Simulizi: Makaburi ya wasio na hatia

...Mjukuu wa chifu,

..SEHEMU YA 55


ILIPOISHIA:
“Tunaenda Chunya, hutakiwi kwenda kinyume na maelekezo tunayokupa, ukifanya uzembe tu, kitakachokutokea ni juu yako,” alisema baba kwa sauti ya msisitizo, nikawa natingisha kichwa kukubaliana naye. Tulikaa chini na kuweka kama duara hivi, tukashikana mikono kisha nikaambiwa nifumbe macho.

SASA ENDELEA...
Kweli nilifumba macho, baba na baba yake Rahma wakawa wanazungumza maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa kwa kuyarudiarudia, kisha nikaanza kusikia kama upepo mkali ukianza kuvuma kwa nguvu, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia baba akinitingisha kwa nguvu.
“Tumeshafika! Fumbua macho,” alisema baba, nikafumbua macho na kujikuta nikiwa kwenye mazingira tofauti kabisa. Sikuelewa tumetumia muda gani maana ninachofahamu mimi kuna umbali mrefu sana kutoka Mbeya mpaka Dar es Salaam, ni safari ya kutoka alfajiri na mapema na kufika usiku.

“Unashangaa nini tumeshafika!” baba alisema huku akinivuta mkono maana kiukweli nilikuwa nimepigwa na butwaa, nikishangaa huku na kule, nikijaribu kukumbuka kama eneo lile nalifahamu.
“Mungu wangu!” nilijisemea moyoni baada ya kugundua kwamba tulikuwa kwenye shule ya msingi niliyosoma pale Chunya, chini ya mti mkubwa uliokuwa nyuma ya shule ambao kwa kipindi kirefu nilikuwa nikisikia watu wakisema kwamba una majini.
“Tumefikaje huku?” niliuliza nikiwa bado nashangaashangaa nikiwa siamini. Yaani nifumbe macho nikiwa kwenye makaburi ya Wagiriki, Kunduchi jijini Dar halafu ninapofumbua macho muda mfupi baadaye, usiku huohuo nijikute nipo Chunya, ilikuwa ni zaidi ya maajabu.
“Huu si muda wa maswali,” baba aliniambia huku akinitaka niongeze mwendo, tukawa tunatembea kuelekea upande wa Magharibi mwa shule, kulipokuwa na njia ya kuingilia na kutokea shuleni hapo.
Baba alikuwa mbele, mimi katikati na nyuma alikuwepo baba yake Rahma, tukawa tunatembea na baadaye tukafika kwenye eneo la uwanja wa shule. Japokuwa ilikuwa ni usiku, uwanja ulionesha kuwa na pilikapilika nyingi sana, watu wengi walikuwa wamekusanyika na kuweka makundi matatu, kundi la kwanza lilikuwa upande wa goli la kwanza, wengine walikuwa katikati ya uwanja na wengine kwenye goli jingine.
Ilionesha kama kuna shughuli fulani zinaendelea ingawa zilionesha kwamba si za kawaida kwa sababu watu wengine walikuwa watupu, wengine walikuwa wakicheza ngoma za kienyeji na wengine walikuwa wamekaa chini.
“Hutakiwi kugeuka nyuma, ni mwiko,” baba aliniambia wakati tukiendelea kuchanja mbuga, tukawa tunapita kwenye njia ambayo wakati nasoma, ndiyo niliyokuwa nikiitumia kwenda na kurudi shule.
Tulipita kwenye vichaka kadhaa na baadaye tukatokezea kwenye nyumba za nyasi zilizokuwa pembezoni mwa kijiji, tukasimama ambapo baba aliniambia kwa sababu mimi ndiye ninayefahamu nyumbani kwa huyo rafiki yangu, Sadoki ambaye ndiye niliyemchagua kumtoa kafara, nitangulie mbele.
Akarudia kunisisitiza kwamba sitakiwi kugeuka nyuma wala kuzungumza hovyo, kazi yangu ni moja tu, kuongoza njia. Nilitii nilichoambiwa huku nikitetemeka sana. Mara kwa mara taswira ya Sadoki ilikuwa ikinijia ndani ya kichwa changu, nikawa najisikia uchungu mno ndani ya roho yangu hasa kutokana na ukweli kwamba yeye ndiye aliyekuwa tegemeo la familia yao.
Niliongoza njia na kwa sababu vichochoro vyote vya Chunya nilikuwa navijua kwa sababu hapo ndipo nilipozaliwa na kukulia, sikupata tabu. Baada ya kutembea kwa dakika kadhaa, hatimaye tuliwasili kwenye nyumba chakavu ya akina Sadoki. Nikaonesha kwa ishara kwamba tayari tumeshafika, baba akanivuka na kutangulia mbele.
Kwa muda wote huo, baba yake Rahma alikuwa kimya kabisa, baba akaanza kutoa maelekezo kwamba tunatakiwa kuizunguka nyumba hiyo mara saba, kutokea upande wa kulia kwenda kushoto. Nilichojifunza, mambo mengi yanayofanywa na watu wa jamii hizi, huwa yanakwenda kinyume na utaratibu wa kawaida, tukaanza kufanya vile baba alivyosema.
Tulikuwa tukipiga hatua fupifupi huku baba na baba Rahma wakiimba nyimbo fulani za kutisha ambazo hata sikuwa nazielewa, tukazunguka mpaka ilipofika raundi ya saba, tukamalizia pale kwenye kona ya nyuma tulipoanzia kuzunguka.
Baba alipiga mguu wa kushoto chini, mara ukuta ukawa kama umefunguka, akatangulia yeye kuingia kinyumenyume, akapotelea ndani.
Tukabaki mimi na baba Rahma, akaniambia na mimi nipige mguu wa kushoto chini kwa nguvu, nikafanya hivyo, ule uwazi ukatokea tena, akanielekeza kuingia kinyumenyume, nikafanya hivyo na kujikuta nipo ndani, pembeni ya baba ambaye alikuwa amesimama akitusubiri.
Mara baba yake Rahma naye akaingia kwa mtindo uleule. Wasichokijua wengi ni kwamba watu wabaya wanapoamua kuingia ndani ya nyumba yako, huwa hawatumii mlango kwa hiyo hata ufunge milango kwa makufuli makubwa, ujenge fensi hata yenye umeme na uweke walinzi wenye silaha nzito, huwezi kuwazuia watu wenye nguvu za giza kuingia ndani kwako.
Maisha waliyokuwa wakiishi akina Sadoki yalikuwa ya chini sana maana hata sebuleni kwao hakukuwa na kitu chochote cha maana zaidi ya viti vya mbao na meza ndogo, na vyombo vya jikoni. Japokuwa nyumba yote ilikuwa giza, cha ajabu ni kwamba nilikuwa na uwezo wa kuona kila kitu, mpaka kijiko.
Tulianza kutafuta chumba anacholala Sadoki na kwa sababu nilishawahi kuwa naingia mpaka chumbani kwake, niliwaongoza, tukaenda mpaka kwenye chumba chake na kumkuta Sadoki akiwa amelala na mdogo wake wa kiume juu ya kitanda cha kamba.
Kwa wale waliowahi kuishi vijijini watakuwa wananielewa vizuri ninapozungumzia kitanda cha kamba. Maskini! Sadoki alikuwa akikoroma pamoja na mdogo wake, wakiwa hawaelewi chochote kinachoendelea.
Baba alinielekeza kukizunguka kitanda hicho na kusimama upande ambao kichwa cha Sadoki kilikuwepo, nikafanya hivyo, baba akasimama upande wa miguuni na baba yake Rahma akasimama pale katikati.
Moyo ulikuwa ukiniuma sana na sikuelewa natakiwa kufanya nini, nikawa nasubiri maelekezo tu, huku moyo wangu ukijihisi kuwa na hatia kubwa mno. Sadoki hakuwa amefanya kosa lolote baya kustahili adhabu kali kiasi kile maana kama ni kupishana maneno, kilikuwa ni kitu cha kawaida kabisa kwa marafiki walioshibana.
Baba alinielekeza kuinamisha kichwa kumuelekea Sadoki pale kitandani, nao wakafanya hivyohivyo kisha baba akaanzisha wimbo ambao mimi sikuwa naujua, baba yake Rahma akawa anaitikia. Niliogopa sana kwa sababu walikuwa wakiimba kwa sauti ya juu ambayo ingeweza kuwaamsha watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya kuimba mara kadhaa, baba alitoa kichupa kidogo kilichokuwa na ungaunga mweusi ndani, akakitingisha kwa nguvu kisha akampa baba Rahma ili anipe mimi, kikanifikia ambapo alinipa maelekezo kwa ishara kwamba nikitingishe kwa nguvu kisha nichukue ungaunga kidogo na kumpaka Sadoki kwenye paji la uso wake.
Nilifanya kama nilivyoelekezwa, nikampaka kwenye paji la uso kwa kuchora ishara kama ya msalaba hivi, kisha baba akanipa maelekezo kwamba natakiwa kugeuka na kumpa mgongo Sadoki, nikageuka, na wao wakageuka kisha baba akapiga makofi akiashiria tugeuke tena.
Tulipogeuka, nilishtuka sana kumuona Sadoki akiwa amekaa kweye kitanda chake lakini akiwa amefumba macho. Baba akanielekeza kwamba nimshike mkono, kweli nikafanya hivyo, nikamshika, akasimama kisha baba akanionesha ishara kwamba nimuangalie kwa makini anachokifanya.
Alisogea kwenye pembe moja ya chumba na kupiga mguu chini kwa nguvu, ukuta ukafunguka ambapo alitoka nje kinyumenyume, huku nikitetemeka na mimi nikasogea kwenye ile kona huku nikiwa nimemshika Sadoki mikono yake yote miwili. Japokuwa alikuwa amesimama, bado alikuwa amefumba macho.
Nikapiga mguu chini kwa nguvu na kugeuka, nikawa nataka kutoka lakini nilishangaa mwili wangu ukiwa mzito kama ninayevutwa na kitu kurudi ndani. Sijui nini kilitokea kwani nilishtukia baba Rahma ameyeyuka, nikabaki mimi na Sadoki, nikapiga tena mguu kwa nguvu na kutaka kutoka lakini safari hii, ukuta haukufunguka kabisa, kijasho chembamba kikaanza kunitoka.
Nikiwa bado nashangaa nikiwa sijui nini cha kufanya, Sadoki alifumbua macho, tukawa tunatazama ana kwa ana. Ni kama fahamu zake zilikuwa zimemrejea kwani alishtuka sana kuniona ndani ya chumba chake, akageuka huku na kule huku akijaribu kujitoa kwenye mikono yangu kwa hofu kubwa.
“Togoo! Umeingiaje humu?” aliniuliza kwa sauti ya juu, nikasikia mlango wa chumba cha pili ukifunguliwa kuashiria kwamba kuna mtu alikuwa amesikia na sasa anatoka.
“Nimekwisha!” nilijisema huku nikigeuka huku na kule, sikumuona baba wala baba yale Rahma, Sadoki akanibadilikia na kunishika kwa nguvu ii nisipate nafasi ya kukimbia.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
SEHEMU YA 57


kama fahamu zake zilikuwa zimemrejea kwani alishtuka sana kuniona ndani ya chumba chake, akageuka huku na kule huku akijaribu kujitoa kwenye mikono yangu kwa hofu kubwa. “Togoo! Umeingiaje humu?” aliniuliza kwa sauti ya juu, nikasikia mlango wa chumba cha pili ukifunguliwa kuashiria kwamba kuna mtu alikuwa amesikia na sasa anatoka. SASA ENDELEA... “Nimekwisha!” nilijisema huku nikigeuka huku na kule, sikumuona baba wala baba yale Rahma, Sadoki akanibadilikia na kunishika kwa nguvu ii nisipate nafasi ya kukimbia. Akili za haraka, zilinituma kutumia nguvu zangu kujiokoa na kwa kuwa nilikuwa na ile kinga yangu ya hirizi mkononi, nilipiga mguu wa kushoto chini huku nikiwa nimevibana vidole gumba na vile vya mwisho. Hii ni mbinu niliyofundishwa ya kutaka kupotea kwenye macho ya watu, yaani unakuwepo sehemu hiyohiyo lakini huonekani. Nilipofanya hivyo, nilishtukia nikiwa mwepesi kama upepo, Sadoki akabaki ameduwaa kwani japokuwa alikuwa amenishika, alishtukia nikiyeyuka mikononi mwake, giza nene likatanda chumba kizima. Mara mlango ulianza kugongwa kwa nguvu, Sadoki akaenda kuufungua maana alikuwa amefunga kwa komeo kwa ndani, mama yake Sadoki akaingia mbiombio akiwa ameshika kibatari. “Una nini Sadoki?” “Mama! Nimemuona Togo kwa macho yangu, hata sijui ameingiaje humu ndani wakati milango ilikuwa imefungwa.” “Togo huyu rafiki yako? Wewe utakuwa unaota, Togo ataingiaje humu wakati milango yote imefungwa? Halafu mbona watu wenyewe hawapo hapa kijijini na hakuna anayejua walikohamia?” mama yake Sadoki alisema huku akionesha kumshangaa mwanaye. “Kweli mama, nimemuona kwa macho yangu!” “Kwanza umemuonaje wakati hukuwa umewasha kibatari? Acha kutushtua wenzako kwa sababu ya ndoto zako,” alisema mama yake Sadoki huku akimulika huku na kule kwa kibatari. Japokuwa nilikuwa mlemle ndani, hakuna aliyeniona, mwanamke huyo akawa anamtuliza mwanaye na kumwambia kwa kuwa wanalindwa na Mungu hakuna jambo lolote baya linaloweza kuwapata. Japokuwa mama yake Sadoki aliamini kwamba mwanaye alikuwa ndotoni, mwenyewe aliendelea kushikilia msimamo wake na alipoona mama yake hamuamini, aliamua kunyamaza lakini mara kwa mara alikuwa akigeuka huku na kule, akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake. “Haya sogea huku tusali,” alisema mama yake Sadoki, akamshika mwanaye mikono, wote wakafumba macho. Kabla hata hawajaanza kusali, nilishtukia nikivutwa kwa nguvu kuelekea nje, kutazama vizuri kumbe walikuwa ni baba na baba yake Rahma, tukadondokea kwenye majani pembeni ya nyumba ya akina Sadoki, wote wakiwa wanahema kwa nguvu. “Mpumbavu sana wewe,” alisema baba huku akinizabua kibao kwa nguvu, nikashangaa kwa nini ananipiga kwa sababu sikuwa nimefanya kosa lolote. “Kwa nini hukumgeuza kinyumenyume kama wewe?” alisema baba kwa ukali, ni hapo ndipo nilipolitambua kosa langu. Wakati nikitoka na Sadoki, mimi ndiye niliyetanguliza mgongo lakini yeye alikuwa ameelekea nilipo mimi kwa sababu nilikuwa nimemshika mikono nikimvuta, hakutanguliza mgongo. “Lakini hukuniambia hivyo baba,” nilisema huku nikiugulia maumivu makali ya kibao cha baba. Muda huo tayari walishaanza kusali, wakawa wanakemea na kutaja jina la Mungu kwa nguvu. Ukweli ambao wengi hawaujui, ambao hata mimi mwenyewe nilikuwa siujui, hakuna sumu mbaya kwa jamii ya watu wa nguvu za giza, kama mtu anayesali na kumuamini Mungu kwa moyo wake wote, bila kujali ni wa dini gani. Hapa nazungumzia wale watu ambao kweli wanafuatisha amri za Mungu, yaani kama ni Mkristo, awe anafuatisha yale yote aliyoagizwa na dini yake na kama ni Muislam vivyo hivyo. Watu wa namna hii, huwa hawagusiki kabisa maana hata pale baba aliniambia kama wasingetumia nguvu za ziada kuingia na kunivuta kwa nguvu, maombi ya Sadoki na mama yake yangenidhuru vibaya sana na hata wao hawajui nini kingenipata. Ila kitu ambacho nilikuja kujifunza baadaye, ambacho ningependa watu wengine wajue, kinga waliyonayo watu wanaomuamini Mungu, haiwahusu wale wanaosali kinafiki, kwamba ukifika kwenye nyumba za ibada unajifanya wewe ni mwema sana lakini kumbe ni mwizi, mwongo, mwasherati au unashinda kwa waganga wa kienyeji. Ilibidi tuondoke haraka pale nyumbani kwa akina Sadoki kwa sababu sasa palikuwa hapakaliki tena kutokana na maombi yaliyokuwa yanaendelea ndani, njia nzima baba akawa ananilaumu kwa uzembe nilioufanya. Kwa bahati nzuri baba Rahma alinitetea kwamba ni kwa sababu sikuwa najua. Kiukweli lawama za baba zilikuwa ni uonevu wa hali ya juu, maelezo aliyokuwa ananipa, alikuwa ananielekeza vitu nusunusu, sasa kwa mfano hapo kwa akina Sadoki, mimi ningejuaje kama natakiwa kumgeuza Sadoki pia atoke kinyumenyume huku nikiwa nimemshikilia bila kupewa maelekezo? “Sisi tunakusaidia wewe mwenyewe kwa sababu ya upumbavu ulioufanya, kwani sisi ndiyo tulikutuma uende kwenye msiba ambao wewe mwenyewe ndiye uliyeusababisha? Utajuana mwenyewe na Mkuu, we fanya masihara utaona mwisho wake,” alisema baba. Tayari tulishakaribia pale kwenye uwanja wa shule ya msingi niliyosoma ambapo ndipo tulipofikia. “Sasa mzee mwenzangu, tukiendelea kufanya mambo kwa hasira, kweli tutampoteza huyu kijana, hapa kinachotakiwa ni kuhakikisha tunamaliza kwanza suala la Mkuu na Togo na kama unavyoona huku ndiyo tayari tumeshakwama na muda unayoyoma,” alisema baba yake Rahma. Mwanzo nilikuwa nalichukulia suala hilo kama jepesi lakini kwa jinsi mazungumzo hayo yalivyokuwa, niligundua kwamba kweli nipo kwenye hatari kubwa kwa sababu ya makosa niliyokuwa nimeyafanya bila kujua. “Hivi si kuna yule mtu aliyepoteza maisha kwenye ile ajali ya bodaboda aliyoisababisha huyu mwendawazimu?” baba aliuliza. Baba yake Rahma akamjibu kwa kutingisha kichwa, nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia baba atasema nini. “Taarifa zinaonesha kwamba amezikwa jioni ya leo, ila sijui amezikwa wapi, kama tukifanikiwa kujua, tunaweza kumtumia kama mbadala wa Sadoki ili tulimalize hili tatizo la huyu mwendawazimu,” alisema baba huku akiendelea kunishutumu. Sikuelewa anamaanisha nini na hata kama tungelijua kaburi lake tungefanya nini. “Twendeni Mlandizi, tutajua hukohuko tukifika, si unalikumbuka eneo la ajali?” baba aliniuliza, nikatingisha kichwa kwa sababu ilikuwa ni palepale kwenye nyumba iliyokuwa na msiba ndipo hiyo ajali nyingine ilipotokea. Yaani baba alivyokuwa akizungumza, utafikiri kutoka Chunya mpaka Mlandizi ni karibu sana. Kukukumbusha tu, hapa aliyekuwa anazungumziwa aliyekuwa ni yule dereva wa bodaboda ambaye wakati nikiwa nakimbia kuokoa maisha yangu baada ya wale wazee kunishtukia pale kwenye msiba, nilimgonga wakati nikivuta barabara, yeye akiwa kwenye bodaboda iliyokuwa kwenye kasi kubwa. Pale alipodondoka hakuweza hata kuomba maji, alipoteza maisha palepale na sikuwa najua mpaka nilipokuja kuambiwa na akina baba ambao hata sijui wao walijuaje. Basi tulienda mpaka pale chini ya ule mti, tukakuta kuna watu wengine wengi wakiwa wanafanya mambo ambayo hata sikuyaelewa lakini yalionesha kuhusiana na nguvu za giza. Tukakaa na kuweka duara kama tulivyofanya kule Kunduchi wakati tukitaka kuondoka, nikaambiwa nifumbe macho na nisifumbue mpaka nitakapoambiwa, lakini baba akanisisitiza kwamba natakiwa kuwa nalifikiria eneo lile ajali ilipotokea. Kweli nilifanya hivyo, wao wakafanya tena mambo yao kama kule Kunduchi na muda mfupi baadaye, upepo mkali ulianza kuvuma, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipokuja kuzinduliwa na baba aliyekuwa akinitingisha kwa nguvu. Yaani kilichokuwa kinatokea, inakuwa kama nimepitiwa na usingizi mzito wa ghafla, kisha nikizinduliwa najikuta nipo kwenye mazingira mengine tofauti kabisa. Nilishtukia nikiwa nimelala pembeni ya barabara ya lami, baba aliponiamsha, nikawa nashangaashangaa, nikageuka huku na kule kama ninayejaribu kuvuta kumbukumbu. Sikuyaamini macho yangu kugundua kwamba tulikuwa Mlandizi, tena jirani kabisa na pale ile ajali ilipotokea. Nilipotazama upande wa pili wa barabara, niliwaona watu wengi wakiwa wamekaa na kuuzunguka moto, pale kwenye ile nyumba iliyokuwa na msiba wa kwanza wa yule mtoto, moyo ukashtuka sana nikikumbuka kilichotokea. “Mbona umeshtuka,” baba aliniuliza. Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 58


ILIPOISHIA:
Sikuyaamini macho yangu kugundua kwamba tulikuwa Mlandizi, tena jirani kabisa na pale ile ajali ilipotokea. Nilipotazama upande wa pili wa barabara, niliwaona watu wengi wakiwa wamekaa na kuuzunguka moto, pale kwenye ile nyumba iliyokuwa na msiba wa kwanza wa yule mtoto, moyo ukashtuka sana nikikumbuka kilichotokea.
“Mbona umeshtuka,” baba aliniuliza.
SASA ENDELEA...
Sikumjibu zaidi ya kumuonesha kidole kwenye ile nyumba ambapo bado watu walikuwa wakiendelea kuota moto huku wakipiga stori za hapa na pale msibani. Baba wala hakuhangaika hata kugeuka, akanitaka kuelekeza akili zangu kwenye jambo lililotupeleka pale kwani muda ulikuwa umetutupa mkono.
Ilionesha baba alikuwa anaelewa kila kitu kilichokuwa kikiendelea, nikawa najiuliza ameyajuaje yote hayo? Kiukweli sikupata jibu, baba Rahma naye wala hakujishughulisha na chochote na wale watu kama baba.
“Onesha aliangukia wapi? Unatupotezea muda,” alisema baba, nikawa najaribu kuvuta kumbukumbu, nikawa natembea pembeni ya barabara kuelekea pale yule dereva wa bodaboda alipodondokea, wakawa wananifuata kwa nyuma.
“Nadhani ni hapa.”
“Unadhani? Kwani huna uhakika?”
“Nilipomgonga aliyumbayumba kwa mita kadhaa, akaja kudondokea hapa, sina uhakika kwa sababu mimi nilikuwa nimesimama kule mbali.
“Hebu nenda ulipokuwa umesimama,” alisema baba. Ilionesha hakuwa akitaka majibu ya kubahatisha, nikageuka na kutazama tena kule msibani. Bado moyo wangu ulikuwa na hofu, nikiamini wale wazee wanaweza kuwa miongoni mwa watu waliokesha pale msibani halafu nikayazua mengine tena.
Nilirudi kwa hofu mpaka pale nilipokatiza barabara nikiwa spidi kali kama kiberenge, nikasimama na kuwageukia akina baba. Niliweza kupata ramani halisi, nikatembea harakaharaka kuelekea mpaka pale nilipokuwa nimewaacha.
“Ni hapa,” nilisema huku nikioneshea kidole katikati ya barabara. Ni kweli nilipatia kwa sababu bado palikuwa na alama za damu na vioo vya ile bodaboda, baba akainama pale katikati ya lami kisha akawa ni kama anaokota vitu fulani hivi.
Baada ya hapo alikuja upande wa pili tulipokuwa tumesimama, akawa anatazama chini kisha akainua uso na kunitazama:
“Walipomtoa pale katikati ya barabara walimlaza hapa,” alisema huku akionesha, ni kweli pale pembeni napo palikuwa na alama za damu nyingi zilizokaukia, kwa kutumia mikono miwili, alizoa udongo uliokaukia damu, kisha akapiga magoti na kuuinua juu, akazungumza maneno fulani kama anayenuiza jambo kisha akausogeza ule udongo puani kwake, akaunusa kisha akapiga chafya mfululizo.
Hakusema chochote baada ya hapo zaidi ya kuinuka na kuanza kutembea kwa haraka kuelekea upande wa kusini, kama anayetafuta kitu, baba yake Rahma alinipa ishara kwamba tumfuate, akawa anatembea kwa kasi huku akiongea maneno ambayo sikuwa nayaelewa.
Alivuka barabara, na sisi tukawa tunamfuata, akawa anazidi kuongeza kasi kiasi kwamba nililazimika kuwa nakimbia ili kwenda nao sawa. Bahati nzuri ni kwamba tulikuwa tukielekea upande tofauti kabisa na kule kulikokuwa na msiba.
Ilifika mahali akachepuka na kuingia vichakani, safari hii akaanza kutimua mbio, sote tukawa tunakimbia kumfuata. Japokuwa ilikuwa ni usiku, tulikimbia vichakani kwa muda mrefu sana, baadaye tukatokezea kwenye makaburi mengi, baba akawa anazunguka huku na kule na mwisho aliishia kwenye kaburi moja lililoonesha kuwa jipya.
“Amezikwa hapa,” alisema baba huku akigeuka huku na kule, nikawa natetemeka kwa hofu, sikujua nini kinachoenda kutokea.
“Simama kwa kule,” alisema baba huku akinielekeza kusimama upande uliokuwa na msalaba ambapo kimsingi ndiyo kichwani. Nilifanya hivyo, baba yake Rahma akasimama upande wa miguuni na baba akasimama katikati, juu ya kaburi.
Baada ya kusimama hapo, aligeuka huku na kule kama anayetafuta kitu kisha akashuka kutoka pale juu ya kaburi na kunifuata, akawa ananiongelea sikioni.
“Huyu amezikwa leo, katika sheria za jamii yetu, anaruhusiwa kutolewa kafara kwa hiyo tutamchukua huyu badala ya Sadoki, kule tutarudi siku nyingine kwa sababu kuna mambo hayakwenda sawa kwa sababu yako, sasa ukifanya ujinga tena na hapa, hakuna wa kumlaumu,” alisema baba.
Hofu ikazidi kuongezeka kwenye moyo wangu. Kama nilivyoeleza, hakuna sehemu niliyokuwa naiogopa kama makaburini, nikawa nahisi kama mwili na akili vinatengana. Kibaya zaidi ilikuwa ni usiku na nimeshawahi kusikia kwamba makaburini nyakati za usiku kunakuwa na mambo mengi sana ya ajabu, sikuelewa baba anavyosema tunamchukua yule dereva bodaboda aliyefariki kwenye ajali, alimaanisha nini.
Ninavyojua mimi, huwezi kufukua kaburi na kutoa maiti kwa sababu kwanza siyo kazi nyepesi lakini pia, lazima watu watakuona ukiwa unalifukua kwa sababu makaburi mengi huwa yanakuwa na ulinzi, na kama si hivyo, mizimu mibaya iliyopo makaburini lazima itakudhuru tu. Sikuelewa malengo ya baba ni nini lakini kama mwenyewe alivyokuwa anasisitiza kwamba lengo ni kunisaidia mimi, ilibidi nitulie kuona mwisho wake.
Baada ya kuzungumza na mimi, alimfuata baba yake Rahma, wakawa wanajadiliana jambo pale, wakazungumza kwa zaidi ya dakika mbili kwa sauti ya chini kiasi kwamba sikuwa nikisikia walichokuwa wanakisema.
Baada ya hapo, baba yake Rahma alinifuata na kuniambia natakiwa kuvua nguo zote na kukaa juu ya kaburi kwa sababu kazi iliyokuwa inaenda kufanyika, si ya kitoto. Nilishtuka, yaani nivue nguo halafu nikae juu ya kaburi? Mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio tena.
Ni kama baba yake Rahma alinielewa jinsi nilivyokuwa na hofu, akaniambia sitakiwi kuwa na hofu yoyote kwa sababu kwenye jamii yao, kukaa bila nguo ni kitu cha kawaida kabisa, isitoshe wao ni baba zangu ambao wananijua tangu nikiwa mtoto mchanga, kwa hiyo lazima nifanye walichoniambia.
Ilibidi nikubaliane naye maana baba alikuwa akisisitiza kwamba muda unakwenda. Nikasogea pembeni na kuvua nguo zote, nikajiziba sehemu ya mbele kwa mikono yangu na kupanda kwenye tuta la lile kaburi, nikawa natetemeka mno.
Baada ya kukaa juu ya tuta la kaburi, nikiwa nimeupa msalaba mgongo kama nilivyoelekezwa, baba na baba Rahma, mmoja akiwa amesimama upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni, walianza kuimba nyimbo za kutisha kwa kupokezana, akiimba baba, baba yake Rahma anaitikia, wakaendelea hivyo kwa dakika kadhaa kisha wakaanza kulizunguka lile kaburi, kutoka kulia kwenda kushoto.
Walifanya hivyo kwa dakika kadhaa, baadaye baba akaniambia nisimame. Nilifanya hivyo huku nikijiziba kwa soni, akanielekeza kuelekea upande ule wa kichwani niliokuwa nimesimama awali, kisha akaniambia niwe makini kutazama anachokifanya.
Milio ya bundi na ndege wengine wa usiku, iliendelea kusikika na kufanya hali iwe ya kutisha mno pale makaburini. Baba alionesha kwa ishara kwamba natakiwa kupiga makofi na kupiga mguu wangu wa kushoto chini kwa nguvu, na vyote vifanyike kwa wakati mmoja.
Alinihesabia kwa alama za vidole kisha akaniruhusu, nikapiga makofi kwa nguvu na wakati huohuo nikapiga kishindo cha nguvu. Alinionesha kwa ishara kwamba natakiwa kufanya hivyo mara tatu, nikarudia mara ya pili, kisha nikafanya kwa mara ya tatu.
Kilichotokea baada ya kufanya hivyo kwa mara ya tatu, kilinifanya nihisi kama mwili wangu unakufa ganzi kwa hofu, sijawahi kushikwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kama baba asingeniwahi, huenda ningedondoka kama mzigo chini maana mwili wote uliisha nguvu.
Japokuwa ilikuwa ni usiku, tena nikiwa sina nguo na kulikuwa na baridi kali, nilihisi kijasho chembamba kikinitoka, ama kweli duniani kuna mambo na ukishangaa ya Musa, utayaona ya Firauni.
Je, nini kilitokea? Usikose next issue.
 
UOTE="jisanja, post: 25346693, member: 183064"]Inapatikana wapi mkuu maana jamaa anatuua na arosto[/QUOTE]
Ingia kwenye website ya global publishers, kwenye kipengele cha hadithi.ila alipoishia ndio hapo hapo ilipoishia na huko.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom