Simulizi ya kipelelezi: Jiji la kamari (gambling city)

FEBIANI BABUYA

JF-Expert Member
Mar 5, 2022
1,034
1,925
Once again tunakutana kwenye mchezo bora huu hapa. Tukapate kumsoma secret agent mmoja ambaye alikuwa assigned kuwa mlinzi wa raisi.

Lakini baadae anagundua kwamba mfumo hauko sawa na yeye ndiye alikuwa amechaguliwa na watu wasio julikana kwa ajili ya kuufuta huo mfumo. Anakuja kushtuka wakati yeye mwenyewe yupo ndani ya mfumo tayari hivyo anakuwa hana namna zaidi ya kudili na watu ambao hakuwa akiwajua na nyuma yao kulikuwa na mambo mazito sana.

Max (jina la kazi) huku jina lake halisi akijulikana kama DONALD DANIEL (DONNY) code no 001. Anaanza kuyafunua yale ambayo alipewa kazi kuyafanya ndipo anagundua kwamba kuna mlima mzito sana wa kuupanda lakini wakati anaanza kuyajua hayo mazito anakutana na jambo baya sana.

Ananasa kwenye HONEY TRAP na kuunguza mchezo mzima hali ambayo inamfanya kuishia kwenye umauti huku akishuhudia raisi ambaye ndiye alitakiwa kumlinda na raisi huyo ndiye alimpa kazi ya kuufuta huo mfumo akiwa anauawa ndani ya ofisi yake.


Muuaji anamuua raisi huku 001 akiwa ma risasi 6 mwilini hana cha kufanya hivyo yeye ndiye anauziwa kesi kwa kuhusika na mauaji ya raisi wa nchi, rasmi anavishwa taji la ugaidi huku ikionekana kwamba ameuliwa akiwa kahusika na mauaji ya raisi wake tena akiwa ndiye mlinzi mkuu wa raisi huyo.

Mwanaume huyo baada ya raisi kufa naye akiwa ana risasi sita kwenye mwili wake, anabebwa na kwenda kuzikwa akiwa bado hai hajakata roho.

001 anafukiwa na kushindiliwa ndani ya shimo la futi sita porini huku mvua ikiwa inausindikiza umauti wake na jina lake linafutwa kwenye idadi ya watu ambao waliwahi kuishi.


Lakini jambo la kutisha zaidi ni kwamba mwanaume huyo ambaye dunia iliamini kwamba alipatwa na umauti na ilithibitishwa kwamba ni gaidi ambaye aliuawa baada ya kumuua raisi akitaka kushambulia na watu wengine, alikuja kuonekana akiwa hai baada ya miaka kumi na mbili kupita.


Sasa alikufaje halafu akaja kuonekana tena akiwa hai miaka kumi na miwili baadae? Baada ya yeye kuonekana ni kipi kilitokea kwa watu wake ambao alifeli kuwafuta na mfumo wao kwa ujumla? Binafsi majibu yote nimekuandalia ndani ya hili andiko bora sana.

Ni muda wako ndio utakufanya uyapate majibu sahihi kwenye moja kati ya simulizi bora sana ya mapigano ya hali ya juu na ya kutisha muda mwingine bila kusahau stori iliyo pangiliwa unono kabisa.


Kwenye kalamu nimesimama mwenyewe Febiani Babuya wengine wapenda kuniita Bux the storyteller.

Here we go
FB_IMG_1706850787768.jpg
 
NOTE:

Please over please sipendi matusi hususani kwenye threads zangu hivyo ukiona simulizi nazoleta hazikuvutii isiwe kigezo cha kusumbua wengine.

Ukiwa na cha kunikosoa wewe kosoa uwezavyo ila matusi achana nayo.


Ni mara mia usome simulizi za watu ambao unahisi wanakuburudisha kuliko kuvamia thread za watu na kuleta mihemko yako hapa.


Good evening
 
Then ukiona una arosto saaana na huwezi kwenda na time table yangu ya kupost na unaona kabisa kwamba wewe huwa haupo tayari kutoa pesa kununua simulizi basi kaa nayo mbali ili usijitengenezee arosto zisizo na maana ukaanza kutukana watu na kuleta emotions za kitoto.

So far kitabu kipo tayari ni 5000 tu kwa mtu ambaye atahitaji full.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 1
USIKU WA KUTISHA

Usiku wa manane mvua ikiwa inanyesha mithili ya kufunguliwa kwa koki iliyopo huko angani, alionekana mwanaume mmoja akiwa ndani ya nguo nyeusi na begi jeusi kwenye mkono wake huku koti lake jeusi refu ambalo lilivuka magotini likikamilisha mwonekano wake wa kuwa moja kati ya wanaume ambao walikuwa wanatisha mno.

Akiwa na kofia yake kubwa aina ya pama kwenye kichwa chake, alikuwa anatembea haraka haraka tena kwa uangalifu mkubwa akionekana wazi kuwa mtu ambaye alikuwa makini sana na begi lake ambalo lilikuwa kwenye mkono wake ili lifike salama mahali ambapo alikuwa anatakiwa kulifikisha usiku huo.

Akiwa kwenye huo mwendo wake wa haraka baada ya kufika katikati ya barabara ndogo ambayo ilikuwa imezungukwa na majengo marefu sana ambayo yalikuwa yamejengwa kwa mawe magumu mno huku pembezoni kukiwa na vichochoro vingi ambavyo vilielekea maeneo tofauti tofauti. Alihisi kwamba hilo eneo ni kama kulikuwa na ugeni, nafsi yake ilimpa taarifa hiyo kwamba walikuwepo watu wengine ukiacha yeye.

Masikio yake yalimtekenya na kumpa taarifa hiyo kupitia mlango wake wa hisia na alikuwa akiziamini sana hisia zake kwa kuamini kwamba zisingeweza kabisa kumdanganya kamwe hivyo akawa na uhakika kwamba alikuwa kwenye hatari majira hayo ya usiku wa kiza totoro, huku taa kwa mbali zilizokuwa zimezunguka kwenye majengo ya karibu yake zikiwa zinatoa mwangaza ambao ulimsaidia kuona kila kitu ambacho kilikuwa pembeni yake.

Alisimama na kuyafumba macho yake kisha akayaweka masikio yake kwenye hali ya utulivu na usikivu mkubwa isivyo kawaida ili aweze kujua kwamba huyo mgeni au hao wageni walikuwa wamejifichia wapi na wangetokea wapi ili aweze kujihami mapema kabla hajapata madhara yoyote yale. Akiwa amesima hapo na begi lake mkononi ambapo mkono mmoja alikuwa ameuweka kiunoni sehemu ambayo ilikuwa na kisu kikali sana, alihisi kwamba kuna kitu kilikuwa kinakuja alipo kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba sikio lake lilicheza kumpa ishara hiyo hivyo aliinama kwa kasi mithili ya mwanga wa radi ambavyo huwa unajitokeza machoni radi ikipiga kisha ungetoweka haraka.

Kuinama kwake kulimsaidia kupishana na shoka la chuma ambalo lilienda kukita kwenye moja ya kuta za majengo marefu ambayo yalikuwa karibu na alipokuwa amesimama. Alihema kwa nguvu kwa tumaini la kushukuru kuweza kupona kwenye dhahama hiyo na kuamua kugeuka kwa kasi kubwa ila wakati anageuka alitumia muda mwingi sana ambao ulimuingiza matatizoni.

Alihisi kifua chake kinamuwasha maana spidi ambayo ilitumika kumkita hapo ilikuwa ni kama umeme unavyo safari kwenye njia zake, alitema damu maana alipokea mishindo mikali ya haraka haraka ya mabuti ambayo yalitoka kwa mtu ambaye alikuwa ana nguvu kubwa sana miguuni na mtu huyo alionekana dhahiri alikuwa amedhamiria kuweza kumuua moja kwa moja.

Mwanaume huyo licha ya kurushwa mbali karibu na kuta za mijengo hilo, mgongo wake ulikuwa umelenga jiwe ambalo lilikuwa lipo kwenye msingi mkubwa wa jengo moja na kama angekita hapo basi moja kwa moja alikuwa anaupoteza uti wa mgongo wake, hakuwa tayari kufa kifala sana namna hiyo hivyo aliutanguliza mkono wake baada ya kujipinda kidogo tu na mkono wake ndio ambao ukakita kwenye jiwe hilo la msingi wa hiyo nyumba. Mkono wake ulikuwa na gloves lakini nguvu ambayo ilitumika kukita kwenye huo ukuta ilifanya koti lake kujivuta kidogo na kuufanya mkono wake uonekane ambapo mkono huo ulikuwa na tattoo (tatuu) iliyokuwa inasomeka 002 mbele yake pakiwa na alama ya nyoka.

Mwanaume huyo alitua chini na kukiweka sawa kifua chake na kuifuta damu ambayo ilikuwa kwenye mdomo wake kisha akageuka kumwangalia mtu huyo ambaye alikuwa amemvamia ndani ya hilo eneo. Kwa bahati mbaya sana mtu ambaye alikuwa mbele yake hakuwa akionekana sura kwani sura yake ilikuwa imefunikwa na kitambaa cheusi huku naye akiwa amevaa mavazi kama yake mpaka kofia kichwani ilikuwa ni kama yake. Kitu pekee ambacho walikuwa wametofautiana ilikuwa ni kwamba mvamiwaji uso ulikuwa wazi na mvamiaji uso wake ulikuwa umefunikwa wote na kumfanya asitambulike kabisa kwamba alikuwa ni nani.

“Tunafahamiana kabla?” mvamiwaji aliuliza swali ambalo halikuwa na majibu, alitabasamu kidogo na kukitoa kisu chake ambacho mara ya kwanza hakufanikiwa kukitoa. Mwenzake alikuwa amesimama tu anamwangalia bila wasiwasi kwenye macho yake. Aliyakanyaga maji ya mvua chini kwa nguvu na kuyafanya yapande juu kuelekea alipokuwepo mvamiaji kisha akakirusha kisu kwa kasi kikiwa kinapita kwenye yale maji huku naye akija kwa nguvu sana kwa hatua ambazo zilikuwa zinapigwa kwa umakini sana.

Mwanaume ambaye alikuwa mbele yake hakukikwepa kile kisu bali alikiacha kikazama kwenye bega lake, wakati huyo mvamiwaji naye alikuwa amefika eneo alilokuwepo ambapo aliituma ngumi yake eneo ambalo lilikuwa na kisu ili akizamishe zaidi ndani. Mvamiaji ni kama alishtuka kutoka kwenye tafakari ambayo alikuwa nayo kwa muda ambao alikuwa hapo hivyo aliteleza kwenye maji kusogea nyuma kidogo ya alipokuwa na kufanya ngumi hiyo ipige hewa.

Mvamiwaji alizunguka teke la chini ambapo mvamiaji aliruka sarakasi ya nyuma na miguu yake ikatua kwenye ukuta na mikono ikidaka sehemu ya jiwe akawa amegeuka miguu juu na mikono uelekeo wa chini akimwangalia mwenzake ambaye aliishia kuyasambaratisha tu maji ambayo yalikuwa chini na hakufanikiwa kumpata mtu wake. Mvamiwaji alichukia sana kiasi kwamba akavua mpaka koti lake na kulirushia pembeni ila wakati anafanya hayo yote mvamiaji alikichomoa kisu kwenye bega lake na kukirudisha kwa mwenye nacho kikiwa kinaenda kwa mwendo mkali ambao ulipatikana kutokana na spidi ya mrushaji kuwa kubwa sana. Mwanaume huyo alijitahidi sana kukikwepa kisu hicho kikaishia kumbaraza kwenye shavu lake ila wakati anapambana kukikwepa kisu hicho mvamiaji alikuwa ameshuka pale juu kama kimbunga.

Alitua kwenye mbavu ya mvamiwaji ambapo ngumi mbili zilitosha kumfanya agugumie kwa maumivu makali ambayo yalijitawanya kila sehemu ya mwili wake. Alirudi nyuma akiwa anayumba yumba, mvamiaji alidunda kwa mkono mmoja na kujibetua na meteke mawili ambayo mvamiwaji aliyaona na kuyakwepa kwa kuinama ila wakati anainuka mvamiaji huyo alizungusha teke la chini na kumzoa mwanaume huyo ambaye angedondokea mgongo kwenye maji ambayo yalikuwa hapo chini yametuama ila hakufanikiwa kuiona ardhi baada ya kushindiliwa mateke mawili ya shingo ambayo yalimburuza mbali sana kwenye maji ambayo yalikuwa hapo karibu.

Alipata maumivu ambayo ilikuwa ni siri yake ndani ya mwili wake namna ya kuweza kuyaelezea, akiwa anatoka damu kwenye mdomo wake na puani huku kifua kikiwa kinawaka moto pamoja na shingo yake, aliinuka kwa maumivu huku akiunguruma kupiga kelela za hasira, aliinyoosha shingo yake mpaka ilipokaa sawa akageukia ule upande ambao alikuwepo mvamiaji ambaye kwa namna alivyokuwa anamshambulia alionekana kwamba alikuwa hapo kuweza kumuua.

