Simulizi: Makaburi ya wasio na hatia

Simulizi: Makaburi ya wasio na hatia

SEHEMU YA 59


ILIPOISHIA:
Kilichotokea baada ya kufanya hivyo kwa mara ya tatu, kilinifanya nihisi kama mwili wangu unakufa ganzi kwa hofu, sijawahi kushikwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kama baba asingeniwahi, huenda ningedondoka kama mzigo chini maana mwili wote uliisha nguvu.
Japokuwa ilikuwa ni usiku, tena nikiwa sina nguo na kulikuwa na baridi kali, nilihisi kijasho chembamba kikinitoka, ama kweli duniani kuna mambo na ukishangaa ya Musa, utayaona ya Firauni.
SASA ENDELEA...
Kitendo cha kufuata maelekezo yale tu, mara kaburi lilifunuka lote, yaani ule udongo wote uliokuwa umetumika kulifukia, ukapotea kiasi kwamba kila kitu kilichokuwa ndani ya kaburi kilikuwa kikionekana.
“Ingia tukasaidiane kumtoa kwenye jeneza,” alisema baba, nikajikuta nguvu za kuendelea kusimama zimeniisha maana miguu ilikuwa ikitetemeka kuliko kawaida, nikakaa kwenye kaburi lililokuwa pembeni, uso wote ukiwa umelowa kwa machozi.
Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini baba alikuwa akiniambia kwamba bado sijakomaa kiakili na sitakiwi kuingizwa kwenye hayo mambo.
“Inuka acha kuleta mambo ya kijinga hapa, upumbavu wako ndiyo uliotufikisha hapa,” alisema baba kwa ukali, nikajikakamua na kusimama huku nikiwa bado natetemeka. Alichokifanya baba baada ya kuona kama nasuasua, alinisukumia ndani ya lile kaburi, nikaporomoka na kwenda kujibamiza kwenye jeneza.
Nilijikuta nikipiga kelele kwa sauti kubwa huku nikitafuta sehemu ya kutokea, kwa kuwa ilikuwa ni ndani ya shimo kelele zangu hata hazikufika mbali, zikawa zinajirudia na kusababishwa mwangwi. Tayari baba naye alishaingia mle kaburini, akaninyamazisha kwa ukali kama kawaida yake.
“Wewe ndiyo unatakiwa uifanye hii kazi, mimi nakusaidia tu,” alisema huku akihangaika kulifungua jeneza lililokuwa na ule mwili.
Nisingependa sana kueleza kuhusu kipengele hiki kwa sababu hata mwenyewe nikikumbuka huwa naogopa sana, lakini kwa kifupi, nilisaidiana na baba kuutoa ule mwili kwenye jeneza, sanda yote ikiwa imelowa damu hasa maeneo ya kichwani inakoonesha marehemu aliumia sana kwenye ile ajali.
Tukautoa na kuulaza pembeni ya kaburi huku lile jeneza baba akilirudishia kama lilivyokuwa mwanzo. Huku nikitetemeka kuliko kawaida, baba aliniamuru tena kufanya kama nilivyofanya mwanzo, nikafanya mara ya kwanza, ya pili, kisha nikafanya mara ya tatu.
Cha ajabu kaburi lilijifukia vilevile na kurudi kama lilivyokuwa mwanzo, tofauti yake ni kwamba kidogo lilikuwa limetitia. Ni hapo ndipo nilipoamini kauli niliyokuwa nikiisikia kwa muda mrefu, kwamba ukiona kaburi jipya limetitia sana, kuna uwezekano mkubwa kwamba kilichozikwa ndani siyo mtu au kama ni maiti, basi imechukuliwa na wachawi.
Baada ya zoezi hilo kukamilika, baba aliniamuru niibebe ile maiti huku baba yake Rahma akinitoa hofu kwamba mtu akishakufa hana madhara yoyote, hawezi kunidhuru kwa namna yoyote, nikajikakamua na kuiweka begani, tukaanza kuondoka makaburini hapo huku ikichuruzika vitu ambavyo hata bila kutazama nilijua ni damu.
Unajua baadaye nilikuja kujifunza kitu kingine, kwamba watu wanaofariki katika mazingira ya kishirikina, unaweza kutambua maiti zao kwa haraka kama na wewe una uelewa kuhusu mambo hayo, kwa sababu kwanza imezoeleka kwamba mtu akifa mwili wake hupoa na kuwa wa baridi sana lakini kama amekufa kwa mipango ya watu, mwili huendelea kuwa na joto kwa muda mrefu.
Pia maiti za namna hii zinakuwa na kawaida ya kutoka damu. Inafahamika kwamba mtu akifa, moyo unakuwa umeacha kusukuma damu kwa hiyo hata mzunguko mzima wa damu nao unasimama lakini kwa watu waliochukuliwa kabla ya muda wao, japo kwa nje anaonekana amekufa, bado mzunguko wa damu unakuwa unaendelea japo kwa kasi ndogo sana na ndiyo maana, utakuta maiti inatoka damu puani, mdomoni, masikioni au kama ni ya ajali kama hiyo, majeraha yanakuwa yanaendelea kuchuruzika damu.
Tulitoka huku nikijikaza kiume na ule mwili begani kwa sababu ulikuwa mzito sana lakini kwa kuwa na mimi kidogo nilikuwa na ubavu, niliweza kuhimili uzito huo mpaka kwenye mti mkubwa uliokuwa pembeni ya makaburi hayo, kama kawaida, maandalizi ya safari yakaanza kufanyika ambapo baba aliniambia niulaze ule mwili chini.
Mchakato ulifanyika na kama kawaida, muda mfupi baadaye, akili ilinitoka, nilipokuja kuzinduka, tulikuwa tayari kwenye lile eneo letu tunalokutania, watu wengi wakiwa wamezunguka na kutengeneza duara kama kawaida huku nyimbo za ajabuajabu zikiendelea kuimbwa na kuifanya hali iwe ya kutisha sana.
“Mkuu akikusogelea, inabidi uinamishe kichwa chako chini na kuweka mikono hivi maana umefanya makosa,” baba aliniambia kwa sauti ya chini, akinielekeza nini cha kufanya. Kwa mbali nikawa namuona Mkuu akija huku kama kawaida yake, vishindo vyake vikisikika eneo lote hilo.
Baba na baba Rahma walimsogelea na kuinamisha vichwa vyao kwa utii, akawa anawagusa na mkia wa mnyama ambaye simjui, aliokuwa ameushika, harakaharaka wakaondoka na kwenda kukaa kule walikokuwa wamekaa wale watu wengine.
Mkuu akanisogelea mpaka pale nilipokuwa nimepiga magoti huku uso wake akiwa ameukunja, nilipomtazama mara moja sikurudia tena kumtazama kwa sababu alikuwa anatisha sana. Nilizoea kumtazama akiwa hajakasirika lakini siku hiyo alikuwa kama mnyama mkali wa porini kwa jinsi alivyokuwa anatisha, midomo ikimchezacheza kwa hasira.
Ilibidi niinamishe kichwa kama baba alivyonifundisha, mikono nikaiweka kifuani kwa unyenyekevu, aliendelea kunitazama bila kusema chochote kwa sekunde kadhaa kisha nikasikia akinipigapiga na ule mkia.
“Sirudie masiku mengine,” alisema Mkuu kwa Kiswahili kibovu huku akiendelea kunipigapiga, kidogo kamoyo kalitulia ila nilichojifunza ni kwamba kumbe nilikuwa nimefanya kosa kubwa sana na pengine bila kufanya kile tulichokifanya kwa msaada wa baba na baba yake Rahma, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu.
Kumbe ndiyo maana ni rahisi sana kusikia wachawi wamekufa ghafla vifo vya kutatanisha, wakati mwingine inakuwa ni kukosea masharti kama kilichotaka kunitokea mimi na adhabu inayomfaa mtu anayekiuka masharti, ni kuuawa na kuliwa nyama, kama siyo yeye basi mtu wake wa karibu.
Baada ya kupitisha msamaha kwangu, niliinua uso wangu, mkuu akaugeukia ule mzigo niliokuwa nao ambapo kwa kutumia kisu kikali alikata ile sanda kisha akanigeukia na kutingisha kichwa, akainua ule mkia wake juu na watu wote wakapaza sauti zao kutamka maneno ambayo hata sikuwa nayaelewa.
Basi kilichoendelea hapo ni utaratibu wa kawaida, watu wakala na kucheza ngoma huku mara kwa mara Mkuu akinikata jicho kama anayenichunga kuhakikisha siharibu kitu kingine.
“Amefurahishwa na kazi uliyoifanya, amesema anataka kukuongeza nguvu maana japikuwa umefanya makosa, lakini kupitia makosa hayo umeweza kuonesha ushujaa ambao wengine huwa wanashindwa, mshukuru sana baba yako,” baba Rahma aliniambia kwa sauti ya chini, nikageuka kumtazama Mkuu, macho yake na yangu yakagongana, nikamuona akiachia tabasamu hafifu.
“Akikupa nafasi ya kuchagua akuongezee uwezo gani utachagua nini?”
“Nataka niwe na uwezo wa kupata hela kirahisi, nataka kuwa tajiri.”
“Tajiri? Utajiri wa kichawi ni mbaya sana, jaribu uone mwenyewe, bora hata uombe kitu kingine chochote,” alisema baba yake Rahma lakini maneno yake wala hayakuwa yakiniingia akilini. Kiukweli na mimi nilikuwa natamani kuwa tajiri kwa sababu tangu nizaliwe, maisha yetu yalikuwa ya kimaskini kule kijijini na umuhimu hasa wa kuwa tajiri, niliuona baada ya kufika mjini.
Vijana wadogo tu kama mimi, wengine hata nawazidi lakini wanaendesha magari ya kifahari barabarani, kwa nini na mimi nisionje kidogo hata kama ni mbaya? Wakati akiendelea kunipa nasaha zake, Mkuu alinipa ishara kwamba nimfuate, harakaharaka nikainuka na kumuacha baba yake Rahma akiendelea kuongea.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
SEHEMU YA 60


ILIPOISHIA:
Vijana wadogo tu kama mimi, wengine hata nawazidi lakini wanaendesha magari ya kifahari barabarani, kwa nini na mimi nisionje kidogo hata kama ni mbaya? Wakati akiendelea kunipa nasaha zake, Mkuu alinipa ishara kwamba nimfuate, harakaharaka nikainuka na kumuacha baba yake Rahma akiendelea kuongea.
SASA ENDELEA...
Alinishika mkono na kusogea pembeni na mimi, mawasiliano kati yetu kidogo yalikuwa magumu kwa sababu alikuwa akiongea maneno ya Kiswahili machache, tena yaliyopindapinda lakini muda mwingi alikuwa akizungumza lugha ambayo siielewi.
Katika yale machache niliyomuelewa, alionesha kufurahishwa na ujasiri wangu, na kuniambia kwamba japokuwa ndiyo kwanza nilikuwa nimejiunga, nilikuwa na kasi nzuri ya kujifunza. Kama alivyoniambia baba yake Rahma, kweli Mkuu aliniuliza ni zawadi gani akinipa nitafurahi?
Sikupepesa macho wala kumung’unya maneno, nikamwambia kwamba nataka dawa za kunifanya niwe tajiri. Alicheka sana, mapengo yake yakawa yanaonekana, ni hapo ndipo nikagundua kwamba kumbe naye huwa anacheka na kufurahi, ingawa sikuelewa nini hasa kilichomfurahisha.
Aliniambia kitu nilichokichagua ni kikubwa sana kuliko uwezo wangu, akaniambia atanipa dawa lakini haitakuwa ya kupata utajiri mkubwa kwa sababu utajiri una masharti magumu na nikipata pesa nikiwa bado mdogo, naweza kufa siku si zangu.
Tulirudi pale katikati alipokuwa ameweka vifaa vyake, akatoa kimkoba chake cha ngozi na kutoa kichupa kilichokuwa na dawa, akatoa na wembe kisha akaniambia nimfuate. Tulitoka pale na kupotelea vichakani kwenye giza, nikiwa namfuata nyumanyuma.
Tulitokezea kwenye eneo ambalo lina uwazi, akanielekeza kwa ishara kwamba nivue shati kisha nikae chini na kukunja miguu, kweli nilifanya hivyo, akanishika kichwani na kuanza kuzungumza maneno nisiyoyaelewa, akayaongea kwa muda mrefu kisha akachukua ule wembe na kuanza kunichanja chale kuanzia kwenye utosi kurudi mgongoni.
Aliponipaka ile dawa, nilisikia maumivu makali sana lakini nikajikaza kisabuni, alipomaliza, aliniambia nitulie hivyohivyo, akapotelea vichakani. Muda mfupi baadaye, aliibuka kutoka vichakani akiwa amembeba nyoka mkubwa, nikashtuka sana na kutaka kusimama nitimue mbio lakini akanionesha ishara kwamba nitulie.
Huku nikitetemeka kuliko kawaida, alimsogeza yule nyoka mkubwa kwenye zile chale, akawa anamlambisha damu zangu huku akiendelea kuzungumza maneno nisiyoyaelewa. Alipomaliza, aliamuachia, yule nyoka akatambaa kwa kasi na kupotelea vichakani.
Mshangao niliokuwa nao, ulikuwa hauelezeki. Akanipa ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo na kuvaa shati langu kisha tukarudi kule walipokuwa wenzetu, akaniambia kwamba baada ya siku saba dawa itaanza kufanya kazi lakini natakiwa kuwa naenda kutoa sadaka kwa yule nyoka mara kwa mara.
Baba alikuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea na Mkuu alipomaliza tu kuzungumza na mimi, harakaharaka baba alinifuata. Ile furaha yote niliyokuwa nayo ndani ya moyo wangu ilitibuka kwani baba alipofika tu, alianza kunifokea kwa sauti ya chinichini na kuniambia kwamba nilichokifanya ni upumbavu wa hali ya juu na yeye hatahusika na chochote kitakachonipata nitakapokosea masharti.
“Masharti gani tena baba?” nilimuuliza kwa mshangao kwa sababu Mkuu hakuwa amenipa masharti yoyote, akaniambia kwamba siyo kwamba yeye hatamani utajiri lakini masharti yake yalivyo magumu, ndiyo maana wengi walikuwa wanaona ni bora waendelee kuishi kimaskini tu.
“Kama hajakwambia basi mimi nakwambia, kuna masharti magumu sana tena usipokuwa makini unaweza kusababisha hata sisi wazazi wako na ndugu zako wa tumbo moja wakawa kwenye hatari kubwa sana, kwa nini hukuuliza kabla?” baba aliendelea kuniwakia kwa sauti ya chini huku mara kwa mara akigeuka na kumtazama Mkuu. Nadhani alikuwa hataki asikie chochote.
Maelezo aliyonipa baba yaliniogopesha sana, japokuwa hakuwa amenifafanulia, ilivyoonesha kulikuwa na masharti magumu kwa sababu hata mimi siku nyingi nilikuwa najiuliza, kwamba kwa nini unakuta mganga anasaidia watu kupata utajiri kwa njia za kishirikina wakati yeye anaishi kwenye kijumba cha nyasi?
Nilikuwa pia najiuliza kwa nini wachawi wengi wanakuwa na maisha ya dhiki sana? Nilitamani kuyajua hayo masharti kwa sababu kama ni maji, yalishamwagika. Baba aliniambia hawezi kuniambia, kama nataka nirudi kwa Mkuu kwenda kumuuliza.
Ile furaha yote niliyokuwa nayo moyoni iliyeyuka, kurudi kwa Mkuu kumuuliza nikashindwa kwani muda nao ulikuwa umeenda sana. Nikiwa bado nimetulilia nikitafakari, yule msichana, Isrina alinifuata, hata sijui alitokea wapi, nilishtukia tu yupo pembeni yangu.
“Hongera,” alisema huku akinipa mkono, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, nilimpa mkono lakini sikuwa nimechangamka.
“Mbona siku hizi huna taimu na mimi? Kuna jambo nimekuudhi?” aliniuliza, nikatingishwa kichwa kukataa lakini ukweli ni kwamba nilikuwa na kinyongo kikali sana dhidi yake.
“Basi nitakutafuta tuzungumze, nakuomba ukubali,” alisema huku akiinuka, nikatingisha kichwa kwa sababu nilikuwa nataka aondoke haraka.
Mpaka muda wa kutawanyika unafika, bado nilikuwa sielewi nini itakuwa hatma yangu na nifanye nini kwa wakati huo. Tulirudi nyumbani kama kawaida ambapo nilijipa muda wa kutafakari mambo yote yaliyotokea kwa siku hiyo maana kiukweli kwenye ulimwengu wa giza, dunia inakwenda kasi sana kuliko unavyoweza kudhani. Kutokana na uchovu niliokuwa nao, nilipitiwa na usingizi mzito, nikiwa na maswali mengi ndani ya kichwa changu ambayo yote hayakuwa na majibu.
Kesho yake nilichelewa sana kuamka kwa sababu ya uchovu, nilipoamka, majira kama ya saa nne hivi, nilimfuata baba yake Rahma nikitaka ufafanuzi zaidi. Tulizungumza mambo mengi lakini kubwa aliniambia utajiri wa kishirikina, huwa unahitaji makafara ya damu mara kwa mara.
Akaniambia kwamba bahati mbaya ni kwamba, sina uwezo wa kuchagua nani atolewe kafara muda wa kufanya hivyo unapofika bali nitakuwa nachaguliwa, kwa hiyo natakiwa kuwa makini sana.
Maelezo hayo yalinitisha sana, nikawa najaribu kuunganisha matukio, ni kweli watu wenye utajiri wa kishirikina, huwa wanasumbuliwa sana na kashfa ya kuwatoa kafara watoto wao, wazazi wao au watu wao wa karibu.
Nilijaribu kujitazama kwa upande wangu, nikawafikiria wazazi wangu na ndugu zangu tuliozaliwa nao tumbo moja, nikawa najiuliza kama siku nitatakiwa kumtoa yeyote kafara nitaweza kweli? Ulikuwa ni mtihani mgumu sana kwangu.
Ila aliniambia jambo ambalo kidogo lilinipa faraja, akaniambia kwamba makafara yanakuwa ni lazima pale utajiri unapokuwa mkubwa sana, lakini kwa mambo ya fedha ndogondogo hakuna ulazima wa kufanya kafara lolote.
Maelezo hayo yalinifurahisha sana ndani ya moyo wangu, nikawa nasubiri kwa hamu hizo siku saba ziishe nikapewe maelekezo ya nini cha kufanya. Nilichojiapiza ni kwamba sitataka utajiri mkubwa, fedha ndogondogo tu za kutesea mitaani zilikuwa zinanitosha sana, hasa ukizingatia kwamba sikuwa na majukumu ya moja kwa moja.
Wakati nikiendelea kusubiri hizo siku saba, niliona huo ndiyo muda muafaka wa kuanza kushughulikia suala la Rahma. Kama nilivyoeleza, kuna ukuta mkubwa ulikuwa umejengeka kati yetu, na kama nisingefanya jambo, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wetu, jambo ambalo lilikuwa likituumiza sana sote wawili, hasa Rahma.
Alikuwa hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu, sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi lakini nilishajipanga kumkabili.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue
 
SEHEMU YA 61



ILIPOISHIA:
Alikuwa hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu, sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi lakini nilishajipanga kumkabili.
SASA ENDELEA...
“Rahma!” nilimuita msichana huyo baada ya kukutana naye koridoni, mimi nikitoka bafuni kuoga na yeye akitoka chumbani kwake. Tofauti na siku zote ambazo alikuwa akinichangamkia sana anaponiona, wakati mwingine hata akinifuata chumbani kwangu, siku hiyo Rahma alikuwa tofauti kabisa, alipooza na alionesha kutotaka kuzungumza chochote na mimi.
“Rahma si nakuita jamani,” nilisema baada ya kumuona amenipa mgongo, akitembea haraka kuelekea sebuleni. Licha ya kutamka maneno hayo, bado hakutaka kusimama, ikabidi nitumia nguvu kumshika mkono na kumgeuza.

“Samahani nina mazungumzo na wewe, naomba unisikilize tafadhali,” nilimwambia kwa upole, akanitazama usoni, macho yake na yangu yakagongana, nikashtuka kumuona akilia.
“Unalia nini Rahma?” nilimuuliza lakini hakunijibu kitu zaidi ya kuendelea kunitazama kwa huzuni. Ilibidi nianze kumbembeleza lakini kwa kuwa tulikuwa tumesimama koridoni, niliona haiwezi kuwa picha nzuri kwani mtu yeyote angetuona tukibembelezana hapo angeweza kutufikiria vibaya.
“Naomba tutoke tukanywe japo soda pale dukani, nina mazungumzo ya muhimu sana na wewe,” nilimwambia Rahma, akatingisha kichwa bila kunijibu chochote kisha akarudi chumbani kwake.
Ilibidi na mimi nirudi chumbani kwangu, nikachukua nauli iliyokuwa imebaki siku nilipoenda Mlandizi na kuitia mfukoni, nikajiweka vizuri na kutoka nje. Nilizugazuga pale nje, nilipoona hakuna anayenifuatilia, nilifungua geti kubwa na kutoka nje. Ile kutoka tu, madereva Bajaj na bodaboda waliokuwa wanapaki pale nje, waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kuanza kunitazama.
Kibaya ni kwamba upande ule waliokuwa wakipaki, kwa mbele kidogo ndiyo kulikuwa na duka ambalo nilipanga tukae pale na Rahma kwa sababu kulikuwa na viti upande wa nyuma, kwa hiyo ilikuwa ni lazima niwapite palepale walipopaki.
Nimewahi kusikia matukio kadhaa ya madereva hao wa Bajaj na bodaboda kushirikiana kufanya uhalifu, hasa pale inapoonekana mmoja wao ameonewa, nikajua lazima watakuwa wamenipania kwa jinsi nilivyomsulubu mwenzao. Hata hivyo, kwa sababu nilikuwa na nguvu za giza, tena za kutosha kabisa, sikuogopa chochote, ndiyo kwanza nikawa napiga mluzi huku nikielekea kule walikokuwa.
Cha ajabu, nilishangaa kuona kila mmoja akikimbilia kwenye chombo chake na kukiwasha, wakaanza kuondoka mmoja baada ya mwingine wakikimbia kwa kasi, sekunde chache baadaye eneo lote likawa tupu.
Hakukuwa na mashaka kwamba walikuwa wakinikimbia mimi, kwa sababu hata kama wanawahi abiria, wasingeweza kuondoka wote kwa mkupuo, tena kwa kasi kubwa wengine wakinusurika kugongana wao kwa wao.
Sikuelewa nini kimetokea mpaka wawe wananiogopa kiasi hicho lakini sikuwajali maana na mimi nilikuwa na majanga yangu mengi kichwani. Nilienda mpaka pale dukani, nikamsalimia muuza duka ambaye aliponiona tu, alishtuka sana, akaitikia kwa woga.
“Naomba Fanta,” nilisema huku nikimeza mate kwani mara ya mwisho kunywa soda, ilikuwa ni siku ile tuliposafiri kuja jijini Dar es Salaam.”
“Hatuuzi soda hapa!” alisema yule muuzaji, kauli ambayo nilishindwa kuielewa ina maana gani. Juu ya meza kulikuwa na chupa tupu za soda kuonesha kwambamuda si mrefu kuna watu walikuwa wakinywa soda, na mara kadhaa nilipita pale na kuona watu wakipata vinywaji, kwa nini aniambie kwamba hawauzi soda?
Nikiwa bado nimeduwaa, nikishindwa nimuulizeje, mara Rahma aliwasili, kumbe hatukuwa tumeachana umbali mrefu, akamsalimia yule muuzaji. Alimuita kwa jina lake na ilionesha wanafahamiana.
“Kumbe anaitwa Vero,” nilijisemea moyoni, alikuwa mwanamke ambaye kwa kumkadiria alionesha kuwa bado mdogo lakini mwenye uso uliokomaa na kupoteza nuru kama walivyo wanawake wengi wa vijijini kama kule kwetu Chunya.
“Huyu ni kaka yangu, unamjua? Anaitwa Togo,” Rahma alisema huku akinishika begani, nikamuona yule mwanamke akijaribu kuvaa tabasamu la uongo usoni.
“Tuletee soda, Togo unakunywa nini?” alisema Rahma, yule mwanamke akawa anababaika, kama anayeshindwa ajibu nini maana mimi aliniambia hawauzi soda. Rahma alinishika mkono huku akionesha kabisa kwamba anailazimisha furaha, tukaenda mpaka kwenye viti na kukaa, tukawa tunatazamana huku tukisubiri yule mwanamke aje atuhutubie.
“Unataka kuniambia nini?” alisema Rahma huku akikwepesha macho yake pembeni.
“Rahma! Najua unanifikiria vibaya sana kwa sasa, najua unaona kama nakufanyia makusudi kwa sababu sikupendi lakini ukweli ni kwamba ni matatizo makubwa sana na badala ya kunichukia, unatakiwa unionee huruma mwenzio,” nilianza kumbembeleza Rahma.
Kama nilivyosema awali, sikuw anajua mambo ya mapenzi kwa hiyo hata kubembeleza kwangu, nilikuwa naungaunga tu ilimradi Rahma anielewe. Niliendelea kushuka mistari kwa kuzunguka, nikamwambia kuna jambo zito ambalo halijui nataka kumweleza.
Maneno yangu yalimbadilisha kabisa Rahma, akawa ananitazama kwa shauku huku ile huzuni aliyokuwa nayo, ikiyeyuka ghafla. Ili kumuweka sawa, ilibidi nibadilishe mada kwanza, nikamuuliza vipi yule muuzaji mbona haleti hizo soda?
“Una kiu? Ngoja nimfuate,” alisema huku akiinuka lakini alipofika pale dukani, yule mhudumu alikataa katakata kutoka, akampa Rahma funguo ya friji na kutaka ajihudumie mwenyewe. Rahma aliichukua, akaniuliza nakunywa soda gani, akatoambili pamoja na yake, akaja mpaka pale tulipokuwa tumekaa, akazifungua zote na kurudisha funguo kwa mwenyewe.
“Kwa nini amekataa kuja kutuhudumia mwenyewe?”
“Hata mimi nashangaa! Achana naye tuendelee na yetu,” alisema Rahma, nikapiga funda moja kisha nikaendelea kuzungumza. Lengo langu lilikuwa ni kumpasulia ukweli kwamba baba yake alikuwa mwanachama wa jamii ya siri, vilevile baba yangu na mimi pia wameniingiza bila ridhaa yangu.
Niliona hiyo ndiyo gia nzuri ya kumuingia kwa sababu kama ningesema mimi mwenyewe ndiye niliyetaka kujiunga, angenishangaa sana na pengine nisingeweza kumshawishi. Nilianza kwa kumdadisi kwa kina kuhusu baba yake, nikitafuta sehemu ya kuanzia.
“Mbona unaniuliza kama una kitu unataka kuniambia? Tatizo langu wala halimhusu baba, ni mimi na wewe.”
“Ni stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.

Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 62



ILIPOISHIA:

“Ni stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.

SASA ENDELEA...

“Mbona sikuelewi Togo?”

“Ni kuhusu wazazi wetu.”

“Wamefanya nini?”

“Wanajihusisha na...” kabla sijamalizia nilichotaka kukisema, jambo la ajabu lilitokea. Yule muuzaji wa lile duka, alifungua mlango na kutoka huku akikimbia, cha ajabu, hakuwa amevaa nguo hata moja.

“Vipi kwani mbonaumeshtuka?”

“Umemuona?”

“Nani? Vero? Nini cha ajabu kwani?” Rahma alinishangaa sana, na mimi nikawa namshangaa. Yaani mtu atoke dukani akiwa mtupu, halafu aanze kukimbia mitaani, siyo jambo la kushangaza hilo?”

“Itakuwa labda kuna anaenda kuomba chenji, tuendelee na mazungumzo yetu,” Rahma alizidi kunishangaza. Sikuelewa kwamba alikichukuliaje kitendo kile kiasi cha kutokipa uzito hata kidogo, hata baadhi ya wateja waliokuwa wamekaa upande wa pili, nao wakipata vinywaji, hawakuonesha kushtuka kabisa.

“Ndiyo atoke bila nguo?”

“Togo, umeanza kuchanganyikiwa nini?”

“Rahma, ina maana huoni kama hajavaa nguo yule? Kwa hiyo kumbe ndiyo maana alikuwa anajificha dukani?”

“Nani hajavaa nguo? Una matatizo gani Togo? Usije kunitia aibu hapa, hebu maliza twende,” alisema Rahma huku akimalizia soda yake. Nadhani alihisi huenda nikatokewa na maruweruwe kama yale yaliyokuwa yakinitokea.

“Basi Rahma, tuendelee na mazungumzo yetu,” nilijaribu kumsihi lakini alishaonesha kama ameingiwa na hofu ndani ya moyo wake, hakutaka kukaa tena eneo lile, ikabidi nimalizie soda yangu na kusimama.

Sikuwa nimemlipa yule muuzaji, lakini Rahma aliniambia kwamba nisijali yeye atampa hata baadaye. Nilijisikia vibaya sana ndani ya moyo wangu kwa jinsi Rahma alivyonipuuza ila sikutaka kumuonesha.

Kwa jinsi alivyonichukulia, hata kama ningemweleza kile kilichofanya nikakutana naye pale, huenda pia angenipuuza kwa hiyo nilichokifanya, niliamua kunyamaza na dukuduku langu moyoni.

“Hujamalizia ulichotaka kuniambia,” alisema Rahma wakati tukitembea kurudi ndani, nikamwambia asiwe na wasiwasi nitamueleza siku nyingine.

“Kwani siku hizi umeshapata mwanamke mwingine anayekuzuzua?”

“Hapana Rahma, na ndiyo maana nilitaka kuzungumza na wewe, lakini basi tuyaache.”

“Sikuelewi Togo na kama unaona ulichokifanya kwangu ni sawa, wala mimi sina cha kusema ila kumbuka chozi langu haliwezi kwenda bure,” alisema Rahma, nikajaribu kumbembeleza lakini ilikuwa sawa na kazi bure.

Mpaka tunaingia ndani, Rahma alikuwa akiendelea kulalamika tu, akaniambia anashukuru kwa yote niliyomfanyia na kumuumiza moyo wake. Nilishindwa cha kusema, ikabidi ninyamaze tu, bado wale madereva bodaboda na Bajaj pale nje hawakuwa wamerejea.

Tuliingia ndani lakini Rahma hakutaka kabisa kujishughulisha na mimi, alienda moja kwa moja sebuleni, mimi nikaenda chumbani huku nikiwa nimekosa kabisa furaha. Nilijilaza kitandani, nikaanza kutafakari tukio la yule muuzaji wa lile duka.

Nilichokihisi kwa harakaharaka, huenda alikuwa akitumia nguvu za kishirikina kwenye biashara yake maana nimewahi kusikia kwamba kuna wafanyabiashara ambao ukiingia kwenye duka lake au sehemu anayofanyia biashara, hata kama umevaa nguo, anakuona kila kitu lakini wapo wengine ambao inakuwa kinyume chake, kwamba muuzaji anakaa kwenye biashara akiwa hana nguo hata moja ingawakwa macho ya kawaida anaonekana amevaa nguo.

Lengo la kufanya hivyo inakuwa ni kuvutia wateja na kiukweli hata kwenye lile duka la pale nje, lilikuwa kubwa lenye kila kitu unachokihitaji na kiukweli alikuwa akifanya sana biashara kwa sababu kwa muda mfupi tu tuliokaa pale, wateja walikuwa hawakauki.

“Ulitaka kumwambia nini Rahma,” sauti ya baba ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Alikuwa amesimama pembeni ya kitanda changu, hata sikukumbuka ameingia saa ngapi, nilichoshtuka ni kumuona akiwa ndani.

“Mimi?” niliongea kwa kubabaika huku nikiinuka pale kitandani.

“Kwani nazungumza na nani?” baba aliniuliza akionesha kuwa na jazba, nikawa nababaika. Kwa jinsi ilivyoonesha, alikuwa anajua kwamba nilitaka kumweleza Rahma ukweli, jambo ambalo walinionya sana kwamba sitakiwi kutoa siri za jamii yetu kwa mtu yeyote asiyehusika.

“Tulikuwa tunapiga stori za kawaida tu.”

“Stori za kawaida ndiyo muende dukani?” baba alinihoji huku akinitazama kwa macho ya ukali, sikuwa na cha kujibu na kwa jinsi baba alivyo, nilitegemea kabisa kwamba pale lazima angenizibua makofi, nikawa nimekaa ‘attention’.

“Kuna maagizo yako kutoka kwa Mkuu, usiku itabidi tukupeleke sehemu, umeyaanza mwenyewe lazima uyamalize,” baba alisema huku akigeuka na kuanza kuondoka, nikabaki na mshangao mkubwa, nikiwa sijui alichokimaanisha. Akiwa anamalizikia kutoka, aligeuka na kunitazama kwa macho makali.

“Ole wako ufumbue domo lako!” Nilishusha pumzi ndefu, mambo yalianza kuwa mengi na kunielemea kwa sababu kabla moja halijaisha, lingine lilikuwa likiibuka. Kwa jinsi nilivyozungumza na baba yake Rahma, nilitambua kwamba hizo salamu kutoka kwa Mkuu lazima zitakuwa zinahusu masharti ya uamuzi nilioufanya.

Niliona kama muda unaenda taratibu sana, sikutoka chumbani, hata chakula nililetewa kulekule na Rahma ingawa safari hii alionesha kuwa na chuki za waziwazi kwangu maana hakutaka hata kunisemesha wala kunitazama usoni.

Hatimaye jioni iliwadia, baba na baba yake Rahma, wakiwa tayari wameshajiandaa, walinifuata chumbani na kuniambia muda wa safari umewadia, wakanitaka nijiandae, baba Rahma akanipa koti kubwa jeusi.

“Kwani tunaenda wapi?”

“Jiandae bwana, maswali mengi ya nini?” alisema baba kama kawaida yake, nikajiandaa na muda mfupi baadaye, safari ilianza. Kwa jinsi nilivyokuwa nimevaa, haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kunitambua, lile koti lilinibadilisha kabisa. Tulitoka na kuelekea moja kwa moja kwenye stendi ya mabasi ya Makumbusho, tukapanda kwenye ‘coaster’ moja ambayo mbele ilikuwa imeandikwa kwamba inaenda Bagamoyo. Sikuwa nimewahi kufika Bagamoyo zaidi ya kusoma tu darasani kuhusu mji huo wa kihistoria.

Basi tulienda mpaka tulipofika sehemu moja iitwayo Mlingotini, tukateremka kwenye gari na kuvuka barabara, tukaanza kutembea kwa miguu. Tulienda umbali mrefu sana maana mpaka inafika saa tano za usiku, bado tulikuwa tukitembea.

Hatimaye tuliwasili kwenye eneo lililokuwa na nyumba kama tatu hivi, moja ikiwa imeezekwa kwa bati na zile nyingine kwa makuti, baba akabisha hodi ambapo sauti ya mwanamke ilisikika ikitukaribisha.

Muda mfupi baadaye, mwanamke mmoja mzee alitoka, ilionesha alikuwa akifahamiana vizuri na baba na baba yake Rahma kwani aliwakaribisha kwa uchangamfu, tukaingia ndani na kukaa kwenye jamvi lililokuwa pale sebuleni.

“Ndiyo huyu?” aliuliza yule mwanamke, baba akamjibu kwamba ndiyo mimi, sikuelewa kwamba ndiyo mimi nimefanyaje na kwa nini ameniuliza, ikabidi niwe mpole.

“Mchumba hujambo? Ukifanikiwa na mimi nataka uninunulie gari,” alisema yule mwanamke huku akitabasamu, mapengo yake yakaonekana. Sikuelewa kwa nini amesema vile, nikazidi kuwa gizani. Alinishika mkono na kuwapa ishara akina baba kwamba wamsubiri, tukatoka nje na kwenda kwenye kibanda cha makuti.

Wakati tunatoka, nilimsikia baba akimwambia baba Rahma kwamba kuwana mtoto kama mimi ni hasara, wakacheka. Sikuelewa kwa nini baba amesema vile lakini sikujisikia vibaya maana mimi na baba kukwaruzana ni jambo la kawaida kabisa, ingawa mimi ndiyo nilikuwa mwanaye kipenzi.

“Nimepata salamu zako kwamba umechagua kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema yule mwanamke, macho yakanitoka pima.

Je, nini kitafuatia?
 
kweli togo ni hasaraaa yan likitoka hili linakuja lile
 
hadi april, 2018 story itafikisha mwaka. inapoteza mvuto kwa kusuasua.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 63
ILIPOISHIA:
“Nimepata salamu zako kwamba umechagua kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema yule mwanamke, macho yakanitoka pima.
SASA ENDELEA...
Nilijiweka vizuri pale chini nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia ataniambia nini, akanitazama machoni kisha akashusha pumzi ndefu na kunisogelea.
“Kwa nini umeamua kupita njia hii?” aliniuliza kwa sauti ya upole, nikashindwa kuelewa alikuwa anamaanisha nini.
“Unalingana na kijana wangu ambaye mwezi wa kumi na mbili angekuwa anatimiza miaka 21, makosa yangu yamesababisha niishi maisha ya kujuta kila siku, sitaki mtu mwingine apite njia kama niliyowahi kupita mimi na kusababisha nimpoteze mwanangu kipenzi,” alisema lakini wala maneno yake hayakuniingia akilini.
“Umeshawishiwa na mtu yeyote au ni maamuzi yako mwenyewe?”
“Nimeamua mwenyewe, wala hakuna aliyenishawishi.”
Kwa jinsi majibu yangu yalivyokuwa, yule mwanamke alishindwa kuendelea kunihoji maana nilishafikia uamuzi ndani ya moyo wangu na hakukuwa na jinsi yoyote ambayo ningebadilisha uamuzi huo.
“Unatakiwa kuwa makini sana na aina ya maisha utakayokuwa unaishi, hutakiwi kunywa pombe wala kuvuta sigara, hutakiwi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote mpaka utakapooa, hutakiwi kulala kitandani, utakuwa unalala chini na hutakiwi kula nyama nyekundu, mengine ni ya vitendo zaidi, nisubiri,” alisema mwanamke huyo na kutoka.
Nilibaki nayatafakari yale masharti aliyonipa, sikuona jambo lolote la kunizuia kwa sababu kama ishu ya ulevi, sikuwa nakunywa pombe wala kuvuta sigara, achilia mbali bangi ingawa katika makuzi ya ujana, kuna wakati nimewahi kujaribu na kuishia kudhalilika.
Suala la uhusiano wa kimapenzi, nilichokuwa nimekiamua kutoka ndani ya moyo wangu, ni kwamba kama Rahma akikubaliana na mimi, nitamuoa awe mke wangu wa ndoa maana alikuwa na kila kitu nilichokuwa nakihitaji, achilia mbali tofauti yetu ya umri. Suala la kutolala kitandani, nalo pia halikuwa tatizo kwangu kwa sbaabu maisha yetu ya kule kijijini, tulishazoea kulala kwenye vitanda vya kamba au kulala chini kwenye mkeka kwa hiyo hilo pia halikuwa tatizo kwangu.
Suala la kula nyama nalo sikuona kama ni shida kwa sababu maisha ya kule kijijini kwetu, nyama tulikuwa tunakula siku za sikukuu au mara chache tunapoenda kuwinda, mboga yetu kubwa ilikuwa ni samaki.
Kimsingi masharti hayo aliyonipa, yalinifanya ile hofu yote niliyokuwa nayo kuhusu kumiliki utajiri, iyeyuke kama theluji iyeyukavyo juani, hamu ya kutamani kuwa na utajiri mkubwa, ikazidi kunijaa.
Moyoni nilijiambia kama masharti yenyewe ndiyo hayo, kwa nini wachawi wanaogopa kuwa matajiri? Wanachokiogopa ni nini hasa? Akilini nilianza kuvuta picha ya jinsi nitakavyokuwa ‘tajiri mtoto’, nikiendesha magari ya kifahari na kuishi kwenye majumba ya gharama kubwa.
Hata ule ushauri alionipa Mkuu pamoja na baba yake Rahma, kwamba kama nataka mambo yasiwe magumu kwangu, nisitamani kuwa na utajiri mkubwa, bali fedha za kawaida tu za kuniwezesha kuishi bila shida, niliutupilia mbali, tabasamu pana likachanua kwenye uso wangu.
Dakika kadhaa baadaye, yule mwanamke alirejea, nikashtuka kumuona akiwa na kisicho cha kawaida. Shingoni alikuwa amebeba nyoka mdogo aliyejiviringisha huku kichwa chake akiwa amekielekezea mbele, akamshika na kumshusha chini, akajiviringisha na kuinua kidogo kichwa chake.
Nilishtuka sana, kama nilivyowahi kueleza, pamoja na ujanja wangu wote, hakuna kitu nilichokuwa naogopa kama nyoka.
“Unashtuka nini? Huyu itabidi umzoee tu,” alisema yule mwanamke, nikawa nimekaa kwa tahadhari kubwa, nikimtazama kwamba akinisogelea tu nikimbie kuelekea nje. Cha ajabu, nilipomchunguza vizuri yule nyoka, alikuwa na madoadoa sawasawa na ya yule nyoka ambaye Mkuu alinichanja na kumlambisha damu yangu.
“Itabidi umtunze na kumheshimu kwa moyo wako wote, huyu ndiye atakayeamua hatima ya utajiri unaoutaka, kadiri anavyozidi kuwa mkubwa ndivyo unayoyataka yatakavyokuwa yanatimia,” alisema mwanamke huyo, bado nikawa najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
“Unamshangaa kwani ndiyo mara yako ya kwanza kumuona? Hebu vua shati huko,” alisema mwanamke yule, ni hapo ndipo nilipoamini kwamba ni kweli nyoka yule ndiyo yuleyule aliyelambishwa damu yangu na Mkuu.
Nilivua shati, yule mwanamke anachukua wembe na kusogelea, akanichanja kwenye mbavu upande wa kushoto, damu zikaanza kunitoka kwa sababu alivyonichanja alikandamiza mkono, akamchukua yule nyoka ambaye sasa alikuwa akitoa ulimi wake na kuchezesha.
Akamsogeza mpaka pale kwenye jeraha langu, hofu niliyokuwa nayo ilikuwa haielezeki. Simulizi kuhusu nyoka nilizowahi kuzisikia, achilia mbali matukio niliyowahi kushuhudia jinsi watu na mifugo inavyopoteza maisha baada ya kung’atwa na nyoka, vilinifanya niwe mwoga sana kwa viumbe hawa.
Alipomsogeza tu kwenye jeraha, alijikunjua na kunigusa kwa ulimi wake, akaanza kuilamba ile damu kwa kasi kubwa. Muda mfupi tu baadaye, jeraha lilibaki kuwa alama tu, damu zote alizilamba nyoka yule na wala nyingine hazikuendelea kunitoka.
“Utamzoea tu wala usijali, si umeamua mwenyewe?” alisema yule mwanamke huku akitingisha kichupa chenye dawa ya majimaji, akanipaka pale kwenye jeraha kisha akamchukua yule nyoka, safari hii alimuingiza kwenye mfuko uliotengenezwa kwa kipande cha gunia, akatoka na kuniacha nikiwaza sana.
Nimewahi kusikia simulizi za watu waliokuwa wakifuga nyoka wakubwa ndani ya nyumba zao kwa ajili ya imani za kishirikina, sikutaka kuamini kwamba na mimi ndiyo naelekea kwenye maisha hayo, nikaanza kuelewa hatari iliyokuwa mbele yangu.
Hata hivyo, bado shauku ya kuwa tajiri haikuniisha, nilijipa moyo kwamba kama wapo watu ambao wanaweza, kwa nini mimi nishindwe? Muda mfupi baadaye, yule mwanamke alirejea na kuendelea kunielekeza mambo mbalimbali, yaani alivyokuwa akiongea na mimi ni kama tayari nimeshakuwa tajiri maana alikuwa akinipa masharti ya namna ya kutumia fedha.
Aliniambia hata niwe na fedha nyingi kiasi gani, sitakiwi kutoa kumpa mtu yeyote fedha siku za Jumatatu, Jumanne na Jumapili, akaniambia hata kama kuna mtu amepatwa na dharura kubwa na kiwango kidogo tu cha fedha kinaweza kumsaidia, sitakiwi kabisa kutoa hata shilingi kumi kwenye siku hizo alizonitajia.
Akaniambia pia kwamba katika siku hizo nilizokuwa na uwezo wa kutoa fedha, muda wa kutoa fedha kumpa mtu yeyote au kufanya kitu chochotye kinachohusiana na fedha, ni saa kumi na mbili jioni, kabla jua halijazama. Maelezo hayo yalinishangaza sana, nikawa najiuliza maswali mengi kichwani yaliyokosa majibu.
Baadaye, aliniambia kwamba natakiwa kurudi tena nyumbani kwake hapo baada ya siku sita kwa ajili ya kwenda kukamilisha baadhi ya mambo. Alinipa mkono na kunitakia maisha mema ya utajiri, mimi bado macho yangu yakawa kwenye ule mfuko aliomuweka yule nyoka mdogo.
Baadaye baba na baba yake Rahma walikuja kunichukua, wakamshukuru mwanamke huyo, tukatoka na safari ya kurejea nyumbani ikaanza. Tayari ilishagonga saa nane za usiku, tukawa tunatembea kwa miguu kuelekea kwenye barabara kubwa ya lami.
Kutoka nyumbani kwa mwanamke huyo mpaka kwenye barabara ya lami, kulikuwa na umbali mrefu sana na kibaya zaidi, ni kwamba tulikuwa tunapita kwenye pori kubwa ambalo kwa usiku ule lilikuwa likitisha sana.
Tukiwa tunaendelea kuchanja mbuga, baba akiwa mbele na baba yake Rahma akiwa nyuma, mara tulianza kusikia sauti za ajabu kutoka ndani ya pori lile, huku kukiwa na purukushani kubwa, mapigo ya moyo wangu yalilipuka na kuanza kunienda mbio kuliko kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 64
ILIPOISHIA:
Tukiwa tunaendelea kuchanja mbuga, baba akiwa mbele na baba yake Rahma akiwa nyuma, mara tulianza kusikia sauti za ajabu kutoka ndani ya pori lile, huku kukiwa na purukushani kubwa, mapigo ya moyo wangu yalilipuka na kuanza kunienda mbio kuliko kawaida.
SASA ENDELEA...
“Nakufaaa! Naku...fa...aa,” sauti ya mwanamke ilisikika, aliporudia mara ya pili kuimba msaada, sauti yake ilikuwa ikikwamakwama na muda mfupi baadaye akaanza kukoroma kuonesha kwamba mtu au watu waliokuwa wakitaka kumdhuru tayari walishafanikisha lengo lao.
Tofauti na hali niliyokuwa nayo mimi, baba na baba yake Rahma hawakuonesha kushtuka chochote, yaani ilikuwa ni kama hakuna kilichotokea na wala hakuna aliyeshughulika kwa chochote.
Muda mfupi baadaye, harufu ya damu mbichi ilitawala eneo lote lile, milio ya bundi na midege mingine ya ajabu ikazidi kuifanya hali iwe ya kutisha mno. Baba aliendelea kupiga hatua ndefundefu, hukumoyo wangu ukiwa umepondwapondwa kwa hofu na mshtuko, na mimi nikawa naongeza mwendo, miguu yangu ikitetemeka kuliko kawaida.
“Unaogopa nini? Hili linaitwa pori la kafara, huku ndiyo watu wanakokuja kutolea makafara ili mambo yao yafanikiwe,” alisema baba yake Rahma huku tukiendelea kusonga mbele, sikumjibu chochote maana bado nilikuwa natetemeka sana.
Jambo ambalo mpaka leo huwa silipatii majibu, ni kwa nini watu wenye imani za giza hawaoni hatari kabisa kuyakatisha maisha ya mtu mwingine? Ni kweli kwamba sote tutakufa na kifo hakiepukiki lakini kwa nini uyakatishe maisha ya mtu mwingine kwa sababu zako binafsi?
Japokuwa na mimi nimefanya sana huo mchezo, natamani kama utokee muujiza nguvu zote za giza zipotee. Ukweli ambao watu wengi hawaujui, katika vifo vinavyotokea kila siku, iwe ni kwa ajali, magonjwa, watu kujinyonga au kuuana, nguvu za giza zinahusika kwa asilimia kubwa sana.
Kuna matukio mengine unaweza kuona kama ni kifo cha kawaida tu lakini mtu mwenye uwezo wa kuona mambo kwa jicho la tatu, anakuwa anaelewa mchezo mzima ulivyotokea. Si kila kifo kinachotokea kipo kama unavyoweza kudhani, humu duniani kuna mambo mengi sana yaliyojificha na kuna watu wanawaonea sana wenzao na kundi kubwa linaloonewa sana, ni wale watu wasio na imani thabiti ndani ya mioyo yao.
Basi tulifika mpaka barabarani, kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, hakukuwa na magari yoyote yaliyokuwa yakipita, barabara ilikuwa kimya kabisa. Nilitegemea baba atasema tutafute sehemu ya kuondokea kama kawaida yetu maana nilikuwa nimchoka sana lakini safari hii alizungumza kitu cha tofauti.
Alisemakwa sababu tulikuwa tumebeba kitu cha muhimu sana, ilikuwa ni lazima tufike nyumbani kwa njia za kawaida. Aliposema tumebeba kitu muhimu sikumuelewa kwa sababu kiukweli hakuna hata mmoja kati yetu aliyekuwa na mzigo wowote. Tulianza kutembea pembezoni mwa barabara ileile ya lami tuliyojia, huku wote tukiwa kimya kabisa. Utaratibu wetu ulikuwa uleule, baba mbele, mimi katikati na baba Rahma nyuma.
Kwa bahati nzuri, tulipofika mbele kidogo, kuna Fuso lilikuwa likitokea upande wa mashambani, likiwa na shehena ya mananasi, kama ujuavyo tena Bagamoyo kunalimwa sana matunda.
Harakaharaka baba alimpungia mkono dereva, akasimamisha gari kabla hajaingia kwenye barabara ya lami, akamfuata na kuzungumza naye ambapo sekunde chache baadaye, baba alitupa ishara kwamba tupande.
Nadhani walishakubaliana, ikawa ahueni maana nilikuwa nikiiwazia sana ile safari. Gari lilikuwa limejaza mananasi mpaka juu kabisa, ikabidi tupande na kukaa juu ya mabomba na kujishikilia vizuri, dereva akaliingiza gari kwenye barabara ya lami na safari ikaendelea.
Japokuwa kule juu kulikuw ana upepo mkali unaochoma mpaka ndani ya kifua, ilibidi tuvumilie maana ilikuwa bora kuliko kutembea kwa miguu. Baada ya kama dakika hamsini hivi, tuliwasili jijini Dar, tukateremka kwenye kituo cha Mwenge, tukamshukuru sana yule dereva, yeye akaendelea na safari yake na sisi tukaanza kutembea kuelekea nyumbani.
Kitu kingine ambacho nilijifunza lakini nisingependa kukizungumzia sana leo, maduka mengi, hasa yale makubwa, yanakuwa na ulinzi wa nguvu za giza hasa nyakati za usiku ambapo kama una uwezo wa kuona mambo yaliyojificha, unaweza kustaajabu sana.
Hii dunia ina mambo mengi sana yaliyojificha, kama nioivyosema, sitaki kuelezea sana kuhusu hili. Basi tuliendelea na safari yetu mpaka tulipofika nyumbani, tayari ilishagonga saa tisa na nusu.
“Unatakiwa kuwa mtulivu na msiri, hakuna kitu cha ajabu tena kwako, umenielewa,” baba aliniambia kwa kauli ya msisitizo wakati tukiagana kwa ajili ya kila mmoja kwenda kulala lakini sikumuelewa anamaanisha nini.
“Kuanzia leo utakuwa unalala peke yako, chumba chako kinatakiwa kuwa kimefungwa muda wote na usiruhusu watu kuingiaingia, hata awe nani, umenielewa?” alisema baba, baba yake Rahma akawa anatingisha kichwa kuonesha kwamba anaunga mkono kile alichokisema baba.
Bado sikuwa naelewa kwa nini wananiambia vile, baba akahitimisha kwa kuniambia kwamba eti hategemei kunisikia nikifanya jambo lolote la ajabu. Tuliagana, nikaingia chumbani kwangu, kweli yule ndugu yangu niliyekuwa nalala naye siku mojamoja hakuwepo, kwa hiyo nilikuwa peke yangu.
Kwa jinsi nilivyokuwa nimechoka, sikutaka hata kufanya kitu kitu chochote, nikavua nguo zote, nikazima taa na kujilaza kitandani. Mwili wangu ulikuwa na maumivu sehemu mbalimbali, lakini pale yule mwanamke aliponichanja usiku huo palikuwa na maumivu makali zaidi.
Nikiwa bado natafakari mambo chungu nzima yaliyotokea kwa siku nzima, nilisikia kitu kilichonishtua sana. Chini ya kitanda changu kulikuwa kama na purukushani fulani hivi kwa mbali, ikabidi harakaharaka niinuke na kwenda kuwasha taa.
Nikainama chini kwa tahadhari kubwa na kuchungulia uvunguni, katika hali ambayo sikuitegemea kabisa, nilikiona kile kimfuko kilichotengenezwa kwa kipande cha gunia, nilichokionakule kwa yule mtaalamu kikiwa chini ya kitanda changu.
Ni kimfuko hichohicho ndicho yule mtaalamu tuliyetoka kwake usiku huo, alichomuweka yule nyoka mdogo baada ya kumlambisha damu yangu. Kilichonishtua zaidi, kimfuko kilikuwa tupu, kwa akili za harakaharaka nikahisi kwamba lazima zile purukushani nilizokuwa nazisikia, zilikuwa ni za yule nyoka akihangaika kutoka.
Sasa kimfuko kimefikaje chumbani kwangu? Na kama kile nilichokuwa nakihisi ni kweli, yule nyoka alikuwa mle ndani, ningelalaje? Nilijikuta usingizi wote ukiniisha, harakaharaka nikapanda juu ya kitanda na kukaa kwenye uchago wa kitanda ili hata akipanda kitandani, asiweze kunifikia.
Ni hapo ndipo nilipoanza kuelewa kauli za baba zilikuwa na maana gani, kuanzia ile ya kule njiani kwamba ‘tumebeba kitu muhimu sana’, mpaka yale maneno aliyoyazungumza muda mfupi uliopita kabla kila mmoja hajaenda kulala.
Nilijiapiza kwamba sitalala mpaka kupambazuke, na ukizingatia tayari muda ulishaenda sana, niliona isiwe tabu. Lakini waliosema usingizi ndugu yake kifo hawakukosea, hata sijui nini kilitokea, nilipokuja kushtuka baadaye, nilijikuta nimelala kitandani na kibaya zaidi, hata taa ilikuwa imezimwa.
Mshtuko nilioupata ulikuwa hauelezeki, nikafumbua macho na kuyakodoa kama nitaona chochote lakini nilijitahidi nisitingishike hata sehemu moja kwenye mwili wangu. Nikiwa nimejikausha kama gogo, nilihisi hali fulani kwenye ile sehemu yule mwanamke aliponichanja usiku huo.
Nilihisi kama kuna kitu kinanilamba hivi, nikaanza kutetemeka huku nikiendelea kujikausha nisisababishe mtikisiko wa aina yoyote, nilipozidi kuvuta utulivu, nikahisi kuna kitu cha baridi kinatingishikatingisha upande ule niliokuwa nalambwa, mapigo ya moyo yakawa yanadunda kama nimetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom