Sehemu ya 40
“Hashim, nimesikia kwamba umeanza kuwaibia watu fedha zao,” ilisikika sauti ya msichana mmoja.
“Ndiyo!”
“Kwa nini unaiba lakini?”
“Kwa sababu ya maisha yetu, huoni kama ni maisha mabaya mno, yemejaa dhiki, hakuna hata uafadhali, tutaomba hela mpaka lini?” aliuliza Hashimu.
Watoto wa mitaani walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa Bahari ya Hindi kulipokuwa na mawe mengi jijini Dar es Salaam. Ilikuwa ni usiku wa saa tano, waliwasha moto na kuanza kuota huku wakisubiri muda wa kulala ufike na hivyo kulala.
Miongoni mwa watoto hao wa mitaani alikuwepo mmoja aliyeitwa kwa jina la Hashimu. Huyu alikuwa miongoni wa watoto wa mitaani aliyekuwa mkorofi mno. Kutembea na kisu, ilikuwa ni sehemu ya maisha yake, hakuamini kwenye kuomba, aliteseka mitaani kwa miaka kumi na saba na hakuona kama maisha yake yangebadilika.
Yeye na wenzake wawili wakaanza kuiba, wakatengeneza kikundi chao cha watu watatu ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuzunguka mitaani na kupora.
Walifanikiwa katika kila walichokifanya, waliwapora wanawake simu zao, waliiba power window kwenye magari na vifaa vingine na kuviuza.
Zilikuwa kazi za hatari lakini hawakuwa na jinsi, miongoni mwa watoto hao wa mitaani alikuwepo Hamidu, Geofrey na huyo Hashimu mwenyewe.
Maisha yalikuwa hivyo, kutokana na fedha walizokuwa wakizipata, maisha yao yakaanza kubadilika, wakaanza kuvaa nguo vizuri, kuwasaidia watoto wenzao wa mitaani wakiwemo Aisha, Ahmed na Mohammedi.
Baada ya miaka miwili, kundi likaanza kupungua hasa baada ya Geofrey kuiba na kukamatwa na wananchi wenye hasira kali ambao waliamua kitu kimoja tu, kumchoma moto.
Lilikuwa pigo kubwa kwa Hashimu na watoto wengine wa mitaani. Kutokana na tukio hilo kubwa, Aisha akazungumza sana na Hashimu na kumwambia aache tabia ya wizi lakini maneno yake yalipitia sikio hili na kutokea sikio jingine, hakutaka kuacha kabisa.
Maisha ya wizi yakamnogea, aliendelea kuiba vifaa vya gari na kuwapora watu, mwaka mmoja baadaye, rafiki yake kipenzi, Hamidu naye akafariki dunia baada ya kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali maeneo ya Ubungo Maziwa.
Hashimu alikosa raha, alisononeka sana lakini hakutaka kuacha. Kutokana na kuambiwa sana kwamba wizi haukuwa mzuri, akaamua kuwaacha watoto wenzake wa mitaani na yeye kupotea.
Alipoelekea, hakukuwa na mtu aliyejua, walijaribu kumtafuta kila kona lakini hawakumpata kabisa, na hata kusikia tetesi kwamba alikuwa sehemu fulani, hawakuzisikia.
Huko alipokwenda, Hashimu hakuacha tabia yake ya kuiba vitu vya gari na hata kuwapora watu mbalimbali. Aliendelea nayo tena kwa mafanikio makubwa mpaka akapata hela na kupanga chumba maeneo ya Magomeni Kagera.
Maisha yaliendelea kama kawaida.
Kila siku alikuwa mtu wa kutoka na kwenda Mikocheni, Masaki na sehemu nyingine alizoamini kwamba ni za watu wenye fedha na kufanya mambo yake huko huku akiwa na vijana wenzake, wengine kabisa ambao nao walikuwa wataalamu wa kufungua vifaa vya magari.
“Unaliona lile gari?” aliuliza mwenzake mmoja.
“Lipi?”
“Lile jeusi...”
“Ndiyo! Ile ni Range Rover SUV, dukani ni zaidi ya milioni mia moja, inatengenezwa na Mjapani, ni gari ya starehe sana,” alisema Hashimu maneno yaliyowafanya wenzake kugundua kwamba mtu huyo aliyajua vilivyo magari.
“Ni lazima tufanye kitu, lina mali zetu, power window, side mirror na redio, tutafanikiwa?” aliuliza jamaa mwingine.
“Ndiyo! Power window yake ni laki sita, side mirror laki nne, redio yake huwa mpaka milioni moja,” alisema Hashimu.
Walibaki wakilizungumzia gari hilo ambalo lilikuwa na tinted. Walipomaliza kulizungumzia, Hashimu akachomoka kwa mwendo wa kasi na kuelekea pale lilipokuwa limeegeshwa huku mkononi akiwa na bisibisi na vifaa vingine.
Alipolifikia, akainama kwa chini huku akiwapa ishara wenzake wasubiri kulekule walipokuwa. Wakati anakwenda, tena kwa tahadhari kubwa, hakujua kama ndani ya gari hilo kulikuwa na watu waliokuwa wakimwangalia vizuri sana, tena walimfuatilia vilivyo.
“Bosi, hawa watu ninawatafuta sana, walikwishawahi kututia hasara, nishuke nimpige risasi?” aliuliza mwanaume mmoja aliyekuwa ndani ya hilo gari.
“Subiri kwanza tuone anataka kufanya nini...”
“Ila mkuu...”
“Usijali Michael...subiri kwanza...”
Hashimu hakuwa na wasiwasi, hakujua kama ndani ya lile gari kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia, aliendelea kuchuchumaa pembeni mwa gari lile tayari kwa kuiba power window na vifaa vingine hasa baada ya kuingia ndani ya gari.
Watu hao waliokuwa ndani waliendelea kumfuatilia. Ghafla wakasikia loki za milango zikipanda juu hali iliyoonyesha kwamba mtu huyo alitumia ufunguo malaya kufungulia mlango wa gari hilo.
Wakati akiwa amekwishafanikiwa kutoa loki, akaufungua mlango na kuingia ndani, alichokutana nacho, ni watu wawili wakiwa wamekaa viti vya nyuma, tena mdomo wa bunduki ukiwa umemuelekea yeye.
“Tulia hivyohivyo...” alisema Michael huku uso wake ukionekana kuwa na hasira.
Hashimu alibaki akitetemeka, hakuamini kile alichokiona mbele yake, alitamani kulia, alitamani kukimbia kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana mahali pale, muda wowote ule angepigwa risasi na kufa.
“Funga mlango...” alisema Michael, bila ubishi, Hashimu akaufunga huku akitetemeka.
“Unajua kuendesha gari kijana?” aliuliza mwanaume aliyevalia suti ambaye ndiye aliyeitwa bosi.
“Ndiyo!”
“Kaa kwenye usukani utupeleke sehemu...”
Hashimu hakubisha kwa kitu chochote kile, kila alichoambiwa, alitii na hivyo kuanza kuendesha gari lile. Wenzake waliokuwa nje walibaki na mshangao, hawakuwa na mpango wa kuiba gari hilo sasa kwa nini Hashimu aliamua kuliiba? Kila walichojiuliza, hawakupata jibu.
Alichokuwa akipewa ni maelekezo tu ya wapi alitakiwa kwenda na wapi hakutakiwa kwenda.
Safari hiyo iliendelea kwa dakika ishirini na ndipo gari hilo likaanza kuingia katika jumba moja kubwa na la kifahari ambalo kwa kuliangalia tu kwa nje, isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba mtu aliyekuwa akiishi humo alikuwa bilionea.
“Twende ndani...” alisema mzee huyo, muda wote huo Hashimu hakuwa na amani hata kidogo.
Wakaingia ndani, huko, mzee yule akamwambia mfanyakazi wa ndani amwandalie Hashimu chakula, ale kwanza kabla ya kuzungumza naye.
Hata chakula alicholetewa hakuwa na hamu nacho japokuwa mzee huyo alimwambia mara kadhaa kwamba alitakiwa ale, asiwe na hofu yoyote ile na amchukulie kama rafiki.
“Ninataka kufanya kazi nawe...” alisema mzee huyo.
“Kazi gani?”
Huyo alikuwa mzee Bruno, mwanaume aliyekuwa mfanyabiashara mzuri wa madawa ya kulevya. Katika kipindi kirefu alikuwa akitafuta kijana ambaye angeweza kufanya biashara hiyo kutokana na vijana wengi aliokuwa nao kunyongwa nchini China baada ya kukamatwa.
Alitafuta vijana kwa kipindi kirefu lakini aliwakosa. Kitendo cha Hashimu kulisogelea gari lake, kuweza kulifungua mpaka kuingia ndani ilimuonyeshea kwamba kijana huyo hakuwa muoga hata kidogo, alijiamini kwa kila alichokifanya.
Katika jumba hilo kubwa, alikuwa akiishi yeye na mfanyakazi wake wa ndani tu, mke wake hakuwa hapo kipindi hicho, alikuwa Kondoa, mkoani Dodoma alipokwenda kusalimia familia yake. Hakubahatika kuwa na mtoto, alitafuta sana lakini juhudi zake zote ziligonga mwamba.
Akavutiwa naye na ndiyo ilikuwa sababu ya kumwambia Michael aachane naye na wala asimpige risasi. Alichokifanya ndani ya nyumba hiyo ni kumwambia Hashimu kwamba alitaka kufanya naye kazi, awe mfanyakazi wake wa kusafirisha madawa ya kulevya kitu ambacho kwa Hashimu, wala hakuwa na tatizo nacho, akakubaliana naye.
“Hakuna tatizo,” alisema Hashimu.
“Nimefurahi sana, kuanzia leo utakuwa ukiishi nami ndani ya hii nyumba mpaka pale nitakapokutafutia nyumba yako,” alisema mzee Bruno huku akionekana kuwa mwenye furaha tele.
Maisha mapya yakaanza ndani ya nyumba hiyo, kila wakati Hashimu alionekana kuwa na furaha, mzee Bruno akatokea kumpenda sana kijana huyo na kuanza kumpa mafunzo, akawapa namba za wateja wake na kuanza kuzungumza nao, alitaka kuwaambia kwamba huyo ndiye alikuwa kijana wake, mjanja, jasiri na ambaye alijiamini katika kila kitu.
Baada ya mwezi mmoja, mkewe akarudi nyumbani. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtambulisha Hashimu kwa mkewe kwamba alikuwa kijana wake mpya katika biashara zake.
Kwa mwanamke huyo aliyeitwa Rosemary, alipomuona Hashimu kwa mara ya kwanza tu, mapigo yake ya moyo yakadunda kwa nguvu, damu ikaanza kuzunguka kwa kasi katika mishipa yake ya damu.
Moyo wake haukutaka kuficha hisia kali za kimpenzi, hapohapo akauhisi ukigalagala mno, ukipelekwa huku na kule, penzi juu ya Hashimu likaanza kumteka, akawa hoi bin taabani.
Uzuri wa kijana huyo ukamuweka katika wakati mgumu. Akashindwa kuvumilia, akashindwa kabisa kukaa hivihivi pasipo kumwambia ukweli kwani moyo wake ukafa na kuoza kwa kijana huyo.
Alimhitaji kwa nguvu zote, hakutaka tena kula penzi lake na mwanaume mzee, alimtaka kijana, mwenye nguvu zake ambaye aliamini kwamba angemfikisha kileleni. Hivyo alichokifanya ni kujipanga, iwe isiwe ilikuwa ni lazima amsaliti mumewe, awe na Hashimu na kumpa penzi lake lote.
****
Je nini kitaendelea....