Ila wakati anageuka tu, umeme ulikatika ghafla sana hata yeye mwenyewe alibaki kwenye mshangao maana lilikuwa ni tukio la haraka sana ambalo hata yeye hakuweza kulitegemea kwamba lingetokea majira hayo na wakati kama huo. Kukatika kwa umeme huo kwake ilikuwa ni ahueni maana angepata muda wa kupumzika japo gizani ingekuwa ni ngumu kumuona adui yake ila aliamini kwamba angekuwa makini na wakati huo angepumua kwanza kwani mtu ambaye alikuwa anapambana naye kama sio umeme kukatika basi ni wazi angemuua mapema mno.

Alitulia na kuweza kusikilizia kujua adui yake alikuwa wapi lakini hakusikia kitu zaidi ya mvua ambayo ilikuwa inaendelea kushuka kwa wingi. Akiwa anahitaji kupiga hatua moja umeme ulirudi tena lakini alishangaa baada ya kugundua kwamba mtu ambaye alikuwa amemvamia kwenye hilo eneo hakuwepo, ikimaanisha kwamba ni muda mrefu sana alikuwa ametoweka hapo. Aligeuka kwa pupa sehemu ambayo begi lake lilidondokea baada ya kupigwa lakini begi halikuwepo kwenye hilo eneo ishara ya mhusika ambaye aliingia hapo kutoweka nalo.

Aliogopa sana na kubaki akitetemeka kwenye mdomo wake, hakuwa anaamini kwamba alikuwa amelipoteza begi kizembe sana namna hiyo na begi hilo lilionekana kuwa la mhimu sana. Akiwa kwenye huo wasiwasi mkubwa aligundua kwamba mita kadhaa kwa chini kutoka alipokuwa amesimama yeye kulikuwa na karatasi nyeupe ambayo ilikuwa na maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwa damu ikiendelea kunyeshewa na mvua pale chini.

Aliisogelea karatasi hiyo na kuiokota ila baada ya kusoma kilichokuwa kimeandikwa hapo, aliiachia ghafla sana na kuanza kurudi nyuma huku akiwa anatetemea mwili mzima mpaka meno yake kwa namna alivyokuwa ameogopa na kushtuka kwani halikuonekana kuwa tukio la kawaida kwake kuweza kuona hali kama hiyo. Karatasi hiyo ilikuwa na maandishi ambayo yalikuwa yanasomeka “KAMARI YANGU YA MWISHO NDIYO KAMARI YAKO YA KWANZA”

Aliogopa sana kwa sababu hiyo ilikuwa ni kauli ambayo alikuwa anaitumia mwanaume mmoja ambaye yeye mwenyewe alimuua kwa mkono wake miaka kadhaa ambayo ilikuwa imepita. Aliangaza ile sehemu ambayo shoka lilikita muda ule lakini hakuliona hivyo aligundua kwamba mhusika alikuwa ameondoka na shoka lake na kilikuwa ni kitendo cha haraka sana, alisogea hatua kadhaa na kukiokota kisu chake na kukipachika tena kiunoni huku akiwa anaitoa simu yake mfukoni akionekana kwamba kuna mtu wa mhimu sana ambaye alikuwa anahitaji kumpatia taarifa za tukio hilo ila kwa bahati mbaya sana simu ambayo alikuwa anahitaji kuitumia kufanyia mawasiliano ilikuwa imevunjika na hapo akakumbuka kwamba ilipasuka baada ya teke zito kuzama hiyo sehemu hivyo aliamua kutoweka haraka sana hilo eneo.


Rasmi tunaanza kuifunua episode 1, ni mwanzo tu wa yale mengi ambayo tunakwenda kuyafunua ndani ya simulizi hii mpya. Nipe muda wako, jicho lako na umakini wako ile twende sawa ndani ya simulizi hii.

Kwenye kalamu nipo mwenyewe.

Tchao.
 
Hakuna kipya chini ya jua
alionekana mwanaume mmoja akiwa ndani ya nguo nyeusi na begi jeusi kwenye mkono wake huku koti lake jeusi refu ambalo lilivuka magotini likikamilisha mwonekano wake wa kuwa moja kati ya wanaume ambao walikuwa wanatisha mno.
Wandishi wa kibongo bhana. Kwahiyo Vyeusi tu ndo huwa vinatisha. 😂😂😂
 
Hakuna kipya chini ya jua

Wandishi wa kibongo bhana. Kwahiyo Vyeusi tu ndo huwa vinatisha.
Nani amekwambia kuna vipya chini ya jua?

Nani amekwambia vyeusi ndo vinatisha? Kwahiyo hata selection ya mavazi ya wahusika wangu ulitaka nije kukuuliza wewe hapo yanayo kufurahisha? Nadhani ulitakiwa kuuliza why nilitumia mavazi meusi kwenye hiyo situation na sio kukimbilia kushambulia.


Soma kinacho kupendeza, kisicho kupendeza achana nacho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 2
MIAKA 12 ILIYOPITA
Ndani ya nyumba za siri za shirika la kijasusi la taifa la Tanzania, vijana wawili walikuwa wanapokea kiapo kikali sana kwa spy master (Director General) kwa lugha rahisi mkurugenzi wao wa shirika la kijasusi mheshimiwa Philipo Tibaigana ambaye alikuwa na asili ya Kihaya. Nyumba hizo za siri ambazo ndizo walizitumia kuweza kula kiapo hicho zilikuwa pembezoni kabisa mwa jiji la Dar es salaam ambalo ndilo lilikuwa jiji kubwa zaidi la biashara ndani ya taifa la Tanzania hivyo mambo mengi yalikuwa yanafanyika ndani ya jiji hilo.

Vijana hao wawili walikuwa wanakula kiapo cha kwenda kumlinda raisi mpya wa taifa la Tanzania ambaye alikuwa ameshinda kwenye uchaguzi ambao ulikuwa umepita kwa kishindo japo kupita kwake nyuma kulikuwa na mambo mengi sana ndiyo sababu vijana hao walikuwa wanapewa kazi ya kuhakikisha raisi huyo anakuwa salama kwa namna yoyote ile. Baada ya kumaliza mafunzo yao ambapo walipelekwa ndani ya taifa la Uingereza, Urusi na Cuba, sasa walikuwa wameiva vya kutosha na walikuwa kamili gado kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaenda kuianza kazi yao hiyo ambayo ilikuwa ni mpya kabisa kwao ila hawakuwa na namna zaidi ya kuipokea amri kutoka kwa kiongozi wao ambaye ndiye alikuwa anawaapisha wakati huo.

Wanaume hao wawili walikuwa ni vijana wa umri wa kawaida tu ila uimara wao na mafunzo makali ambayo walikuwa wamefanikiwa kufuzu na kushika nafasi za juu miongoni mwa wengi ambao walikuwa wanatengenezwa kwa ajili ya kuja kudumisha ulinzi kwa viongozi wao ndiyo sababu kubwa ambayo iliwafanya wao ndio wapate hiyo nafasi ya kuweza kuchaguliwa kutekeleza majukumu ya taifa.

“Itifaki za nchi zinamtaka raisi wa kike kuweza kulindwa na mwanamke na hilo litafanyika lakini kuna mabadiliko kidogo yatafanyika, mlinzi wake wa kike atakuwepo lakini ninyi ndio ambao mtakuwa mnaongozana na huyo mlinzi kwa sababu sina imani na usalama wa mheshimiwa na sitaki tatizo lolote litokee nikiwa nipo kwani nitaonekana kama siwezi kuitekeleza kazi yangu vizuri kitu ambacho sijawahi kukubali nipate aibu ya kijinga kama hii hivyo nina imani mnajua ni kipi mtatakiwa kufanya si ndiyo?” aliuliza mheshimiwa huyo akiwa anawaangalia vijana hao wawili ambao walikuwa wamesimama kikakamavu sana.

“Ndiyo bosi” walijibu kwa pamoja kwa kujiamini sana.

“Mnajua kazi ya mhimu inayo wapelekea kule?”

“Kumlinda mheshimiwa raisi hata ikitulazimu kuyatoa maisha yetu itakapo hitajika kufanya hivyo”

“Nadhani sasa mshakula kiapo tayari na kazi iliyobakia ni nyie kutekeleza kile ambacho kipo mbele yenu. Kitu ambacho mnatakiwa kukikumbuka kila wakati kwenye vichwa vyenu ni kwamba serikali imetumia pesa nyingi sana kuweza kuwatengeneza nyie hapo ili mje kuifanya kazi hii, pesa hizo zingeenda hata kwa watoto yatima au wagonjwa lakini zinakuja kwenu kwa sababu ni jambo la mhimu sana kuilinda tunu ya taifa. Hakuna lolote ambalo unatakiwa kumuuliza wala kuhoji hata kama unaona anakosea hiyo siyo kazi yako wala siyo majukumu yako kuingilia kwa lolote. Haijalishi anaua ni mtu asiye na hatia, haijalishi anatukana mbele yenu, haijalishi anamtaka nani na hamtaki nani hamtakiwi kufanya upumbavu wowote wala kufanya kituko chochote maana sio majukumu yenu kabisa hivyo msije mkavuka mipaka maana mtakufa siku hiyo hiyo na nitawaua kwa mkono wangu mwenyewe, mnanielewa?”

“Ndiyo bosi tunakuelewa”

“Kumbukeni kwamba yule amechaguliwa na wananchi hivyo wananchi wanatarajia usalama wake kupewa kipaumbele kabla ya jambo lolote lile kutoka kwa vyomba vya ulinzi na usalama, hakuna kosa linatakiwa kufanyika. Naamini sana juu ya uwezo wenu, naamini sana kile ambacho mnacho ndani yenu, najua nyie ni wazalendo wakubwa hivyo mheshimiwa anatakiwa kuwa salama, hakuna kitu au mtu ambaye anatakiwa kugusisha hata mkono wake japo kwa bahati mbaya kwenye mkono wa mheshimiwa raisi. Wala hakuna risasi au kitu kilichorushwa kumpata hata kwa bahati mbaya ikiwa mpo hai na kama hilo linatokea basi litokee nyie mkiwa mmeshakufa tayari, mnanielewa?”

“Ndiyo bosi tunaapa kwa katiba ya nchi hii kuweza kumlinda mheshimiwa raisi hata kuyatoa maisha yetu pale ambapo itatubidi kufanya hivyo”

“Good. Kuanzia leo mnapewa majina mapya na namba zenu za siri ambazo ndizo zitakuwa code ambazo mtakuwa mnazitumia. Majina na hizi namba mnapewa kuendana na uwezo wenu na sio kigezo cha umri.”

“Sawa bosi” alimgeukia mmoja ambaye alikuwa anaonekana mkubwa kuliko mwenzie akiwa anamwangalia machoni kwa msisitizo.

“Wewe ndiye mkubwa kuliko mwenzako ukiwa na miaka ishirini na mitano tu lakini nina uhakika hata wewe mwenyewe unaelewa kwamba mwenzako amekuzidi kwa uwezo, hivyo kuanzia leo wewe jina lako ni Dax na namba yako ya siri ambayo utakuwa unaitumia kwenye mawasiliano ni 002” alimpatia vitambulisho vyake pamoja na kumbana na mashine kwenye mkono wake wa kulia ambapo tattoo hiyo ilijichora hapo japo alipata mauamivu makali ila hakushtuka maana hicho alichokuwa anapewa ndio ulikuwa utambulisho wake” kiongozi huyo baada ya kumalizana na kijana wa kwanza alimgeukia kijana wake wa pili.

“Una miaka ishirini na mitatu tu pekee lakini nakuamini na kukupa nafasi hii kubwa ya kuweza kumlinda mheshimiwa raisi wa nchi. Wewe ni miongoni mwa wachache sana ambao taifa limebahatika kuwapata kutokana na uwezo wako kuwa mkubwa sana kuliko hata umri wako hivyo hili jukumu la usalama wa raisi nalikabidhi kwenye mikono yako kwa sababu nakuamini sana. Wewe ndiye ambaye utakuwa unatoa ripoti kwangu na kunipa kila taarifa ya ambacho kitakuwa kinatokea na wewe ndiye ambaye utatakiwa kuwa wa kwanza kuyatoa maisha yako kama mheshimiwa atakuwa kwenye hatari yoyote ile ambayo inaweza kupelekea kuhatarisha maisha yake. Hakikisha hakuna kosa lolote lile ambalo linajitokeza hata kwa bahati mbaya. Umenielewa?”

“Ndiyo bosi, nakuahidi nitaifanya hii kazi kwa usahihi na uzalendo mkubwa mpaka pumzi yangu ya mwisho”
“Kuanzia leo jina lako wewe ni Max na namba yako ya siri ni 001” aliongea akiwa anamkabidhi vitambulisho vyake pamoja na kumbana na mashine ambayo ilikuwa kwenye mkono wake mpaka ilipo jichora hiyo tatuu ambayo ilikuwa na hiyo namba 001” baada ya kumalizana nao, kuna wanaume waliingia wakiwa kwenye suti zao kuwachukua vijana hao wawili ambao walikuwa wanaenda kuanza kuifanya kazi ya kuweza kumlinda mheshimiwa raisi wa nchi ya Tanzania ambaye alikuwa ameshinda uchaguzi wake ambao hata yeye hakuwahi kutarajia kama anaweza kufika hapo alipokuwa amefikia kwa siku hiyo.

