Simulizi: Makaburi ya wasio na hatia

Simulizi: Makaburi ya wasio na hatia

(Makaburi ya Wasio na Hatia)- 65
ILIPOISHIA:
Nilihisi kama kuna kitu kinanilamba hivi, nikaanza kutetemeka huku nikiendelea kujikausha nisisababishe mtikisiko wa aina yoyote, nilipozidi kuvuta utulivu, nikahisi kuna kitu cha baridi kinatingishikatingisha upande ule niliokuwa nalambwa, mapigo ya moyo yakawa yanadunda kama nimetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
SASA ENDELEA...

Nilitulia tuli huku nikiendelea kutetemeka, mara nikaanza kuhisi kile kitu kikitambaa na kunivuka mwili, kutoka upande mmoja kuelekea upande mwingine. Japokuwa kulikuwa na giza niliweza kukitambua vizuri kiumbe hicho kuwa alikuwa ni nyoka. Hata sijui ushujaa wa kutulia vile niliupata wapi maana kama nilivyowahi kusema, hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa maishani mwangu kama nyoka.
Basi yule nyoka mdogo alinitambuka na kupotelea upande wa pili wa kitanda, nikashusha pumzi ndefu kisha kwa tahadhari kubwa nikainuka pale nilipokuwa nimelala, nikasimama kwenye uchago wa kitanda na kujivuta mpaka kwenye swichi ya taa, nikaiwasha.
Japokuwa kulikuwa na baridi kali ya usiku, mwili wote ulikuwa umelowa jasho, nikajitazama kwenye lile jeraha langu ubavuni, nikashtuka kugundua kwamba lilikuwa limeanza kujichimba na kutengeneza kidonda. Kumbe wakati yule nyoka akinilamba, alikuwa akitoa ganda la juu ambalo lilikuwa likiashiria kuanza kupona, nikashtuka mno huku nikiwa sielewi nini hatma yangu.
Cha ajabu ni kwamba safari hii sikuwa nasikia maumivu kabisa. Nikageuka na kutazama pale kitandani, hapakuwa na kitu zaidi ya shuka, nikalivuta na kujaribu kujikung’uta nikihofia kwamba yule nyoka anaweza kuwa bado yupo lakini hakukuwa na chochote.
Nikashuka na kuchungulia chini ya kitanda, pale palipokuwa na ule mfuko uliotengenezwa kwa kipande cha gunia. Cha ajabu, ulikuwa umefungwa vilevile, nikashusha pumzi ndefu na kurudi kitandani.
Kama ingekuwa amri yangu, siku hiyo nisingelala kabisa lakini usingizi ulikuwa ukinitesa sana. Nilichoamua, ilikuwa ni kufungua mlango na kuuegesha ili kama hali ikitokea tena, nitoke mbio mpaka nje. Sikuzima tena taa kama mwanzo, nikataka kuona nini kitatokea tena.
Nilipojiegesha kitandani tu, usingizi mzito ulinipitia, nilipokuja kuzinduka, tayari kulishakuwa kumepambazuka kabisa, harakaharaka nikashuka kitandani na kuchungulia kule chini ya kitanda.
Cha ajabu ni kwamba ule mfuko haukuwepo, niliangaza kila kona lakini sikuuona, nikahisi labda yule nyoka alitambaa nao na kujifuicha kwenye nguo zilizokuwa chini, nikapekua kila sehemu lakini sikuona dalili zozote.
“Unatafuta nini?” sauti ya baba ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, naye akawa ananitazama.
“Kuna kitu kimenitokea usiku sijakielewa.”
“Kitu gani?” baba aliniuliza kwa mkato, ikabidi niinue shati na kumuonesha pale ubavuni palipokuwa na kidonda, nikaanza kumueleza jinsi nilivyoshtuka na kukutana na mauzauza ya yule nyoka chumbani kwangu na jinsi alivyokuwa akinilamba pale kwenye kidonda.
Tofauti na nilivyotegemea, baba alicheka kwa dharau, akaniambia kama naipenda pepo kwa nini naogopa kufa? Sikumuelewa anamaanisha nini, ikabidi nimhoji, akanijibu kwa mafumbo na kutoka zake, akaniacha nikiwa na mawazo tele kichwani mwangu.
Baadaye nilitoka na kwenda kuoga, nikarudi na kujiandaa kisha nikatoka na kwenda kibarazani ambako baba yake Rahma alikuwa amekaa akisoma kitabu. Nilipomsalimia, aliacha kila alichokuwa anakifanya na kuitikia salamu yangu kwa uchangamfu.
Kwa jinsi alivyonipokea, nilipata nguvu ya kumuuliza kwa kina kuhusu mambo mbalimbali ambayo nilikuwa siyaelewi, akaniambia jambo ambalo lilinishtua sana. Aliniambia kwamba usiku wakati tukirejea nyumbani kutoka Bagamoyo, kuna sehemu tulipita na kusikia mwanamke akipiga kelele za kuomba msaada.
Akaniambia kwenye msitu ule ndipo mahali watu waliochagua njia kama yangu, ya kuwa na utajiri wa kichawi, wanapoenda kutolea makafara yao, akaniambia hata mimi mambo yakichanganya nitakuwa naenda kutoa kafara kwenye msitu huo. Nilishtuka sana kutokana na maneno aliyoniambia, nikawa nahisi kama nipo ndotoni.
“Ukiwa mwanachama wa kawaida, unatoa kafara za kawaida, kama ambazo tayari wewe umeshazitoa, si unakumbuka umeshatoa mara ngapi?” aliniuliza baba yake Rahma huku akigeuka huku na kule kuhakikisha hakuna anayetusikiliza.
“Mara mbili!” Nilimjibu. Kiukweli mpaka wakati huo tayari nilikuwa nimesababisha matukio yaliyoondoa nafsi za watu wasio na hatia wawili, la kwanza lilikuwa ni lile la ajali iliyoyakatisha maisha ya yule mtoto wa Mlandizi na ya pili ikiwa ni ile ya bodaboda aliyepata ajali mbaya baada ya kugongana na mimi, mita chache kutoka pale kwenye msiba wa yule mtoto.
Jaribio lingine la kumtoa kafara Sadoki, rafiki yangu kipenzi wa Chunya lilikuwa limegonga mwamba huku ikibakia kidogo nidhalilike kutokana na nguvu ya upako aliyokuwa nayo Sadoki na mama yake.
“Sasa ka njia uliyochagua, utatakiwa kuwa unatoa sadaka za damu mara nyingi kadiri iwezekanavyo, ndiyo maana kuanzia mwanzo nilikwambia kwamba utajiri huo ni mgumu sana, bora ubaki maskini,” alisema baba yake Rahma.
Japokuwa kweli niliogopa kwa kiasi fulani, lakini tamaa ya utajiri ilishawaka ndani ya moyo wangu kiasi kwamba sikuwa nataka kusikia jambo lingine lolote la kunirudisha nyuma. Nilimkatisha kijanja na kumuuliza kuhusu kile kilichotokea usiku kuhusu yule nyoka.
Alinifafanulia kwamba ni kawaida ya mtu yeyote anayemiliki au anayetaka kumiliki utajiri kwa nguvu za giza, kufuga mnyama huyo na kuongeza kwamba chakula chake kikubwa, ukiachana na vyakula vya kawaida ambavyo nyoka hupewa, ni lazima kila siku awe anakunywa damu yangu.
“Mungu wangu!” nilishtuka sana na kujikuta nimelitaja jina la Mungu. Kwa maneno hayo ya baba yake Rahma, ni kwamba kile kilichotokea usiku haukuwa muujiza na kwamba ni jambo ambalo litakuwa linatokea kila siku kwa kipindi chote cha maisha yangu, nilijikuta nikichoka.
“Kadiri utakavyokuwa unamtunza vizuri na kumpa mahitaji yake yote, ndivyo atakavyokuwa anaongezeka ukubwa na kadiri atakavyokuwa anaongezeka ndivyo utajiri wako utakavyokuwa unaongezeka kwa hiyo ukiwa mvumilivu, unaweza kufika mbali,” alisema baba yake Rahma, nikawa na shauku kubwa ya kuendelea kumuuliza, hasa kuhusu nyoka huyo lakini mazungumzo yetu yalikatishwa na Rahma.
“Kaka Togo za asubuhi? Naomba unisindikize dukani mara moja,” alisema Rahma kwa heshima, baba yake akanipa ishara kwamba niende, nikainuka na kutoka naye.
Tofauti na siku zote, pale nje palikuwa peupe kabisa, wale madereva Bajaj na bodaboda hawakuwepo, Rahma akaniambia eti walikuwa wameamua kuhamisha kituo chao na kukipeleka sehemu nyinginekwa sababu pale hakuna abiria.
Nilijikuta nikicheka tu maana ukweli haukuwa hivyo, moyoni nilibaki nikijiuliza, ina maana nimekuwa na nguvu kiasi cha kuwatisha watu kiasi kile?
“Mlikuwa mnazungumza nini na baba? Maana naona mnaelewana sana, sijawahi kumuona baba yangu akiwa karibu na mtu kama ilivyo kwako, siku hizi hata mimi hanipendi kama anavyokupenda wewe,” Rahma alisema wakati tukitembea taratibu kuelekea dukani.
Sikumjibu kitu chochote cha maana zaidi ya kuleta masihara kwa sababu jana yake nilipotaka kumweleza ukweli aliniona kama nimechanganyikiwa.
“Mbona mimi nakuuliza maswali ya msingi wewe unanijibu kimasihara?” Rahma alinihoji, ikabidi niache kuchekacheka na kuvaa ‘usiriasi’, nikamwambia hata mimi mwenyewe sielewi.
“Tunaenda wapi kwani?”
“Nataka twende pale tulipokaa jana, nahitaji kuzungumza na wewe,” aliniambia, moyo wangu ulisita kwani niliamini naweza kukutana na hali kama ya jana Rahma akaendelea kuniona mwendawazimu. Hata hivyo nilishindwa kumkatalia, tukaelekea mpaka pale dukani.
Cha ajabu, tulipofika tu, yule dada tuliyemkuta jana yake, aliponiona tu alikurupuka kwa kasi na kukimbia huku akiacha mlango wazi. Hakuwa amevaa nguo na nadhani hiyo ndiyo sababu iliyomfanya akimbie, Rahma akawa anashangaa akiwa haelewi kinachoendelea.
“Mbona unavuja damu nyingi hapo, umepatwa na nini?” alisema Rahma, nilipojitazama pale ubavuni, nilishtuka sana baada ya kuona damu nyingi nzito zikiwa zimenitoka bila mimi mwenyewe kujua chochote na kulowanisha kabisa shati langu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 66
ILIPOISHIA:
“Mbona unavuja damu nyingi hapo, umepatwa na nini?” alisema Rahma, nilipojitazama pale ubavuni, nilishtuka sana baada ya kuona damu nyingi nzito zikiwa zimenitoka bila mimi mwenyewe kujua chochote na kulowanisha kabisa shati langu.
SASA ENDELEA...

Sikujua nini cha kufanya, nilitamani nirudi haraka ndani kabla mambo hayajazidi kuharibika lakini Rahma akaning’ang’ania, kwanza akitaka kujua kwa nini yule muuzaji alikuwa akinikimbia lakini pili nini kimetokea mpaka shati langu lilowe damu kiasi kile.
Kiukweli sikuwa na majibu, nikawa naendelea kuhangaika kuzuia damu isiendelee kunitoka. Rahma alivua kitenge chake na kunipa, naye akawa ni kama haelewi kilichokuwa kinaendelea.
Tukiwa tunaendelea kuhangaika, mara nilisikia ile hirizi yangu mkononi ikinibana sana, nikajua mambo yameshaharibika. Nilishaambiwa kwamba nikiona inanibana ghafla, ujue mahali nilipo kuna mtu mwenye nguvu za giza na kuna jambo baya anataka kulifanya.
Harakaharaka nilifanya kama nilivyokuwa nimeelekezwa, niliunganisha kidole gumba na kidole kidogo kwenye mkono wa kushoto, nikafanya hivyo kwenye mkono wa kulia, nikaviminya kwa nguvu huku nikigeuka huku na kule kuangalia ni nani atakayeonesha dalili zisizo za kawaida.
Nilifundishwa kwamba kama kuna mtu yeyote anataka kukujaribu kwa nguvu za giza, ukifanya hivyo basi umemkomesha na kama nguvu zake ni ndogo, anaweza kuumbuka hadharani.
“Mmefuata nini hapa?” sauti ya mwanaume ilisikika kutoka kwenye lile duka, wote tukageuka kutazama ni nani aliyekuwa akitusemesha.
“Shikamoo mzee!” Rahma alimsalimu mwanaume mzee aliyekuwa ndani ya duka hilo kwa uchangamfu. Ilionesha wanafahamiana. Badala ya kujibu, yule mzee alimuuliza Rahma mimi ni nani na nimefuata nini pale.
“Ni kaka yangu, anaitwa Togo, tuna mazungumzo ya kifamilia tulitaka tunywe soda huku tukiendelea kuzungumza.”
“Hapana! Hatuuzi soda hapa, ukitaka huduma uje peke yako, siyo na huyo,” alisema mwanaume huyo huku akiwa amenikazia macho, Rahma akashtuka na kunigeukia. Kadiri yule mzee alivyokuwa akizidi kunitazama, na mimi ndivyo nilivyozidi kuminya vidole huku nikiwa nimemkazia macho kwani nilihisi ndiye mbaya wangu mwenyewe.
“Ondokeni! Ondokeni,” alisema mzee huyo kwa kupaza sauti, wateja wengine waliokuwa pembeni wakawa wanashangaa kwa sababu hakukuwa na jambo lolote baya tulilofanya. Rahma aligeuka na kutaka kuondoka huku akishangaa iweje mzee huyo atubadilikie kiasi hicho lakini mimi wala sikutishika kwa sababu nilishaanza kuiona hofu ilivyomjaa ghafla.
Niliendelea kumtazama huku nikiendelea kuminya vidole vyangu kwa nguvu, nikashangaa kumuona akianza kutokwa na jasho jingi huku akitingisha kichwa kama kunipa ishara kwamba niache nilichokuwa nakifanya. Mara alianza kutetemeka, jasho likazidi kumtoka na kufumba na kufumbua, akaanza kutapatapa kama anayetaka kupandwa na kifafa, akadondoka chini kama mzigo, puh!
Kitendo hicho kilinishtua sana kwani alipodondoka tu, ile hirizi nayo iliacha kunibana, sijui nini kilinituma niangalie juu ya mlango wa kuingilia kwenye duka hilo ambalo lilikuwa limejaza vitu vingi vya thamani, nikashtuka mno kuona kitu kama fuvu la mtoto mdogo likiwa limeninginizwa juu ya mlango.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilisikia sauti ya baba kutokea nyuma. Kumbe wakati nikiendelea kuvutana na yule mzee, Rahma alikimbilia nyumbani na kwenda kumuita baba yake pamoja na baba, harakaharaka wakaja.
“Unafanya nini Togo?” baba aliniuliza kwa sauti ya chini, nadhani hakutaka asikike kwa watu ambao walishaanza kukusanyika kwa lengo la kutoa huduma ya kwanza na kutaka kujua nini kimetokea.
“Hamna kitu baba, tulikuwa tunataka kuagiza soda, hakuna kingine,” nilisema huku nikiendelea kukitazama kile kitu kama fuvu.
“Ondoka haraka, hili eneo si salama, fanya haraka,” alisema baba, nikageuka na kukutana ana kwa ana na Rahma ambaye naye alikuwa ananionesha ishara ya kutaka tuondoke haraka eneo hilo maana tayari watu walishajaa.
Nikarudi kinyumenyume, nikajichanganya kwenye umati wa watu waliokuwa wakiendelea kujaa, Rahma akanishika mkono na kuanza kunivuta haraka tuelekee nyumbani.
“Togo, kuna kitu unanificha si ndiyo? Nataka leo unieleze ukweli, ngoja kwanza nikaangalie kinachoendelea, nakuomba usitoke, baba amesema ikibidi nikufungie chumbani kwako na funguo,” Rahma aliniambia huku akipumua kwa kasi, akarudia kunisisitiza kwamba nisitoke kisha harakaharaka akaondoka.
Nilikaa kitandani na kuvua shati ambalo lilikuwa limelowa damu, nikawa najitazama pale damu ilipokuwa inanitoka. Ilikuwa ni kwenye kile kidonda changu, nikawa nashangaa iweje nitokwe na damu nyingi kiasi kile wakati sikuwa nimejitonesha? Nilijiuliza maswali mengi ambayo yote hayakuwa na majibu.
“Ina maana yule ndiyo mmiliki wa lile duka? Kwa nini anatumia uchawi kwenye biashara yake? Kile pale mlangoni ni fuvu kweli? Ina maana alimuua mtoto ili kuvutia wateja kwenye biashara yake?
“Kwa nini yule mdada amekimbia tena kwa mara nyingine, tena akiwa mtupu? Ina maana ndiyo mchezo wake kuuza akiwa hana nguo mwilini?” niliendelea kujiuliza kwa sauti ya chini, maswali yalikuwa mengi sana ndani ya kichwa changu, hata sikujua ni nani atakayenipa majibu.
Dakika kadhaa baadaye, niliwasikia baba na baba yake Rahma wakirejea wakiwa wanazungumza kwa sauti za chinichini. Muda mfupi baadaye, Rahma naye akarejea na kuja moja kwa moja mpaka chumbani kwangu.
“Vipi, nini kimeendelea?” nilimuuliza Rahma huku nikisimama, nikiwa kifua wazi, akashusha pumzi ndefu na kabla hajanijibu chochote, macho yake yakatua kwenye ile hirizi niliyokuwa nimeivaa mkononi, akashtuka kidogo kisha akahamishia macho pale kwenye jeraha dogo ambalo bado lilikuwa likichuruzika damu.
“Hapo umefanya nini?” alisema huku akinisogelea na kuinama kunitazama vizuri, nikarudi nyuma huku nikimuonesha ishara kwamba asiniguse. Akanitazama usoni na kuyagandisha macho yake, tukawa tunatazamana.
“Hizo damu zimetoka wapi?” sauti ya baba ndiyo iliyotuzindua. Kumbe wakati nikipita pale koridoni kuelekea chumbani kwangu, matone ya damu yalikuwa yakidondoka chini mpaka kwenye mlango wangu.
Alipoingia na kunikuta nipo kifua wazi, tukitazamana na Rahma, alinisogelea na kitu cha kwanza, macho yake yalitua pale kwenye jeraha langu, akapatazama kwa sekunde kadhaa kisha akanitazama usoni, naye tukawa tunatazamana.
“Rahma hebu kamuite baba yako haraka,” alisema baba, harakaharaka Rahma akatoka.
“Haya ndiyo mambo niliyokuwa siyataki mimi, umeona huo utajiri unaoutaka ulivyo na mambo magumu? Hutakiwi kutembeatembea mpaka zipite siku saba, siku nyingine utakutana na magwiji watakuua, una bahati yule mzee bado hajakomaa kwenye haya mambo,” alisema baba, akaingiza mkono mfukoni na kutoa karatasi alilokuwa amelikunja, akalifungua na kutoa ungaunga mweusi, akachukua kidogo na kunipaka huku akinitaka kuwa makini.
“Naona na wewe umeanza kuonesha ukidume wako, unawaona watu si ndiyo?” alisema baba huku akiachia tabasamu hafifu. Ilikuwa ni nadra sana kwa baba kutabasamu, akanipigapiga mgongoni huku akiendelea kutabasamu.
Muda mfupi baadaye, baba yake Rahma aliingia, nikashangaa wote wanacheka na kugongesheana mikono, naye akarudia kuniambia kwamba niwe makini na nisiende tena kwenye lile duka, kama nahitaji soda ni bora niagize niletewe nyumbani. Hawakukaa sana, wakatoka na kuniacha mle chumbani, sekunde chache Rahma akaingia tena.
“Nataka uniambie ukweli Togo, nini kinachoendelea?”
“Hujanijibu swali langu kuhusu kilichotokea.”
“Watu wanasema eti yule mzee ni mchawi na biashara zake amekuwa akiziendesha kwa uchawi sasa leo amekutana na kiboko yake, wamempeleka kwa mganga lakini hali yake siyo nzuri,” alisema rahma, nikashusha pumzi ndefu na kukaa vizuri, Rahma akanisogelea huku bado akionesha kuwa na shauku kubwa ndani ya moyo wake.
“Togo wewe ni mchawi?” Rahma aliniuliza swali ambalo lilinishtua mno moyo wangu, nikamtazama, akarudia tena swali lake huku akisisitiza kwamba anataka mimi mwenyewe ndiyo nimweleze ukweli kama kweli nampenda.
Nikashusha pumzi ndefu huku nikijiuliza, nimweleze ukweli? Uamuzi niliofikia, ilikuwa ni kumweleza tu maana hayo ndiyo yalikuwa malengo yangu tangu jana yake, sikutaka kujali ataupokeaje ukweli, nikameza mate na kumtazama.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom