MTOTO WA BABA PAROKO
Sehemu ya Saba
Padri Mapunda Afanya Jaribio La Mwisho
“Eric, nenda kapumzike kesho asubuhi tutaongea. Usijali sawa?” Padri Mapunda alimwambia Eric huku akimgongagonga mgongoni.
Aliondoka kuelekea nyumba ya mapadri wanapoishi na kumwacha Eric akielekea kwenye mabweni yao. Kipindi kile kilikuwa ni cha likizo kwa hivyo hakukuwa na wanafunzi. Wengi wakiwa wametawanyika kwenye mikoa yao wakihudumu kwenye Parokia wanazotokea.
Eric alifika chumbani na kukaa kwenye kitanda na cha kwanza alimpigia mama yake simu.
“Mama, sikuwa najua kuwa padri Mapunda ni mjomba wako. Hukuwahi kuniambia”, Eric alianza kuuliza kwa mshangao.
“Tuna ujomba wa mbali sana mwanangu na si ndugu tuliokuwa nao karibu ndio maana sikuwa nataka hata kujihusisha nae. Amekwambia nini?”, MariaClara, mama mzazi wa Eric alijibu kwa kujiumauma maneno.
“Ameniambia nipumzike na kwamba kesho tutazungumza ila amesema nisiwe na hofu sasa sijui atanisaidieje”, Eric alijibu.
“Mwombe sana Mungu mwanangu, naumia sana hujui tu. Kwani ulifanya nini?”, MariaClara alihoji.
Eric alianza kumweleza mama yake kisa kizima lakini aligeuza maneno hakuthubutu kumwambia mambo ya Lucia. MariaClara alisikitika sana na kumshangaa ni kwanini amekuwa hana utii wakati si tabia yake kabisa na sivyo alivyomfunza.
“Eric mwanangu, hivi ikishindikana kusaidiwa itakuwaje? Usipende kukengeuka bila sababu, wewe ni kijana mkubwa sasa”. MariaClara aliongea katika lugha ya upole sana.
Eric alikuwa ni kijana mkubwa sasa, miaka 32 sio umri wa kufanya mambo kama mtoto mdogo asiyejua madhara ya ayafanyayo au hata matokeo yake. Eric na mama yake waliongea kwa kirefu na kisha waliagana na kukata simu.
Baada ya kukata simu Eric alijilaza kitandani na kuhema kwa nguvu.
Alianza kuwaza nini kimemfikisha pale na akili ilimrudisha mpaka kwa Lucia. Alivuta picha ya Lucia na wakati huu badala ya kuja picha ya msichana mrembo ilimjia picha tofauti. Kiufupi hakutaka kusikia kitu kinaitwa Lucia.
Akiwa anatafakari kwa kina mlango ulifunguliwa na Padri Mapunda aliingia kumwita wakapate chakula. Alitoka na kuelekea sehemu maalumu ambayo mapadri wa pale seminari hupata chakula.
********************************
‘’Baba askofu Tumsifu Yesu Kristu”, Askofu Kengele alimsalimia muhashamu Baba Askofu Shemsika wa jimbo katoliki Tanga.
“Milele amina Kengele. Mnaendeleaje Dar es Salaam?”, Askofu Shemsika alijibu kwa sauti ya upole na kichungaji.
Askofu Kengele alijibu na kuanza mazungumzo na Askofu Shemsika. Alimtaarifu pamoja na mambo mengine nia ya kumpeleka mmoja wa vijana wake kwa ajili ya maangalizi kwa muda wa miaka miwili. Alipendekeza ampange Parokia ya Kwedizinga inayoongozwa na Paroko Damian Kijazi.
Alimwambia Padri Kijazi anamfahau kama padri aliye na ujuzi mwingi wa malezi ya vijana na hivyo atamfaa kumrudisha Eric kwenye mstari. Alimwambia pia baada ya mazungumzo yale angetekeleza taratibu zote zinazohitajika kwa ajili ya jambo hilo.
Askofu Shemsika alikubaliana na ombi la askofu Kengele na kuwa yupo tayari kwa ajili ya malezi hayo.
“Lakini Kengele huyu kijana alibakiza muda gani ili kupata daraja la upadri?”, Shemsika alihoji.
“Ilikuwa bado miaka mwili”, Askofu Kengele alijibu.
“Basi napata hofu kama tutafanikiwa kwa sababu kitendo cha yeye kukaa kwa maangalizi kwa miaka miwili ina maana haihesabiki masomoni na sasa itamlazimu kuitumikia tena akiwa seminari hivyo ni miaka minne mpaka kuja kuwa padri. Vijana wa siku hizi niwajuavyo watakimbia”, Askofu Shemsika alihoji na kumshirikisha wasiwasi wake Askofu Kengele.
“Naelewa lakini ndio haswa dhana ya utii, anataka kuwahi kwenda wapi? Akae avumilie tujiridhishe kweli amekuwa tayari kuwa mtii”, Askofu Kengele alijibu.
“Nimeshauri hivyo kwasababu ninao vijana watatu nimeshawapoteza kwa namna hii. Ukichukua rasimilimali tulizowekeza kwao kwa miaka mingi tokea wakiwa seminari ndogo mpaka sasa halafu wakaondoka ni hasara kwa kanisa Askofu.
Mimi nashauri linapotokea suala kama hili vijana wasione ni adhabu bali tuifanye kama sehemu ya malezi, hivyo tuwaambie kabisa kuwa tutakuweka kwenye maangalizi kwa muda wa miezi sita na akiwa huko anaendelea na masomo kwa maana ya vitabu na mazoezi madogomadogo. Dunia ya sasa inahitaji mapadri wasio na woga na hofu bali wenye kujikubali kwa hiyari. Tuangalie namna bora ya kulienenda suala hili”, Askofu Shemsika alishauri.
“Naelewa Askofu lakini kwa Eric atakaa miaka miwili. Sihitaji mapadri wasumbufu” askofu Kengele alionekana kutoelewa.
Walikubaliana na kuagana.
****************************
Baada ya wiki moja Askofu Kengele alipiga simu kwa padri Damian Kijazi wa Parokia ya Kwedizinga Tanga kumuuliza kama Eric alishawasili. Alistaajabu kuambiwa kuwa mpaka wakati ule hakuwa amefika.
Alipiga simu kwa padri Mapunda kumuuliza kulikoni lakini simu haikuwa ikipokelewa. Alianza kupatwa na wasiwasi. Aliwaza labda sasa maneno ya Askofu Shemsika yameanza kutimia kuwa Eric ameamua kuachana na mambo ya upadri. Alivumilia.
Siku ya pili yake padre Mapunda alimpigia simu askofu Kengele na kumweleza kuwa tayari Eric alikuwa njiani kuelekea Tanga. Askofu Kengele aliridhika.
Padre Mapunda alidanganya, Eric alikuwa bado yupo seminarini pale Kipalapala. Kwa mara ya kwanza padre Mapunda alimdaganya Askofu toka azaliwe. Midomo ilimtetemeka sana.
**********************************
‘’Bonjour ractor Dominique’’ (Habari Dominique) alikuwa ni Padri Mapunda akisalimiana na Padri Dominique ambae ni mkuu wa seminari (ractor) wa seminari kubwa ya Mtakatifu Francis, wenyewe wakiita Saint Francis de Sales Major Seminary huko Ufini (Finland).
“Louange à Jésus Christ Padre’’, (Tumsifu Yesu Kristu Padri). Padre Dominique alijibu.
Mazungumzo yalianza kwa lugha ya Kifaransa. Padri Mapunda alikuwa mjuvi wa lugha sita kwa ufasaha. Aliongea Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kiitaliano, Kilatini na Kihangari.
Padri Mapunda aliongea kwa kina na Padri Dominique juu ya yeye kutaka kumpa mwanafunzi wake Eric akasome kwenye seminari yake na kuhitimu huko na kupata upadri hukohuko. Alimweleza kwa kina maendeleo ya Eric na kuwa ni moja ya vijana mashuhuri sana na mwenye uwezo mkubwa kimasomo.
Padri Mapunda hakuwa na njia nyingine zaidi ya kumtorosha kijana wake Eric akasome nje ya nchi. Alijua vyema taratibu zinazohitajika na kuwa ilikuwa haiwezekani kinyemela namna hiyo lakini aliamua iwezekane kwa njia yoyote ile.
‘’Padre Mapunda, vous savez que ce n'est pas possible de ne pas mentionner le risque que vous allez mettre mon séminaire en’’ (Padre Mapunda, unajua kabisa suala hili haliwezekani na isitoshe unafahamu ni kwa namna gani utakuwa umeiweka seminari yangu katika doa kubwa). Padri Dominique aliongea kwa masikitiko makubwa.
‘’Je connais Padre, mais c’est pourquoi je vous ai contacté car je veux que cela soit possible’’ (Naelewa Padri, na ndio maana nikaona niwasiliane na wewe), Mapunda alijibu.
‘’Je ne peux pas aider’’ (Siwezi kukusaidia), Padri Dominique alijibu kwa ufupi sana.
‘’S'il vous plaît trouver un moyen de m'aider. Il est mon fils’’ (Tafadhali tafuta namna ya kunisaidia. Huyu ni mtoto wangu), Padri Mapunda ilibidi afunguke kwa padri Dominique.
‘’Jesus Christ!! Comment cela pourrait-il être possible. Vous me demandez et demande scandaleuse’’. (Yesu Kristu!! Unaniomba mambo ya ajabu), Padri Dominique alijibu kwa kushangaa sana.
Alishangaa kuwa inawezekana vipi Padri Mapunda kuwa na mtoto na tena isitoshe anataka kumfanya awe padri tena kwa njia za panya. Alishangaa kwa kweli.
‘’Dominique, je n'ai rien fait de plus choquant que toi qui sodomise des adolescents. Si vous avez réussi à le faire pendant des années et que l'église n'a pas réussi à vous identifier, vous pouvez m'aider à résoudre ce problème et l'église ne pourra pas l'identifier’’.
(Dominique, mimi sijafanya kitu chochote cha ajabu kukuzidi wewe unaelawiti vijana wadogo. Kama uliweza kufanya vitendo hivyo kwa miaka yote na kanisa limeshindwa kukugundua naamini hata sasa unaweza kunisaidia shida yangu hii na kanisa halitaweza kugundua). Padri Mapunda na yeye alionekana kuongea kwa hasira kidogo.
Jibu la padri Mapunda lilimpasua moyo padri Dominique huko Finland. Hakuamini alichosikia. Alitoa simu sikioni na kuitazama kwa macho.
‘’Tout ce qui est caché dans les ténèbres entrera dans la lumière’’. Padri Dominique alijisema kwa sauti ya taratibu sana huku mapigo yake ya moyo yakiwa kama yamesimama hivi kwa sekunde kadhaa.
Maneno hayo ni maneno wanayoambiwa mashemasi kabla ya kupewa daraja la upadri kuwa kama kuna chochote ambacho wanakijua kuhusu wao na hawajaliambia kanisa basi waseme kwani hakuna chochote kilichofichwa gizani ambacho hakitaletwa mwangani .
Padri Dominique alitoa macho kwa mshtuko.
**************************************
Dr. Dominique Fernandez na Dr. Boniface Mapunda ni marafiki wa siku nyingi. Dominique akiwa mzaliwa wa Ufaransa na Mapunda mzaliwa wa Tanzania mkoa wa Songea walikutana huko Marekani mwaka 1990 wote wakiwa katika masomo yao ya Uzamivu (PhD) katika Theolojia katika chuo cha kanisa katoliki kilichojulikana kwa kimombo kama
Aquinas Institute of Theology kilichopo St.Louis, Missouri.
Wote wakiwa mahiri sana katika masomo yao waliongoza ujumbe wa wanafunzi wenzao katika mjadala mkubwa wa kwanini Kanisa Katoliki lafaa liruhusu mapadri wao kuoa. Ni kati ya vijana na wasomi wa kanisa waliotikisa sana kanisa kwa hoja zao.
Padri Mapunda akiwa yupo na msimamo wa kuruhusu kanisa kuoa yeye padri Dominique alipinga vikali. Ulikuwa ni mjadala uliowajenga sana na kuwajengea majina miongoni mwa wasomi wengi wa kanisa Katoliki.
Ni umahiri wao huo uliowafanya wote kuteuliwa kuongoza seminari kubwa na zenye vijana wenye hoja ngumu baada ya kurudi katika nchi zao. Japo yeye padri Dominique alikuwa ni mfaransa lakini shirika lake lilimpangia kazi nchini Finland.
Seminari nyingi, wakuu wake ni watu wenye uelewa mpana sana wa mambo. Ni mapadri wasomi tena wenyewe huitwa ‘wajuao yote’ kwa maana ya kuwa hakuna hoja wanafunzi watauliza washindwe kujibu na kushawishi ukubaliane nao.
Kanisa hufanya hivi ili kuhakikisha mapadri wanaohitimu wanakuwa wametoshelezwa haja zao zote za kifalsafa na theolojia na kuwa wanapata upadri bila wasiwasi wa kiuelewa. Ilikuwa huwezi kutaja mapadri wasomi Tanzania ukaacha kumtaja padre Mapunda.
**************************************
Wakiwa Marekani padri Mapunda alianza uchunguzi binafsi dhidi ya padre Dominique na hili lilitokana na ukweli kwamba mara nyingi kwenye mijadala padri Dominique alionekana kumzidi kwa hoja padri Mapunda.
Padri Mapunda alishindwa kuelewa inakuwaje mwenzake anaweza kusimama kidete kupinga mapadri kuoa wakati ni mwanaume aliekamilika. Hakuelewa, alitaka kujua mapadri aina ya Dominique wanaishije?
Yeye padri Mapunda wakati ule damu ilikuwa ikichemka. Haikuwa mara moja wala mbili kutafuta mwanamke na kuzini nae lakini mwenzake hakuwahi kumuona akiwa katika harakati hizo.
Ndipo siku moja alipoujua ukweli. Hakuamini. Kwa miaka mingi alisikia kashfa za ulawiti lakini siku hiyo hakuamini macho yake kile alichokishuhudia.
******************************************
Je,Padri Mapunda Alishuhudia Nini Na Ilikuwaje? Je, Atafanikiwa Kumsaidia Kijana Wake Eric?
Usiache Kufuatilia Simulizi Hii Itakayokusisimua.