Simulizi: Penzi lisilo Na Mwisho

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
152,998
453,945
Mtunzi Nyemo Chilongani
Sehemu ya 01

“Nahitaji kubadilisha tairi, unaweza kunisaidia kaka?” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja akimuuliza kijana aliyekuwa amekaa pembeni kwenye tofali.

“Hakuna tatizo, kuna hela?”
“Kunisaidia tu mpaka hela?”
“Ndiyo! Hakuna msaada bila hela, hasa kwa nyie mnaomiliki magari ya kifahari! Yaani Range Rover SUV, thamani zaidi ya shilingi milioni mia moja, ushindwe hata kunitoa buku teni! Acha masihara.”

“Basi sawa! Nitakupa! Nisaidie kwanza.”
Ukimya ulikuwa umetawala sehemu kubwa ya Posta Feri, watu wachache walikuwa wamesimama pembeni kwa ajili ya kusubiri pantoni waweze kuvuka na kuelekea Kigamboni.

Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa ni saa sita usiku muda ambao si watu wengi waliokuwa wakivuka eneo hilo kwenda Kigamboni.

Gari zuri la thamani, Range Rover SUV nyeusi ilikuwa imesimama pembezoni mwa barabara ya kuingia katika kivuko cha pantoni karibu kabisa na Kituo cha Polisi cha Magogoni.

Halikuwa limeegeshwa kwa makusudi bali kutokana na tairi lake kupata pancha, dereva hakutaka kuendelea na safari, ilikuwa ni lazima kubadilisha tairi na kuweka tairi jingine kabla ya kuendelea na safari yake.

Mwanaume huyo mwenye mwenye hilo gari ambaye alikuwa Mwarabu, Razak Mahmoud alisimama pembeni ya gari hilo akimwangalia jamaa aliyekuwa akihangaika kutoa tairi la gari lake kwa ajili ya kuweka jingine.

Muda wote, Razak alionekana kuwa na haraka mno, kila wakati alikuwa akiangalia saa yake huku akitembea huku na kule, kwa kumwangalia harakahara ilikuwa ni rahisi kujua kwamba alikuwa na uharaka wa kwenda kule alipotaka kwenda.

“It’s impossible, I have to see him right now!” (haiwezekani, ni lazima nimuone sasa hivi!) alisema Razak huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.

Japokuwa kijana yule aliyekuwa akimsaidia alijitahidi kufanya kazi hiyo kwa haraka lakini kila alipomwangalia, aliona akiifanya kazi hiyo taratibu sana, alitamani kumuharakisha, amalize haraka ili aendelee na safari yake lakini kufanya hivyo lilikuwa jambo gumu.

“Vipi?” aliuliza.
“Ndiyo naendelea kiongozi, nitamaliza sasa hivi,” alijibu jamaa huyo.
“Hivi Kigamboni kutakuwa na bodaboda niende na kuacha gari hapa?”

“Sasa hivi?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Sidhani, na kama zitakuwepo inabidi uwe makini tu, si unajua usiku una mambo mengi,” alisema kijana huyo.
“Kwa nini?”

“Kwani wewe unataka kwenda wapi?”
“Mji Mwema!”
“Kuna nini usiku wote huu? Au ndipo unapoishi?”

“Hapana! Kuna mtu nakwenda kumcheki mara moja,” alisema Razak.
Muda ulizidi kusonga mbele, ilipofika saa sita na dakika arobaini usiku, tayari kijana yule alimaliza kufanya kazi aliyokuwa akiifanya na hivyo kulipwa fedha aliyotaka kulipwa na kuondoka zake.

Alikuwa amekwishajiandaa tayari kwa kuvuka kivuko hicho, kitu kilichomshangaza ni kwamba bado geti lilikuwa limefungwa. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, ikambidi ateremke na kwenda kwenye kidirisha na kuuliza kilichokuwa kikiendelea, akaambiwa kwamba ilikuwa ni utaratibu wa kivuko kila ifikapo saa sita usiku, kufungwa kwa saa moja kisha baadaye safari kuendelea.

“Kwa hiyo mpaka saa saba?”
“Ndiyo!”
“Sawa.”

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 02

Razak akarudi ndani ya gari na kukaa. Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, mambo aliyokuwa akipitia yalimpa changamoto iliyomfanya kuchanganyikiwa mno.

Alitoka katika familia ya kitajiri, alipata kila kitu alichokihitaji, maisha mazuri, kubadilisha magari na kufanya mambo yote aliyokuwa akiyataka, lakini pamoja na hayo yote, bado mapenzi yaliusumbua moyo wake.

Aliyekuwa akikisumbua kichwa chake alikuwa msichana Sabrina tu, msichana aliyetokea kumpenda lakini ndiye kila siku alikuwa kwenye ugomvi naye. Sabrina hakuwa msichana masikini, kama alivyokuwa Razak, hata naye alitoka katika familia ya kitajiri.

Katika maisha yake, hakujua shida ilifananaje, alipata alichokitaka, alikwenda alipopataka, alizunguka katika nchi nyingi za Kiarabu kwa sababu baba yake alikuwa mfanyabishara mkubwa wa mafuta aliyejiwekea heshima kubwa Afrika Mashariki.

“Sabrina, tutagombana mpaka lini, kwa nini mapenzi hayana furaha kabisa, kila siku, ugomvi, ugomvi, ugomvi, ugomvi mpaka lini Sabrina?” aliuliza Razak huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Mpaka kiama...”
“Unasemaje?”
“Kwani umesikiaje?”
“Hebu niambie ukweli! Kwa nini mambo yanakuwa hivi? Una mtu mwingine?” aliuliza Razak.

“Unataka kujua ili iweje?”
“Nijue tu, nahisi hakuna uhusiano ulio kama hivi halafu nyuma ya pazia kukawa kusafi, kuna kitu. Hebu niambie, kuna nini mpenzi?” aliuliza Razak.

“Wewe Razak, mbona unapenda kunisumbua? Kila siku mapenzi, mapenzi tu, mapenzi, wengine yanatuchoshaaaa...” alisema Sabrina.
“Kweli unaniambia hivyo?”
“Ndiyo!”

Hayo yalikuwa mazungumzo yaliyokuwa yakijirudia kichwani mwake wakati huo alipokuwa ndani ya gari. Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia katika uhusiano huo uliojaa misukosuko ya kila aina.

Kila siku alimuomba Mungu, mambo yabadilike, awe na furaha kama siku za kwanza alipokutana na Sabrina lakini kitu cha ajabu, kila siku alijiona kuishi katika tanuru la moto, maumivu kila siku.

Moyo wake uliumia na kuumia, alikosa kimbilio, alipowaambia wazazi wake, kitu kimoja tu ndicho walichomwambia kwamba ilikuwa ni lazima amuoe Sabrina kwani wao na wazazi wake walikuwa kwenye uhusiano mzuri.

“Hivi wanajua ninayoyapitia?” alijiuliza.
“Au wanahisi ninaogelea kwenye dimbwi la mahaba?” alijiuliza Razak lakini akakosa jibu.

Dakika ziliendelea kwenda mbele, alichoka lakini hakutaka kurudi kule alipotoka. Magari binafsi machache yalikuwa yamepaki kwenye foleni yakisubiria muda ufike, geti lifunguliwe na safari ya kuvuka kivuko kuanza.

Hapo alikuwa safarini kuelekea Kigamboni ili kuonana na rafiki yake, Jafari Saydou kwa lengo la kuzungumza naye kuhusu msichana Sabrina.

Jafari alikuwa rafiki yake wa kipindi kirefu, mwanaume huyo alikuwa akisoma chuo kimoja na Sabrina. Akili ya ya Razak ilimwambia kwamba ilikuwa ni lazima kuna kitu kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia juu ya msichana wake huko chuoni.

Usiku huo japokuwa ulikuwa umekwenda sana lakini alitaka kuonana na rafiki yake huyo, alitaka kuzungumza naye ili amwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea chuoni.

Alimtafuta sana kwenye simu, hakumpata, alimtumia meseji, zilikwenda lakini hazikufika, alichoka, alikuwa na haraka ya kutaka kujua na ndiyo maana aliamua kufunga safari na kumfuata hukohuko Kigamboni.

“Puu...Puu...Puu...” alishtuka kutoka kwenye lindi la mawazo baada ya kusikia kioo cha gari lake kikigongwa na mtu aliyekuwa nje, akakishusha.
“Kuna nini?”

Je nini kitaendelea?
 
Sehemu ya 03

“Chokoraa wameng’oa taa za nyuma ya gari lako,” alisema jamaa huyo maneno yaliyomfanya Razak kushtuka, akafungua mlango na kutoka ndani ya gari, akaelekea nyuma, kweli taa mbili za gharama zilikuwa zimeng’olewa, hasira zikampanda, akarudi ndani ya gari na kuchukua bastola yake.

“Wamekimbilia wapi?” aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.
“Wameshuka chini karibu na bahari, kule kwenye mawemawe...” alijibu jamaa huyo.

Razak hakutaka kusubiri, alionekana kama mbogo aliyejeruhiwa hivyo kuanza kuteremka kule baharini kulipokuwa na mawe mengi. Alikimbia kwa kasi kubwa, bunduki ilikuwa mkononi mwake na alikuwa tayari kwa kila kitu, hata kuua, siku hiyo alikuwa radhi.

Mbele yake, kwa mbali kabisa aliweza kuwaona watu wawili wakikimbia, walikuwa watoto wa kiume, akaongeza kasi kwa kujua kwamba hao ndiyo walikuwa wezi walioiba taa za gari lake.

Mawe yalikuwa mengi, giza lilikuwa totoro lakini hakujikwaa, alikuwa imara na aliweza kukimbia kwa kasi kana kwamba alikuwa akikimbia sehemu iliyokuwa na mchanga.

Alipofika mbele kabisa, cha kushangaza, aliangalia huku na kule, hakuona mtu, yaani watoto wale waliokuwa wakikimbia, walimpotea, na mbele yake palikuwa peupe.

“Wapo wapi?” alijiuliza huku akiangalia huku na kule, wakati mwingine akahisi kama walitumbukia ndani ya bahari.
“Mna bahati mmekimbia, ningewaua paka nyie...” alisema Razak kwa sauti ya juu kana kwamba alikuwa akiongea na mtu aliyekuwa umbali wa hatua mia moja toka pale alipokuwa.

“Wakina nani?” ilisikika sauti ya msichana mmoja, ikamfanya Razak kuogopa, akageuka kule sauti ilipotoka, akanyoosha bunduki kuelekea kule.
“Unataka kuniua?” ilisikika sauti hiyo ikiuliza.

“Wewe ni nani?” aliuliza Razak huku kwa mbali akitetemeka, alihisi kama alikutana na jini kutokana na muda na mahali penyewe.

“Naitwa Aisha...”
“Aisha wa wapi?”
“Wa hapahapa...”
“Unataka nini?”
“Kwani wewe unataka kuwaua wakina nani?”

“Wewe nani?”
“Kwani nimekwambia mimi nani?”
Muda wote Razak alikuwa akitetemeka, japokuwa alikuwa pembezoni mwa bahari hivyo na upepo mwingi kupuliza lakini kitu cha ajabu kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Alitetemeka, alihofia, moyo wake ulimwambia kwamba yule aliyesimama mbele yake hakuwa binadamu bali alikuwa jini ambalo kazi yake ilikuwa ni kukaa pembezoni mwa bahari kwa ajili ya kufanya mawindo yake.

Msichana yule alisimama sehemu iliyokuwa na giza, Razak hakuweza kumuona uso vizuri hivyo kubaki akiyafikicha macho yake ili aweze kumuona vizuri msichana huyo aliyekuwa amesimama sehemu isiyokuwa na mwanga wa kutosha.

Je nini kitaendelea..
 
Sehemu ya 04

“Nikusaidie nini?” aliuliza Razak, hata sauti yake, ilionyesha ni jinsi gani alikuwa na hofu.

“Nataka unisaidie hela ili kesho nikale...” ilisikika sauti ya msichana yule ikijibu.
Hapo ndipo Aisha alipoanza kupiga hatua kuelekea kule alipokuwa Razak ambaye alisimama na bastola yake.

Alipotokeza na kusimama sehemu yenye mwanga, Razak hakuamini yule mtu aliyekuwa akimwangalia. Alikuwa msichana mrembo mno, mzuri wa sura mwenye umbo matata ambalo lilimfanya kutulia na kumwangalia vizuri.

Kichwa chake kikaanza kumwambia kwamba msichana yule alikuwa jini kwani kulikuwa na majini mengi yaliyokuwa yakijitokeza nyakati za usiku tu, tena yalikuwa mazuri ambayo kazi zao kubwa zikiwa ni kuua na kunyonya damu.

Mkono wake ulishika bastola lakini hakuweza kufanya kitu chochote kile, mwili wake ulikuwa ukimsisimka, hofu ikamshika moyoni, akabaki akiwa amesimama tu akimwangalia msichana yule.
“Wewe ni nani?” aliuliza Razak, swali moja alilolirudia mara ya pili.

“Nilisema naitwa Aisha...”
“Mmmh!”
“Nini?”
“Nikusaidie nini?”
“Hela ya kula!”

“Kwani wewe ni ombaomba?”
“Hapana! Ni chokoraa tu, sina kitu, kila siku ninashinda mitaani na wenzangu...” alijibu Aisha.

“Na wale waliokimbia unawajua?”
“Ndiyo!”
“Ni wakina nani?”
“Ahmed na Mohammed, mapacha wanaoishi mitaani kama mimi,” alijibu msichana huyo kwa sauti ya upole.

“Una miaka mingapi?”
“Kumi na saba!”
“Kwa nini upo hapa?”
“Mbona maswali mengi na wewe kama polisi! Unanisaidia hunisaidii?”

Razak aliyatuliza macho yake kwa Aisha, kila alipokuwa akimwangalia, hakuamini kama angewahi kukutana na msichana aliyekuwa na sura nzuri kama aliyokuwa nayo Aisha aliyesimama mbele yake.

Akashindwa kuvumilia, kule aliposimama alijiona akiwa mbali hivyo kuanza kumsogelea. Moyo wake ulianza kwenda sehemu nyingine kabisa, kulikaribia dimbwi zito la mahaba.

Ni kweli alikuwa amekutana na wasichana wengi wazuri akiwemo Sabrina lakini yule aliyesimama mbele yake, alikuwa mzuri zaidi ya wote. Japokuwa alikuwa na mavazi machafu lakini hilo halikufanya kuuficha uzuri wake.

Alipokuwa akimsogelea, naye Aisha akaanza kurudi nyuma, alikuwa akitetemeka, hakuwa akijiamini hata kidogo, alimuogopa mwanaume huyo na ile bastola iliyokuwa mkononi mwake ikamuongezea hofu zaidi.

Aisha hakutaka kusimama, alihisi kwamba mara baada ya Razak kuwakosa vijana wale basi angeweza kumkamata yeye mwenyewe, alichokifanya ni kuanza kukimbia kuelekea Feri.

Alikuwa mzoefu wa njia, alijua wapi palikuwa salama wapi palikuwa hatari, alikimbia harakahaharaka huku nyuma Razak akipiga kelele kumuita lakini hakusimama, akatoweka machoni mwake.

“Aishaaaa...Aishaaa...” alibaki akiita, mbele yake hakukuwa na mtu, aliangalia huku na kule, alikuwa peke yake hali iliyomfanya kurudi lilipokuwa gari lake, akaingia ndani ya gari, mawazo yalimjaa juu ya msichana huyo aliyekutana naye usiku wa siku hiyo, hata safari ya kuelekea Kigamboni, haikuendelea, akageuza gari na kurudi nyumbani kwao, Osterbay huku kichwani akiwa na mawazo mengi juu ya Aisha.

*****

Je nini kitaendelea......
 
Sehemu ya 05

Asubuhi ilipofika, Razak akaamka, akayafikicha macho yake na kutoka kitandani. Akaanza kukumbuka kile kilichotokea usiku uliopita kama kilitokea kweli alikuwa alikuwa katika moja ya ndoto fulani.

Alitulia na kukumbuka vizuri, kichwa chake kikamwambia kwamba kile kilichotokea hakikuwa ndoto bali kilikuwa kitu halisi, ni kweli alikutana na msichana mrembo ambaye hakuwahi kumuona maisha yake yote.

Alijaribu kuivuta sura ya msichana yule kichwani mwake, urembo wake ukautetemesha moyo wake, hakuamini kama kweli ndani ya dunia hiihii kungekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Aisha huku akiwa chokoraa.

Siku hiyo alitaka kumuona tena Aisha, alikuwa na uhitaji naye, ikiwezekana amwambie kwamba awe mpenzi wake na mwisho wa siku kumuoa.

Wakati akiyafikiria hayo, mara akasikia simu yake ikiwa imeingia ujumbe mfupi, kwa harakaharaka akaichukua simu ile na kuanza kuusoma ujumbe huo uliotoka kwa Sabrina.

“Nataka uniache na maisha yangu,” ulisema ujumbe huo kutoka kwa mpenzi wake, Sabrina.

“Poa, mimi mwenyewe ndiyo nilitaka kukwambia hivyohivyo” naye alijibu.
Muda huo haukuwa wa kumfikiria Sabrina, alimchoka msichana huyo kwa sababu katika kipindi cha karibuni katika uhusiano wao, haukuwa umetulia, kila siku ilikuwa ni kugombana tu.

Moyo wake ulikuwa kwa msichana mwingine kabisa, chokoraa ambaye alikutana naye usiku wa kuamkia siku hiyo, kwa jinsi alivyomjibu Sabrina ujumbe ule, hata yeye mwenyewe alijishangaa kwani alimpenda sana msichana huyo, cha ajabu, ujumbe ule aliujibu harakahara pasipo kujifikiria.

Alipomaliza kuoga, akatoka sebuleni, akakutana na wazazi wake, akazungumza nao kisha kuwaambia kwamba ana safari ya kueleka sehemu fulani ambapo kulikuwa na mtu muhimu alitaka kumuona.

“Nani?” aliuliza baba yake.
“Rafiki yangu! Nitarudi...” alijibu Razak.
“Usichelewe, kuna mengi nitataka kuzungumza nawe...”
“Hakuna tatizo.”

Razak akatoka nje, sehemu ya kupaki magari, kulikuwa na magari mengi ya kifahari, alibaki akiwa amesimama, macho yake yalikwenda kwenye moja baada ya jingine, alitaka kuchukua gari ambalo lingemfanya kuonekana wa kawaida huko atakapokwenda, mwisho wa siku akaishia katika Porte ya kijivu, akaifuata na kuingia, baada ya hapo, akaanza safari ya kuelekea Posta.

Siku hiyo hakutaka kufanya kitu chochote kile, alichokitaka ni kuonana na msichana Aisha tu. Alitokea kumpenda sana, alimhitaji kuliko msichana yeyote yule.

Aliendesha gari mpaka Feri ambapo aliamini kwamba angeweza kuonana na Aisha. Alipofika huko, akalipeleka gari lake katika sehemu ya maegesho, akaliacha hapo na kuanza kuzunguka huku na kule akimtafuta Aisha.

Alizunguka kila sehemu, kwenye yale mawe yaliyokuwa pembezoni mwa bahari, Feri kwenyewe lakini kote huko hakuambulia kitu.

Baada ya saa mbili, akawa amechoka mno lakini hakutaka kurudi nyumbani, alichokitaka ni kumuona msichana huyo hata kabla hajarudi nyumbani, alitaka kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hivyo awe wake.

Ilipofika saa saba, tumbo lake likaanza kuuma, alihisi njaa kali hivyo kuondoka na kwenda kwenye mgahawa mmoja wa gharama na kula chakula huko.

Wakati akila huku akiangalia nje, macho yake yakatua kwa vijana wawili, ombaomba waliokuwa wamefanana sana.

Alipowaona, akayakumbuka maneno aliyoongea Aisha usiku uliopita kwamba wale aliokuwa akiwakimbiza walikuwa Ahmed na Mohammed, mapacha ombaomba waliokuwa wakiishi pembezoni mwa bahari.

Je nini kitaendelea....
 
Sehemu ya 06

Hata chakula hakikupita, akachomoka ndani ya mgahawa ule na kuelekea nje, alipofika, akawaita vijana wale ambao walikuja harakaharaka mpaka alipokuwa.

“Nani Ahmed hapa?” aliuliza Razak na kuwafanya vijana wale kushtuka.
“Mimi?” alijibu mmojawapo huku akionekana kuogopa.

“Sawa! Mna njaa?”
“Hapana!” alisema Ahmed kwa harakaharaka, alionekana kumuogopa Razak.

“Mimi ninayo...” alisema Mohammed, Ahmed akamkanyaga mguu yaani akatae lakini Mohammed aliendelea kusema kwamba ana njaa.

Hao ndiyo walikuwa watu pekee ambao aliamini kwamba kupitia wao angeweza kumpata Aisha aliyekuwa akimtafuta tangu asubuhi. Akawachukua na kuwaingiza ndani ya mgahawa ule na kuagiza chakula na kuwataka kula.

Ahmed hakula kwa raha, kila wakati alimwangalia Razak kwa jicho lililoonyesha hofu kubwa. Hakumwamini, hakuona kama mwanaume yule alikuwa mtu mzuri, yaani kutoka alipotoka na kuwanunulia chakula, tena kwa kuwajua majina yao, aliogopa mno.

“Asante kaka...”
“Sawa....”
Razak akaanza kujifikiria ni kwa namna gani angeweza kuwauliza vijana wale kuhusu Aisha ambaye ndiye mtu pekee aliyemfanya kuwa mahali hapo alipokuwa.

Kila alipowaangalia vijana wale, walionekana kuwa na hofu lakini kwa upande wa pili walionekana kuwa watu wajanja ambao wangeweza kufanya jambo lolote lile na kwa wakati wowote.

Ndiyo haohao walioiba taa za gari lake usiku uliopita ila hilo hakutaka kulikumbuka, kwake, taa hazikuwa na thamani yoyote ile, angeweza kuzinunua muda wowote atakao, kitu alichokitaka ni kuonana na Aisha tu.

“Mnamfahamu Aisha?” aliwauliza.
“Aisha?” aliuliza Mohammed huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo!”
“Kwa nini unamuulizia? Wa nini?”
“Nataka kuonana naye?”
“Ili?”

“Nimsalimie...”
“Hapana! Haiwezekani!” alisema Mohammed aliyeonekana muongeaji zaidi ya mwenzake.
“Mohammed...naomba mnisaidie nionane na Aisha...”

“Una hela?”
“Ndiyo! Mnataka kiasi gani?”
“Elfu tano!”
“Sawa!” alisema Razak, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha shilingi elfu ishirini na kuwapa kiasi hicho ambacho kwao kilionekana kuwa kikubwa mno.

Alichokisema Ahmed ni kuondoka hapo mgahawani na kuelekea Kariakoo ambapo huko ndipo Aisha alipokuwa akifanya shughuli zake za kuombaomba hata kutafuta chakula katika migahawa mbalimbali.

Razak aliposikia hivyo, moyo wake ukamuuma mno, hakuamini kama msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote alikuwa ombaomba katika migahawa, yaani kuchukua mabaki ya chakula na kula.

Hakutaka kujali sana, alichokifanya ni kuondoka nao, ila Kariakoo isingewezekana kwenda kwa miguu, akawapeleka lilipokuwa gari lake.
“Ndinga lako hili kaka?” aliuliza Mohammed.
“Ndiyo!”

“Ipo poa sana...umeipataje? Inaelekea una mapene sana...” alisema Mohammed huku akilishikashika lile gari.
“Kawaida tu, hata nyie pia mnaweza kuwa na gari kama hili, ingieni twende,” alisema Razak na mapacha hao kuingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Kariakoo kuanza.

Je nini kitaendelea...
 
Sehemu ya 07

Njiani, Mohammed ndiye alikuwa kinara wa kuongea, hakunyamaza, alikuwa na maswali mengi yaliyomfanya Razak kukasirika kwani alihitaji ukimya kwa sababu alitaka kumfikiria Aisha tu.

“Kwa hiyo Kariakoo sehemu gani?”
“Kule karibu na soko, hukohuko!”
“Sawa.”

Njiani kulikuwa na msongamano wa magari, iliwachukua saa moja kutoka Posta mpaka hapo Kariakoo Sokoni ambapo Mohammed akateremka na kuwaambia wasubiri kwani alikuwa akienda kumuita Aisha ambaye mara kwa mara alipenda sana kwenda kwenye mgahawa mmoja uitwao Inshallah kujitafutia riziki.

Mapigo ya moyo wa Razak yakaanza kudunda kwa nguvu, moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kumuona msichana aliyeuteka moyo wake, aliyemfanya kumfikiria usiku mzima.

Wala haukupita muda mrefu, Mohammed akaanza kurudi pale huku akiongozana na msichana mmoja aliyekuwa amevaa nguo chafuchafu ila kwa kumwangalia, uzuri wake ulionekana vilivyo.

“Ndiye yeye!” alijisemea Razak huku akihisi moyo wake kuwa na amani tele, furaha ikaanza kujirudi tena.
“Ingia twende...” alisikika Mohammed.
“Twende wapi?” aliuliza Aisha huku akigoma.

“Kuna mtu anataka kukuona.”
“Nani?”
“Simjui! Ila alikuulizia, akatununulia chakula na kutupa hela, ingia uonane naye,” alisema Mohammed.

“Ni nani?”
“Wewe ingia tu.”
“Siwezi kuingia mpaka uniambie yeye ni nani...” alisema Aisha huku akigoma japokuwa tayari mlango ulifunguliwa nusu.

“Ingia kwanza, utamjua hukohuko...”
Wakati wakiendelea kubishana, Ahmed akafungua mlango na kuteremka kisha kumwambia Aisha aingie.

Kidogo Aisha akapata uhakika kwamba inawezekana mtu huyo alikuwa mwema kwani alimwamini sana Ahmed kuliko Mohammed kutokana na ujanja mwingi aliokuwa nao.

Akaingia ndani ya gari, macho yake yalipokwenda kwa dereva, alikuwa yuleyule ambaye alikutana naye usiku uliopita, Aisha alishtuka sana.

“Karibu Aisha...” Razak alimkaribisha Aisha huku akiachia tabasamu pana, kwa mbali msichana huyo akaanza kutetemeka.

Je nini kitaendelea....
 
Hilo ni kweli baadhi hupenda shari hata pasipostahili kuwa na shari na huja na kauli za kuudhi ili mradi tu kutokee VARANGATI! Ni watu wapuuzi hao na ni KUWAPUUZA TU!

Ila mm nadhani mtu akikuchoka utatamani ardhi ipasuke, mkipatana leo kesho anakuja na jingine, unajikuta unakuwa kama mtumwa vile kama ww bado unampenda
 
Hilo ni kweli baadhi hupenda shari hata pasipostahili kuwa na shari na huja na kauli za kuudhi ili mradi tu kutokee VARANGATI! Ni watu wapuuzi hao na ni KUWAPUUZA TU!
Kumpuuza inakuwa ngumu kwa sabab tayari nyie ni wapenzi ama mmekuwa mwili mmoja , unabaki na subira labda labda atabadilika, lkn wakati huo unaumia
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom