Simulizi: Mtoto wa Baba Paroko

Simulizi: Mtoto wa Baba Paroko

Mtoto wa Baba Paroko : SEHEMU YA SITA

Cc. Shunie lovelovelove Smart911 hearly Luno G moneytalk sweet pie kisukari instanbul havanna kuku mweus Lubebenamawe Uncle Yoso TsotsiKwesta ichumu lya

Damu Nzito Kuliko Maji

Mwaka 1986, Boniface Mapunda akiwa shemasi tayari akisubiri kula kiapo cha upadri alichagua kwenda kufanya kazi Jimbo Katoliki Sengerema katika kilichokuwa kigango cha Nyagawa.


Katika maeneo ya kiutawala ya Kanisa Katoliki, basi eneo dogo kabisa huitwa Jumuiya, jumuiya kuanzia mbili na kuendelea huzaa kile kiitwacho Kigango, vigango viwili na kuendelea huzaa Parokia kisha Parokia mbili na kuendelea huzaa Jimbo. Jimbo ndio eneo la mwisho kiutawala ambalo huongozwa na Askofu ambaye ndiye kiongozi wa juu wa kanisa katika ngazi ya jimbo.


Boniface Mapunda alichagua kwenda Sengerema kwani ndipo chimbuko la mama yake mzazi. Baba yake akiwa Mngoni wa Songea mama yake alikuwa Msukuma wa Sengerema. Alipenda kutumia muda ule kwenda kuhudumu kule kwanza kama sehemu ya shukrani kwa mama yake lakini pia alitaka kubadili mazingira kwani muda mwingi wa likizo zake akiwa seminari kuu Peramiho alitumia akiwa kwao Songea.


Boniface Mapunda ndiye leo ni Padri Mapunda, Mkuu wa Seminari ya Kipalapala Tabora.

**************************************

MariaClara, binti wa mzee Alphonce Mabula alikuwa na umri wa miaka 19 mwaka 1986. Hakuwa tu msichana mzuri kwa kumtazama kwa macho lakini pia sauti yake na haiba aliyokuwa nayo hakika ilimuhakikishia mzee Alphonce Mabula ng’ombe za kutosha kama mahari pindi binti yake atakapotaka kuolewa.


MariaClara alikuwa binti wa kanisani, siku hizi tungemwita, kwa ‘swaga’ za kizazi kipya ‘church girl’ na pengine kwenye ukurasa wake wa Instagram kwenye ‘bio’ angekuwa ameandika ‘God Fearing’ au ‘Born again’, lakini hayo hayatuhusu sana, tuyaache.


Kama alivyokuwa baba yake yaani mzee Mabula, MariaClara nae alikuwa hivyo hivyo. Usafi wa kanisa, kuhudumia maua na kujitolea kufua mavazi yaliyotumika madhabahuni ndiyo hasa ilikuwa kazi MariaClara akizifanya tena kwa kujitolea na bila kulazimishwa.


Ni katika mazingira hayo Padri Mapunda, aliyekuwa akiitwa Shemasi Mapunda wakati ule, alipokutana na MariaClara. Shemasi Mapunda akiwa nae kijana wa miaka kama 33 hivi alivutiwa sana na MariaClara. Uzuri wa MariaClara haukumuacha salama.


Shemasi Mapunda damu ilikuwa ikimchemka sana wakati ule na ukweli ni kuwa si mara moja wala mbili alishawahi kuvunja amri ya sita tena akiwa katika masomo ya kuhitimu upadri. Alijikaza sana lakini alishindwa na aliamua kusema na MariaClara.


MariaClara alikataa katakata kwani mpaka wakati ule bado alikuwa hamjui mwanaume na isitoshe alijua ukali wa baba yake. Kukataa kwa MariaClara hakukuzuia harakati za shemasi Mapunda kuhakikisha anampata binti Maria.


