Sehemu ya 54
Tulikaa kwa robo saa kisha alitoka kijana aliyekuwa amevaa rubega la kaniki na kuzungumza maneno ambayo yalikuwa kama ya Kimakonde huku akiashilia kutuita.
Sikusimama nilimsikiliza mkalimani wangu ili kujua yule kijana anasema nini.
“Tunaitwa ndani,” mkalimani wangu alinieleza huku akinyanyuka.
Nilimfuata hadi ndani ya kilinge na kukaribishwa kwenye ngozi ya chui, tulikaa mbele yetu kulimkuta mzee aliyekuwa amekula chumvi. Kichwa na ndevu zake zilikuwa nyeupe.
Baada ya kukaa alisema neno ambalo sikulielewa, nilimtazama mkalimani wangu ambaye aliuniliuza.
“Anauliza tunatoka wapi? Nimwambie?”
Kabla sijajibu mganga alizungumza kwa lugha ya kiswahili iliyotushtua wote.
“Mnatoka Tanzania?”
“Ndiyo,” nilijibu.
“Karibuni.”
“Asante.”
Mganga alibadili lugha tukawa tunazungumza kiswahili.
“Mna shida gani?”
Nilimwelezea sababu ya mimi kufunga safari toka nyumbani Tanzania mpaka pale. Baada ya kunisililiza alitoka nje na kuchukuma tawi la mnyaa na kuja nao ndani. Kisha alikaa kwenye ngozi ambayo sikujua ya mnyama gani.
Baada ya kukaa alinipa tawi la mnyaa na kunieleza ninuie yote yanayonisibu.
Kwa vile nilikuwa nimeisha kuwa mzoefu, nilipokea na kunuia, niliyasema yote yanayonisibu.
Baada ya kunuia nilimpa tawi la mnyaa alilichukua na kulibana na mdomo kisha aliziba masikio yake kwa mikono yake na kufumba macho na kutulia bila kupumua kwa muda kisha alipumua kwa kasi na kurudia kubana tena pumzi.
Kwangu yalikuwa maajabu kwani alitulia zaidi ya dakika tatu bila kupumua kitu kilichoniogopesha na kuona mapya. Baada ya muda alitoa mikono masikioni na kubakiza tawi la mnyaa mdomoni na kuwa kama anazungumza na mtu kwa kutikisa kichwa kama kukataa wakati mwingine anakubali kwa kunyanyua kichwa juu.
Alifanya vile kwa zaidi ya robo saa kisha aliutema ule mnyaa na kuuweka kwenye ungo mdogo ulikuwa mbele yake na kusema:
“Kijana umetoka mbali kwa ajili ya mapenzi, kweli?”
“Kweli?”
“Umeua watu wa ajili ya mapenzi, kweli?”
“Mmh! Kweli,” nilisita kidogo lakini kwa vile jambo lilikuwa wazi nilishindwa kukataa. “Umepoteza mzazi na mtoto wa ajili ya mapenzi, ni kweli?” yote aliniuliza bila kunitaza macho yake yaliangalia kwenye ungo.
“Ni kweli.”
“Na safari yako ya kuja hata kusudio lako kubwa kuua, ni kweli?”
“Ni kweli.”
“Unataka uue watu wangapi?”
“Kivipi?” swali lake sikulielewa.
“Nakuuliza unata uue watu wangapi maana mpaka sasa umeua wanne?”
“Wanne?” nilishtuka kusikia nimeua wanne wakati najua wawili.
“Jibu kwanza, unataka kuua wangapi?” Mganga muda wote aliniuliza bila kunitazama.
“Kwa vile wameniulia familia yangu lazima na wao wabakie jina tu,”
“Nani kamuua baba na mtoto wako?”
“Kuna kijana mmoja alitembea na mke wangu, mimi sikukubali nikaamua kulipa kisasi.”
“Kisasi kipi?”
“Nilimuulia mbali.”
“Baada ya hapo?”
“Nasikia familia yake iliponiendea kona zote za dunia kutaka kuniua, waliponishindwa wakaamua kuimaliza familia yangu na kuua baba na mwanangu wa mwisho.”
“Baada ya hapo?”
“Nilikwenda kwa mtaalamu na kunisaidia kuzuia ndizi zilizoiva ili zisidondoke, lakini bahati mbaya moja ilikuwa imeisha dondoka. Mama na mke wangu walikuwa wafe kwa mpigo kwa msaada wako walipona.”
“Unajua kilichoiva kikikaa muda mrefu kinakuwaje?”
“Kinaoza.”
“Basi hawajafanya lolote kwa vile ndizi walizozizuia kuanguka muda si mrefu zitaanza kuoza.”
“Na zikioza?” niliuliza kwa mshtuko.
“Zitatoa wadudu.”
“Kwa hiyo?”
“Ile ilikuwa sawa na mgonjwa wa kichwa kumeza dawa ya maumivu, lazima baada ya muda maumivu yapo palepale. Kwa hiyo kifo cha pamoja kipo palepale.”
“Mungu kwangu, nitafanyaje?” niliuliza mikono kichwani.
“Nitakusaidia kuyaondoa maisha yao kwenye ndizi na kuyarudisha katika hali ya kawaida.”
“Nitashukuru sana mzee wangu, lazima niwamalize wote.”
“Ukiwamaliza wote pamoja na familia yako na wewe mwenyewe.”
“Kwa nini?”
“Unajua nani aliyeua familia yako?”
“Mzee si nimekueleza ndugu ya jirani yangu.”
“Hapana, wao hawahusiki,” jibu la mganga lilinishtua.
“Nani sasa muuaji?”
“Wewe mwenyewe.”
“Mimi?” nilishtuka kusikia vile.
“Ndiyo, hapa inaonesha wewe ndiye muhusika wa vifo vyote, kuanzia mgoni wako wa kwanza mpaka mzazi wako na mwanao.”
“Mzee! Mimi?” nilizidi kushtuka na kushanga.
“Ndiyo.”
“Mzee mimi nitauaje familia yangu kisha nije huku kutafuta msaada?”
“Kumbuka bila wewe kuanza kuua usinge poteza baba na mwanao.”
“Sasa ningefanyaje kama mtu katembea na mke wangu?”
“Zipo njia nyingi za kutatua tatizo si kuua, waganga wengi wamekuwa na tamaa ya fedha kuliko kutatua tatizo. Uliua ukiamini ndiyo suruhu ya tatizo lako lakini bado mkeo aliendelea na tabia zake chafu.Umeua tena kibao kimekugeukia mwenyewe.
“Nataka kukueleza uchawi wa kisasi una nguvu sana, hata kama nitaiteketeza familia yake, bado kuna watu wangebakia na kwenda pande za dunia, lazima wangekubaliza tu, uchawi unazidiana.”
“Sasa nifanyeje?” nilijikuta nikihamishwa kwenye dhamira yangu.
“Sikiliza siku zote vita huwa haina kikomo, pia uganga unazidiana naweza kusema mimi ni zaidi kuna mwingine akawa zaidi yangu na kuweza kukuteketeza kama pamba na moto.”
“Nimekuelewa, sasa nifanyeje mzee wangu?”
“Jiepushe kuchukua uamuzi mkubwa kila wakati bila kujua madhara yake, kama unaweza kuua basi kuna wengine wanaweza kukuua.
Mfano watu hao wangekuja kwangu kulipa kisasi cha kuuliwa ndugu yao umebakia jina. Lakini siku hizi waganga tumekuwa tuna tamaa na kuwasilikiza wateja bila kuangalia mbele atapatwa na nini. Wengine wanajua kabisa alichokufanyia ni bomu litakalokuypasukia mbele lakini kwa vile wana tamaa ya fedha wanafanya tu na kukuachia likulipukie.
Kama mwanamke hatulii mbona zipo dawa nyingi tu za kumfanya atulie. Kwa nini mkimbilie kuua?
Sawa niwaue wabaya yako, umerudi nyumbani mkeo kafanya ujinga wake utaua wangapi?”
“Mzee wangu yaani hata sijui nahitaji msaada wako,” nilijikuta nikizidi changanyikiwa nilijiuliza yule kweli mganga au ndiyo yamemshinda akaamua kunitisha. Lakini kwa upande mwingine nilikubaliana naye hakuwa tofauti na alivyo nishauri Simon.
“Kijana wangu nataka nikuase na waganga wenzangu, tujiepusheni kutoa roho ya kiumbe ovyo. Kulipa kisasi sawa, lakini hata chuki tu za kibinadamu. Mganga mzuri ni yule anayekushauri madhara ya kitu unachotaka kufanya.
“Mfano tatizo kama lako lililojirudia mara mbili bado wanaua watu. Hii ndiyo sababu hata dini zinaona kuwa waganga wa jadi ni chukizo la Mungu kwa waganga wenye tamaa na wasio zingatia taaluma.
Wamejisahau na kuendekeza tamaa kumbe kazi yetu kutibu na si kuua ovyo. Najua utashangaa mganga kama mimi kukataa kuua?”
“Hapana mzee najua nimefanya makosa naomba msaada wako,” maneno ya mganga yalinibadili na kujiona nimefanya makosa makubwa kutoa roho za watu kwa ajili ya mwanamke. Nijifikiria kama ningesikiliza rafiki yangu Simon nisingempoteza baba na mwanangu.
“Sasa hivi umeishakuwa mchawi, najua kwa dhamira yako upo tayari hata kula nyama ya mtu ili kumfurahisha mkeo. Hivi uliposikia mtu uliyemroga amekufa ulijisikiaje?”
“Kwa kweli mzee naomba unisaidie, maneno yako yamenichanganya sana hata sijui nijibu nini, moyo unaniuma sana kwa yote niliyoyatenda.”
“Sishindwi kukufanyia unachotaka, lakini mbele kuna vita kubwa ambayo itakufanya ufe kifo cha aibu. Baada ya kifo cha mwisho cha mwanao, ni baada ya kumzika mama yako na mkeo, ungekuwa chizi na usingepona kwa mganga yoyote mpaka unakufa kifo cha aibu.”
“Mungu wangu!” nilizidi kuchanganyikiwa.
“Usiseme Mungu wangu! Kuna watu katika familia ile hawafi cha mzizi wala kafara mpaka kudra ya Mungu. Lazima nao baada ya tukio la kupukutika kwa familia yao, wangepita juu chini kukumaliza. Siku zote vita haina udogo.”
“Nimekusikia mzee wangu, nifanyeje sasa?”
“Kijana wangu, sawa unampenda mkeo, tatua tatizo la mkeo si kukimbilia kuua, kama nilivyo kueleza zipo dawa nyingi na moja nitakupa hutaamini, kama mkeo akitembea tena nje njoo uvunje mikoba yangu.
“Kama haya ninayo kwambia unaona nakudanganya, nenda popote kwa mganga makini utakuta wewe ndiye uliyemuua baba yako na mwanao.
“Waganga wengi tumekuwa tunaangalia tatizo bila kuangalia chanzo cha tatizo. Matokea yake wamekuwa wanakimbilia kuua tu.
Kama ungekuwa umeonewa kweli, ningekufanyia kazi ambayo hakuna yeyote angeingiza mkono kila mtu asingekuona. Ningetengeneza kiza ambacho wangekwenda mashariki na magharibi wasingeona kitu.”
“Mzee wangu nimekusikiliza vizuri na nimekuelewa, utanisaidia vipi?”
“Nitakusaidia kuyaondoa maisha wa mama na mkeo katika ndizi kisha nitakupa dawa ya kumtuliza mkeo.
Nina imani ukiondoka hapa utatulia na mpenzi wako najua unampenda basi tatizo limekwisha ila jiepushe kupenda kuua damu ya watu nyingine ni nuksi unaweza kuandamwa na matatizo kila mganga halioni kwa vile aliyetenda kesha kufa.”
“Mzee wangu nakuapia kwa Mungu sitarudia tena nikitoka hapa nakuwa kiumbe kipya.”
“Wapo waganga wanasifika kwa kuua lakini, mimi nasifika kwa kutibu yakiwemo matatizo kama yako.”
“Nashukuru mzee wangu, nimejifunza kitu. Naamini nitakuwa mwalimu mwema kwa wengine.”
“Fanya hivyo ili tupunguze mauaji yasiyo na sababu, kazi ya Mungu tumuachie Mungu, toka nianze uganga sijawahi kuua na sitaua.”
Baada ya makubaliano mganga alituomba tukapumzike nje ili kusuburi muda wa kufanya kazi yangu. Tulitoka kwenda kukaa sehemu ambako tuliletewa maziwa na viazi vya kuchemsha.
Kwa vile tulikuwa hatujala toka asubuhi tulishambulia chakula chote. Baada ya chakula tulioneshwa sehemu ya kupumzika kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Kutokana na uchovu wa safari tulilala mpaka siku ya pili.
USIKOSE SEHEMU YA MWISHO ITAKAYOKUJIA KESHO.