Teodensia Mpanzi, ndilo lilikuwa jina la aliyekuwa raisi wa nchi ya Tanzania, mwanamama ambaye alikuwa ameyabeba maono ya watanzania wengi, mwanamama ambaye aliamini kwamba nchi ilikuwa inapaswa kwenda mbali zaidi ya pale ilipokuwa imefika huku akiwa ana imani kwamba watangulizi wake hawakuifanya kazi ambayo walitakiwa kuifanya ili kuhakikisha kwamba nchi inajengekea na kuwa moja kati ya mataifa makubwa na yenye nguvu sana duniani.

Alikuwa ameapishwa tayari na ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza tangu akabidhiwe ofisi yake, na ndiyo muda ambao waliingia walinzi wa Ikulu huku wakimpa taarifa mheshimiwa kwamba kulikuwa na ugeni wa wanaume wawili ambao walikuwa wameletwa hapo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba yupo salama muda wote lakini habari hiyo yeye hakuisadiki kabisa wala kuikubali. Alimpigia simu Philipo Tibaigana ili aweze kulijibia hilo na kujua kama alikuwa na taarifa juu ya ujio wa vijaan hao ambao aliambiwa kwamba muda mfupi wangeripoti hapo ofisini kuweza kuanza kuifanya kazi ya kumlinda yeye.

“Mzee wangu habari ya kazi?” alimsalimia kwa kumheshimu kwa sababu alikuwa amemzidi umri.

“Salama mheshimiwa, heshima yako kiongozi wangu”

“Nasikia kuna vijana wanakuja kunilinda hapa, kwamba haujaona walinzi wa kike kwamba wananitosha mpaka uniletee hawa vijana wako ambao sijui hata lengo lako la kuwaleta ni lipi? Unahisi kweli itafaa mimi kuendelea kukubakisha kwenye hiyo nafasi?”

“Naomba unisamehe sana mheshimiwa, najua kwamba unaweza ukampa nafasi hii mtu yeyote yule ambaye unamtaka wewe lakini mimi nimefanya hivyo kwa sababu za usalama zaidi na itifaki ya nchi. Walinzi wa kike ni wengi sana na wapo wa kutosha ila nina sababu za mhimu kukuletea hao vijana kwani ndio vijana pekee ambao wamepata alama za juu kabisa za haya mafunzo na serikali imetumia pesa nyingi sana kuwapa mafunzo kwenye nchi mbali mbali takribani miaka mitano hivyo wamebobea sana kwenye taaluma hii ndiyo maana nikawaleta kwako ukizingatia namna ulivyokuwa unafanya kampeni zako ulipokea vitisho vingi sana hivyo sitataka raisi wangu upate matatizo mimi nikiwa madarakani maana bado hatujui nani yupo upande wako na nani hayupo upande wako”

“Mhhhhh wazo lako ni zuri sana ila sidhani kama kweli haujui nani yupo upande wangu na nani hayupo upande wangu, sisi sio watoto wadogo. Najua unalielewa hili taifa ndani nje na wewe ni miongoni mwa watu ambao walikuwepo tangu enzi za mtangulizi wangu na unamjua vizuri namna alivyo kwahiyo ukisema hauelewi unakuwa unanipa sana mashaka. Nitawapokea na nitaangalia uwezekano kuhusu nafasi yako kama utaendelea kubaki au nikupe ubalozi mataifa ya mbali huko, uwe na siku njema”

“Asante sana mheshimiwa” kiongozi huyo wa shirika la kijasusi alijibu lakini hakuridhika kwani kwake aliona kama dharau, yaani licha ya kujitoa kwake kote bado alikuwa anatishiwa kupelekwa kuwa balozi kwenye mataifa ya mbali huko, kwake ilikuwa ni zaidi ya dharau hiyo maana raisi huyo ni kama alikuwa anahitaji kumtoa nje ya mfumo wake.

Teodensia Mpanzi baada ya kuikata simu hiyo ambayo aliipiga kwa mkurugenzi, alitoa amri kwamba vijana hao waingizwe ndani ya ofisi yake anahitaji kufanya nao mazungumzo ya siri akiwa yeye na wao tu pekee. Baada ya dakika kumi waliletwa vijana hao wawili na mlinzi wa humo ndani kisha baada ya kuwafikisha akawaacha wao wawili tu na mheshimiwa raisi maana yeye mwenyewe ndiye alikuwa ametoa amri iwe hivyo.

Aliwaangalia kwa umakini sana, vijana hao hawakuwa na sura za kutisha sana kwa mtazamo wao. Mkubwa zaidi angalau alikuwa ana sura ambayo ilikuwa imekomaa zaidi lakini ambaye alikuwa anaonekana mdogo sura yake ilikuwa kama barobaro mtaani japo wakati huo alikuwa kwenye suti ambayo ilikuwa imemkaa vyema sana.

“Nimepata taarifa zenu kutoka kwa mr Philipo Tibaigana lakini yule mhaya simwamini sana maana kuna muda huwa anapenda sana kusifia vitu ambavyo havitakiwi kusifika, nawaaminije juu ya uwezo wenu na kuwapa dhamana ya kuweza kunilinda ingali sijui hata uwezo wenu upoje?”
“Mimi nimepata mafunzo yangu ndani ya taifa la Tanzania lakini baada ya kufuzu nikapata nafasi ya kwenda Cuba kwa ajili ya mapigano. Huko nilifanya vizuri zaidi nikapata nafasi ya kwenda kupata mafunzo ya kijasusi ndani ya nchi ya Uingereza ambapo nilikaa mwaka mmoja ndipo nikafaulu vizuri na kufanikiwa kwenda kumalizia mafunzo yangu ndani ya nchi ya Urusi” Dax alitoa maelezo yake kikakamavu sana huku akiwa amemkabidhi mheshimiwa taarifa zake na wakati anaendelea kuyatamka hayo maneno mheshimiwa raisi alikuwa anaendelea kuzipitia taarifa zake na baada ya mwanaume huyo kumaliza mheshimiwa aliinua uso wake na kumwangalia usoni kwa umakini maana sifa zilizokuwa zimeandikwa pale kuhusu yeye ni kama hakuwa akiendana nazo kabisa.

“Jina lako unaitwa Karistus Dickson (KD) lakini unatambulika kama Dax na namba yako ya utambulisho ni 002?”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Mhhh hizi ni taarifa zako kweli? Mbona zimeandikwa taarifa ambazo haziendani na mwonekano wako?”

“Hizo ni zangu mheshimiwa ndiyo maana nipo hapa na naapa kukutumikia mpaka pumzi yangu ya mwisho, nitatii na kufanya kila ambalo unalitaka lakini lengo kubwa ni kuyalinda maisha yako hata ikiwezekana kuyatoa maisha yangu kwa ajili yako”

“Una uhakika upo tayari kufa kwa ajili yangu?”

“Ndiyo mheshimiwa” mwanaume huyo alijibu akiwa amesimama kijasiri sana, raisi alimwangalia kwa umakini sana akiwa haamini hayo maneno hivyo alizunguka mpaka kwenye droo yake na kuitoa bastola ambayo ilikuwa imekokiwa kabisa.

Episode ya pili natundika daruga hapa.

Tukutane wakate ujao.

Tchao.
 
NOTE:

Please over please sipendi matusi hususani kwenye threads zangu hivyo ukiona simulizi nazoleta hazikuvutii isiwe kigezo cha kusumbua wengine.

Ukiwa na cha kunikosoa wewe kosoa uwezavyo ila matusi achana nayo.


Ni mara mia usome simulizi za watu ambao unahisi wanakuburudisha kuliko kuvamia thread za watu na kuleta mihemko yako hapa.


Good evening
Of course, ukiacha upumbavu wako kama unaoufanya kwenye riwaya zako zengine tutaacha matusi! Shenzi taipu!
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 3
“Jina lako unaitwa Karistus Dickson (KD) lakini unatambulika kama Dax na namba yako ya utambulisho ni 002?”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Mhhh hizi ni taarifa zako kweli? Mbona zimeandikwa taarifa ambazo haziendani na mwonekano wako?”

“Hizo ni zangu mheshimiwa ndiyo maana nipo hapa na naapa kukutumikia mpaka pumzi yangu ya mwisho, nitatii na kufanya kila ambalo unalitaka lakini lengo kubwa ni kuyalinda maisha yako hata ikiwezekana kuyatoa maisha yangu kwa ajili yako”

“Una uhakika upo tayari kufa kwa ajili yangu?”

“Ndiyo mheshimiwa” mwanaume huyo alijibu akiwa amesimama kijasiri sana, raisi alimwangalia kwa umakini sana akiwa haamini hayo maneno hivyo alizunguka mpaka kwenye droo yake na kuitoa bastola ambayo ilikuwa imekokiwa kabisa.

“Hii ni bastola ambayo ina risasi zote sita na imeshakokiwa tayari, hivyo nahitaji ujipige risasi ili niamini kwamba kweli upo tayari kufa kwa ajili yangu” alimaliza maelezo yake huku akiwa anamkabidhi mkononi na mwanaume huyo hata hakujiuliza mara mbili, aliilengesha bastola hiyo kwenye kichwa chake kisha akaachia risasi lakini aligundua kwamba ndani hakukuwa na risasi yoyote ile, ina maana raisi alikuwa anampima kama kweli yupo tayari kufanya lolote kwa ajili yake. Mheshimiwa alimpigia makofi na kumpongeza mwanaume huyo wa kazi kisha akamgeukia ambaye alikuwa anaonekana mdogo kuliko mwenzake na kulishika faili lake bila kumpa ruhusa ya kuweza kuongea lololote.

“Donald Daniel (Double D (DD), jila lake la utani DONNY lakini jina la kazi ni Max na namba yake ya utambulisho ni 001. Ndiye mwanafunzi bora wa mafunzo ya miaka mitano ndani ya taifa la Tanzania akiwa ameyapatia mafunzo yake ndani ya taifa la Tanzania, Cuba, Uingereza pamoja na Urusi na huyu ndiye atakaye ichukua nafasi ya kuweza kuhakikisha usalalama wa mheshimiwa raisi mahali popote na kwa muda wowote ikilazimu hata kuweza kuyatoa maisha yake kwanza kabla mheshimiwa hajapata madhara” mheshimiwa raisi alibaki ameduwaa akiwa anasoma ripoti ya huyo kijana kutoka kwa mkurugenzi. Ni kama alikuwa haamini kile ambacho alikuwa anakisoma hivyo akawa anamwangalia kijana huyo mara mbili mbili.

“Hizi zilizo andikwa humu ni taarifa zako wewe?”

“Ndiyo mheshimiwa”

“Nataka unithibitishie kwa macho yangu sidhani kama inawezekana kweli wewe ndo uwe hivi, baadae kidogo kuna watu nahitaji ufanye nao mazoezi ya mapigano ndipo nitathibitisha kama hizi taarifa ni za kweli, na kama ni kweli basi kuanzia leo nawapa hiyo ruhusa ya kuweza kunilinda lakini kama ukishindwa basi wote nawaua kwa kuniletea taarifa za uongo pamoja na huyo mkurugenzi wenu. Mmenielewa?”
“Ndiyo mheshimiwa” wanaume waliruhusiwa kuweza kutoka ndani ya ofisi ya raisi wa nchi na huo ndio ulikuwa mwanzo wao wa kukaa karibu na mheshimiwa raisi na kuwa walinzi wake rasmi.

ALEXIOS ARENA
Ulikuwa ni ukumbi mkubwa sana ambao ulikuwa unaendesha Kamari hususani za mapigano. Ni ukumbi ambao ulikuwa unajulikana mpaka na viongozi wa serikali ila walikuwa wanafumba macho na kuziba masikio kila jina hilo linapo tajwa bila kujulikana kwamba kwanini walikuwa wanafanya mambo hayo licha ya kujua kwamba ndani ya ukumbi huo kulikuwa kuna mambo mengi sana ya kutisha ambayo yalikuwa yanafanyika hapo. Sio kila mtanzania alikuwa anaweza kwenda kuingia ndani ya ukumbi huo kwani walikuwa wanahitajika watu wenye pesa za kutosha na ukwasi mkubwa ndio ambao walikuwa wanapata nafasi ya kwenda kutazama mapambano ya wanaume humo ndani.

Ni ukumbi ambao ulikuwa umeshamiri kwa uchezaji wa Kamari na wacheza Kamari maarufu ndani ya nchi ungewakuta humo ndani. Mapigano ambayo yalikuwa yanafanyika humo ndani yalikuwa ni ya mauaji, kama ungepanda ulingoni na ukashindwa kushinda basi moja kwa moja ulikuwa unauawa na hivyo ndivyo wanaume wa shoka walivyokuwa wanautafuta ugali na kuyaishi maisha ndani ya ukumbi huo wa kutisha. MLINZI ndiyo ilikuwa maana ya ukumbi huo mkubwa kwa tafsiri ya Kiswahili ambapo ilidaiwa kwamba muasisi wa ukumbi huo ndiye ambaye alipewa jina hilo lenye asili ya kigiriki ikiwa na maana ya kwamba ndiye ambaye alikuwa anausimamia ukumbi huo na kuhakikisha kwamba upo salama.

Wanawake walikuwa wanafanya biashara za kuuza miili humo ndani tena kwa dau kubwa mno kwa sababu maskini haikuwa sehemu yao sahihi zaidi ya kuishia kusimuliwa tu raha zipatikanazo ndani ya ukumbi huo, kulikuwa na makasino ya bei ghali sana humo ndani na kila kitu kilipatikana lakini chini kabisa ya ukumbi huo kulikuwa na ulingo wa mapambano ambapo walikuwa wanapatikana wanaume wa shoka haswa ambao walikuwa wanauana ili kuweza kutengeneza ufalme na pesa kwa ajili ya kuweza kuishi maisha mazuri.