Hatimaye shemasi Mapunda alifanikiwa, MariaClara kwa mara ya kwanza alimjua mtu mume kwa kulala na shemasi Mapunda. Ni katika mahusiano yale MariaClara alitambua kuwa jina lingine la Boniface Mapunda aliitwa Kapalata na kwasababu yeye ni msukuma, aliamua awe anatumia jina hilo pindi awapo faragha na shemasi Mapunda. Hivyo jina Kapalata ni moja kwa moja linahusiana na mahusiano ya padri Mapunda na MariaClara na si vinginevyo.


Mahusiano haramu kati ya shemasi Mapunda na MariaClara yaliendelea kwa siri kubwa na Mapunda alimsihi sana MariaClara afanye siri kati yao tu kwani ingejulikana basi asingeweza kupata tena kutimiza ndoto yake ya kuwa padri. MariaClara, kwanza kwa kujua ukali wa baba yake na imani na dini aliyokuwa nayo, hakika kama ni siri ilifika pahala pake kwani hakuna hata rafiki yake mmoja aliewahi kujua kuwa MariaClara ana mahusiano na shemasi Mapunda.


Baada ya kumaliza muda wake wa mapumziko shemasi Mapunda aliondoka Sengerema na kumwacha MariaClara. MariaClara alikuja kugundua ana uja uzito miezi miwili baada ya shemasi Mapunda kuondoka. Alijiapiza na kwa kuogopa kutomtaja muhusika wa ule ujauzito. Kwanza alihisi atatengwa kwa kukubali kulala na Shemasi, alijionea dhambi kubwa mbele ya jamii. Kitimtimu cha kipigo cha baba yake kilimkimbiza kijijini na kwenda Dar es Salaam.


Alipofika Dar es Salaam, MariaClara akiwa amefikia kwa mjomba wake aliyejulikana kwa Majina ya Jibril Mgeni. Aliendeleza jitihada za kumtafuta shemasi Mapunda ili angalau aweze kumsaidia katika changamoto alizokuwa anapitia. Njia aliyotumia ni kuuliza kwa mapadri mbalimbali aliokuwa akiwasiliana nao kwenye parokia alizowahi kusali, kwani MariaClara hakuacha kujitolea kazi za kanisa hivyo alifahamiana na kuzoeana na mapadri wengi wa Parokia mbalimbali za Jimbo la Dar es Salaam hasa maeneo aliyowahi kuishi.


Siku moja alifanikiwa kuwasiliana na Padri Mapunda baada ya miezi minne tokea afike mjini, wakati ule mimba ya Eric ikiwa na miezi sita. Alimweleza jinsi alivyopata tabu na ujauzito ule na kumuasa aangalie namna ya kumsaidia. Wakati ule, Padri Mapunda ndiyo kwanza ametoka kula kiapo cha wito wake na kuwa padri kamili alimsihi sana Maria kuwa aitoe ile mimba kwani haiwezekani wala haitawezekana yeye kuwa na mtoto katika wito wake ule.


Majibu ya Padri Mapunda yalimtia simanzi sana MariaClara, alilia na kujutia ila akakumbuka kuwa kwa hali ilivyo ni kweli Padri Mapunda hana namna. Maria alikumbuka nyakati walivyokuwa wakiwa pamoja kule Sengerema na alisikitika hali ile kutokea.


Kupata mawasiliano na padri Mapunda ilikuwa tabu sana hivyo kuanzia siku ile MariaClara aliamua kuachana na suala la kumtafuta juu ya mtoto. Alipojifungua aliamua kumwita mwanae Eric Nyagabona.


Japo MariaClara hakuwasiliana tena na padri Mapunda kwa miaka 32 sasa, lakini hakuacha kujua nini kinaendelea kwa Padri Mapunda. Kutumia mapadri mbalimbali MariaClara alikuwa akijua kila mwenendo wa padri Mapunda. Mapenzi na padri Mapunda hayakuwahi kwisha, labda kwasababu alijua Eric ni damu yake.


Siku Eric alipomwambia kuwa amepangiwa Seminari ya Kipalapala MariaClara ilitoa machozi. Eric alipomuuliza alimwambia ni machozi ya furaha na kuwa sasa ana uhakika mwanawe anakwenda kuwa padri. Eric hakuelewa.


Leo Askofu Kengele anataka kufanya nini? MariaClara uvumilivu ulimfika kikomo. Ukimya wa miaka zaidi ya 30 unaishia hapa.

***********************************

“Padri kuna nini?”, Eric alimuuliza Padri Mapunda baada ya kumuona haeleweki baada ya kuongea na simu na kisha kuikata ghafla na kubadilika sura.


“Eric wewe asili ya kwa mama yako ni wapi? Najua hatujafikia hatua hii ya kuwachunguza ila nikuulize leo”, Padri Mapunda aliuliza.


“Mimi kwa mama ni Nyagawa, Sengerema kwa baba ni jirani kulekule”, Eric alijibu kama alivyofundishwa na mama yake. Aliambiwa kuwa babake ni Msukuma pia japo alifariki.


“Babu yako mzaa mama aliitwa nani?” Padri Mapunda aliuliza tena.


“Alphonce Mabula” Eric alijibu.


Jibu lile lilimtia ganzi Padri Mapunda, alijua aliyepo mbele yake ni kijana wake, hakuamini.


Wakati akiwa anatafakari aseme neno gani tena, simu ya Eric aliyokuwa ameishikilia yeye ilianza kuita tena na aliyekuwa akipiga alikuwa ni mama yake Eric, yaani MariaClara.


“Maria”, Padri Mapunda wakati huu aliita huku machozi yakianza kumtiririka mashavuni. Ni miaka 32 imepita sasa hakuwahi kusikia sauti ya MariaClara, achilia mbali kusumbuliwa nae hata kwa nukta moja. Sasa, Padri Mapunda alikuwa ni mzee wa miaka 65, hakuamini.


“Kapalata”, MariaClara alimwita Padri Mapunda kwa jina lile alilozoea siku zote.


“Eric ni mwanao. Nimefanya yote uliyoniambia, sikuharibu wito wako tena hata kukutaka shilingi moja ya kumtunza Eric, leo nakuomba jambo moja tu hakikisha Eric anapata upadri. Ni hilo tu baba”, MariaClara aliongea kwa uchungu sana uliomfanya Padri Mapunda awe analia kama mtoto. Mzee wa miaka 65 alilia machozi mengi.


Padri Mapunda kwa wakati ule uchungu mwingi ulimwingia. Hali ya ubaba ilimwingia kabisa, alijisikia usaliti usio kifani. Hali ya kuwa yeye ni Padri ilimtoka kabisa na hakika moyo na macho yake vyote vilishuhudia kuwa aliepo mbele yake ni kijana wake na yeye kama baba halali wa Eric anao wajibu wa kuhakikisha ndoto za kijana wake zinafikiwa.


“Maria, nawezaje kukiuka maagizo ya askofu? Nami nitakuwa nimetenda kosa lilelile alilotenda Eric la utovu wa utii. Na uzee huu unataka niende wapi?”, Padri Mapunda alimjibu MariaClara aliyekuwa akitoa kwikwi ya kilio.


“Kapalata, maisha yangu yaliharibikia mikononi mwako leo unataka maisha ya damu yako mwenyewe nayo yaharibikie mikononi mwako?” MariaClara alimuuliza Padri Mapunda kwa uchungu mkubwa.


Alimkumbusha mstari katika biblia wa kitabu cha Esta 4:14 pale ambapo mjomba wa Esta yaani Modekai alipoona wayahudi wanauawa kwa amri ya mfalme Ahusero iliyochagizwa na jemedari wake Hamani na kumwambia Estayeye akiwa kama malkia anayependwa sana na mfalme aingilie kati kutetea wayahudi na kumwambia, “Wajuaje kuwa umekuwa malkia kwa ajili ya wakati kama huu?”


“Kapalata, huwezi kujua ilitokea vile mimi kubeba ujauzito wako tena na mwanao kuja kusoma seminari ambayo wewe ndiyo mkuu wake kwa ajili ya wakati kama huu. Usipomtetea wewe nani atamtetea mwanangu?” MariaClara aliendelea kuongea mfululizo.


“Maria, nafahamu lakini sioni jinsi naweza kumsaidia zaidi ya kumtii askofu kwanza” Padri Mapunda au kama afahamikavyo Kapalata kwa Maria alijibu tena.


“Kapalata, do something. He is your son for God’s sake!”(Kapalata fanya jambo. Huyo ni mwanao ati!). MariaClara aliongea kwa kiingereza cha kuibia alichojifunza kwenye shirika la misaada la tajiri Jaques Lorento alikokuwa akifanya kazi za usafi.

Alimaliza kusema hivyo na kukata siku kwasababu kilio kilimzidi na hakutaka kuamini kuwa mtu wa mwisho aliyedhani anaweza kumsaidia mwanae Eric anadai hawezi.


Sentensi ya mwisho ya MariaClara ilimuingia sana padri Mapunda, aligeuka na kumwangalia Eric tena. Alisogea na kumkumbatia.


“Mama yako ni mjomba wangu” Padri Mapunda alimwambia Eric ili kumtoa kwenye lengo.

Eric alimkumbatia padri Mapunda kwa hisia kubwa kuliko kawaida.


“Mjomba nisaidie, bado napenda kumtumikia Mungu kwa wito wa Upadri” Eric akiwa amemkumbatia Padri Mapunda alimsihi.


“Deum nemo vidit umquam unigenitus Filius autem sacrificium quod paratus eram ut ego sum”, Padri Mapunda alimwambia Eric kwa kilatini huku akiwa amemkumbatia kwa nguvu kabisa na akibubujikwa machozi. Eric alishangaa kusikia maneno hayo lakini hakuelewa ni kwanini padre Mapunda aliyatamka, alibaki kimya.


Maneno hayo yalimaanisha kuwa ‘Mungu alikuwa tayari kumwacha mwanae wa pekee (yaani Yesu Kristu) ateseke kwa ajili ya ulimwengu lakini yeye hataweza na kuwa ni lazima afanye jambo kuokoa jahazi na kuhakikisha Eric anaupata upadri.’

**************************************

Je, Padri Mapunda Anataka Amsaidieje kijana Wake Eric? Ataweza Kuruka Vizingiti Vya Uchunguzi Vya Kanisa katoliki Lenye Ujasusi Usiomithilika Katika Taasisi Zake? Usiache Kufuatilia Simulizi Hii Itakayokusisimua siku ya Jumamosi

the Legend☆
 
Mapigo ya moyo yakiongezeka kama Pikipiki ya msafara wa Rais,,, ,ahaaaaa
Mtoto wa Baba Paroko : SEHEMU YA TANO

Cc. Shunie instanbul lovelovelove kuku mweus

Barua Ya Askofu Kengele Yasababisha Simanzi Nzito. Mama Wa Eric Asababisha Sintofahamu


Eric ni kijana alielelewa na mama yake na wajomba. Alilelewa kwa taabu sana hata kuna wakati mama yake alikuwa akipata msaada wa kusomeshewa Eric kutoka shirika la kusaidia watoto wa wasiojiweza linalofadhiliwa na Jaques Laurento tajiri mmoja wa Kifaransa. Msaada huu aliupata baada ya kuwa akifanya kazi za usafi katika ofisi za shirika hilo zilizopo Masaki jijini Dar Es Salaam.


Mama yake Eric alieitwa MariaClara Alphonce alipata uja uzito wa Eric akiwa na miaka 19. Ni ujauzito ule uliosababisha afukuzwe na baba yake huko Sengerema na kukimbilia Dar kwani baba yake alitishia kumuua kwa kusema alimdhalilisha sana.


Baba yake MariaClara yaani mze Alphonce Mabula alikuwa ni katekista wa kanisa katoliki Jimbo la Sengerema Parokia ya Nyagawa. Ni yule mzee asiekosa ibada hata ziwe 12 kwa siku. Mzee Alphonce alitambulika pia kwa ukali uliopitiliza tena asie na masihara.


Aliongoza kwa kuwasema mabinti wa wazazi wenzake kuwa wana tabia mbaya na kuwalaumu wazazi wenzie kwa malezi mabovu ya mabinti zao. MariaClara alipopata ujauzito ilikuwa ni aibu isiyomithilika kwa mzee Mabula. Kwanza mamake MariaClara alikula kipigo cha mbwa koko ktoka kwa mumewe mzee Mabula kwa kuambiwa alikuwa wapi wakati binti yao akifanya ‘uchafu’. Alimpiga sana.


MariaClara yaani mamake na Eric alipoona kichapo kile alikimbia nyumbani na hakurudi tena. Mamake alimtumia salamu kuwa akimbilie Dar kwa mjomba wake aliekuwa akifanya biashara ya kuuza ng’ombe kutoka Sengerema kwenda Dar. MariaClara kwa kusaidiwa na mjomba wake mwingine aliekuwepo kule Sengerema alifanikiwa kwenda Dar na kuanza maisha huko.


Haikuwa rahisi kwani alipofika tu kitu cha kwanza mke wa mjomba wake alichotaka kujua ni ile mimba ni ya nani na nani atamlea huyo mtoto akizaliwa. MariaClara hakutaka kusema mimba amepewa na nani. Katu hakusema. Hata mjomba wake alipomuuliza MariaClara alidanganya kuwa mtoto yule alipewa na utingo wa moja ya malori yaliyokuwa yakienda kusweka ng’obe kule kijijini.


Alipoulizwa jina alidanganya, sasa kwa sababu mjomba wake ni mfanyabiashara hiyo ya ng’ombe alijaribu kuchunguza kwenye malori yanayokwenda kusweka ng’ombe Sengerema lakini hakuweza kumjua huyo utingo. Siri ya baba wa Eric alibaki nayo mamake Eric yaani MariaClara.


Ni katika mazingira yale MariaClara aliilea mimba ya Eric kwa taabu sana. Alianza kufanya kazi ndogo ndogo za kumuingizia kipato mpaka akajifungua na baada ya kupumzika aliendelea na kazi mbalimbali. Kazi kama za mama ntilie, usafi wa majumbani, kuuza genge ni shughuli zilizomlea Eric.


Katika makuzi ya Eric kila wakati mamake alimkumbusha kuwa hataki chochote kutoka kwa mwanae ila amuone akihudumu madhabahuni kama padre.


Katika ukuaji wa Eric MariaClara alimwambia mwanae huyo kuwa babake alifariki na kuwa Eric hana baba. MariaClara alijitahidi sana na kwa uwezo wote kumlea Eric katika mazingira na tamaduni za dini na maadili na hakika hilo alifanikiwa sana. Eric alikuwa ni aina ya kijana asietiliwa shaka hata kidogo.


Japo MariaClara alikimbia kwao kumwogopa baba yake lakini ilifikia hatua baba yake yaani mzee Alphonce alielewa kuwa wakati mwingine watoto hukengeuka na hivyo alimsamehe binti yake na kumtaka arudi nyumbani lakini MariaClara alikataa.


Kipigo alichoshuhudia mama yake akipigwa na babake kilimuumiza akili sana. Alimchukia sana baba yake kiasi kwamba hata mzee Alphonce alipokuja kuugua sana hakwenda kumtazama. Mama yake alimsihi sana aende lakini Maria alikataa. Maria alikuwa anaweza kwenda Sengerema na kushukia kwa wajomba zake na mama yake kwenda kuonana nae hapo lakini kwa miaka 10 tangu akimbie nyumbani katu hakuwahi kurudi.


Wakati wa kifo cha mzee Alphonce Mabula kila ndugu alimsihi Maria aende kumzika baba yake lakini Maria alishikilia msimamo wake kuwa yule si baba yake kwa kitendo alichomfanyia. Mzee Alphonce alizikwa.


Ni baada ya kukaa na kujitafakari sana ndipo Maria alipogundua alifanya makosa. Hasa baada ya malezi ya Eric kuchanganya na kuona uchungu anaoupata pale Eric anapofanya jambo kinyume na alichomfundisha. Aligundua baba yake alipatwa hasira kutokana na kitendo chake cha kubeba ujauzito huku yeye akiwa kinara wa kufundisha watoto wa wengine na mzee muheshimiwa pale parokiani.


Roho ilimuuma sana baada ya kugundua kuwa hata Eric hamjui babu yake na wao kuzaliwa wasichana watupu ilikuwa ni fahari sana kwa mzee Mabula kama angemjua Eric kama mzaliwa wa kwanza wa kiume kwake.


Ni katika hali hiyo Maria aliamua kurudi kijijini baada ya miaka 3 toka babake afariki na kufika kwenye kaburi la babake na kuomba msamaha huku akilia sana.


Alimwahidi babake kuwa ni kwa sababu hiyo atahakikisha Eric sio tu anakuwa mpenda dini kama yeye mzee Mabula bali atakuwa padre kama ambavyo yeye baba yao alitaka sana mtoto wa kiume ili awe padre. Maria alilia sana kaburini mwa mzee Mabula siku zile.


MariaClara tangu kuzaliwa kwa Eric alimpa jina la Nyagabona yaani jina la ukoo wa mama yake, ndio kusema Eric alijulikana kama Eric Nyagabona na hata baada ya ndugu kuuliza sana baba wa Eric mwisho walichoka wakakaa kimya na maisha yakaendelea.

****************************


Baada ya padre Mapunda kumaliza kuisoma ile barua ya askofu macho yaligeuka kuwa mekundu. Alisikitika sana, alimwangalia Eric kama dakika tatu hivi bila kuongea jambo.


Eric alikuwa ni miongoni mwa waseminari wenye akili sana. Alijituma, alikuwa na uelewa mkubwa wa mambo na katika vijana padre Mapunda alikuwa akijivunia katika seminari yake ile basi Eric asingekosa kwenye tatu bora.


Padre Mapunda hakuona sababu hasa ya Eric kusimamishwa masomo na askofu Kengele lakini kwa mujibu wa kanisa na taratibu utovu wa Utii ni kosa kubwa sana kwa kanisa. Ni sawa na jeshini mkubwa amwambie mdogo‘Mbeleee tembea’ halafu yule mdogo abaki amesimama anamwangalia tu. Yani askari kama huyu ataondolewa hapo haraka kwa sababu ipo siku mtakuwa kwenye uwanja wa vita umwambie apige adui risasi halafu atakugomea tena ili awe salama atakupiga wewe unaempa amri usije ukaamrisha mwingine ampige na kumuua. Ni watu hatari sana wanaokosa utii kwa mamlaka.


Ni kwa muktadha huo Eric kwa askofu Kengele alikuwa ni mtu hatari kwa kanisa na alistahili adhabu kali tena haraka kabla hajageuka kuwa bomu kubwa zaidi. Askofu Kengele aliwaza wale mapadre wanaofanya mambo kinyuma na maagizo halafu wanajizolea umaarufu na kuungwa mkono matokeo yake hata akisimamishwa anayumbisha parokia ama jimbo kwa wengine kumfuata ama kuhama kanisa kwa kuliona halina haki. Askofu Kengele aliona ni bora wakawa wanadhibiti watu wa namna hii katika hatua hizi za chini na ndio maana kwake ukosefu wa utii ni mbaya kuliko jambo lingie lolote.


Padre Mapunda hakuwa na la kuficha, alimwambia Eric kuwa barua ile imemwelekeza kumsimamisha masomo mpaka hapo askofu Kengele atakapoamua vinginevyo na kwa muda huo ampange Parokia ya Kwedizinga huko Tanga kama sehemu yake ya kuangaliziwa na mafunzo.


Askofu Kengele alisema atawasiliana na askofu Shemsika wa jimbo katoliki Tanga ili afanye maandalizi hayo.


Taarifa ile ilimuumiza sana Eric, alilia sana. Uchungu ule ulitokana na ukweli kwamba ukipelekwa kwenye uangalizi kama vile basi kuna mawili ni aidha unaishia huko na upadre utausikia bombani au yawezekana kweli askofu akakukumbuka na kukurudisha kumalizia masomo. Vyote viwili kwa Eric vilikuwa ni vichungu. Alilia kama mtoto mdogo alienyang’anywa titi la mama wakati ana njaa kali.

************************


Baada ya Eric na padre Mapunda kubembelezana Eric aliomba ampigie simu mama yake kumtaarifu, kwa wakati ule hata wazo kuwa kuna kiumbe kinaitwa Lucia halikuwepo. Lucia kwa wakati ule alipotea kabisa kwenye mawazo ya Eric na sasa alikuwa akipigania wito wake.


Eric alishika simu huku akitetemeka, alijua taarifa ile ina matokeo mawili. Moja ni kumfanya mama yake afariki kwa mshtuko ama kumfanya awe kichaa. Yaani MariaClara na kutaka Eric awe padre kulishamtengenezea addictionyaani ndio kitu pekee kilikuwa kikimpa matumaini ya kuishi kwa wakati ule.


Padre Mapunda alimwambia Eric kama anadhani taarifa ile itasababisha sintofahamu kwa mama yake basi amuachie yeye ndio ataangalia namna ya kuongea nae. Japo padre Mapunda hajawahi kuongea na mamake Eric na wala hamfaham ila taarifa za kuugua kwake anazifahamu kwa sababu ya ruhusa za mara kwa mara Eric alizokuwa akiomba kwenda kumtazama.

Eric aliomba aongee mamake mwenyewe.


“Shikamoo mama”, Eric alisalimia na mara baada ya maongezi mawili matatu Eric alianza kumweleza mama yake kilichotokea. Alimweleza huku akibubujikwa na machozi.


“Nisamehe mama nimekuangusha ila najua bado Mungu ananiita kumtumikia mama”, Eric alikuwa akiongea kwa uchungu uliochanganyika na kwikwi ya kilio huku akimtia moyo mama yake. Ilikuwa ni ngumu kuamini kuwa Eric alikuwa ni kijana wa umri wa miaka 30 kwa jinsi alivyokuwa akilia.Mama yake alikuwa akisikiliza kwa makini huku kukisikika sauti ya kwikwi pia.


“Mama” Eric aliita baada ya kuona hakuna neno mama yake anajibu.


“Mama”, Eric aliita tena.


“Eric mpe simu Padre Mapunda”, MariaClara mamake Eric alimwambia Eric ampe ile simu padre Mapunda mkuu wake wa Seminari.


Eric alishangaa iweje mamake ameomba ombi lile. Katika miaka mitatu ya Eric kukaa seminari kuu ya Kipalapala mamake hakuwahi ongea na padre Mapunda. Kwanza alishangaa hata jina amelijuaje maana hakumbuki hata siku moja kuongelea mkuu wao wa seminari.


“Padre, mama anaomba kuongea na wewe”, Eric alimwambia padre Mapunda huku akimpa simu.


“Tumsifu Yesu Kristu mama”, Padre Mapunda alimsalimia mamake Eric kwa sauti ya upole na masikitiko.


“Milele amina Kapalata”, mamake Eric alimjibu padre Mapunda na kutulia kimya.


Hakika kama kuna kitu padre Mapunda kilimshtua basi ni kusikia mtu anamwita kwa jina la Kapalata. Jina hilo ni jina lake alilokuwa akilitumia utotoni tena alilopewa na babu yake mzaa mama yaani mzee Kapalata aliyekuwa Msukuma. Mara ya mwisho kuitwa jina hilo ni kama miaka 30 iliyopita.Isitoshe, si jina alilowahi kulitumia kabisa na aliitwa kwa nadra sana tena hasa na babu yake huyo ambae alishafariki. Alishtuka sana.


“Naongea na nani?”,padre Mapunda aliuliza kwa mshangao uliomfanya hata Eric ashangae.


“Unaongea na MariaClara mama wa huyo mwanao hapo Eric”, mamake Eric alijibu tena kiufupi na kutulia.


Padre Mapunda alikata simu haraka huku akiwa ametoa macho kama mjusi aliebanwa na mlango wa korido za mahakama huku akimtazama Eric na mapigo ya moyo kiongezeka kwa kasi ya pikipiki ya msafara wa Rais.

****************************

Usiache Kufuatilia Sehemu Ya Sita Ya Simulizi Hii.

the Legend☆

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom