Mtoto wa Baba Paroko : SEHEMU YA TATU
Eric Aingia Kwenye Kumi Na Nane Za Askofu Kengele
Jioni ya siku ile Lucia alikuwa akisubiri kwa hamu kupigiwa simu na Eric au hata kuona akimtumia ujumbe mfupi. Kama ilivyo hulka ya mtoto wa kike tena mwenye haiba na malezi bora, alijionea aibu kuanza kumtafuta yeye. Alidhani kwa kufanya hivyo ni kujishushia utu wake kama mwanamke kutokana na tamaduni alizolelewa za ki Afrika. Lucia alisubiri sana na hatimaye subira ikageuka hasira.
Aliwaza sana ni kwanini Eric alimdanganya, au alikuwa akimpima? Alianza kujisikia vibaya kuwa sasa Eric anaesomea upadre labda alikuwa akifanya majaribio fulani yanayohusiana na masomo yao.
Alimchukia na kujiapiza kamwe kutopokea simu wala kujibu ujumbe wake. Tena alijisemea moyoni kuwa hata akimuona atakuwa akimkwepa. Kwa ufupi alikasirika na hakutaka kusikia jambo lolote kuhusu Eric.
Masikini Lucia hakujua hasira ile ni kwa sababu moyo ulishampenda kijana Eric na hivyo ulikasirika ni kwanini umemdanganya. Hakika, penzi la Eric lilianza kuzama kwa Lucia bila hata kutamkwa.
Lucia alionekana mnyonge jioni ile na mama yake alipomuuliza kulikoni mbona tangu kutoka kituo cha watoto yatima anaonekana mnyonge namna ile? Alikosa jibu na kusingizia uchovu tu wa kawaida. Alikuwa akishika simu kutaka kuanza yeye kumtafuta Eric lakini moyo unamkatalia, alizidi kuugua ndani kwa ndani.
****************************
Baada ya Askofu Kengele kuona Eric hajibu alimwomba Sista Kadadaa aongoze masifu ya jioni na baada ya muda Eric alionekana kama kushtuka na kuungana nao kusali.
Baada ya masifu kuisha Askofu aliomba kuongea na Eric kabla ya kuelekea kupata chakula cha jioni. Maongezi ya Askofu Kengele yalijikita katika kusisitiza nadhiri ambazo Eric anakwenda kuziapa siku za usoni. Alimwambia juu ya nadhiri ya useja na usafi lakini nadhiri ya utii na umaskini. Lakini alikadhia haswa ya nadhiri ya useja.
Haya ni mafunzo wanayofundishwa seminarini lakini Askofu aliyarudia kana kwamba Eric hayafahamu. Alichokuwa anakifanya Askofu tungeweza kukiitaMultiple targets attacking kama tungekuwa vitani, yaani unapiga tageti nyingi kwa wakati mmoja na kumwacha adui hoi asijue achomokee wapi.
Ni dhahiri Askofu Kengele alikuwa akifuatilia nyendo za Eric pale kituoni Kurasini na kwa uzoefu wake wa saikolojia alijua kinachoendelea akilini mwake. Aliamua kumsaidia. Usoni, Eric alionekana kuelewa lakini akilini hakuna kilichoeleweka. Lucia aliiteka serikali ya akili yake.
“Eric unadhani Upadre ni wito wako na kuwa utauweza?” hili ni swali kutoka kwa Askofu lililorudisha sawa akili ya Eric. Ni swali lililoshtusha sana hasa ukizingatia linatoka kwa Askofu. Kwa utaratibu wa kanisa Askofu ana uwezo wa kusema neno moja tu kuwa “Hastahili” na upadre wa Eric akausikia kwenye bomba maisha yake yote.
Eric alishtuka sana. Hakutaka kuamini wala kutaka kusikia neno ‘hastahili’likitamkwa na kinywa cha Askofu. Aliwaza inakuwaje Lucia anataka kuharibu jambo alilolipenda toka utotoni mwake, alilolihangaikia na kulisomea maisha yake yote na sasa yupo hatua za mwisho.
“Baba, ndiyo, upadre ni wito wangu na nitauweza kwa uwezo wa Mungu”, Eric alijibu kwa unyenyekevu mkubwa huku akimwangalia Askofu kwa amcho ya huruma.
“Elige unum”, Askofu Kengele alirudia tena maneno yale ya kilatini yenye kumtaka mtu achague moja. Baada ya hayo alimwalika Eric chakula na kisha kuagana kila mmoja kuingia chumbani kwake.
*************************
Kipalapala ni moja ya Seminari kubwa kabisa ya Kanisa Katoliki. Seminari hii ipo Jimbo Kuu Katoliki Tabora na jina lake halisi ni Seminari Kubwa ya Mtakatifu Paulo. Ilianzishwa mnano mwaka 1923 na shirika la mapadri lijulikanalo kamaWhite Fathers. Ni kati ya seminari kuu tatu za kimajimbo, au kwa kingereza ikijulikana kama ’Inter-diocesan regional seminaries’. Nchini Tanzania ipo Kipalapala, nyingine ipo Peramiho na ile ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea.
Kipalapala ni moja ya seminari iliyotoa mapadri wa kikatoliki wasomi na wajuvi katika nyanja ya Imani, Falsafa na Elimu ya Ufahamu. Mfano, itamchukua mtu miaka minne kusoma masomo ya Theolojia ili kufuzu na kupewa daraja la upadri, achilia mbali masomo mengine ya kitaaluma na utambuzi kama vile Saikolojia, Sosholojia na Falsafa.
Mtu kufikia hatua ya kuingia katika seminari hii ni maana kuwa tayari umeshakata shauri na kuwa yu tayari kimwili na kiakili kulitumikia kanisa.
Ni katika seminari hii Eric ndiyo alikuwa akisoma na sasa akiwa amebakiza miaka miwili kuhitimu. Eric, mmoja wa wanafunzi mahiri kwa wakati ule alikuwa katika kipimo kikubwa cha kuamua kulitumikia kanisa ama kuitikia wito mwingine wa ndoa.
****************************
Eric usiku ule hakulala. Ilikuwa shida kwake kidogo kupata usingizi. Alijawa mawazo sana kuwa Lucia atamwelewa tena kweli? Hamu ya kuongea na Lucia ilimzidi. Simu alikuwa amezima na kuiacha kwenye kikapu pale sebuleni kwa maelekezo ya Askofu.
Alijigaragaza pale kitandani lakini wapi. Aliamua atoke akaichukue simu kwa siri, aiwashe angalau amtumie ujumbe mfupi tu maneno Lucia kisha aizime airudishe. Hakutaka kugombana wala kujulikana na Askofu. Maneno ya Askofu kuwa achague moja aliyoambiwa mara mbili yalimwingia kichwani. Alijua yatakapomtoka Askofu kwa mara ya tatu basi kitakachofuata ni hatari kwa mustakabali wa wito wake.
Aliwakumbuka watu kadhaa ambao kwa mwaka wa 30 sasa wameishia kuitwa ma Brothers pasi kuwa ma padre kamili kwa sababu tu walikosea mahali fulani fulani na hivyo kubakia kwenye jamii ya watumishi wa kanisa bila kuoa lakini pia bila kupewa u padre.Hakutaka hali hiyo imkute.
***************************
Kengele alikuwa ni askofu mkimya, ila mwenye roho ya ukali wa sirisiri. Ni askofu ambaye aliweza kuwafungia kutoa huduma mapadri wengi kama adhabu ya utovu wa nidhamu. Aghalabu wapo mapadri wawili ambao alihakikisha wanafutiwa kabisa haki ya kuhudumu kanisa katoliki na Papa Benedict XVI kwa sababu tu ya utovu wa nidhamu na kutoelewana ane. Hakuna padri ambae hamwogopi Askofu Kengele. Hata wanaoishi naye hapo kwenye makazi yake wanamuogopa kweli kweli.
Japo ana mapungufu yake hayo lakini ni Askofu anayependa sana maendeleo, kwani ni chini ya awamu yake tangu akabidhiwe jimbo amewezesha kufanikisha ujenzi wa vyuo vya ufundi na vya Elimu ya juu, hospitali iliyofanywa na serikali kuwa ya rufaa, shule nyingi kuanzia za awali mpaka za kidato cha tano na sita.
Ni yeye aliwezesha kufungua kituo cha redio, runinga na gazeti la kanisa. Tena ni yeye amewezesha kupanua uenezi Injili jimboni kwa kufungua vigango vingi zaidi kuwahi kutokea. Hakika ni ngumu kuliongelea kanisa katoliki na maendeleo makubwa bila kumtaja Askofu Kengele.
Mbali na hayo yote pia Askofu Kengele ni mpenda ibada sana. Kama hana ziara popote basi kila siku jioni utamkuta kanisa kuu la Jimbo akiabudu Ekaristi takatifu. Ni askofu aliyependa kufunga na kusali novena. Lakini la zaidi ni namna ambayo kila siku saa sita usiku lazima aamke na kusali novena ya Bikira Maria.
*******************************
Baada ya kuona usingizi hauji Eric alikata shauri kuwa atatoka aende kuichukua simu na kuwasiliana na Lucia japo kwa sekunde kadhaa kisha airudishe simu yake kwenye kikapu. Taratibu Eric alitoka kwenye chumba alichokuwa amelala upande wa kushoto mwa makazi yale ya Askofu kisha akaambatana na korido kwa kunyata akielekea sebuleni.
Alipita mlango unaokatiza kuelekea kwenye ngazi zinazoelekea ghorofani ambapo hulala masista kisha akapita kwenye korido ndogo inayoelekea kwenye chumba cha askofu halafu akakatiza kulia ili kuelekea sebuleni.
Eric alifika sebuleni na haraka huku akitetemeka alikijongea kikapu alichokuwa ameweka simu yake. Katika hali ya mshangao hakuikuta ile simu na akiwa ameshangaa ni nani ameichukua ama kuihamisha alisikia kutoka nyuma yake “Ninayo hapa”. Eric alipogeuka alikuta ni Askofu Kengele akiwa amesimama akimtazama.
**********************************
the Legend☆