Simulizi: Milango ya mafanikio

ndugu moneytalk
 
SEHEMU YA KUMI.

Kikao kilibadilika ghafla, macho ya Kila mmoja yalikuwa yakimtizama mtu mmoja Masoud, ambaye ndiye aliyeonekana kuwa mzungumzaji kuliko mwenzake ambaye alikuwa kasizi tu.

Masoud alitoa short story tangu walipompokea dogo toka kwa boss wao huku akisema mambo mengine dogo ataeleza mwenyewe.

"Tumeamua kumrudisha nyumbani kwasababu kule kazi ni ngumu sana lakini pia tumejaribu kumuuliza alitoka vipi huku , akatuambia alitoroka , tukaona kama ni hivyo si jambo zuri hivyo anatakiwa arudi hasa ukizingatia umri wake bado ni mdogo sana.
aliongea Masoud huku akidanganya sababu iliyofanya wamrudishe Samson, kwakuwa aliona si rasmi lakini ingeleta maswali mengi ambayo asingeweza kuyajibu.

Watu walishangilia huku wakiwapongeza Masoud na jamaa yake kwa kuwa na hekima isiyokuwa na mfano ya kuweza kujiongeza na kurudisha furaha iliyopotea kwenye familia ya mzee Mgaya. Lakini pia kundi Zima lilimgeukia mtaalamu au mganga wa kienyeji wakiwa na hisia mbaya kwa mganga yule ni kwa Nini alikuwa anawaongopea, huku baadhi ya wanakijiji wenye hasira Kali wakimwaga dawa zake na kurushia mawe vifaa vyake.

Mwenyekiti kuona vile akaingilia Kati.

Kwanza kwaniaba ya wanafamilia na Wana Kijiji kwa ujumla naomba nijitambulishe japo wengi wenu mnanifahamu(huku akitaja jina lake mwenyekiti wa Kijiji kile).
Kusanyiko hili halijawa hivi kwa bahati mbaya bali ni kwa kuombwa na familia ya mzee wetu ambaye alipotelewa na kijana wake.

Hivyo katika Mila na desturi zetu, Kila mtu au wengi wetu bado tuna Imani na wataalamu hawa na tushasimamia shughuli nyingi zenye kuwahusisha wataalamu hawa ikiwemo kutoa uchawi, kufanya mazindiko na mengine mengi. Je, huu ni utaratibu wetu au ni mgeni kwetu? aliuliza mwenyekiti.

Watu wote wakajibu kuwa ni utaratibu uliozoeleka kwa miaka mingi.

Mwenyekiti akaendelea.............

Hivyo basi serikali ya kijiji hiki ilitoa kibali siyo kwamba inamwamini mtaalamu moja kwa moja hapana ila ni kwasababu nyinyi wenyewe mlimwamini. Hivyo natoa amri kuwa maadam kijana, mtoto wetu na ndugu yetu karudi salama salimini, nasema kila mmoja arudi kwenye shughuli zake hakuna haja ya kuendelea kukaa hapa maana kilichokuwa kimetukusanya hapa kimepatikana. aliamrisha mwenyekiti kwa ukali maana alitambua watu wale kuendelea kubaki pale ni kuzalisha matatizo mengine lakini hata kifo maana wananchi walikuwa na hasira sana.

Kutokana na agizo lile watu wengi walitawanyika huku wakirusha maneno ya vitisho na matusi kuhusu mganga kutaka kuwapotezea muda kwa ufundi wake wa uongo. Ikawa wameondoka wakabaki wanafamilia na ndugu kadhaa akiwemo dada yake na mzee Mgaya ambaye naye alikuwa ana aibu fulani kwakuwa alikuwa mstari wa mbele kumpromote yule mganga.

Sasa ndugu zanguni ni kwamba kwanza tunapaswa kumshukuru mwenyezi MUNGU kwa kuweza kuturudishia mtoto wetu, Sasa Mimi kama kiongozi na ndugu yenu kabisa mzaliwa wahapa naomba niondoke na huyu mtaalamu kwa usalama wetu, wake na Kijiji kwa ujumla. alisema mwenyekiti huku wasaidizi wa mganga wakiwa washaandaa vitu vyao tayari kwa kuondoka eneo lile ambalo usalama ulikuwa mdogo, kama watu wangejipanga kuleta mashambulizi. Wakaondoka huku mwenyekiti na baadhi ya wanamgambo wakiisindikiza ile timu ya mganga.

