Simulizi: Penzi lisilo Na Mwisho

Sehemu ya 29

“Razak...Razak....baridi linaniumiza...” alisikika Aisha kwa sauti ya chini.
“Baridi linakuumiza?”
“Ndiyo!”
“Subiri nikazime kiyoyozi...” alisema Razak.

Ilikuwa ni usiku wa manane, wote walikuwa wamelala chumbani, ukimya mkubwa ulitawala, dakika zilizidi kusonga mbele lakini ghafla, Aisha akashtuka kutoka kitandani, alikuwa akilia kwa maumivu makali ya tumbo yaliyomfanya kulalamika mno.

Harakaharaka Razak akainuka kutoka kitandani, akaifuata rimoti ya ya kiyoyozi na kuikizima. Bado Aisha alikuwa akilalamika kwa maumivu makali ya tumbo, Razak alishangaa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mpaka msichana huyo kulalamika kwa maumivu makali.

Kila alipouliza, hakupewa jibu zaidi ya msichana huyo kuendelea kulalamika zaidi. Razak akaogopa, akahisi kwamba kama asingefanya kitu cha ziada basi mpenzi wake angeweza kuwa kwenye hali mbaya zaidi.

“Inuka twende hospitali...” alisema Razak.
“Siwezi....naumia, tumbo linauma Razak mpenzi....nisaidie...” alisema Aisha kwa sauti ya chini iliyojaa maumivu makali.
Razak hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kumbeba Aisha na kuanza kuelekea naye nje ya chumba kile huku lengo likiwa ni kuchukua gari na kuelekea hospitalini.

Walipofika nje, Aisha akazidi kulalamika kwa maumivu makali, baridi walilokutana nalo nje lilimtesa, akapiga kelele mpaka zikafika katika nyumba za jirani, harakaharaka Razak akaufungua mlango na kumuingiza msichana huyo ndani ya gari lake, akaelekea upande wa pili, akaufungua na kuingia ndani.

“Pole mpenzi....vumilia...” alisema Razak, akawasha gari na kuondoka mahali hapo.
Ndani ya gari, kelele zilikuwa nyingi, Razak alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alitamani kumfuata Aisha na kumbeleza lakini upande mwingine, alitamani kuliendesha gari kwa kasi kuwahi hospitalini.

Hakuchukua dakika nyingi, akawa amefika hospitali ambapo akafungua mlango huku akiwaita manesi ambao walifika na machela, wakampakiza na kuanza kuisukuma kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo.

Walipofika katika chumba kilichoandikwa ‘Theatre’ akaambiwa kusubiri katika mabenchi yaliyokuwa nje, akatulia. Hapo, kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakujua ni kitu gani kilimsibu mpenzi wake, japokuwa ilikuwa ni usiku wa manane lakini hakuweza kupata usingizi kabisa.

Alikuwa mtu mwenye mawazo mengi, alitulia katika benchi lililokuwa nje ya kile chumba huku akionekana kuwa na mawazo mengi.

Hakuishia kukaa tu, wakati mwingine alisimama na kuanza kuzunguka huku na kule, hakika alichanganyikiwa na kilichomuumiza kichwa zaidi, Aisha alikuwa na tatizo gani?
“Tatizo nini?” alijiuliza pasipo kupata jibu lolote lile.

Watu aliowafikiria kwa kipindi hicho walikuwa wazazi wake, alitakiwa kuwapa taarifa na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea hospitalini hapo. Muda ulikwenda sana lakini hakutaka kuacha kuwapigia ili hata kama lingetokea tatizo kubwa zaidi basi wawe na taarifa.

Akachukua simu yake na kuanza kuwapigia. Simu ikaanza kuita, iliita na kuita mpaka kukata pasipo kupokelewa. Hakujiuliza sana, alijua kwamba muda huo wangekuwa wamelala, alichokifanya ni kupiga tena simu.

“Haloo...” ilisikika sauti nzito ya baba yake, ilionyesha kabisa kama alitoka kuamka.

“Baba...Aisha amezidiwa, nimemleta hospitali...” alisema Razak kwa huzuni.
“Anaumwa nini?”
“Sijui chochote kile...”
“Mpo hospitali gani?”
“Hospitali ya Mediteranian..”
“Tunakuja...”

Simu ikakatwa na Razak kutulia kwenye benchi. Mawazo hayakumtoka na kila alipokaa, aliisikia sauti ikimwambia kwamba ni lazima mpenzi wake afariki dunia hapohapo kitandani kwani tatizo alilokuwa nalo lilikuwa kubwa mno.

Wasiwasi ukamshika lakini hakutaka kukata tamaa, kila wakati alimuomba Mungu atende muujiza na vipimo vitakavyopimwa basi ionekane hana tatizo lolote zaidi ya tumbo kuchafuka tu.

Dakika ziliendelea kukatika, baada ya dakika kadhaa, wazazi wake wakafika hospitalini hapo na moja kwa moja kuelekea kule alipokuwa. Walipomuona, walijua tu kwamba kulikuwa na tatizo, jinsi alivyoonekana, ilikuwa rahisi mno kugundua kwamba kijana wao alikuwa kwenye matatizo makubwa.

“Pole sana Razak,” alisema baba yake huku akimkumbatia, kumbatio lililomfanya kuanza kububujikwa na machozi kwa mara nyingine.

Wakakaa naye chini na kuanza kumuuliza maswali kadhaa ni tatizo gani alilokuwa nalo Aisha, hapo, akaanza kuwaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba alishtuka usiku wa manane huku akiugulia maumivu, baada ya hapo, akamchukua na kumpeleka hospitali.

“Kwa hiyo haijajulikana tatizo nini?” aliuliza mama yake.
“Bado, tangu waingie ndani, hawajatoka...” alijibu Razak.
“Ngoja tusubiri...”

Muda ulizidi kwenda, dakika zilikatika mpaka ilipofika saa kumi alfajiri, mlango ukafunguliwa na daktari mmoja wa kike mwenye koti kubwa jeupe lililokuwa na kibati kilichoandikwa Dk. Mimi kifuani kutoka ndani ya chumba hicho.

Hapohapo Razak akasimama na kuanza kumsogelea, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea lakini pia alitaka kufahamu ni tatizo gani alilokuwa nalo mpenzi wake.

“Nifuateni...”
Hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kuanza kumfuata Dk. Mimi ambaye alikwenda mpaka kwenye chumba kilichoonekana kuwa ofisi yake na kukaa kwenye kiti kilichokuwa nyuma ya nyumba huku akiwataka wageni wake kukaa vitini.

Kabla hajazungumza lolote, akachukua baadhi ya mafaili yaliyokuwa mezani kwake, akaandika, akashusha miwani kidogo na kuwaangalia kwa zamu huku akionekana kabisa kutaka kuzungumza kitu.

“Kwanza poleni kwa matatizo mnaliyokutana nayo....” alianza kusema Dk. Mimi.
“Asante sana, nini kinaendelea? Anaumwa nini? Atapona?” aliuliza Razak maswali matatu mfululizo.

“Tumemchunguza kwa kipindi kirefu na tumemkuta ana tatizo ambalo nashangaa ilikuwaje mpaka mkasubiri kwa kipindi kirefu mpaka tatizo kuwa sugu namna hii,” alisema Dk. Mimi.

“Tatizo gani?”
“Kwanza mpo na mgonjwa kwa kipindi gani?”
“Kama miezi miaka miwili..” alidanganya Razak.

“Katika kipindi chote hamkugundua kwamba ana tatizo lolote?”
“Hapana! Kwani kuna nini dokta?”
“Na mlikuwa mnacheki afya yake mara kwa mara?”
“Hapana!”

“Tumekuta binti yenu ana tatizo kubwa sana, lilianza kidogokidogo, likawa linakua, likakua na kukua na mwisho wa siku kuwa kubwa kabisa ambalo haliwezi kabisa kutibika,” alisema Dk. Mimi, taarifa hiyo ilimshtua kila mmoja.
“Tatizo gani?”

“Ana kansa ta utumbo mpana ambayo kitaalamu inaitwa Colon Cancer,” alijibu daktari huyo.

“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Ni tatizo kubwa sana ambalo linaua maelfu ya watu kila mwezi hapa duniani. Huwa linaanza taratibu sana, unapolipuuzia, linakua na kukua, kosa kubwa lililofanyika ni kwamba hakuangaliwa afya yake kipindi cha nyuma, ila kitu kinachosikitisha zaidi.....” alisema Dk. Mimi, hata kabla hajamalizia sentensi yake, akabaki kimya.

“Kitu gani?” aliuliza baba yake Razak, wakati huo, kijana wake alikuwa akilia tu.
“Au basi, mengine tutaongea siku nyingine...” aliseema Dk. Mimi.

“Hapana! Haiwezekani, haiwezekani utuache hewani, tuambie hicho kingine ni nini,” alisema mama yake Razak, alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Tutaongea siku nyingine...” alisisitiza Dk. Mimi.

“Dokta, umetuambia kwamba Aisha ana kansa mbaya, tumekubaliana nawe, unajua ni jinsi gani tulivyoumia, naomba usituache njia panda, tuambie hilo lingine ni lipi,” alisema mama yake Razak.
“She has Terminal Cancer,” (Ana kansa isiyopona) alijibu daktari kwa sauti ya chini, hata yeye mwenyewe, alionekana kuumia sana.

“What is that?” (Ndiyo nini hiyo?)
“Hatoweza kupona, hiyo ni kansa inayoua, imesambaa sana, hatoweza kupona, ni lazima atakufa, ni ndani ya miezi mitatu tu,” alijibu daktari huku akiwaangalia wote wawili.

Hakukuwa na siku ambayo Razak alilia kama siku hiyo, ilionekana kama kuna msiba ndani ya ofisi ya daktari, alilia kwa sauti pasipo kuona kama pale palikuwa hospitali au la.

Moyo wake uliumia, hakuamini kile alichokisema daktari kwamba msichana Aisha asingeweza kupona, yaani ile kansa ilikuwa ni lazima imuue. Alitamani kuona kile alichokisikia kiwe ndoto, yaani ghafla ashtuke kutoka katika usingizini, Aisha awe pembeni yake na amwambie kwamba kila kitu alichokiota, kilikuwa ndoto tu.

Hiyo haikuwa ndoto, alijaribu kuziuma lipsi zake ili kuona kama angeshtuka kutoka usingizini lakini wapi, bado kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilikuwa kitu halisi na hakikuwa ndoto kama alivyokuwa akihisi.

Watu wote waliokuwa ndani ya chumba kile wakaanza kumbembeleza Razak lakini hakunyamaza, alimpenda Aisha kupita maelezo, alikuwa radhi kupoteza kitu chochote katika maisha yake lakini si kumpoteza Aisha ambaye alionekana kuwa kila kitu kwake.

Kulia sana, kumbembelezwa sana hakukuweza kubadilisha matokea, ukweli ukaendelea kuwa palepale kwamba mpenzi wake alikuwa mgonjwa wa kansa ya utumbo mpana na kamwe asingeweza kupona, ilikuwa ni lazima afariki dunia.
“Siwezi kukaa....ninataka kumuona mpenzi wangu, ninataka kumuona Aishaaaaa...”

alisema Razak huku akionekana kama kuchanganyikiwa, hakutaka kubaki mahali hapo, hapohapo akasimama na kutoka nje, akaanza kukimbia kule kulipokuwa chumba alichoingizwa Aisha....wazazi wake na Dk. Mimi wakaanza kumfuata kwa mwendo wa kasi, walijua ni kwa jinsi gani Razak alikuwa amechanganyikiwa.

Je nini kitaendelea....
ndo nini sasa,tunaanza kuumia mapema hivi
 
Sehemu ya 35

Baada ya kufika jijini Dar es Salaam, Sabrina hakutaka kufanya haraka kwenda nyumbani kwa Razak na kumuomba msamaha kwa kila kitu kilichotokea, alitaka kukaa kwa wiki moja nyumbani ndiyo aende huko.

Mawazo hayakuisha, alikumbuka namna alivyoona mwanaume aliyemchukia, Sharifu alivyouawa kikatili. Moyo wake ukagawanyika, kulikuwa na upande uliokuwa unafurahi lakini upande mwingine ulihuzunika kama binadamu wa kawaida.

Nyumbani, alikuwa mkimya zaidi ya kipindi kingine, hakutaka kuzungumza kitu chochote, hakutaka kuwaambia wazazi wake kwamba alisafiri na kwenda Dubai ambapo huko alikwenda kwa lengo moja tu la kumuua Sharifu.

Baada ya wiki moja kutimia, hapo akaona kwamba ndiyo ulikuwa muda sahihi wa kwenda nyumbani kwa kina Razak.

Aliendesha gari huku akiwa na mawazo lukuki, hakujua angeanzia wapi kumuomba msamaha mwanaume huyo lakini hilo hakutaka kujali sana, kilichokuwa mbele yake kilikuwa ni kumuomba msamaha na ikiwezekana aweze kuolewa na kuwa kama zamani.

Alipofika nyumbani kwa kina Razak, akapiga honi ambapo mlinzi akatoka ili kuona ni nani aliyekuwa amefika nyumbani hapo.

Alipoliona gari la Sabrina hata yeye mwenyewe alishtuka, hakuamini kama mwanamke huyo angeweza kurudi tena kwani hali aliyoiacha kwa Razak ilikuwa ni ya maumivu makali mno.

“Sabrina...ni wewe?” aliuliza mlinzi huyo huku akionekana kushangaa.

“Ni mimi! U mzima Kachichi?”
“Nipo poa tu...karibu sana...”
Mlinzi yule akamfungulia geti na kuingia ndani. Mapigo yake ya moyo yakawa yanamdunda kwa nguvu mno. Hakujua angeonekanaje machoni mwa wazazi wa Razak, hakujua kama angekubaliwa kusamehewa au la.

Akateremka na kuufuata mlango wa kuingia sebuleni, alipoufikia, akaufungua na kuingia ndani ambapo alikaribishwa na wafanyakazi wa ndani, hata mapokezi aliyopewa, hayakuwa kama zamani, yaani ilikuwa ni kama kila mmoja alimchukia, hakutaka kujali, alichokitaka ni kuonana na Razak tu.

“Sophia...Razak yupo?” alimuuliza dada aliyekuja kumfungulia mlango.
“Hayupo...”

“Amekwenda wapi?”
Wakati ameuliza swali hilo, hata kabla hajajibiwa, mama yake Razak akatokea sebuleni hapo, alipomuona Sabrina, chuki ya waziwazi ikaanza kuonekana usoni mwake.

Sabrina aliligundua hilo lakini hakutaka kujali. Alijiona kustahili kuchukiwa, na si hivyo tu hata wangesema wampige, kwake alistahili lakini mwisho wa kila kitu, alichohitaji kilikuwa ni msamaha kutoka kwao na kwamba mtoto wao tu.

“Umefuata nini hapa?” aliuliza mama yake Razak ambaye kwa muonekano wa siku hiyo hakuonekana kuamka vizuri.
“Naomba unisamehe mama!”
“Haujanijibu swali langu, umefuata nini hapa?”

“Nimekuja kuonana na Razak...”
Wewe uonane na Razak, umesahau nini kutoka ndani ya nyumba hii?” aliuliza mwanamke huyo kwa sauti ya juu ambayo kwa uswahilini ingekuwa ni kuwapa faida majirani.

“Najua nimekosa mama, nahitaji msamaha wenu, nilikuwa kipofu, sikuona mbele, naomba mnisamehe,” alisema Sabrina huku akilia kama mtoto.

Alimaanisha alipoomba msamaha lakini mama yake Razak hakutaka kumuelewa hata kidogo. Alikumbuka namna mtoto wake alivyoumia kipindi ch nyuma, alimuacha kipindi kibaya, kipindi alichohitataji faraja kubwa.

Huku wawili hao wakiendelea kuwa hapo sebuleni, baba yake Razak akatokea. Kama alivyokuwa mkewe, naye alikuwa hivyohivyo.

Alimwangalia msichana huyo kwa macho yaliyojaa hasira kali, hakutaka kumuona, alimchukia kwani alimuumiza mtoto wake kitu ambacho hakutaka hata siku moja kitokee kwa kuwa Razak ndiye alikuwa mtoto pekee kutoka kwake.

“Umefuata nini wewe malaya?” aliuliza baba yake Razak.
“Naomba unisamehe baba....”
“Sikiliza wewe malaya, hakuna mtu aliyekuita hapa. Unauona huo mlango ulioingilia, tena tokea mlango huohuo...” alisema mzee huyo kwa hasira.

Japokuwa aliomba sana msamaha lakini hakukuwa na mtu aliyemsikiliza, kila mmoja alimchukia, hakukuwa na aliyemsikiliza, kila mmoja alimtaka kuondoka mahali hapo.

Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kuona kile kilichotokea. Kitu alichohitaji ni kuonana na Razak tu, aliamini kwamba kama angefanikiwa katika hilo na Razak kumsamehe, lisingekuwa tatizo lolote lile kwani hata wazazi hao wangekubaliana naye.

Akatoka nje, akalifuata gari lake, akaingia na kuanza kuondoka mahali hapo. Mlinzi akaanza kulifunga geti, ila hapohapo akajikuta akiitwa na msichana huyo.

“Naomba unisaidie kitu Kachichi...” alisema Sabrina.
“Kitu gani?”
“Razak yupo wapi?”
“Amehama hapa...”
“Amehama! Amehamia wapi?”

“Si lazima upajue, wewe jua kwamba amehama....yupo na mchumba wake hukoooo...” alisema mlinzi yule maneno yaliyomfanya Sabrina kuumia mno.
“Naomba uniambie, nataka nikamuone...”

“Haiwezekani...”
Kachichi alidhamiri kukataa kumwambia Sabrina sehemu alipohamia Razak. Hakuukuwa na kitu kingine ambacho angekitumia zaidi ya kumuonyeshea hela.

Harakaharaka akaingiza mkono wake katika mkoba aliokuwa nao, alipoutoa, alikuwa na noti za shilingi elfu kumi, akamuonyeshea Kachichi.
“Kweli hauwezi kuniambia?” aliuliza Sabrina.

Fedha zile zikamzuzua Kachichi, kwake kilikuwa kiwango kikubwa cha fedha ambacho kukiacha hivihivi lingekuwa kosa kubwa. Akaangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu aliyemuona, alipoona kwamba kulikuwa salama, akazichukua harakaharaka.
“Amehamia Kijitonyama...”
“Ni kubwa sana, ipi sasa?”

Kachichi akaanza kumuelekeza Sabrina nyumba aliyokuwa akiishi Razak kwa kipindi hicho, alipohakikisha kwamba aliielewa vizuri njia ya kufika mpaka nyumbani huko, hakutaka kupoteza muda, akawasha gari lake na kuondoka mahali hapo.

Njiani, moyo wake haukutaka kutulia, bado uliendelea kusumbuka kumfikiria Razak, mwanaume aliyekuwa akimpenda mno lakini mwisho wa siku akaamua kuwa na mwanaume mwingine, tapeli wa mapenzi ambaye aliuumiza sana moyo wake.

Japokuwa hakuwahi kwenda msikitini kwa miaka saba mfululizo lakini akajikuta akimuomba Mungu aweze kumsimamia katika suala lake lote la kuomba msamaha na mwisho wa siku mwanaume huyo akubaliane naye na hatimaye kumuoa kama alivyotaka kipindi cha nyuma.

“Nitamuomba msamaha tu, naamini atanisamehe...” alijifariji Sabrina huku akiendelea na safari yake kwa kufuata njia zote kama alivyoelekezwa.

Hakuchukua muda mrefu akawa amefika mbele ya nyumba kubwa ambayo aliambiwa kwamba hapo ndipo alipokuwa akiishi Razak. Akalisimamisha gari lake kwa mbali kidogo na kisha kuteremka.

Kwa hatua za taratibu, akaanza kupihga hatua kuelekea kulipokuwa nyumba ile. Alipofika, akapiga hodi na geti kufunguliwa na mlinzi aliyekuwa na kirungu mkononi mwake.

Mlinzi alipomuona Sabrina, akaonekana kuchanganyikiwa, uzuri wa msichana huyo ukampagawisha mno, akabaki akimwangalia kwa macho ya matamanio, hakujua kama alikosea njia au ilikuwaje.
“Karibu dada...” alimkaribisha mlinzi yule.
“Asante...hapa ndipo anapoishi Razak?” aliuliza Sabrina.

“Ndiyo! Karibu sana.”
Sabrina akashusha pumzi nzito, hakuamini kama ameweza kupafahamu mahali hapo. Akaingia ndani huku akiongozana na mlinzi. Walipoufikia mlango wa kuingilia sebuleni, wakaufungua na kuingia ndani.

Japokuwa mlinzi huyo alitakiwa kuwasiliana na watu wa ndani juu ya msichana huyo lakini hakufanya hivyo, kichwa chake kilichanganyikiwa na kuona kama angefanya hivyo basi angemkasirisha msichana huyo mrembo na hivyo kuonekana kuwa na roho mbaya.
*****

“Kuna nini mpenzi?” aliuliza Aisha huku akionekana kutokuelewa kilichokuwa kikimliza mpenzi wake.
“Hakuna kitu mpenzi...”
“Sasa mbona unalia?”
“Hakuna kitu...”
“Unachukia mimi kuwa na mimba yako?”

“Hapana mpenzi...”
“Kumbe tatizo nini?”
Razak hakujibu swali hilo, alibaki kimya huku moyo wake ukiendelea kuwa kwenye maumivu makali. Bado ugonjwa wa mpenzi wake ulikuwa siri kubwa, hakutaka afahamu kwani kama angemwambia ukweli basi msichana huyo angeumia zaidi.

Alichokifanya Razak ni kumgeukia Aisha na kisha kumkumbatia palepale kitini. Hakuona sababu ya kuendelea kulia kama ilivyokuwa bali kipindi hicho kilikuwa ni cha kumuonyesha Aisha kwamba alikuwa na furaha mno.

“Nakupenda Aisha wangu...” alisema Razak kwa sauti ya kunong’oneza.
“Nakupenda pia ila unanitisha...”
“Usijali mpenzi...nashindwa kuamini kinachoendelea...”
“Kwa nini?”

“Niliambiwa kwamba sitoweza kuzaa kwa kuwa mbegu zangu hazina nguvu, kitendo cha kuniambia una mimba, hakika kimenishtua na kunipa furaha, nimeshindwa kuamini na ndiyo maana nimejikuta nikilia, naomba unisamehe kama ulifikiria tofauti,” alisema Razak.

“Usijali....utakwenda kuitwa baba ndani ya miezi michache ijayo...” alisema Aisha huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

Wakati wakiwa wamekumbatiana, mara mlango ukafunguliwa na mlinzi kuingia ndani ya nyumba hiyo huku akiwa ameongozana na Sabrina.

Razak alipoyainua macho yake na kumuona msichana huyo, kwanza hakushtuka, hakujua ni kwa namna gani msichana huyo alifika nyumbani hapo.
“Sabrina.....umefuata nini?” aliuliza Razak kwa sauti ya juu.

Harakaharaka Sabrina akamsogelea Razak pale aliposimama, akapiga magoti na kuishika miguu ya mwanaume huyo na kuanza kumuomba msamaha kwa kila kitu kilichotokea.

Aisha alibaki akiangalia tu, hakumfahamu msichana huyo ila jina lake halikuwa geni kabisa. Alikwishawahi kumsikia kutoka kwa mpenzi wake, Razak ambaye alilalamika kwamba alimwacha na kumfuata mwanaume mwingine.

Razak akaanza kusogea nyuma, alitaka kukaa mbali na msichana huyo kwani alikuwa na uhakika kwamba hakuwa na mapenzi ya dhati, kumsamehe alikuwa alikwishamsamehe lakini ishu ya kurudiana naye hakika kilikuwa kitu kisichowezekana hata kidogo.
“Sabrina...” alimuita.

“Abeee...”
“Naomba uniache....”
“Naomba unisamehe Razak, dunia imenifunza, nilipokwenda hakukuwa sahihi, wewe ndiye mwanaume wangu sahihi, naomba unisamehe...” alisema Sabrina huku akilia kama mtoto.

“Kurudiana na wewe! Hicho ni kitu kisichowezekana kabisa, yaani sahau,” alisema Razak huku akionekana kumaanisha alichokizungumza.

Shakira hakutaka kukubali hata mara moja, aliendelea kumbembeleza Razak akubaliane naye kwani msamaha peke yake haukutosha lakini mwanaume huyo hakutaka kabisa kumsikiliza, akili na moyo wake ulikuwa kwa mpenzi wake Aisha ambaye alitarajia kumuoa ndani ya siku chache.

Naomba niwe nawe tena...” alisema Sabrina huku akiendelea kulia kama mtoto.

“Nadhani haunifahamu...” alisema Razak.
Hasira zake zilimpanda kichwani kabisa, alichokifanya ni kumbeba Sabrina juujuu na kumpeleka nje ya nyumba hiyo, huko, akamtupa na kisha kuufunga mlango.

Ni sauti ya kilio ndiyo iliyosikika kutoka kwa msichana huyo huku akihitaji kufunguliwa mlango lakini hakukuwa na mtu aliyemfungulia zaidi ya mlinzi kumwambia kwamba alitakiwa kuondoka mahali hapo hata kabla hajachukua uamuzi mwingine.

“Nakuhitaji Razak, pleaseee nakuhitaji,” alisema Sabrina kipindi alichoshikwa na mlinzi na kutolewa nje ya geti.

Wala hakujali sauti ya msichana huyo mrembo, alichokitaka ni kufanya kile alichoagizwa na bosi wake kwamba ilikuwa ni lazima msichana huyo atolewe ndani ya nyumba hiyo, hivyo akafanya hivyo.

Ndani ya nyumba, Razak alionekana kuwa na hasira mno, alimchukia sana Sabrina, hakutaka kumuona mbele ya macho yake.

Alikumbuka namna alivyomuacha kwenye wakati mgumu mara baada ya kuyalazimisha sana mapenzi, aliumia, hakuamini kama kuna siku moyo wake ungepata faraja tena kutoka kwa msichana mwingine kabisa.

Alibaki akizungukazunguka ndani kwa hasira tena huku akiipiga mikono yake. Aisha alikuwa kimya, kila alipomwangalia mpenzi wake, alijua fika kwamba alikuwa kwenye hasira kali, hakutaka kumwambia kitu chochote kile, alimsubiri mpaka hasira zake zitakapopungua ndiyo azungumze naye.
“Nitamuua huyu msichana...” alisema Razak.

“Usifanye hivyo mpenzi...”
“Aliutesa sana moyo wangu...nitamuua huyu msichana...” alisema Razak.
Aisha akamsogelea, alipomfikia, akamvuta na kisha kumkumbatia.
Hakutaka kuona mpenzi wake akiwa na hasira namna hiyo, alitamani kila wakati awe na furaha ili amfariji kwani bado alikuwa akiumwa huku akiwa kwenye kiti cha matairi.

“Naomba uachane naye....”
“Ila kwa nini ananifuatafuata?”
“Usijali mpenzi....achana naye...kuwa nami tu, usimfikirie, atakuumiza kichwa,” alisema Aisha kwa sauti ya chini, kidogo maneno yake yakaupoza moyo wa Razak.
*****

Je nini kitaendelea...
 
Sehemu ya 36

“Bosi...bosi...bosi...” ilisikika sauti kutoka upande wa simu ya Razak.
“Unasema Casmir...”
“Yadi inaungua...”
“Unasemaje?”

“Yadi ya magari inaungua bosi...inateketea kwa moto muda huu,” ilisikika sauti ya mfanyakazi huyo.
“Ipi?”

“Hii ya Kinondoni...wahi bosi, inateketea kwa moto...” aliendelea kusisitiza Casmir.
“Moto umean...” alitaka kuuliza swali lakini kabla hilo swali halijakamilika, simu ikakatwa na kubaki akiita tu lakini simu hiyo haikuwa hewani tena.

Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya ni kuangalia saa yake, tayari ilikuwa ni saa saba usiku, harakaharaka akakurupuka kutoka kitandani, akawasha taa na harakaharaka kuvaa suruali yake kwa ajili ya kuondoka mahali hapo.
Wakati anajiandaa, Aisha akashtuka kutoka usingizini.

Akapigwa na mshangao, hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mpaka mpenzi wake kuvaa nguo harakaharaka namna ile tayari kwa kuondoka mahali hapo.

“Kuna nini tena?” aliuliza Aisha.
“Yadi inateketea kwa moto...”
“Unasemaje?”

“Nakuja...”
Razak hakutaka kubaki mahali hapo, kwa haraka sana akachomoka chumbani na kuelekea nje, huko, akapanda ndani ya gari lake, mlinzi akafungua geti na kuondoka mahali hapo huku akiwa amechanganyikiwa.

“Yaani yadi inateketea kwa moto, haiwezekanio...haiwezekani...” alisema Razak huku akionekana kuchanganyikiwa kwani miongoni mwa biashara zilizokuwa zikimuingizia kiasi kikubwa cha fedha, ilikuwa hiyo yadi ya magari.
*****
Razak aliendesha gari kwa kasi, alikuwa amechanganyikiwa, taarifa ile ya kuteketea kwa yadi yake ya magari ilimchanganya mno. Kwa kuwa ilikuwa ni usiku sana hakukuwa na foleni barabarani hivyo hakuchukua muda mrefu akawa amekwishafika katika eneo hilo.

Kitu cha ajabu kabisa alichokiona, hakukuwa na dalili za moto wowote ule. Alibaki akishangaa, yadi yake ya magari ilikuwa salama kabisa, sasa kwa nini msimamizi wake wa yadi hiyo alimwambia kwamba yadi yake ya magari ilikuwa ikiteketea kwa moto?

Hakutaka kubaki garini, akateremka na kuelekea ndani ya yadi ile. Ukimya mkubwa ulikuwa umetawala mahali hapo, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

Hakukuwa na mlinzi wala hakuwepo Casmir kitu kilichomshangaza sana kwani haikuwa kawaida hata kidogo. Alichokifanya ni kuanza kuita lakini hakukuwa na mtu aliyeitikia.

Akaanza kuyahesabu agari yaliyokuwa mule ndani, hakukuwa na gari lolote lile lililopungua, yote yalikuwa kama alivyoyaacha, magari mia moja na hamsini.

Hakuridhika, hatua iliyofuata ni kwenda kwenye kibanda cha mlinzi, mlango ulikuwa umefungwa kwa nje na ufunguo kutolea, alichokifanya ni kuanza kuugongwa.

Hakusikia sauti za watu zaidi ya miguno ya watu wawili iliyomfanya kujua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea humo ndani.

Harakaharaka akaanza harakati za kuuvunja ule mlango, wala hakukuwa na tatizo, mlango ukafunguka, alichokiona ni kwamba mlinzi na Casmir walikuwa wamefungwa kamba na kulazwa chini, akawafungua.
“Kuna nini?” aliwauliza.
“Kuna watu walikuja, wakatufunga kamba...”

“Ni majambazi?”
“Hatujui, ila walikuja na kutufunga kamba kisha kumwambia Casmir aongee nawe maneno waliyoyataka ayaongee huku wakikuita mahali hapa,” alisema mlinzi, wakati huo Casmir alikuwa kimya.
“Ni wakina nani?”

“Bosi...sijawahi kuwaona kabisa, ila walikuja na bunduki...” alisema Casmir.
Wote wakatoka ndani ya kijumba kile, kuhesabu magari haikutosha, walichokifanya ni kuanza kufungua gari moja baada ya jingine ili kuona kama kulikuwa na vifaa vimetolewa, kila gari lilikuwa salama kabisa.

“Labda kuna mtu alitaka kunisumbua tu...nyie endeleeni na kazi, tutazungumza kesho nikija,” alisema Casmir, akaingia ndani ya gari na kuondoka.

Mpaka kipindi hicho, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alibaki akiwashangaa majambazi hao ambao waliwateka watu wake na kisha kumwamuru Casmir kumpigia simu na kumwambia habari mbaya ambayo haikuwa na ukweli wowote ule.

Alibaki akitabasamu, alitoa kicheko kidogo na kuwaona watu hao kwamba walikuwa wajinga sana.

Hakuchukua muda mrefu akawa amefika nyumbani kwake, kitu kilichomshangaza sana, alianza kupiga honi lakini kitu cha ajabu, mlinzi hakutokea kufungua geti.

“Amelala au?” alijiuliza huku akiteremka.
Akalifuata geti kisha kulifungua, akaingia ndani na kuanza kuelekea katika kibanda cha mlinzi, kilichomshangaza, hakumkuta, hakujua alielekea wapi, hakutaka kujali sana, akalifungua geti, akalirudia gari lake, akaingia kisha kuliingiza.

Alipohakikisha amelipaki sehemu sahihi, hapohapo akateremka na kuelekea ndani. Huko ndipo alipogundua maana ya ile simu aliyokuwa amepigia, walipoingia ndani, kitu kilichomshtua, mpenzi wake Aisha hakuwepo.

Alichanganyikiwa, akaanza kumtafuta huku na kule, alihisi kwamba inawezekana alikwenda nje baada ya kuona ametoka usiku sana huku akiwa amechanganyikiwa, aliita kwenye kila chumba, hakuisikia sauti ya Aisha kitu kilichomfanya kuwafuata wasichana wa kazi.

“Aisha yupo wapi?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“SI yupo ndani!”
“Ndani hayupo...hakuja huko kwenu?”
“Wala hakuja...”

Razak akatoka nje, akazunguka katika eneo zima la nyumba yake, alipofika katika bustani ya maua, akakutana na mlinzi akiwa hoi chini, amefungwa kamba huku damu zikimtoka kichwa.

“Kuna nini tena?”
“Tulivamiwa, nimepigwa na watu nisiowajua...” alijibu mlinzi...”
“Wakina nani?”
“Sijui ila walikuja na bastola....wakaingia ndani...”
“Kisha....”

“Sijui ila nilisikia wakilitaja jina la shemeji...” alijibu mlinzi yule.
Hapo ndipo Razak akachanganyikiwa zaidi, akatoka nje mbio na kuanza kukimbia katika barabara huku akiangalia huku na kule. Muda wote mikono yake ilikuwa kichwani, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea.

Alizunguka sehemu kubwa ya Kijitonyama, alikwenda mpaka Tandale na Mwananyamala, kote huko aliambulia patupu hivyo akarudi na kuwapigia simu wazazi wake.

“Unasemaje?”
“Aisha ametekwa...”
“Na nani?”
“Hakuna anayejua....naomba mje...” alisema Razak.

Hakutulia, simu nyingine kupiga ilikuwa ni ya Kituo cha Polisi cha Mabatini, akawaeleza polisi kile kilichotokea, baada ya muda, polisi hao wakafika nyumbani kwake, kitu cha kwanza kabisa wakaanza kuzungumza na mlinzi.

“Walikuwa wangapi?”
“Kama wanne...”
“Kama wanne au wanne?”

“Nasema kama kwa sababu walikuja wawili, wengine nilisikia sauti zao kwa nyuma...”
“Ikawaje?”
“Wakanipiga, wakanifunga kamba na kuingia ndani..”

“Walikuwa na silaha gani?”
“Bastola ndogo...”
“Usoni walivaa vinyago?”
“Hapana...”
“Hukuwatambua?”
“Nilishindwa kuwatambua mkuu...” alijibu mlinzi huyo.

Wakati wote wa mahojiano, Razak alisimama pembeni, alionekana kuwa na hasira mno, alichanganyikiwa, mwili wake ulikuwa ukimtetemeka, alionekana kutokuamini kilichokuwa kimetokea.

Mtu wa kwanza kabisa aliyemfikiria alikuwa msichana Sabrina, alijua hali aliyokuwa nayo na msichana huyo, baada ya kumuomba kuachana naye, aliachana naye na hata msichana huyo aliporudi, tayari alikuwa na msichana mwingine hivyo kuhisi kwamba ili kulipa kisasi, msichana huyo aliamua kumteka Aisha.

“Huyu atakuwa Sabrina tu...haiwezekani, lazima nimtafute...” alisema Razak huku akionekana kuwa na hasira mno.
****

Je nini kitaendelea....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom