasamu.
.
.
.
.
****