Sehemu ya 59
Yule mlinzi aliongea kwa dhihaka. Alinichukulia kama mimi ni malaya tu ninayejiuza huko mtaani. Kwa kuwa nilikuwa na jambo langu ninalotaka kulijua, sikupenda kushindana na yule bwana.
Aliniletea daftari la kusaini, nikaandika jina la uongo kisha nikaruhusiwa kuingia ndani ya vyumba vile.
Niliogopa kumuuliza mlinzi huyo mwenyeji wangu yupo chumba gani, nilihofia angeweza kunitengenezea udadisi na kuniona mimi sikuwa mtu wa kawaida kwenye makazi hayo.
Baada ya kusaini niliingia ndani, nikawa nazipanda ngazi za ghorofa lile, katika kila korido ya ‘floor’ kulikuwa na korido ambazo zilikuwa na milango ya vyumba. Kulikuwa kimya. Utulivu ulikuwa wa hali ya juu. Ilikuwa ni kama vile hapakuwa na watu waliokuwa wakiishi kwenye vyumba ama nyumba hiyo.
Huyu mume wangu na mchepuko wake wanaishi wapi? Niliendelea kujiuliza kimoyomoyo. Niliendelea kuzikwea ngazi kwenda juu, ilikuwa ni kama kuna kitu kinaniambia endelea kupandisha juu.
Wakati namaliza ghorofa ya pili ile naanza orofa ya tatu, mara nikamwona mwanaume mmoja amenipa mgongo. Alikuwa ni mume wangu Alex. Alikuwa anaongea na simu akiwa emesimama kwenye dirisha la korido lililokuwa likiangalia upande wa nyuma wa ghorofa lile.
Nilipiga tambo refu, nikarudi nyuma haraka sana, nikajibanza kwenye kona, pale alipokua amesimama Alex, mume wangu aliendelea kongea na simu bila kujua lolote.
Alikuwa amevaa taulo bukta, miguuni alivaa sendozi. Alionekana ni kama alikuwa ametoka au anajiandaa kupumzika. Roho iliniuma, nilihisi kama nachunwa ngozi ningali hai. Mume anauma asikwambie mtu. Ingawa nilikuwa bado sijathibitisha kama yupo na mwanamke, niliamini kwa asilimia zote bwana yule yupo na mchepuko. wakiponda raha mule ndani.
Alipomaliza kuongea na simu alirudi ndani. Nilibaki pale kwenye kona, mapigo yangu ya moyo yakinienda kasi, kuninyima kote kule haki yangu ya ndoa, kumbe haki hiyo alikuwa akipewa mwanamke mwingine.