Masoud na jamaa yake waliondoka huku wakipewa zawadi nyingi sana, ikiwemo kuku ambao waliwafurahia sana maana kule kambini kwao huwa mboga kubwa ni maharage tu, labda na samaki siku moja moja ambao huwa wanawatega miferejini nao si wengi sana. wakaondoka kwa furaha huku wakisindikizwa na mzee Mgaya na timu yake.

Mida ya saa mbili usiku kulikuwa na kikao rasmi sasa ambacho kilimhusisha Samson, ajenda ikiwa kwanini atoroke?
Maana mabaya yote ambayo yangetokea angesababisha yeye, lakini pia hasara ambayo wangeipata kwa kutapeliwa na mganga angesababisha yeye wakaona anastahili adhabu ya viboko.ili iwe fundisho kwa watoto ambao watawapa Presha wazazi wao.

Hapana, nasema hapana msimpige.
Mwanangu Samson ulitaka kuniua kwasababu gani? aliuliza mama Mgaya ambaye alikonda huku akionekana mzee sana tofauti na umri wake.

Samson hakuwa na la kujibu zaidi ya kuomba msamaha.
Licha ya watu wengine kusema huyu achapwe lakini mzee Mgaya alikataa katakata, akisema Samson aachwe tu maana mateso aliyopata akimuwazia kijana wake yanatosha na hapaswi kulipa kisasi kwa kumpiga mwanaye.

Kwa maelezo yale ya wazazi watubaki wakaona kama wazazi wanasema hivi sisi wengine ni akina nani tushupaze misuli kwa jambo lisilotuhusu? Wakaachana nalo.

Kesho asubuhi na mapema Samson aliamka, akakaa nje huku baridi ikimpiga lakini wala hakujali alichojua yeye ni kuwa bado ni kama mahabusu mbele ya mahakama kuu akijua hukumu inaweza kutoka muda wowote ule hakuamini kama kasamehewa kirahisi tu namna ile.

Wakati akiwa pale nje alisikia sauti za watu wawili huku mmoja akiwa katangulia na begi kubwa sana kichwani, baada ya kukaribia aliwatambua ni baba yake mkubwa aishiye Dar es salaam walisalimiana Kisha akakaribishwa ndani.

Ni kaka yake na mzee Mgaya ambaye alituma barua kama mwezi uliopita akitoa taarifa ya ujio wake na mzee Mgaya alitarajia ugeni ule, kilichowashangaza wote ni yeye kuja asubuhi, lakini akawaeleza kuwa ameshuka kwenye gari saa Saba za usiku pale stand ya Mafinga mjini lakini akapata usafiri wa Lori ambalo nalo limemwacha tu njiani kwakuwa lenyewe linaelekea Madibira huko hivyo ikabidi aje pale kwa miguu .
Walimpa pole kwa kushindwa kupata usingizi lakini ikabidi aandaliwe maji ya moto kwaajili ya kuondoa uchovu na vumbi .

Aisee ndugu yangu naona kilimo kimewashika na kuwakamata kweli kweli, si mchezo ama kweli hii ni December. alisema kaka yake na mzee Mgaya.

Kwanini unasema hivi kaka, aliuliza Mzee Mgaya.

Nisiwafiche mmekonda, Tena shemeji namuona kaisha kabisa, Nini tatizo ndugu yangu , na ndiyo maana serikali ya awamu hii ya tatu ina mikakati ya kuboresha hasa kwenye eneo la kilimo Ina mpango wa kuleta mapinduzi hasa kuleta pembejeo na vifaa vya kisasa kwaajili ya kuleta mapinduzi kwenye hii sekta maana hii si sawa kabisa. aliongea kwa huzuni kaka yake na mzee Mgaya.

Ndugu yangu ni kweli unachoongea kwanza tu takribani miaka mingi hatujaonana, najua muonekano wa nyie wenzetu mnaoishi mjini na sisi ni tofauti, lakini bado na sisi huwa tuna afya njema na zenye kuridhisha, ila hali unayoiona hapa hasa shemeji yako pengine ungekuta jina la shemeji yako na si kama unavyomuona na umechelewa kidogo sana kama ungekuja Jana ungeyakuta mambo hapa usingesimuliwa , ndipo alipomsimulia kisa choooote cha Samson namna alivyowachezesha wiki zaidi ya tatu huku wao wakishindwa hata kula vizuri kutokana na kijana kutoonekana. Mzee Mgaya alisimulia hatua kwa hatua huku sehemu anazosahau akikumbushwa na mama Mgaya pamoja na wanae.

Yule mgeni yaani kaka yake na mzee Mgaya alisikiliza kwa umakini huku akiwa hajatoa jibu lolote huku sentensi ya kusema Samson kaachwa hajapewa adhabu yeyote ikiwa imemuumiza sana akaona ni uzembe, akamkamata Samson na kuanza kumuangushia kipigo Cha mbwa mwizi, ikawa kazi ya Mzee Mgaya na familia yake kuamulia wakiona Samson atakufa

Baada ya muda fulani, wakapoa huku Samson akionekana kavimba kwa kunyooshwa kisawasawa.

Mnasema huyu kamaliza darasa la Saba si ndiyo,? aliuliza yule mgeni

Ndiyo na wala hakuna wasiwasi wa yeye kufaulu kwakuwa yupo vizuri sana darasani. alijibu Jane akimtetea Samson.

Kule nyumbani wale watoto wangu wawili mapacha nao wamehitimu mwaka huu na tayari nimeshawatafutia hata shule na Kila kitu kipo sawa lakini pia sikujua kama na huyu alifika level hiyo siyo mbaya kwakuwa muda upo ningemchukua ili akaanze masomo kule mjini lakini kwa tabia zake za ukaidi mlizoniambia huyu hatoweza kukaa na Mimi , siwezi kuishi na mtoto mkorofi mimi nitakuja kumuua bure nipate kesi aliongea kwa vitisho yule mgeni.

Na kama ilivyo kawaida kwa wengi waishio mjini wakipewa hata heshima wasiyostahili basi kaka yake na mzee Mgaya aliogopeka sana na familia ile ukijumlisha na stori zake za kusema alipigana Hadi vita vya Uganda na Kagera basi alitisha sana wakati nyuma ya pazia Wala hakuwa mwanajeshi kamili ila alikuwa sehemu ya jeshi la akiba akitolewa huko kwenye shirika fulani na reli.

Je, atamuacha kweli Samson au atamchukua?

Ni wapi milango mafanikio halisi ya Samson itafunguka?

Usikose sehemu ijayo. .....
 
SEHEMU YA KUMI NA MOJA

Kulikuwa na utulivu fulani kwenye familia ya mzee Mgaya, si baba Wala mama Wala mtoto yeyote Kila mtu alikuwa kimya sana akiwaza jambo lake wakati huo mgeni wait alikuwa kwenye chumba alichopewa akibadilisha nguo.

Hapa naona ni vyema nikawasalimia na ndugu wengine, maana ni miaka mingi jamani, naona na maendeleo do haba watu wanazidi kuelimika.
aliongea kaka yake na mzee Mgaya, huku akitupa macho huku na huku akiangalia baadhi ya vibanda na nyumba anazozifahamu zikiwa zimewekwa bati badala ya makuti, Lakini pia vijana wadogo wadogo ndio walionekana kuleta chachu ya maendeleo ya Kijiji kile kwani Kila kijana alimiliki kibanda Cha bati.

Kaka mtu alifurahishwa na hatua ile wakamuaga mama Mgaya wakawa wanaenda nyumba Hadi nyumba hasa kwa wale ndugu wahusika wakisalimia.

Nafasi hii ilikuwa nzuri kwa mama Mgaya kuongea na mwanae Samson.

Pole mwanangu najua umetukosea sana wazazi wako, Lakini kitendo alichofanya Huyu shemeji yangu Mimi sijakipenda hata kidogo, yeye anaweza kuwa na uchungu na wewe kuliko sisi wazazi wako,
Kifupi kaniudhi basi tu, hebu nambie Sam hivi ulijisikiaje ulivyotoroka , na ungejisikiaje kama ningekufa au hata baba yako angepoteza maisha kwa ujinga wako, unadhani ingekuwa hasara ya nani. alilaumu Mama Mgaya.

Kwanza samahani mama yangu pili naomba wote familia nzima mnisamehe tu, magumu niliyokutana nayo huko sitarudia tena kwenda sehemu ambayo siijui inafananaje, kama mama mngekuwa na uwezo Bora hata ningeendelea na shule tu, nimejaribu kuchunguza nimeona kama maisha ya nilikokuwa ni Bora hapa nyumbani. aliongea Samson kwa hisia Kali huku mama yake akimwelewa vizuri sana.

Sasa nimeelewa kuwa unajuta, na kitendo Cha kuitamani shule kimenifurahisha na kunifariji mno, hivyo Siyo mbaya nafasi tunayo.

Nafasi Gani Tena mama?
Samson alimkatisha mama yake akishindwa kujua ni nafasi ipi hiyo wakati hali halisi ya pale kwao inajulikana.

