Simulizi: Mtoto wa Baba Paroko

Simulizi: Mtoto wa Baba Paroko

Mtoto Wa Baba Paroko- Sehemu Ya Kumi Na Moja

Eric Akutana Na Lucia Kanisani.


Tangu mara ya mwisho Lucia kujaribu kumpigia simu Eric na kushindwa kumpata alibaki katika majonzi makubwa. Hakuelewa kimetokea nini hadi ameshindwa kuwasiliana nae tena, au Eric amefikiria nini hadi kuamua kumfanyia kile watoto wa mjini wanaita ‘kumfungia vioo’.

Kama kuna jambo linaweza kumpa msongo wa mawazo mtoto wa kike basi ni pale anapoonyeshwa kupendwa sana na kijana halafu baada ya yeye kuonyesha mrejesho chanya kijana yule kuingia mitini. Huwa wanaumia sana kwani mara nyingi huona kuwa jamaa alikuwa anamjaribu tu, na kitendo cha kuondoka baada ya kufunguliwa mlango wa moyoni basi ni kuwaonesha kuwa nao wanaweza kupatikana tu. Mawazo yalimsumbua sana.

Ni ukweli ulio wazi Eric hakuacha kuwasiliana na Lucia kwasababu nyingine yeyote isipokuwa kutaka kuokoa jahazi la wito wake. Hakika mapenzi ya Eric kwa Lucia yalikuwa na nguvu lakini wito na hitaji lake la kutaka kutimiza ndoto za mamaye zilizidi uzito. Jambo moja Eric alilokuwa ameamua kulifanya ni kujisahaulisha kuhusu Lucia, kufanya jitihada atoke kwenye mawazo yanayomuhusu mpenzi wake huyo ili aweze kuendelea na maisha ya utawa na kupigania wito wake.

Lucia alianza kuamini kuwa pengine ni kwasababu Eric anasomea utawa na kuwa yamkini amegundua jambo alilokuwa anataka kulifanya halikuwa sahihi. Lakini mawazo hayo hayakukubalika kwenye ubongo wake.
***********************************************

“Lucia, what’s wrong with you my Princess” (Lucia, unatatizo gani binti yangu) Babaye Lucia mzee Chagula alimuuliza binti yake wakiwa wamekaa nje ya baraza ya nyumba yao iliyo kubwa sana.

Mzee Chagula alikuwa anasoma majarida yake ya Uchumi akijiandaa na wasilisho la mada kwenye mkutano wa Uchumi wa Kanda ya Afrika na ile ya Bara la Ulaya hasa nchi za Nordic (Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland) ulioandaliwa na Benki Kuu ya Dunia. Kwa mada yake ilihitajika ajiandae vyema.

Yeye akiwa kama Mchumi Mwandamizi kutoka kanda ya Afrika nchini Tanzania alipewa nafasi hiyo kuwa miongoni mwa wanajopo saba watakaowasilisha mada katika mkutano ule uliokuwa unachukua wiki moja na ukifanyika jiji la Helsinki huko Ufini.

Nyumba ya kina Lucia ilikuwa ni ya kifahari sana, mbali na vyumba vingi vilivyojengwa kujitegemea (Master bedroom), Sebule mbili moja ikiwa juu ghorofani na nyingine ikiwa chini,Jiko zuri kubwa na la kisasa kabisa mzee Chagula aliweka pia vyumba vingine vitatu muhimu.

Chumba cha kwanza kilitumika kama maktaba na ofisi yake ya nyumbani ama sehemu ya watoto wake kujisomea, Lucia na mdogo wake mmoja wa kiume aliyekuwa akisoma Uingereza walikitumia kama sehemu ya kujisomea nyumbani. Aliweka pia sehemu ya kufanyia mazoezi aliyoijaza vifaa vingi vya mazoezi na mwisho aliweka chumba alichokuwa akikitumia kama kikanisa kidogo (Chapel).

Nyumba ile ilikuwa na wafanyakazi wa ndani wawili na wa nje wa kiume wawili. Waliishi yeye mzee Chagula, Lucia, mamaye Lucia na mtoto wa mdogo wake mamaye Lucia ambae alikuwa akilelewa pale. Ilikuwa ni shurti kila jioni wote kuanzia wafanyakazi kuingia kwenye kile chumba cha sala na kufanya sala ya pamoja. Walikuwa ni wakatoliki wa kindakindaki. Ni aina ya nyumba yenye miiko na maadili ambayo kwa kiasi kikubwa yalimsaidia sana Lucia kujitunza na kujiheshimu.

Japo kulikuwa na kila aina ya mazingira mazuri ya mzee Chagula kukaa ndani ya maktaba na kuandaa mada zake mara nyingi hasa siku za mwisho wa wiki alipendelea kukaa nje kwenye baraza kubwa ya mbele na kufanyia mambo yake hapo. Alipenda upepo mwanana wa pale barazani kwani kulizungukwa na miti na maua mazuri yaliyoleta utulivu wa akili na kumfanya aandike mambo kwa kina.

Akiwa amekaa pale barazani Lucia nae alitoka na kukaa kwa upande wa pembeni mwa baraza ile kulipokuwa na bustani ambapo kulining’inizwa bembea akiwa na glasi ya juisi akiivuta taratibu huku akiwa na mawazo yaliyoweza kuonekana waziwazi. Haikuwa mara ya kwanza Lucia kuonekana na hali ile. Hali ile ilikuwa ikimtokea mara kwa mara kumbukumbu za Eric zinapomjia. Mara nyingi wakiwa wanakula pamoja mezani mamaye humuuliza kinachomsibu lakini Lucia hukataa kusema.

Mamaye Lucia hakuwa mtu wa kubembelezana sana na Lucia. Japo Lucia alikuwa mtoto wake pekee wa kike lakini alipendelea sana kumfuatilia Derick yaani mdogo wake Lucia wa kiume kuliko Lucia. Ni yeye aliyemlazimisha mumewe yaani mzee Chagula ampeleke Derick kusoma nje ya nchi Uingereza japo mzee Chagula hakuwa akipendelea sana watoto wake kusoma nje ya nchi.

Ni katika hali ile ya mamaye Lucia kutokuwa karibu sana na Lucia ilipelekea Lucia na baba yake kujenga ukaribu sana na hakika kama ungetaka umuumize mzee Chagula basi ilikuwa ni umsababishie majonzi binti yake huyu. Alimpenda sana.

“Come on honey, come closer” (Sogea hapa kipenzi changu). Mzee Chagula alimwambia tena Lucia mara baada ya kuona alipomuuliza ana tatizo gani Lucia alianza kutoa machozi.

Mzee Chagula alisogeza meza na kufungua mikono na kumwita Lucia amsogelee. Lucia alikuwa ni binti wa miaka 21 lakini mbele ya babaye alionekana kama mtoto mdogo mwenye miaka sita. Alijua fika namna babaye anavyompenda na katika maisha yake hakutaka kabisa kumuumiza kwa kufanyia mambo kinyume na mafunzo aliyokuwa amepewa na wazazi hasa baba yake.

Lucia alitoka pale kwenye bembea na kumsogelea baba yake karibu pale barazami. Mzee Chagula alimuuliza kuna jambo gani linalomsumbua? Alitaka Lucia amweleze bila wasiwasi. Swali lile lilikuwa gumu kwa Lucia, aliwaza ataanzaje kumweleza baba yake masuala ya hisia zake juu ya Eric? Tena mwanafunzi anaetarajiwa kuwa padri.

“Daddy...am...am. Am I grown enough? Lucia alimuuliza baba yake ili kupata uhakika kama anayotaka kuongea yanastahili kwa umri wake ama la. Alisita sana.

Mzee Chagula ilibidi amuanzishie risala Lucia kumweleza kuwa yeye sasa ni binti mkubwa na anaweza kuwa na maamuzi japo ni vyema kama hana uhakika nayo akamuuliza mamaye au hata yeye ikibidi. Alimweleza kuwa anatakiwa awe huru kuongea naye kwani yeye ni baba yake. Mzee Chagula aliwalelea watoto wake katika hali ya kuwajengea kujiamini kuwauliza mambo ili awape muongozo.

“Daddy, kwa mara ya kwanza nilitokea kumpenda kaka mmoja hivi nilikutana nae kanisani. Huyu kijana aliniambia anasoma Chuo Cha Mtakatifu Agustino Mwanza na baada ya kukutana nae kama mara mbili ama tatu hivi tulipeana namba ya simu na kuwa tungeendelea kuwasiliana lakini sasa kuanzia wakati ule hakupokea simu zangu na sasa hapatikani tena”, Lucia alimwambia babaye kwa macho ya aibu.

“Did you two....”? Mzee Chagula alihoji na kuishia katikati.

“No!”, Lucia alijibu kwa kutoa macho kwani alielewa haraka swali la baba yake kuwa aliuliza ikiwa walishakutana kimwili.

“Is this your first time to love someone?”, Mzee Chagula aliuliza tena.

“To love someone so much like this...Yes dady”, Lucia alijibu.

Mzee Chagula alielewa kwa haraka ni lazima huyu atakuwa ni kijana wa kwanza kwa binti yake kumpenda kwani hakuwahi kumuona binti yake katika hali ile kabla ya wakati huu. Alielewa pia kuwa ni wakati muafaka sasa wa kumwelekeza binti yake mambo sahihi ya kufanya badala ya kuanza kumkaripia au kumweleza mambo nje ya uhalisia.

Alikumbuka dhana ya wazazi wengi wa kiafrika, watoto wao aidha wa kike ama wa kiume wanapofikia hatua kama hizi huwapa maonyo makali, wengine kuwapiga ama kuwakaripia kana kwamba hawaelewi nini huwa kinatokea ama wao hawakupitia hatua hizo. Kitendo hicho huwafanya watoto aidha kuharibikiwa zaidi ama kutengeneza tabia ambazo zinakuja kuwaletea shida baadae kwasababu hutenda kwa siri bila wazazi wao kufahamu. Mzee Chagula hakutaka kulifanya kosa hili.

“Mwanangu naelewa hali unayopitia, hata mimi nilipompenda mama yako na ikatokea nikawa siwezi kuwasiliana nae ama kumuona nilipata shida sana. Ila nilikuja kugundua kuwa kumbe na yeye alikuwa anashindwa kutokana na wazazi wake na wakati mwingine mazingira aliyokuwa nayo lakini upendo alikuwa nao tu.

Lakini pia Lucia katika kipindi kama hiki hutakiwi kuumiza kichwa sana kwa mambo kama haya muda utafika tu mbona mwanangu na yule anayekupenda kweli utampata tu. Binti mzuri ni yule anaetulia akichunguza huyu na yule ili asianguke kwenye mikono ya waovu. Hivi hupendi siku moja na wewe uje upate mume mzuri kama mimi baba yako?

Sasa usiwaze sana, sasa hivi angalia ni namna gani utamaliza shahada yako na uwe mwanansheria Ha ha ha, na kama yupo kijana atakayetaka uwe nae maishani, hata mimi ningependa kumuona. Sasa wewe jiandae next month ninapokwenda Finland kwenye mkutano tutakwenda wote yamkini ukanipatia mkwe mzungu huko Ha ha ha”. Mzee Chagula aliongea kwa utani kwa binti yake ili kupunguza mzigo wa mawazo na kumrudisha katika hali yake ya kawaida.

Lucia aliona ni kama ametua mzigo. Maneno ya baba yake yalimpa faraja kubwa. Hayakuondoa ukweli kuwa Eric alibaki moyoni mwake lakini hakutarajia kama baba yake angeongea nae kwa hekima na utaratibu namna ile. Maongezi ya baba yake yalirudisha tabasamu tena usoni mwa Lucia na alifurahi aliposikia kuwa atasafiri na baba yake kwenda Finland.

Kusafiri nje ya nchi kwa Lucia ilikuwa ni jambo la kawaida kwasababu kila mwisho wa mwaka walisafiri kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya mapumziko lakini safari hii ya Finland ilimfurahisha zaidi kwasababu haikuwa mapumziko bali aliona mapenzi ya baba yake ya kutaka asiwe na mawazo. Lakini pia, alijua huko angekutana na watu mbalimbali watakaokuwa wanahudhuria mkutano ule na wangeweza kubadilishana mawazo na mawasiliano.

“Thank you dady’’. Lucia alimshukuru baba yake baada ya maongezi ya kama dakika ishirini hivi.
Aliondoka pale kibarazani na kuingia ndani na baada ya dakika kumi alitoka na kumuaga baba yake kuwa anatoka kwenda kutembea ufukweni. Aliondoka na moja ya magari ya mama yake aina ya Toyota Fortuner ya mwaka 2018. Mzee Chagula alimwangalia binti yake huku akitabasamu.
*******************************

Macho ya Lucia yalishindwa kuamini kama yule anayeangaliana nae ni Eric, vivyohivyo kwa Eric alishindwa kuamini kuwa anayemtazama pale ni Lucia. Macho yao yaligandamana kwa muda kila mmoja akishindwa kumuamini mwenzake.

“Eric go and deliver the first session” (Eric nenda kasome somo la kwanza). Alikuwa ni Padri Tom akimshtua Eric asogee kwenye membari ili kusoma somo la kwanza.

Eric hakuwa ameelewa imekuaje sala za mwanzo zimeshaisha na sasa umefika wakati wa somo la kwanza. Ibada ilikuwa imeendelea bila Eric akili kuwa pale. Hakika kama kuna siku aliamini kuwa dunia ni ndogo, basi ilikuwa ni siku ile.

Eric alishtuka na kusogea kwenye membari, alianza kusoma somo la kwanza huku macho yake akiwa ameyanyanyua kila wakati kuelekea mahali alipokaa Lucia. Alikuwa akisoma somo lile huku akiwa na tabasamu kubwa sana usoni. Ulimwengu wa Eric ulibadilika na alianza kuwa na uso wenye kuonesha uhai na furaha kila wakati.

“Eric, you are reading wrong scripture son. This is the seventh Dominique of Liturgical Year C. You are reading from Liturgical year A.”(Eric, unasoma somo ambalo sio sahihi mwanangu. Hii ni Jumapili ya saba ya mwaka C wewe unasoma ya mwaka A). Alikuwa ni Padri Tom akimsahihisha Eric baada ya kugundua amefungua Misale ile somo ambalo silo.

Misale ni kitabu kinachotumika na Kanisa Katoliki kuelekeza ni masomo gani yanatakiwa kusomwa siku hiyo. Kanisa Katoliki limeugawa mwaka katika matukio mbalimbali na hivyo kuna mwaka wa kanisa ambao hesabu zake huenda tofauti na mwaka wa kawaida.

Kwa utaratibu wa kanisa kuna mizunguko mitatu ya mwaka yaani mwaka A, B, na C kisha unarudi tena kuanza mwaka A. Ndani ya mwaka kuna matukio yaani jumapili za kawaida na zile zinazoelekea ama zinazofuata baada ya tukio ama sherehe fulani. Mfano jumapili nne kabla ya sikukuu ya Krisimasi huitwa Jumapili za Majilio kisha itakuja sikukuu ya Noeli na nyingine kabla hatujaanza kuhesabu Jumapili ya kwanza ya mwaka ya kawaida.

Kisha kitakuja kipindi cha Kwaresma ambapo watu hufunga kabla ya sikukuu ya Pasaka kisha zitafuata Jumapili kama saba hivi za Pasaka na sikukuu nyingine chache kisha hurudi tena kuendelea kuhesabu jumapili za kawaida.

Mtoa somo hupaswa kuwa mwangalifu anasoma kutoka mwaka gani na Jumapili ipi kwasababu huwa ni tofauti na yote yapo kwenye Misale moja. Eric jana yake ndiye aliagizwa atayarishe masomo hayo na alisahau kufanya hivyo. Kitendo cha kufika pale kanisani na kumuona Lucia akili ilimruka na hakika kila alichokuwa akikifanya pale hakuwa akiwaza hata kidogo.

Padri Tom alifungua somo sahihi na Eric alianza kusoma. Alisoma kama mtoto aliekuwa akijifunza kusoma siku hiyo maana alikatiza katiza sana maneno. Padri Tom kwa mara ya kwanza alichukizwa na kitendo kile lakini akajikaza. Hakuamini kama kijana aliyesoma seminari mpaka kufikia hatua ile angekuwa anasoma kwa mtindo ule.

Baada ya somo lile Padri Tom alimsimamisha kijana mmoja mtumishi “Ministrant” ili akasome somo la pili na kisha yeye alikwenda kusoma Injili na kutoa tafakuri ya siku hiyo. Baada ya tafakuri ibada iliendelea na ilifikia hatua ya kupeana mikono kutakiana heri na amani.

Katika hatua hii waumini wote hupeana mikono ishara ya kusameheana tayari kujiandaa kujongea altare ya Bwana kushiriki sakramenti. Eric alitumia nafasi hii moja kwa moja mpaka mwisho wa kanisa alipokuwa ameketi Lucia.

Akiwa amevaa kanzu nyeupe alifika na kumkumbatia Lucia kwa nguvu sana. Lucia moyo wake ulienda mbio kuliko treni ya umeme.

“Lucia, I can’t believe”. Eric alimnong’oneza Lucia sikioni.

Lucia alibaki kimya akigugumia tu, hakika hakujua amjibu nini Eric. Eric alimwangalia huku akicheka sana, Lucia nae alikuwa na sura iliyoshindwa kuelezeka kama anafuraha ama analia kizungu tungesema ambiguous expression. Ukweli ni kwamba Lucia hakuamini kabisa.

Eric alimpa mkono Lucia na kumwambia wataonana baada ya ibada. Kanisa halikuelewa maana ya kumbatio lile la Eric kwa Lucia. Walijua ni kwasababu wote ni watu weusi yamkini wanafahamiana. Padri Tom pekee ndiye aliewekea maanani kumbato lile.

Baada ya Eric kuondoka huku ibada ikiendelea Lucia alikaa chini na kuinamisha kichwa. Alifanya hivyo kwani hisia za furaha zilizosababisha machozi zilimshinda nguvu. Alitoa kitambaa chake cha mikono na kuanza kujifuta machozi yaliyokuwa yakianza kutona kidogo kidogo machoni kwake.

Ibada iliendelea na hakika Eric aliona kama vile inachukua mwaka mzima ibada kuisha lakini hatimaye ilikwisha. Eric na padri Tom walitoka kwanza kama utaratibu wa Ibada unavyotaka na kisha waumini wote walitoka.

Eric akiwa na Padri Tom waliingia sakrestia, chumba maalumu cha kujitayarishia kabla na baada ya ibada ili waweze kuvua mavazi yale ya Ibada. Eric aliyavua mavazi yake kwa kasi ya ajabu kama kibaka aliyekuwa akikimbia defender ya polisi. Alipomaliza akachomoka mbio.

Eric alikimbia kuelekea mbele ya kanisa ambapo alimkuta Lucia akiwa amesimama pembeni mwa lango kuu. Huku Eric akiwa anakuja kwa mwendo wa haraka sana alipokutanisha macho kwa macho na Lucia alipunguza mwendo.

“Lucia”

“Eric”

Kila mmoja alijikuta akimuita mwenzake kwa sauti ya upole iliyojaa mahaba makubwa. Walikutana mwili kwa mwili na kukumbatiana huku Lucia wakati huu akishindwa kujizuia kutoa amchozi ya wazi na hadharani kabisa.

Lucia wakati huu hakuwa na chembe ya hofu, ilikuwa ni kama wapenzi wa siku nyingi waliokuwa wamepotezana. Hakika kila mmoja alitamani moyo wa mwenzake uingie kwa mwingine kwa jinsi mahaba yao yalivyoshibana katika hali isiyo kawaida. Eric alisahau yeye ni nani na ana wito gani. Lucia alisahau kuwa pale wapo eneo gani wote ni kama walidungwa sindano za ganzi ya aibu. Walidhihirisha ule usemi usemao ‘Mapenzi ni upofu’

“Come this way”, Eric alimwambia Lucia huku akimvuta kumwingiza ndani ya kanisa.

Alimpeleka nyuma ya kibanda ambacho watu hukitumia kwa ajili ya kufanyia kitubio. Kanisa lilikuwa wazi saa ile na ibada yao ile ndiyo ilikuwa ya mwisho. Kibanda kile huwekwa nyuma kabisa ya kanisa.

“Eric nilijua sitakuona tena” Lucia alimwambia Eric walipofika nyuma ya kibada kile huku akimtazama Eric machoni na macho yake yakiwa yamejaa machozi.

“Shhh shhhh am sorry Lucia” Eric alimnyamazisha Lucia alieonekana kutaka kuanza kulia kwa sauti.

“Why did you....” Kabla Lucia hajaanza kuongea Eric alimuwahi na kuanza kumbusu mdomoni. Ilikuwa ni hisia zisizo mfanowe tena ndani ya kanisa.

Huku wakiwa wanapeana mabusu motomoto wakiwa wamekumbatiana kwa nguvu zenye hisia nzito ghafla.......

“Precor hoc iustum est somnium”, Alikuwa ni Padri Tom akiwa katika hali ya mshangao mkubwa alihamaki kwa saiti kubwa kwa lugha ya ki Latini akisema anaombea hicho alichokuwa akikitazama iwe ni anaota na sio kweli kuwa ndicho kinachofanyika.

Eric na Lucia walitamani ardhi ipasuke wazame ndani yake.
************************************
 
Hii story ndo imetokomea kusikojulikana au vipi manake kimya mnoo
 
Ingia kwenye playstore app ya "simulizi Africa" utaikuta
 
Daaaah story iendeleea basi
Kabla sijaroga mtu hapa
 
Back
Top Bottom