Usiku wakati pambano moja likiwa linaendelea ndani ya ulingo wanaume wakiwa wanapimana mabavu, upande wa juu kabisa walikuwa wamekaa wanaume watatu ambao wote walikuwa wamejifunika vikoi na kubakia sehemu za uso tu kwa mbali wakiwa wanashuhudia mpambano ambao ulikuwa unaendelea chini. Kujifunika kwao ni wazi ilionekana kwamba hawakutaka kabisa kuweza kujulikana na mtu yeyote kwamba walikuwa wapo ndani ya ukumbi huo.

“Huu ni moja kati ya uwekezaji bora sana ambao umewahi kuufanya mheshimiwa” aliongea mwanaume mmoja akiwa anashushia wine taratibu kwenye bilauri la thamani ambalo liliwekwa kwenye sinia la bati.

“Unajua uongozi ni dhamana ya muda mfupi sana ila wengi huwa hawaelewi, ndani ya huo muda mfupi ndio ambao unaweza kuamua hatima ya maisha yako ya baadae itakuwaje. Kuna watu wanataka sifa tu za kusifiwa halafu mwisho wa siku wanakuja kutia huruma lakini kuna watu ambao ni wapambanaji haswa wanaamua kuziweka sifa pembeni na kuamua kuwekeza sana kwa ajili ya baadae yao na mimi ndicho nilicho kifanya. Nilikuwa mwenye furaha sana mbele ya kila mtu kitu ambacho kilifanya nipendwe sana na wananchi lakini sikuwa mjinga nilijua kuna siku nitatoka ofisini hivyo nikaanza kutengeneza mazingira ya uwekezaji kila kona ya nchi na kila kona ya dunia ili nikitoka ofisini nianze kuyaishi maisha bila wasiwasi na sasa tupo hapa leo mnajionea moja kati ya sehemu ambayo nimewekeza licha ya kutupa burudani lakini pia inatuingizia mabilioni ya fedha kwa siku moja tu pekee” mheshimiwa huyo ambaye alikuwa amekaa katikati yao aliongea kwa majivuno kweli kweli huku mbali kidogo na walipokuwa wamekaa wakiwa wamesimama wanaume ambao walikuwa wanaonekana ni watu wa kazi haswa kulingana na namna miili yao ilivyokuwa.

“Mara ya kwanza wakati unanikalisha chini na kunipa mpango wa kuwekeza pesa zangu hapa, niliona kama ni wazo la kijinga sana ila kwa sasa nimekuja kuelewa kwamba ni kwanini ulichaguliwa kuwa kiongozi wa hii jumuiya yetu ya watu ambao tutatengeneza pesa ambazo vizazi vyetu vitaishi maisha ya kifahari sana mpaka miaka zaidi ya miamoja ijayo” mwanaume mwingine ambaye alikuwa mnene kuliko wote aliongea akiwa anacheka kwa furaha sana.

Hao ndio ambao walikuwa wamiliki wa eneo hilo, mwanaume ambaye alionekana kuwa kiongozi wa hiyo sehemu alikuwa anaitwa Denis Kijazo, huyu alikuwa raisi ambaye ndiye alikuwa ametoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Teodensia Mpanzi. Mwanaume kibonge alikuwa anajulikana kwa jina la Madilu Mpagazi, huyu alikuwa ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa sana ndani ya taifa la Tanzania na alikuwa mfanya biashara mkubwa sana.

Mwanaume ambaye alikuwa wa tatu ndani ya sehemu hiyo alikuwa anaitwa Msafiri Kigoti, huyu alikuwa ni gavana wa benki kuu ya taifa la Tanzania, ndiye alikuwa anakamilisha hesabu ya wanaume watatu ambao usiku huo walikuwa ndani ya ukumbi mkubwa wa ALEXIOS ARENA ambapo wao ndio walikuwa wawezekezaji wakuu ndani ya sehemu hiyo.

“Akili ni nguvu kubwa lakini nguvu ya kweli ni pesa, akili bila pesa ni upigaji wa kelele tu kama hautakuwa na mzigo wa kutosha kwenye mifuko yako hivyo kwangu huwa natumia vyote, akili na nguvu ya pesa ndiyo maana niliweza kuja na wazo kubwa sana kama hili kwa sababu najua nchi hii kuna mafisadi wengi sana ambao wana pesa nyingi mno na hawana cha kufanyia. Sasa tunawezaje kuzichukua pesa hizo kwenye mifuko yao bila wao kushtuka? Ndipo nikatengeneza huu mchezo ili waje kula maisha huku kwa pesa kubwa sana na zingerudi tena kwetu bila kugombana nao kwani wengi ni vijana wangu na wanafanya kazi chini yangu hivyo usingekuwa ustaarabu kama ningetumia nguvu kuchukua pesa ambazo niliwaahidi, nilitengeneza mfumo ambao watazirudisha kwangu bila wao kujua na kwa sababu wengi wao ni watu wa starehe sana imekuwa rahisi hata kuliko nilivyo tarajia” Denis Kijazo aliongea huku akishuhudia ulingoni mtu akitolewa koromeo na mwanaume mwenzake ambaye alikuwa anaihusudu zaidi pesa.

“Uko sahihi ila unahisi huyu raisi wa sasa ataruhusu hili liendelee? Kumbuka hauko ofisini na wewe ndiye ambaye ulikuwa unatulinda na kulinda kila mali zetu zisiguswe na mtu yeyote yule. Wewe ndiye ambaye ulikuwa unahakikisha hatulipi kabisa kodi na kuwaacha maskini waendelee kulumbana na kupigiana kelele huko, vipi una imani na huyu mama kwamba hatatuzingua kwa sasa na kuanza kuingilia kwenye hizi biashara zetu?” Madilu Mpagazi alionyesha wasiwasi wake moja kwa moja mbele ya mheshimiwa huyo huku akiwa hana imani sana na hali ambayo ilikuwepo wakati huo.

“Upo sahihi, hilo suala nililiwaza kwa ukaribu sana kabla hata ya kufanya haya maamuzi, ni jambo ambalo hata mimi liliniumiza sana kichwa maana lilikuwa limeshika hatima nzima ya maisha yangu ya baadae na kama ningekosea basi ingekuwa hatari sana kwangu. Huyu raisi ni kijana wangu mimi ambaye nimemuweka mwenyewe pale Ikulu baada ya kutokea mpasuko mkubwa sana ndani ya chama kuweza kubishana juu ya nani ambaye alikuwa anastahili kuingia Ikulu huku kila mtu akitaka mtu wake akae pale, hata mimi nilikuwa na mtu wangu mwingine ambaye nilikuwa nimemuandaa kuingia pale ila kulingana na ile hali nilifanya kumteua bibie na kumpa nafasi ya kuingia pale Ikulu ili kuweza kuhakikisha mambo yanakuwa sawa ionekane kwamba kila mtu amekosa na hapo ndipo watu wakatulia baada ya kuona hata mtu wangu kakosa”

“Nilifanya hayo yote ili kurudisha imani zao kwanza maana ingekuwa ni hatari sana kama mpasuko ule ungeendelea ndani ya chama tungekuja kuvuana nguo wenyewe na kuanza kuuana wenyewe. Lakini yule bibie ambaye nimemuweka pale Ikulu ni kijana wangu mtiifu wa muda mrefu sana ambaye amepikwa kwenye mikono yangu mwenyewe hivyo nina imani kwamba atatii kila kitu na kwa hali yoyote ile lazima atafanya ambacho mimi nakitaka. Vijana wangu ambao wameshindwa tutawaingiza kwenye baraza la mawaziri, kijana wangu ambaye alitakiwa kuwa raisi anatakiwa kuwa waziri mkuu au anaweza kuingia tu kama waziri wa kawaida lakini hata nyie watu wenu ambao mlikuwa mnataka wakasimamie maslahi yenu nafasi zao zipo na nimelizingatia hilo vyema kabisa na kwa sasa ninavyo ongea na nyie nimesha mtumia listi ya watu ambao wanatakiwa kuingia huko kwenye nafasi za juu na sehemu ambazo wanatakiwa kuwepo hivyo uaminifu wake wa kwanza unaanzia hapo. Anatakiwa kuwaweka watu ambao nawataka mimi kwahiyo nadhani hamna haja ya kuogopa kila kitu kipo ndani ya mpango”

“Yes, hilo ni jambo la mhimu sana kuweza kufanyika na nikupongeze kwa hilo ila kuna jambo moja huenda lisiwe sawa sana. Vipi kuhusu yeye kufuatiliwa kwa umakini, tujue anawaza nini, anawazaje, anamtumia nani kufanya maamuzi yake na nani na nani ambao ni waaminifu sana kwake kiasi kwamba kama kutakuwa na hali ya sintofahamu tuweze kuishughulikia haraka sana. Kwenye haya maisha hatupaswi kumuamini mwanadamu moja kwa moja kwani wanadamu wanabadilika sana, tunaweza kuja kushtuka wakati tumeshachelewa ikawa ni tatizo sana kwa upande wetu” Gavana wa benki kuu mheshimiwa Msafiri Kigoti alikuwa makini sana kuhakikisha maslahi yao yanalindwa ipasavyo ndiyo maana alitaka uhakika wa kila kitu.

Episode ya 3 leo naihitimisha hapa, panapo majaliwa tukutane ndani ya sehemu zinazo fuata.

Wasalaam,

Febiani Babuya.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 4
“Vijana wangu wote ni watiifu sana kwangu labda kama huyu ndiye atakuwa wa kwanza kuanza kwenda kinyume na mimi na kama akifanya hivyo basi nitamfanyia kitu kibaya sana ambacho hatasahau kwenye maisha yake yote. Nimeshampa maagizo mkurugenzi wa usalama kwamba anatakiwa haraka sana kuweza kuwatuma vijana wa kwenda kuongeza ulinzi huko na tayari amefanya hivyo kwa kuwapa vijana hao wawili kazi lakini hao ndio ambao wataifanya hiyo kazi ambayo wewe ulikuwa unaiongelea hapa saivi”

“Mmoja wa vijana hao anajua kazi ambayo anaenda kuifanya kule Ikulu ila mmoja hajui na huyo ambaye hajui amepewa nafasi ya kuripoti kila kitu kwa mkurugenzi hivyo tutakuwa tunapata taarifa sehemu zote mbili huku mmoja akiwa anatoa taarifa bila kujua kwamba zinatumika kwenye nini na mmoja atakuwa anafanya kazi akiwa anajua kile ambacho anatakiwa kukifanya. Ondoeni shaka kama ambavyo nimewaambia tangu mwanzo kwamba kila kitu kipo ndani ya mpango”

“Hakika wewe ni mtu mwenye maono ya mbali sana mheshimiwa”
“HILI NI JIJI LA KAMARI ndugu yangu, namna unavyojua kuicheza hiyo Kamari yako ndiyo ambavyo unajihakikishia nafasi ya kuwa mshindi na bingwa ndani ya eneo lako, hahahaha hahahah” mheshimiwa alicheka sana huku akiitoa simu yake na kuipiga moja kwa moja Ikulu ambapo ilifika kwa mheshimiwa raisi moja kwa moja.

“Hongera sana kwa ushindi wako, kuna kijana anakuja na bahasha hapo ipitie vizuri kisha ufanye kama bahasha inavyo jieleza. Ni matumaini yangu utanifanya nijivunie sana uwepo wako, uwe na bahati njema” ni maelezo mafupi sana ambayo alikuwa amempatia mheshimiwa raisi Teodensia Mpanzi kisha akaikata simu yake bila kusubiri salamu wala jibu kutoka kwa mtu ambaye alikuwa amempigia simu. Wanaume hao watatu wote walinyanyuka na kupeana mikono kisha wakaanza kutoka ndani ya jengo hilo kubwa sana wakiwa na ulinzi mkali isivyokuwa kawaida kwani haikutakiwa mtu yeyote ajue kwamba ni akina nani ambao walikuwa hapo. Hawakuwa watu ambao walikuwa wanajulikana kwamba ndio walikuwa wamiliki halali wa eneo hilo, baada ya kufika kwenye lango kuu la kuingilia hapo ndani mwanaume ambaye alifungua geti la chuma ambalo lilikuwa hapo aliinama kutoa heshima huku kwenye mkono wake akiwa na shoka kubwa sana ambalo lilikuwa na cheni ndefu ambayo iliunganishwa mpaka kwenye surali yake ambayo ilikuwa mwilini huku usoni kwake akiwa na alama kubwa sana ya kovu ambayo bila shaka alikuwa amekatwa vibaya sana siku za huko nyuma.

Simu hiyo kutoka kwa mheshimiwa Denis Kijazo ilimkuta raisi Teodensia Mpanzi ndani ya chumba chake cha kulala usiku huo. Alichukizwa sana na kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kwani ilikuwa ni kama kukosewa heshima kwa kiasi kikubwa sana, mtu ambaye alimpigia simu wakati huo hakumpa hata nafasi ya kujibu, alitoa tu maagizo na kuikata simu hiyo kuonyesha kwamba alikuwa anatoa amri na sio ombi.