Nafasi pekee ni kumtumia Huyu baba yako mkubwa, tena yeye mwenzetu ana uwezo mkubwa sana huku mjini Dar es salaam ana nyumba mbili kama ulivyosikia akimwambia baba yako lakini pia ana kazi nzuri inayomfanya apate pesa nyingi sana. na ukisikia nyumba ya mjini Siyo kama hii ya kwetu hii si nyumba mwanangu hiki ni kibanda , nyumba za huko ni kubwa sana. aliongeza mama Mgaya na kufanya wanae wote washangae tu.

Kwahiyo majumba yote mawili na mnasema ni makubwa anakaaje? aliuliza Jane Binti yao mkubwa.

Hapana hizo nyumba siyo kwamba kajenga sehemu Moja hapana kajenga sehemu tofauti yaani nyingine wanakaa wapangaji.
Mama Mgaya alizidi kuwasimulia wanae huku akiwafahamisha zaidi maana ya wapangaji na nyumba ya kupangisha.

Kwahiyo baba mkubwa ni tajiri eeh? aliuliza Samson maana vitu anavyomiliki huyo baba yake mkubwa vilimshangaza sana.

(Huku akicheka)hapana wanangu, ni kwamba ana maisha mazuri tu na anaweza kutusaidia hata baadhi ya watu kama sisi lakini yeye hawezi kuwa tajiri , utajiri una maana nyingine kubwa sana wanangu , alizidi kuwatoa tongotongo wanaye.

Sasa mama nimekusikia unasema baba mkubwa ana uwezo wa kumsomesha Samson, sawa.
Lakini Mimi namuona mkali mno huoni alivyompiga kaka Sam hapa, anaweza kuishi na mtu yule kweli mbona Mimi namuogopa sana.

Hapana ujue ndiyo mjifunze kuwa na adabu, heshima na uaminifu Leo na kesho sisi wazazi wenu tunaweza kuaga Dunia wanangu,
Hivyo lazima mjifunze kuishi kwa unyenyekevu na hii itasaidia kuweza kuishi na walimwengu.

Stori zilikuwa ni nyingi Kati ya mama Mgaya na watoto wake, lakini pia Samson licha ya kupigwa na baba yake mkubwa, bado alipanga kumweleza ukweli namna anavyoipenda shule, na kama kungekuwa na namna ya kusaidiwa basi iwe hivyo, kitendo Cha kusimangwa na wahuni wa kule kuwa umri wake hauendani na shughuli zile.

Huku wakimshauri kuwa kama ana wazazi basi awashawishi wampeleke shule, neno shule lilinasa kwenye antenna za kichwa Cha Samson. tofauti na kutoipenda shule akiwa shuleni kipindi yupo shule ya msingi akitamani ahitimu shule aendelee na kutafuta maisha, safari hii aliipenda shule maana alishaonja joto la maisha na msako wa maisha, aliona badala ya kutafuta maisha, maisha yakawa yanamtafuta yeye.

Mwezi ule wa kumi na mbili karibu kabisa na sikukuu za kuzaliwa kwa kiristo zikiwadia ulikuwa ni mwezi wa wa watu wenye uwezo kwenda hadi wilayani kuchungulia matokea ya watoto wao, hili lisingeweza kufanyika kwa baba yake na Samson maana uwezo wao kiuchumi ulijulikana.

Mzee Mgaya na kaka yake ambaye alionekana mtu mwenye hela kutokana na mwili wake mkubwa wastani lakini pia kaunda suit yake nyeusi na jinsi alivyochana nywele zake baadhi ya wanakijiji wasiomtambua vyema walimhofia wakaona isije kuwa ni moja ya viongozi wakubwa kwenye nchi hii.

Walirudi wakapata Chakula huku wakitoka tena, safari hii wakielekea kwa fundi mmoja aliyechimba msingi kwenye nyumba ya mzee Mgaya wakitaka wakampe maelekezo ili aje arekebishe maana kaka yake na mzee Mgaya aliona ile nyumba ni ndogo mno akataka ramani mpya.

Samson aliogopa kuongea na baba yake mkubwa uso kwa uso kutimiza hitaji lake akaamua kuchukua makaratasi yake ya mitihani hasa Yale ambayo alikuwa na wastani mzuri akayabandika ukutani yakiwa mchanganyiko ya darasa la nne, tano hadi la saba. Hakika matokeo yale yalipendeza na yalishawishi, akazidi kubandika , mama yake aligundua lengo la Samson akamhurumia sana hakumzuia, lakini pia hata yeye hangeweza kumface shemeji yake akiomba amsomeshe mwanaye,
Aibu ilimtawala.


Itaendelea......................
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…