Hali hiyo ilimfanya raisi achukie sana, alivaa nguo zake haraka sana na kutoka usiku huo huo kwenda ofisini kwake ambako alimkuta kijana anamsubiri akiwa na bahasha mkononi mwake.
“Nani amekupa ruhusa ya kuweza kuingia kwenye hii ofisi?” alimuuliza kijana huyo ambaye alikuwa ameingia mpaka ndani ya ofisi hiyo ambayo hakuna mtu alikuwa anatakiwa kuingia bila ruhusa yake.

“Samahani mheshimiwa mimi nimegizwa hapa nilete hii bahasha na nimeambiwa nisipokukuta niingie moja kwa moja mpaka humu ndani kukusubiri”

“Kuanzia leo hii usije ukaonekana tena maeneo ya hapa Ikulu, hauna kazi tena ya kufanya hapa hivyo utoweke haraka sana na nitampa taarifa kiongozi wako ya kukufuta kazi, huwezi ukawa unaikosea heshima ofisi kubwa ya nchi unaingia kama kwako”
“Lakini mheshim…….”

“Toka humu ndani nisije nikakupiga risasi bure hapa mpuuzi wewe” mheshimiwa alikuwa na hasira kali sana wakati huo kwani aliona kama huyo mtangulizi wake na watu wake walikuwa wanamkosea heshima pakubwa sana. Baada ya kijana huyo kutoka alihema kwa nguvu na kutulia akiwa anaangaza kila sehemu humo ndani, kuna kifaa ambacho alikitoa kwenye mfuko wake wa koti na kukiwasha kikawa kinapiga alamu kuelekea kwenye sofa moja ambayo ilikuwa jirani na alipokuwa amesimama.

Alizamisha mkono wake pembezoni mwa sofa hiyo ndipo alipokutana na kifaa cha kunasa sauti, ina maana kijana huyo alikuwa amewahi hapo na kutegesha hicho kifaa ili kila ambacho raisi atakuwa anakizungumza au kuwasiliana na mtu kwa njia ya simu waweze kukipata haraka sana. Alikikanyaga chini na kukipasua huku akicheka kwa nguvu ila kwa hasira mno, aliinyanyua simu yake na kuipiga kwa walinzi wa nje ambapo alitoa taarifa kwamba kijana huyo ambaye alikuwa ametoka hapo alitakiwa kuwekwa chini ya ulinzi haraka sana na usiku huo hakuna mtu ambaye alitakiwa kutoka au kuingia ndani ya hilo eneo mpaka ambapo angetoa amri nyingine ya kipi ambacho kilikuwa kinatakiwa kufuatia.

“Huyu atakuwa wa mfano kutuma ujumbe kwao kwamba huenda wanacheza na mtu ambaye hawatakiwi kabisa kumchezea kijinga au kumgusa kwa lolote lile” aliongea akiwa anafoka pekeyake ndani ya ofisi hiyo na kusogea taratibu pale mezani ambapo kijana yule alikuwa ameiweka ile bahasha ambayo alikuwa ameambiwa kwamba alitakiwa kuifanyia kazi na kama maelezo yalivyokuwa yanajieleza ndani yake.

Baada ya kuifungua ila bahasha alishangazwa mno na jambo ambalo lilikuwa ndani yake, ilikuwa ni orodha ya majina na nafasi mbali mbali ambazo watu wa majina hayo walitakiwa kuteuliwa, alipigwa na butwa baada ya kuona yeye kama raisi anapangiwa kwamba nani na nani wanatakiwa kuteuliwa na wapi ambao wanatakiwa kutenguliwa. Alitabasamu akiwa na hasira sana na kwenda kuichoma orodha hiyo ambayo alipewa kisha akafungua droo yake baada ya kuingiza namba za siri ambazo alikuwa ameziweka, akaitoa bahasha ambayo alikuwa ameiandaa yeye.

“Hii ndiyo serikali ambayo naenda kuwa nayo mimi na hawa ndio watu ambao naenda kufanya nao kazi mimi ila sio watu wa kupangiwa. Kuna kosa moja kubwa sana umelifanya mheshimiwa kuhisi kwamba mimi unaweza kuniendesha unavyotaka na mimi naweza kukaa hapa nikafanya kazi zako eti kwa sababu tu wewe ndiye ambaye umenifanya nimekuwa hapa. Nimekuwa mtiifu miaka yote hii na kujifanya mjinga ila kiuhalisia mimi sio mjinga, mimi sio mtu ambaye unaweza kunifanyia kile ambacho wewe unakihitaji na kuamua kadri unavyo taka wewe”

“Mimi ndiye raisi wa nchi hii, mimi ndiye bosi wa taifa, mimi ndiye mtu mkubwa zaidi na mwenye nguvu zaidi ndani ya nchi hii, sasa wewe ni nani hasa mpaka uhisi kwamba unaenda kunipangia cha kufanya? Kama kuna kosa kubwa ambalo umelifanya kwenye maisha yako basi ni kunipa mimi hii nafasi ya kuwa raisi, nakuhakikishia wewe na mafisadi wenzako nitawanyoosha na mtajuta sana kuzaliwa kwenye taifa hili” alitamka kwa hasira akiwa anapigiza kwenye meza wakati huo alikuwa anaongea mwenyewe ndani ya ofisi yake hiyo.

Alikuwa anaongea na nafsi yake ila aliamini kwamba nafsi yake ilikuwa inaongea na huyo kiongozi ambaye alihisi kwamba anaweza kufanya jambo lolote lile ambalo yeye alikuwa anahitaji kulifanya. Aliinuka muda huo huo wa usiku na kumpigia simu msemaji mkuu wa serikali pamoja na watu wake watoe taarifa kwa vyombo vya habari kwamba ndani ya nusu saa ijayo mheshimiwa raisi alikuwa anatoa mkeka wa baraza la mawaziri ambao angeenda kufanya nao kazi na siku ya kesho yake angefanya mabadiliko mengine makubwa sana ndani ya maeneo mbali mbali ya kiutendaji.

“Hawa wajinga natakiwa kuwatoa watu wao wote kwenye mfumo kisha niwaweke watu ambao hawajulikani sana ambao nina imani wanaweza kunisikiliza na kunitii na hili litakuwa jambo kubwa sana kwangu kwa maana nitakuwa na watu wengi sana wa kunilinda lakini pia natakiwa kutengeneza timu yangu mwenyewe ambayo itakuwa na watu watakao yapigania maisha yangu kwa namna yoyote ile maana hawa mafedhuli hawataniacha kama nikicheza vibaya. Kitu cha kwanza natakiwa kuwafanya waanze kuniogopa kwanza na natakiwa kuonyesha mfano kwa hawa mafisadi ambao listi yao yote ninayo” baada ya kumaliza kujishauri tena mwenyewe, mheshimiwa aliishika bahasha yake na kutoka nje ya ofisi yake ambapo palikuwa na ulinzi mkali sana akawa anaelekea kwenye ukumbi wa mikutano ya Ikulu ili kwenda kutoa hiyo taarifa na mkeka wa watu ambao wangeenda kuwa mawaziri chini ya utawala wake.

Hiyo ni taarifa ambayo ilimshtua kila mtu hususani wale ambao huwa wanapenda sana kuitumia mitandao ya kijamii. Walishangazwa na tukio hilo kwani walizoea mambo hayo kuweza kuyaona mchana hivyo walishangaa sana kuona yanafanyika usiku tena usiku sana, ila hayo hayakuzuia mheshimiwa kuweza kutekeleza kile ambacho alikuwa amekikusudia kukifanya usiku huo.

Mheshimiwa raisi Teodensia Mpanzi alitoa listi nzima ya majina ya mawaziri kila mtu na wizara yake ambayo alikuwa amepangiwa. Listi hiyo nzima ilikuwa ya kushangaza kwani watu ambao waliteuliwa hapo hawakuwa watu ambao walikuwa na majina makubwa kabisa serikalini na kwa wale ambao walikuwa na majina makubwa walikuwa ni wachache sana hususani wale ambao walikuwa wanayapigania sana maslahi ya nchi na wengine akiwa amewatoa vyama vya upinzani jambo ambalo lilizua taharuki kubwa sana ila kwa bahati mbaya sana yeye ndiye ambaye alikuwa ni mwamuzi wa mwisho juu ya kila kitu.

Uteuzi huo ulimshtua zaidi raisi ambaye alikuwa ametoka madarakani Denis Kijazo, ni usiku huo huo alitoka kujinasibu kwa wenzake kwamba huyo alikuwa ni kijana wake na hakuwa na jambo lolote la kufanya mbele yake zaidi ya kutii kile ambacho alikuwa anakitaka yeye mwenyewe lakini kilichofanyika, kilikuwa nje kabisa na matarajio yake na mpaka wakati huo hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kinaendelea.

Aliipasua kwa kuipiga risasi runinga ambayo ndiyo ilikuwa inatumika kuangalizia taarifa hiyo, baada ya kumaliza kuisikiliza orodha hiyo, alikuwa mtu mwenye hasira sana kiasi kwamba hata mdomo wake ulikuwa unacheza cheza huku akiwa anatabasamu. Kijana wake alikuwa ameenda kinyume na matarajio yake na maagizo yake kiufupi ni kwamba alikuwa amemsaliti tena vibaya sana kitu ambacho hakuwahi kukitegemea kwamba kinaweza kutokea kwani alimlea na kumtengeneza yeye mwenyewe hivyo aliamini kwamba angekuwa mtiifu mkubwa sana kwake.

“Huyu mshenzi nadhani bado hajanifahamu vizuri, hajui kwamba mimi ndiye mmiliki wa hii nchi, hajui kwamba kila kitu kwenye hii nchi kipo kwenye mkono wangu, hajui kwamba kila mtu ndani ya taifa hili ananitii mimi. Bado hajazaliwa binadamu wa kutaka kuweka ligi na mimi tena kijana ambaye nimempika kwa mkono wangu mwenyewe? Hilo kosa ambalo analifanya atalilipa kwa gharama kubwa sana ambayo itayafanya maisha yake yawe mafupi kuliko hata alivyokuwa ametarajia” aliongea bastola yake ikiwa kwenye mkono wake, aliitoa simu na kuitafuta namba ya raisi huyo kisha akapiga.

Ilimkutia raisi akiwa ndani ya ofisi yake baada ya kutoka kutoa orodha ya baraza jipya la mawaziri ambalo angefanya nalo kazi mpaka pale ambapo angeona kwamba kulikuwa kuna ulazima wa kuweza kulibadilisha tena, aliiangalia simu hiyo ambayo iliita mpaka ikakata, ilianza kuita tena, aliliweka koo lake sawa kisha akaipokea.

“Unataka vita na mimi?” ilikuwa ni sauti kutoka upande wa pili, sauti ambayo ilikuwa nzito lakini ya upole tena yenye utulivu mkubwa sana ndani yake.

“Unaongea ukiwa kama nani?” mheshimiwa raisi aliuliza kwa ujasiri ambao ulikuwa na majivuno ndani yake, upande wa pili ulikuwa kimya kwa muda kwanza kusikilizia kile ambacho kilikuwa kinatokea ikionyesha wazi mtu huyo wa upande wa pili hakuwa akiamini kile ambacho kilikuwa kinaendelea.
“Ushakuwa mkubwa sio?”

Episode 4 inafika mwisho tukutane sehemu inayo fuata.

Tchao.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 5
“Unaongea na raisi wa nchi yako ambaye kimsingi ni bosi wako, mimi ndiye bosi wa taifa hili hivyo sitataka vitisho vyovyote kutoka kwako wala kwa mtu yeyote yule kutoka kwenye upande wako na kama kuna mtu atafanya hivyo basi nitamfanyia kitu kibaya sana” mwanamke huyo ambaye alikuwa ana siku chache sana tangu aipate hiyo nafasi alionekana kubadilika vibaya sana isivyokuwa kawaida.

“Kuna usemi wa zamani huwa unasema; ukifanikiwa basi usisahau ulikotoka na usiwasahau wale ambao walikufikisha ulipo kwa wakati huo hata kama utakuwa na majivuno kiasi gani. Nnimekutoa kwenye danguro ambalo nilikuwa nakuja mara nyingi kupata huduma ya kimwili kwako, siku ambayo nilikuvua nguo na kuuona uchi wako ni siku ambayo ulinipa penzi ambalo hata kwa mke wangu wa ndoa sikuwahi kulipata kabisa. Ile ni siku ambayo mimi nilikufanya wewe kuwa Malaya wangu tu na sikutaka mwanaume mwingine yeyote aje akuvue tena nguo baada ya mimi kukuvua siku ile.

Licha ya wewe kuwa hodari sana kwenye kukata viuno sana ila ulilia sana na kupiga magoti ukihitaji nikutoe kwenye yale maisha na ikiwezekana nikupe nafasi serikalini kwani ulionekana kuwa mwanamke ambaye ulikuwa unavutiwa sana na siasa na kwa sababu haukuwa na elimu ya kutosha sana nikakutoa kwenye danguro na kukutafutia elimu japo hukustahili maana nilitumia nafasi yangu kukuingiza kila sehemu ambayo walitolewa watu wenye sifa zilizo stahili. Baada ya pale nikakuingiza kwenye siasa ambapo leo hii nimekuweka mpaka Ikulu halafu unakuja kuanza kwenda kinyume na mimi na kunitishia kabisa kwamba utanifanyia kitu kibaya? Unajua unacho kifanya bibie au ni madaraka yameanza kukulevya ikiwa bado ni mapema sana namna hii?” mwanaume huyo alimpa kwa ufupi sana historia ya mahali ambako alikuwa amemtoa tena kwa upole sana.

“Nashukuru sana kwa kuniweka hapa na kunikumbusha uliko nitoa ila kwa muda mrefu sana nilikuwa natamani sana niweze kupata hii nafasi ili niitengeneze nchi hii na kuitoa kwenye udhalimu mkubwa sana ambao ulikuwa umeutengeneza kwa miaka mingi sana. Na kesho asubuhi nina zawadi yako ambayo utaipokea hapo” mwanamke huko baada ya kuongea hivyo aliongea kwa hasira sana na kuikata simu hiyo wakiwa hata hawajafikia mwafaka wa maongezi yao, kuambiwa ukweli kwamba aliokotwa kwenye danguro ulikuwa ni ukweli ambao ulikuwa unamuuma sana kwenye nafsi yake na alikuwa anaona kwamba hakuwa tayari kuweza kuubeba na kuumeza kwenye nafsi yake ndiyo maana alikasirika sana. Alinyanyuka na kutoka ndani ya ofisi hiyo kukiwa kumeanza kupambazuka tayari maana alitumia muda mrefu sana kukaa humo na safari hiyo ilikuwa ni kuelekea kule ambako yule kijana ambaye alimletea bahasha alikokuwa amehifadhiwa baada ya kutoa amri kwamba akamatwe kwa kushindwa kuiheshimu ofisi yake.

Kijana ambaye alikuwa amekamtwa kwa kuingia kwenye ofisi ya raisi bila taarifa na kuweza kukiacha kifaa cha mawasiliano mle ndani baada ya kukamatwa alikuwa amehifadhiwa kwenye vyumba vya siri vya mateso ambavyo vilikuwepo ndani ya Ikulu hiyo. Mheshimiwa raisi baada ya kutoka kwenye ofisi yake alihitaji apelekwe huko ambako alikuwepo huyo kijana.

Walitembea na kushuka kwenye lifti kuelekea chini ya ardhi ambako ndiko vilikuwepo vyumba hivyo, baada ya kufika huko alikutana na hali ya kama pango hivi kwani ni mawe ndiyo yalikuwa yamechimbwa na kutengenezewa vyumba ambavyo havikuwa vikijulikana kwenye dunia ya kawaida, hata yeye mheshimiwa alikuwa akivishangaa mno kwani ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuweza kushuka huko chini lakini kwa msaada wa walinzi wake ambao walikuwepo hapo Ikulu hata kabla yake yeye haikuwa taabu kubwa sana kuweza kufika huko.

Baadhi ya vyumba vingine vilikuwa vina watu ambao walikuwa wamekondeana sana wengi wakiwa ni wale viongozi waliokuwa wamepita ambao walikuwa na midomo iisivyo kawaida, wengine walikuwa ni watu ambao walikuwa wamepotea uraiani kwa sababu ya kujifanya wao ndio ambao walikuwa wanajua sana kuongea. Mheshimiwa hakuwa na mpango nao sana zaidi ya kujali kile ambacho alikijia huko mpaka pale alipofanikiwa kufika kwenye chumba ambacho mtu wake alikuwa amehifadhiwa.

Kijana huyo alikuwa amelionja joto kidogo akiwa bado kwenye suti yake, mikono yake ilikuwa imefungwa kwa minyororo huku miguu yake ikiwa imebanwa kwa makufuli ya chuma kiasi kwamba alikuwa hawezi hata kuhamisha kidole chake pale alipokuwepo.

“Umefanya kazi hapa Ikulu kwa muda gani kijana?” raisi aliuliza akiwa anamzunguka kijana huyo lakini kijana huyo hakutoa jibu lolote zaidi ya kubaki kimya tu kama ishara ya kudharau kile ambacho raisi huyo alikuwa anakiongea. Teodensia alitabasamu kwa uchungu sana, aliona kabisa ndani ya nchi yake kuna watu ambao walikuwa hawajali kabisa kuhusu yeye na hawakuwa wakimheshimu kama raisi hivyo alitakiwa kuwafundisha adabu kwanza kwa kuwanyoosha ipasavyo. Alimpa ishara moja kati ya walinzi wake ili ampatie bastola, mlinzi alitii amri na kumpa kiongozi wake bastola hiyo, aligeuka haraka sana na kumpiga kijana huyo risasi ya goti hali ambayo ilimfanya awe kama amekurupuka kutoka usingizini kwa kupiga makelele kwa nguvu sana.

Kupiga kwake makelele bila utaratibu maalumu ilikuwa ni sababu nyingine ya kumuongeza risasi kwenye misuli ya mikono yake yote miwili.

“Kuna muda ukijaribu sana kuwa mwema watu wanaanza kukukosea heshima, nilitaka nikuhoji kistaarabu ila wewe umeonekana kuwa miongoni mwa wale watu ambao huwa wanaelewa kwakutumia nguvu hivyo nimeichagua hiyo njia ambayo unaitaka wewe. Upo tayari kufanya mazungumzo sasa?”

“Ndiyo mheshimiwa, nipo tayari kufanya jambo lolote lile ambalo utahitaji nilifanye, naomba usiendelee kunifanyia zaidi ya hiki ambacho umenifanyia” kijana huyo alijibu akiwa anahema maana damu ilikuwa inamtoka kwa wingi sana. Mheshimiwa raisi aliletewa kiti na kuvua koti la suti kisha akaakaa.

“Unajua mimi ni miongoni mwa wanadamu wachache sana ambao wameingia kwenye hii nafasi kwa bahati mbaya sana. Nasema kwa bahati mbaya kwa sababu sikuzaliwa kuwa kiongozi kwa aina ya maisha ambayo nimeishi nyuma huko lakini pia sikuzaliwa kwenye familia ambayo ina viongozi kiasi kwamba niseme labda nina watu wa kuja kunishika mkono hapo baadae hivyo nilijua kabisa mimi nitakuwa mtumwa siku zote za maisha yangu”

“Hali hiyo ilinifanya nisiwe na chaguo tena kwenye maisha yangu maana sikuwa na cha kupoteza na sikuwa na tumaini lolote lile yaani nilikuwa kama mtu ambaye tayari nilishakufa muda mrefu sana lakini siku isiyo na jina ndiyo ilinipa mimi tumaini jipya la kuweza kuishi na kuiona nuru mpya kwenye maisha yangu. Ni siku ambayo binadamu aliyekuwa na mamlaka makubwa sana alipokuja kwenye njia yangu na kunihitaji mimi tu miongoni mwa wanawake warembo zaidi ya mia moja ndani ya ile sehemu. Sitaki kusema kwamba labda mimi nilikuwa mzuri zaidi ya wote ila niseme huenda ilikuwa ni bahati yangu tu siku ile au ilipangwa mimi niwe hapa leo. Unajua ilikuwaje?” mheshimiwa alicheka kwanza akiwa analielezea hilo mbele ya kijana huyo, alimsogelea mpaka kwenye sikio lake na kumpa siri hiyo.

“Nguvu ya mwanamke ipo katikati ya mapaja yake, hiyo ndiyo sehemu ambayo inaweza kumfanya mwanamke akaiendesha dunia kwa namna anavyotaka yeye. Pale bosi wako alipo thubutu tu kusimama katikati ya mapaja yangu ndiyo siku ambayo niliuchukua umalikia na ufalme wa taifa hili kwa kumpa vitu ambavyo nilijua watoto wa mjini hawawezi kumpatia. Ile ndiyo siku ambayo niliiteka akili yake jumla na akaamua kunifanya mwanamke mwenye nguvu zaidi nchini huku akiamini kwamba kweli mimi nilikufa kwake, nimemtii kwa muda wote ambao alinifanya mtumwa wake mpaka hii leo, nilikuwa mtiifu sana kiasi kwamba alijua nikiwa hapa nitakuwa kama mbwa wake kwenda sehemu ambayo yeye angenituma lakini alisahau jambo moja tu”

“Alisahau kwamba kila binadamu huwa ana chaguo, alisahau kwamba kila mtu huwa ana kusudio lake moyoni sehemu yoyote ile ambayo anakuwepo. Ukiona mwanamke anauza mwili wake jua ana sababu kubwa ambayo imemfanya awe pale hata kama ana tabia hizo za kimalaya ila tambua kuna sababu nyuma yake sasa na wewe ukikurupuka kumfuata bila kujua sababu ambayo imemuweka pale wewe ndiye ambaye unaumia vibaya sana huku ukihisi unamkomoa yeye. Bosi wako alisahau juu ya kile ambacho mimi nilikuwa nakiwaza moyoni mwangu, tangu muda wakati najisogeza kwake niliapa kwamba ipo siku kwa kutumia jina lake nitakuwa mtu mkubwa sana hapa nchini na baada ya hapo nitadili naye na watu wake ambao wengi nilifanikiwa kuwajua nikiwa naye kwa weledi mkubwa sana hivyo kwa sasa ameanza kuiona rangi yangu halisi hasa na nataka nimuonyeshe ni kwa namna gani raisi anafaa kuwa na nchi inatakiwa kuendeshwa vipi” mheshimiwa alikuwa akimnong’oneza kijana huyo mambo hayo kiasi kwamba hakuwa akihitaji kabisa watu wengine waweze kusikia.

“Kwanini unayafanya haya yote?”

“Unataka kujua kwamba ni kwanini nafanya haya?”

“Ndiyo”

“Mimi nimezaliwa kwenye maisha ya kimaskini sana, napokwambia kimaskini lielewe hilo neno na kama halieleweki kwako basi nikwambie kwamba nimezaliwa kwenye maisha ya ufukara wa hali ya juu sana. Yale maisha ni mazuri ukiwa unayasoma kwenye vitabu wakati watu wanatiana moyo ila ukiyaishi kwenye uhalisia wake ni maisha mabaya na magumu sana kwa mwanadamu wa kawaida kuweza kuyaishi, sasa mimi nimezaliwa huko kwenye hayo maisha”

“Mimi nimemshuhudia mama yangu mzazi akifa mbele yangu kwa sababu ya kukosa kuchomwa sindano tu baada ya kung’atwa na mbwa mwenye kichaa na sumu kali. Mama yangu alikufa kwa sababu ndogo sana ya pesa ndogo ambayo watu hawa wanazitumia kwenda kwenye madanguro, wanazitumia kwenda kununua madawa ya kulevya kwa ajili ya watoto wao, wanazitumia pesa hizo kwa ajili ya kuchezea kamali na kununua majumba ya kifahari. Lakini unajua pesa hizo zinatoka wapi?”

“Hizo ni kodi za hao wananchi maskini ambao kwao wengine mkate mmoja tu wakiupata wanapiga magoti kwa nusu saa nzima kushukuru kwa kupata tumaini jipya la maisha lakini mkate huo huo si chochote kwa hawa watu ambao wakiupata wanautupa tena kwa dhihaka kubwa huku wakimlaumu Mungu kuwa ndiye sehemu kubwa ya kupata kwao mkate mmoja wakati wao wanastahili kiwanda kizima”

“Kwahiyo unataka kufanyaje?”

“Nataka nirudishe mali zao zote kwa wananchi, nahitaji kila walicho kichukua kirudi kwa wananchi kama ilivyokuwa mwanzo. Nahitaji kodi za wananchi zifanye maendeleo kwa ajili ya taifa lao na sio pesa hizo kuingia kwenye akaunti za hawa mafisadi na nitahakikisha hili linafanyika. Lakini nataka niibadilishe Tanzania kuwa sehemu ya kivutio zaidi ulimwenguni na nahitaji wananchi wa taifa hili wasijutie tena kuwa watanzania bali waweze kujivunia kuwa wananchi wa hili taifa zuri sana”

“Nakusikitikia sana, huenda una hiyo mipango mikubwa juu ya taifa hili ila kwa bahati mbaya sana haumfahamu hata kidogo huyo mtu ambaye unataka kucheza naye, nina uhakika haumjui vizuri bado Denis Kijazo. Nina imani lile tabasamu lake huwa linakudanganya na kuhisi kwamba unaweza kummud……….” Kijana huyo alitaka kuendelea lakini alikatishwa na raisi huyo kwa kicheko.

“Hahaha hahaha hahaha, wewe hapo ndo unaniambia kwamba mimi simjui yule? Mimi naujua hadi mwili wake wote ulivyo ukiwa uchi, mimi naijua hadi saizi ya uume wake halafu unaniambia kwamba simjui? Kwa kipi labda? Haujui kama mimi nimekomazwa kisiasa na yeye mwenyewe? Haujui kama yule ndiye kanipika mimi kisiasa? Namjua kuanzia akili yake akilala anawaza nini na akiamka anawaza nini hivyo mimi ndiye ambaye napaswa kukuuliza wewe kama unamfahamu bwana mdogo”

5 naweka nukta.

Tchao.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 1
USIKU WA KUTISHA

Usiku wa manane mvua ikiwa inanyesha mithili ya kufunguliwa kwa koki iliyopo huko angani, alionekana mwanaume mmoja akiwa ndani ya nguo nyeusi na begi jeusi kwenye mkono wake huku koti lake jeusi refu ambalo lilivuka magotini likikamilisha mwonekano wake wa kuwa moja kati ya wanaume ambao walikuwa wanatisha mno.

Akiwa na kofia yake kubwa aina ya pama kwenye kichwa chake, alikuwa anatembea haraka haraka tena kwa uangalifu mkubwa akionekana wazi kuwa mtu ambaye alikuwa makini sana na begi lake ambalo lilikuwa kwenye mkono wake ili lifike salama mahali ambapo alikuwa anatakiwa kulifikisha usiku huo.

Akiwa kwenye huo mwendo wake wa haraka baada ya kufika katikati ya barabara ndogo ambayo ilikuwa imezungukwa na majengo marefu sana ambayo yalikuwa yamejengwa kwa mawe magumu mno huku pembezoni kukiwa na vichochoro vingi ambavyo vilielekea maeneo tofauti tofauti. Alihisi kwamba hilo eneo ni kama kulikuwa na ugeni, nafsi yake ilimpa taarifa hiyo kwamba walikuwepo watu wengine ukiacha yeye.

Masikio yake yalimtekenya na kumpa taarifa hiyo kupitia mlango wake wa hisia na alikuwa akiziamini sana hisia zake kwa kuamini kwamba zisingeweza kabisa kumdanganya kamwe hivyo akawa na uhakika kwamba alikuwa kwenye hatari majira hayo ya usiku wa kiza totoro, huku taa kwa mbali zilizokuwa zimezunguka kwenye majengo ya karibu yake zikiwa zinatoa mwangaza ambao ulimsaidia kuona kila kitu ambacho kilikuwa pembeni yake.

Alisimama na kuyafumba macho yake kisha akayaweka masikio yake kwenye hali ya utulivu na usikivu mkubwa isivyo kawaida ili aweze kujua kwamba huyo mgeni au hao wageni walikuwa wamejifichia wapi na wangetokea wapi ili aweze kujihami mapema kabla hajapata madhara yoyote yale. Akiwa amesima hapo na begi lake mkononi ambapo mkono mmoja alikuwa ameuweka kiunoni sehemu ambayo ilikuwa na kisu kikali sana, alihisi kwamba kuna kitu kilikuwa kinakuja alipo kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba sikio lake lilicheza kumpa ishara hiyo hivyo aliinama kwa kasi mithili ya mwanga wa radi ambavyo huwa unajitokeza machoni radi ikipiga kisha ungetoweka haraka.

Kuinama kwake kulimsaidia kupishana na shoka la chuma ambalo lilienda kukita kwenye moja ya kuta za majengo marefu ambayo yalikuwa karibu na alipokuwa amesimama. Alihema kwa nguvu kwa tumaini la kushukuru kuweza kupona kwenye dhahama hiyo na kuamua kugeuka kwa kasi kubwa ila wakati anageuka alitumia muda mwingi sana ambao ulimuingiza matatizoni.

Alihisi kifua chake kinamuwasha maana spidi ambayo ilitumika kumkita hapo ilikuwa ni kama umeme unavyo safari kwenye njia zake, alitema damu maana alipokea mishindo mikali ya haraka haraka ya mabuti ambayo yalitoka kwa mtu ambaye alikuwa ana nguvu kubwa sana miguuni na mtu huyo alionekana dhahiri alikuwa amedhamiria kuweza kumuua moja kwa moja.

Mwanaume huyo licha ya kurushwa mbali karibu na kuta za mijengo hilo, mgongo wake ulikuwa umelenga jiwe ambalo lilikuwa lipo kwenye msingi mkubwa wa jengo moja na kama angekita hapo basi moja kwa moja alikuwa anaupoteza uti wa mgongo wake, hakuwa tayari kufa kifala sana namna hiyo hivyo aliutanguliza mkono wake baada ya kujipinda kidogo tu na mkono wake ndio ambao ukakita kwenye jiwe hilo la msingi wa hiyo nyumba. Mkono wake ulikuwa na gloves lakini nguvu ambayo ilitumika kukita kwenye huo ukuta ilifanya koti lake kujivuta kidogo na kuufanya mkono wake uonekane ambapo mkono huo ulikuwa na tattoo (tatuu) iliyokuwa inasomeka 002 mbele yake pakiwa na alama ya nyoka.

Mwanaume huyo alitua chini na kukiweka sawa kifua chake na kuifuta damu ambayo ilikuwa kwenye mdomo wake kisha akageuka kumwangalia mtu huyo ambaye alikuwa amemvamia ndani ya hilo eneo. Kwa bahati mbaya sana mtu ambaye alikuwa mbele yake hakuwa akionekana sura kwani sura yake ilikuwa imefunikwa na kitambaa cheusi huku naye akiwa amevaa mavazi kama yake mpaka kofia kichwani ilikuwa ni kama yake. Kitu pekee ambacho walikuwa wametofautiana ilikuwa ni kwamba mvamiwaji uso ulikuwa wazi na mvamiaji uso wake ulikuwa umefunikwa wote na kumfanya asitambulike kabisa kwamba alikuwa ni nani.

“Tunafahamiana kabla?” mvamiwaji aliuliza swali ambalo halikuwa na majibu, alitabasamu kidogo na kukitoa kisu chake ambacho mara ya kwanza hakufanikiwa kukitoa. Mwenzake alikuwa amesimama tu anamwangalia bila wasiwasi kwenye macho yake. Aliyakanyaga maji ya mvua chini kwa nguvu na kuyafanya yapande juu kuelekea alipokuwepo mvamiaji kisha akakirusha kisu kwa kasi kikiwa kinapita kwenye yale maji huku naye akija kwa nguvu sana kwa hatua ambazo zilikuwa zinapigwa kwa umakini sana.

Mwanaume ambaye alikuwa mbele yake hakukikwepa kile kisu bali alikiacha kikazama kwenye bega lake, wakati huyo mvamiwaji naye alikuwa amefika eneo alilokuwepo ambapo aliituma ngumi yake eneo ambalo lilikuwa na kisu ili akizamishe zaidi ndani. Mvamiaji ni kama alishtuka kutoka kwenye tafakari ambayo alikuwa nayo kwa muda ambao alikuwa hapo hivyo aliteleza kwenye maji kusogea nyuma kidogo ya alipokuwa na kufanya ngumi hiyo ipige hewa.

Mvamiwaji alizunguka teke la chini ambapo mvamiaji aliruka sarakasi ya nyuma na miguu yake ikatua kwenye ukuta na mikono ikidaka sehemu ya jiwe akawa amegeuka miguu juu na mikono uelekeo wa chini akimwangalia mwenzake ambaye aliishia kuyasambaratisha tu maji ambayo yalikuwa chini na hakufanikiwa kumpata mtu wake. Mvamiwaji alichukia sana kiasi kwamba akavua mpaka koti lake na kulirushia pembeni ila wakati anafanya hayo yote mvamiaji alikichomoa kisu kwenye bega lake na kukirudisha kwa mwenye nacho kikiwa kinaenda kwa mwendo mkali ambao ulipatikana kutokana na spidi ya mrushaji kuwa kubwa sana. Mwanaume huyo alijitahidi sana kukikwepa kisu hicho kikaishia kumbaraza kwenye shavu lake ila wakati anapambana kukikwepa kisu hicho mvamiaji alikuwa ameshuka pale juu kama kimbunga.

Alitua kwenye mbavu ya mvamiwaji ambapo ngumi mbili zilitosha kumfanya agugumie kwa maumivu makali ambayo yalijitawanya kila sehemu ya mwili wake. Alirudi nyuma akiwa anayumba yumba, mvamiaji alidunda kwa mkono mmoja na kujibetua na meteke mawili ambayo mvamiwaji aliyaona na kuyakwepa kwa kuinama ila wakati anainuka mvamiaji huyo alizungusha teke la chini na kumzoa mwanaume huyo ambaye angedondokea mgongo kwenye maji ambayo yalikuwa hapo chini yametuama ila hakufanikiwa kuiona ardhi baada ya kushindiliwa mateke mawili ya shingo ambayo yalimburuza mbali sana kwenye maji ambayo yalikuwa hapo karibu.

Alipata maumivu ambayo ilikuwa ni siri yake ndani ya mwili wake namna ya kuweza kuyaelezea, akiwa anatoka damu kwenye mdomo wake na puani huku kifua kikiwa kinawaka moto pamoja na shingo yake, aliinuka kwa maumivu huku akiunguruma kupiga kelela za hasira, aliinyoosha shingo yake mpaka ilipokaa sawa akageukia ule upande ambao alikuwepo mvamiaji ambaye kwa namna alivyokuwa anamshambulia alionekana kwamba alikuwa hapo kuweza kumuua.

Ila wakati anageuka tu, umeme ulikatika ghafla sana hata yeye mwenyewe alibaki kwenye mshangao maana lilikuwa ni tukio la haraka sana ambalo hata yeye hakuweza kulitegemea kwamba lingetokea majira hayo na wakati kama huo. Kukatika kwa umeme huo kwake ilikuwa ni ahueni maana angepata muda wa kupumzika japo gizani ingekuwa ni ngumu kumuona adui yake ila aliamini kwamba angekuwa makini na wakati huo angepumua kwanza kwani mtu ambaye alikuwa anapambana naye kama sio umeme kukatika basi ni wazi angemuua mapema mno.

Alitulia na kuweza kusikilizia kujua adui yake alikuwa wapi lakini hakusikia kitu zaidi ya mvua ambayo ilikuwa inaendelea kushuka kwa wingi. Akiwa anahitaji kupiga hatua moja umeme ulirudi tena lakini alishangaa baada ya kugundua kwamba mtu ambaye alikuwa amemvamia kwenye hilo eneo hakuwepo, ikimaanisha kwamba ni muda mrefu sana alikuwa ametoweka hapo. Aligeuka kwa pupa sehemu ambayo begi lake lilidondokea baada ya kupigwa lakini begi halikuwepo kwenye hilo eneo ishara ya mhusika ambaye aliingia hapo kutoweka nalo.

Aliogopa sana na kubaki akitetemeka kwenye mdomo wake, hakuwa anaamini kwamba alikuwa amelipoteza begi kizembe sana namna hiyo na begi hilo lilionekana kuwa la mhimu sana. Akiwa kwenye huo wasiwasi mkubwa aligundua kwamba mita kadhaa kwa chini kutoka alipokuwa amesimama yeye kulikuwa na karatasi nyeupe ambayo ilikuwa na maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwa damu ikiendelea kunyeshewa na mvua pale chini.

Aliisogelea karatasi hiyo na kuiokota ila baada ya kusoma kilichokuwa kimeandikwa hapo, aliiachia ghafla sana na kuanza kurudi nyuma huku akiwa anatetemea mwili mzima mpaka meno yake kwa namna alivyokuwa ameogopa na kushtuka kwani halikuonekana kuwa tukio la kawaida kwake kuweza kuona hali kama hiyo. Karatasi hiyo ilikuwa na maandishi ambayo yalikuwa yanasomeka “KAMARI YANGU YA MWISHO NDIYO KAMARI YAKO YA KWANZA”

Aliogopa sana kwa sababu hiyo ilikuwa ni kauli ambayo alikuwa anaitumia mwanaume mmoja ambaye yeye mwenyewe alimuua kwa mkono wake miaka kadhaa ambayo ilikuwa imepita. Aliangaza ile sehemu ambayo shoka lilikita muda ule lakini hakuliona hivyo aligundua kwamba mhusika alikuwa ameondoka na shoka lake na kilikuwa ni kitendo cha haraka sana, alisogea hatua kadhaa na kukiokota kisu chake na kukipachika tena kiunoni huku akiwa anaitoa simu yake mfukoni akionekana kwamba kuna mtu wa mhimu sana ambaye alikuwa anahitaji kumpatia taarifa za tukio hilo ila kwa bahati mbaya sana simu ambayo alikuwa anahitaji kuitumia kufanyia mawasiliano ilikuwa imevunjika na hapo akakumbuka kwamba ilipasuka baada ya teke zito kuzama hiyo sehemu hivyo aliamua kutoweka haraka sana hilo eneo.


Rasmi tunaanza kuifunua episode 1, ni mwanzo tu wa yale mengi ambayo tunakwenda kuyafunua ndani ya simulizi hii mpya. Nipe muda wako, jicho lako na umakini wako ile twende sawa ndani ya simulizi hii.

Kwenye kalamu nipo mwenyewe.

Tchao.
Naweka kiti hapa
 
ItaishaaAaaa😀😀😀
NOTE:

Please over please sipendi matusi hususani kwenye threads zangu hivyo ukiona simulizi nazoleta hazikuvutii isiwe kigezo cha kusumbua wengine.

Ukiwa na cha kunikosoa wewe kosoa uwezavyo ila matusi achana nayo.


Ni mara mia usome simulizi za watu ambao unahisi wanakuburudisha kuliko kuvamia thread za watu na kuleta mihemko yako hapa.


Good evening
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 6
“Ndiyo maana nakwambia kwamba bado haumjui yule mtu na kama unamjua basi unamjua kwa namna ambavyo yeye alitaka wewe umjue, alikuwekea mitego ambayo na wewe ukawa umeingia kingi bila kuwaza. Hivyo ndivyo alivyo, huwa ni bingwa wa kucheza na akili za watu kwa kukupa uhuru wa kuamini kwamba unamjua na unaweza kummudu ila siku ukiingia kwenye njia zake ndipo utajua kwamba hakuna unalo lijua kuhusu yeye. Wewe unacho kijua kwake ni lile ganda lake la nje au naweza kusema mwonakeno wake wa nje tu ila akili yake bado hauijui” kijana huyo alimeza mate na kuendelea.

“Mimi nimefanya kazi kwake kwa miaka kumi na mitano, nimeanza kufanya kazi kwake nikiwa na miaka kumi na saba tu na kwa sasa nina miaka thelathini na miwili bado nipo kwake, unahisi mimi sikuwahi kutamani kuwa na uhuru wangu na kutoka kwake? Unahisi kwanini sijatoka mpaka leo? Kumbuka kitu kimoja, umenikuta nikiwa kwake licha ya kwamba leo umekuwa kiongozi mkubwa wa nchi ila unatakiwa kutambua kwamba amekuweka hapo kwa ajili ya kazi maalumu ambazo aliamini wewe ungezitekeleza ila kwenda naye kinyume ni kwamba utakuwa na muda mfupi sana wa kuwa hai ukiwa kwenye hicho kiti”

“Mhhhh unamtisha raisi wa nchi?”

“Sikutishi nakwambia ukweli”

“Kipi kinakupa hiyo imani wakati mimi ndiye mtu ambaye nina nguvu zaidi ndani ya taifa hili tangu tu pale ambapo niliapishwa rasmi kuwa raisi?”

“Kwa sababu watu wengi kama sio wote ambao wanaijua vizuri hii nchi wanamtii yeye, hata kama utabadilisha vipi watu kwenye hizo nafasi bado huwezi kuwamaliza watu wake kwa sababu amewapatia maisha mazuri sana na kuwaahidi yaliyo mema kwa baadae, unadhani kuna mtu anapenda kuwa upande ambao unashindwa kwenye vita? Hayupo na hiyo ndiyo sababu kuna muda utajikuta upo pekeako na huna msaada. Nakushauri bado haujachelewa sana japo umemuudhi ila nenda kampigie magoti umuombe msamaha atakusamehe wewe ni kijana wake ambaye alikuwa anakuamini sana”

“Mimi nimpigie magoti yule mjinga?”

“Hiyo ndiyo njia pekee ya wewe kuwa hai”

“Hahahaa ndiyo maana ukaja kutegesha kifaa cha mawasiliano ofisini kwangu sio”

“Mheshimiwa bado haujachelewa fanya hiv….” kijana huyo akiwa anaendelea kusisitiza jambo hilo alipigwa na risasi kwenye paji la uso maana alionekana kwamba anamuogopa mtu mwingine kuliko hata raisi wake tena akisisitiza raisi akampigie magoti raia mwingine wa kawaida kabisa kwenye taifa lake.

“Mpuuzi huyu na huu ni mwanzo tu, nataka niwaonyeshe kwamba mimi ni raisi wa taifa la Tanzania. Beba huu mwili nenda kautupe nje ya nyumba ya raisi mstaafu Denis Kijazo” alitoa maagizo kwa vijana wake ambao walikuwa hapo kisha yeye akatoka humo ndani.

Taarifa ambayo ilikuwa mezani ilikuwa ni mbaya sana kwa mheshimiwa Denis Kijazo, alihuzunika na kusikitika kwa kiasi kikubwa sana baada ya kugundua kwamba alikuwa anasalitiwa kwa kiasi kikubwa sana. Kusalitiwa kwake halikuwa jambo geni wala jipya kwamba ndilo lililo muumiza sana, hapana bali kilicho muuma ni kijana wake mwenyewe ambaye alimlea kwenye mikono yake halafu kiwepesi tu aliamua kumuasi na kuanza kuyaishi maisha ambayo hakuyatarajia ghafla sana tena akiwa na siku chache tu ofisini.

Akiwa kwenye masikitiko makubwa sana ya taarifa ambazo hakuzitarajia lakini ndizo ambazo alizipokea, asubuhi ya mapema sana wakati kunapambazuka alishtushwa na ujio wa taarifa nyingine ambayo ilimshtua na kumpa hasira kwa kiasi kikubwa mno. Moja ya vijana wake wa kazi ambao alikuwa anawaamini sana na aliwaacha pale Ikulu kwa ajili ya kumfanyia kazi zake alikuwa ameuliwa tena kikatili mno huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa kwenye gunia na kuletwa kwenye geti la mheshimiwa huyo ambaye alikuwa anaishi nje ya mji sehemu ambayo ilikuwa na ulinzi mkali isivyokuwa kawaida lakini walinzi wake wengi hawakuwa wakitambulika na serikali.

Baada ya kutoka nje kabisa ya jumba lake hilo alikuta mwili huo umetolewa kwenye gunia na kufunikwa na shuka, alisogea mpaka ulipo na kutaka ufunuliwe ambapo alisikitika kwa namna kijana huyo alivyokuwa ameuliwa kikatili sana.
“Hamjawakamata ambao wameuleta huu mwili mpaka sasa?” aliwauliza vijana wake ambao walikuwa karibu na huo mwili.
“Tumeshindwa cha kufanya kwa sababu ni watu ambao wamekuja hapa na gari za ikulu bosi”

“Kuna kingine ambacho mmekikuta kwenye mwili wake?”

“Ndiyo bosi” kijana huyo alijibu huku akiwa anamsogezea bosi wake bahasha ambayo ilikuwa imeloa damu lakini hakujali, aliipokea akiwa amechuchumaa kwenye huo mwili wa kijana wake. Bahasha hiyo ndani ilikuwa na ujumbe mzito sana pamoja na kile kifaa ambacho alimpa kijana wake ili akategeshe ndani ya ofisi ya raisi. Baada ya kuusoma ujumbe huo alisonya kwa nguvu na kutukana kwa hasira huku akiwa anacheka kwa nguvu mithili ya mtu ambaye alikuwa ameshinda beti. Ujumbe huo ulikuwa umetoka kwa mheshimiwa raisi Teodensia Mpanzi akimpa tahadhari kiongozi huyo kwamba alikuwa anatakiwa kusalimisha mali zake zote ambazo amefuja serikalini pamoja na miradi yote ambayo amewapa wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa maslahi yake binafsi.

Barua hiyo ilimtaka arudishe pesa zote ambazo alikuwa amezihifadhi kwenye mabenki ya nje ya nchi. Haikuishia hapo tu bali barua hiyo ilikuwa inatoa maagizo kwamba ule ukumbi wake mkubwa wa ALEXIOS ARENA anatakiwa kuufunga yeye mwenyewe au kama hataki basi mwanamama huyo angeubomoa kwa lazima halafu mtu huyo asingekuwa na kitu cha kumfanya. Alisisitiza kwamba amempa hiyo nafasi kwa sababu ni mtu ambaye alikuwa akimheshimu sana ila kama angeamua kutumia nguvu huenda hata yeye angeishia jela kwa udhalimu ambao alikuwa ameufanya ndani ya taifa.

Mheshimiwa hakuongea lolote lile zaidi ya kuikunja karatasi hiyo kwa hasira sana na kurudi ndani, alitoa maagizo rubani wake aje haraka sana hapo kwake kwani kulikuwa na safari ya ghafla ambayo alitakiwa kuifanya wakati huo kwenda nje ya alipokuwa. Ilichukua nusu saa tu rubani huyo ambaye umri ulienda kufika hapo, alitoa heshima kwa bosi wake na kupewa maelekezo kwamba alitakiwa kuitoa helkopita hilo eneo na kwenda Morogoro milimani huko.

Hakukuwa na maswali mengi kwa sababu ndiyo ilikuwa kazi yake, kiongozi huyo mkubwa wa zamani wa taifa la Tanzania alipanda na walinzi wake wawili tu basi pamoja na rubani jumla walikuwa wanne ambapo helikopita hiyo ilitolewa hilo eneo haraka sana. Haukupita muda mrefu sana helikopita hiyo ilienda kutua ndani ya mji wa Morogoro milimani, kulikuwa na sehemu ambayo ilikuwa imetengenezwa vyema sana kwa ajili ya helikopita hiyo kutua na baada ya mheshimiwa kutua hilo eneo kuna watu walikuwa wanatoka kwenye miti na kuinama kumpa heshima. Wanaume hao walikuwa ni mabanditi, hata mavazi yao na silaha zao zilisaidiki hilo, hakuwa hata na muda nao maana alikuwa na hasira sana. Alitembea mpaka kwenye mti mmoja ambapo aliweka mkono wake ukatokea mlango ambao ulitengenezwa kwa mitambo maalumu akawa ameingia kama kwenye lifti akiwa na walinzi wake hao wawili.

Walishuka mpaka chini kabisa ambako kulikuwa na shughuli zinaendelea kama kawaida, watu ambao walikuwa wamevaa mavazi meupe mithili ya madaktari walikuwa wakiendelea na shughuli zao huko chini bila wasiwasi. Alitembea kwa kasi sana huku kila mfanyakazi ambaye alikuwa ndani ya jengo hilo ambalo lilikuwa chini ya ardhi akiwa anatoa heshima kwa mwanadamu huyo ambaye walionekana kumuogopa sana lakini hata hivyo hakuwa na muda nao na baada ya dakika kadhaa alifika kwenye chumba ambacho alihitaji kuwa mwenyewe na mtu ambaye alikuwa amehifadhiwa ndani ya chumba hicho licha ya walinzi wake kusita sana kumuacha pekeyake ila aliwapa ishara ya kutoka hapo maana yalikuwa ni mazungumzo ya watu wakubwa na wao hawakupaswa kabisa kuyasikia.

“Sikuwahi kufikiria kabisa kwamba siku zangu za uzee nitazimalizia sehemu kama hii ambayo sijui kwamba nipo wapi wala dunia haitambui kuhusu uwepo wangu, kitu pekee ambacho kinaniuma sana ni kutoweza kuiona familia yangu huku wao wakiamini kwamba mimi ni mwanadamu ambaye ni mfu”

“Niliwahi kukwambia mzee Mande kwamba taifa hili haitakiwi kabisa kuwa mzalendo kwa sababu wananchi wake hata uwafanyie nini watakushangilia tu kwa muda mfupi ila ukiingia kwenye matatizo ni siku mbili tu washakusahau na hakuna mwenye muda na wewe tena zaidi tu unaacha familia yako inateseka bure wao wakiendelea kuyafurahia maisha. Licha ya yote hayo ambayo nilikwambia lakini ulikuwa mbishi sana kunisikiliza na kunielewa wakati ulikuwa na nafasi nzuri tu ya kuyazuia haya. Wewe umewahi kuwa mtu mkubwa sana ndani ya jeshi lakini baadae ukawa gavana bale benki kuu, kazi ndogo tu ya kunisaidia kutakatisha zile pesa ukaona taabu kubwa sana ukajifanya unataka kuniweka wazi ili wananchi wanichukie nifungwe lakini angalia ulipo ishia sasa. Hakuna binadamu ambaye anajua wala anayejali kwamba unaishije, una muda huenda hata tarehe ulisha isahau na hata mwaka huenda hujui tupo mwaka gani huu. Inanisikitisha sana muda mwingine kama mwanadamu ila sina namna maana haya uliyataka wewe mwenyewe ila hongera kwako kwa kukubali kunifanyia kazi ili familia yako ibaki salama maana bila ya hivyo ningewaua waote” Denis Kijazo aliongea akiwa amesimama na kujishika kiuno akiwa anamwangalia mzee huyo ila baada ya kumaliza hayo alisogea karibu na alipokuwa mzee huyo ambaye alikujulikana kwa jina la Mande na kuketi akiwa anamwangalia usoni.

“Sema kilicho kuleta humu ndani sio kuanza kunikumbushia uharamia wako ambao uliufanya nyuma huko ambao kuna siku utaulipia kwa majuto sana, inawezekana nisikujibu unacho kihitaji kwangu pia”

“Mhhhh kwanza nimefurahi kuona unajua kwamba kila nikija hapa basi lazima nimekwama mahali, lakini sijaja hapa kukuomba unijibu, ni lazima ufanye hivyo maana kama hautakuwa tayari nadhani unajua kile ambacho kitatokea”
“Acha kuzunguka nambie kilichokuleta hapa”

“Unamkumbuka Teodensia Mpanzi?”

“Si yule hawala wako wa kwenye madanguro?”
“Usinikosee sana heshima bwana Mande wakati nimekuja kistaarabu tu, sioni sababu ya sisi kuanza kupunguzana viungo eti kwa sababu tu umeshindwa kuutumia mdomo wako vyema”

“Nakusikiliza”

“Nimemfanya kuwa raisi wa taifa hili”

“Nadhani utakuwa unanitania sio?”

“Mimi sijawahi kuwa mtani wako naanzia wapi kukutania?”
“Una uhakika kichwa chako kinafanya kazi sawa sawa? Unawezaje kumfanya changudoa kuwa raisi wa nchi?”
“Ndiyo maana nipo hapa”

“Umeshafanya maamuzi yako tayari sasa hapa unataka nini?”
“Hivi labda mzee utafanyaje pale mtu ambaye unakuwa na matumaini naye makubwa halafu baadae anakuja kukuangusha kwa tamaa za kijinga?” mzee huyo alitabsamu sana kwani alianza kumuelewa mtu huyo kwamba alikuwa anamaanisha nini hata kabla hajafika mbali.

Episode 6 naweka nukta hapa.

Tchao.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom