Simulizi: Makaburi ya wasio na hatia

SEHEMU YA 51



ILIPOISHIA:
“Sikuwahi kudhani kwamba unaweza kuwa na nguvu kubwa kiasi hicho, hongera sana, utanifaa sana wewe,” alisema huku akipitisha mkono wake mmoja begani kwangu kichovu kisha akanigeukia, tukawa tunatazamana. Katika hali ambayo sikuitegemea hata kidogo, nilishangaa yule mwanamke akinibusu, tena mdomoni, nikashtuka mno.
“Hongera sana, ila inabidi upunguze mambo ya wanawake, utakuwa na nguvu zaidi ya hizi ulizonazo,” aliniambia huku akinitazama usoni.
SASA ENDELEA…
“Sijakuelewa,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kukaa vizuri pale juu ya zulia. Bado si Raya, Shamila wala Firyaal waliokuwa wamezinduka.
“Utanielewa tu,” inabidi kwanza tukaoge kuondoa uchovu halafu tuwasaidie na hawa nao warudi kwenye hali yao ya kawaida, tuna kazi nyingine ya kumsaidia Shenaiza, ni lazima arudiwe na fahamu zake, tena ikiwezekana haraka iwezekanavyo,” alisema mwanamke huyo kisha akapiga miayo mfululizo na kujinyoosha.
“Kwa kawaida, kila binadamu huwa anazalisha nguvu, nadhani hilo nilishakueleza kutoka mwanzo ingawa ni wachache sana wanaolitambua hili.
“Yaani ni kama kupepesa kope, unajua ni mpaka mtu akukumbushe kwamba muda wote macho yako yanapepesa kope ndiyo unakumbuka?” alisema, nikawa sioni chochote kipya kwenye mazungumzo yake kwa sababu ni jambo ambalo nilikuwa nimeshalisikia sana maishani mwangu kwamba kila binadamu anazalisha nguvu zisizoonekana.
“Nguvu tunazozalisha huwa zinatengeneza kitu kinachoitwa aura ambacho wengine huwa wanakiita ni mwili usioonekana juu ya mwili unaoonekana. Sasa kwa mtu mwenye utambuzi wa nguvu hizi, anao uwezo wa kuuona mwili huu.
“Kwa mtu ambaye anaishi maisha ya kitakatifu, yaani hanywi pombe, havuti sigara, hafanyi zinaa, hawasemi vibaya watu wengine, hana wivu wala kinyongo, ana upendo wa dhati kwa watu wote na ambaye moyo wake uko safi, hii aura huwa na kawaida ya kung’aa sana. Mtu akikutazama tu anaiona nguvu inayokuzunguka.
“Lakini vilevile kama mtu anaishi maisha ya hovyo, pengine ni mlevi sana, anafanya ngono hovyohovyo, ana wivu, hasira, vinyongo na tabia mbayambaya, kwa kawaida huwa aura yake inafifia sana na kama una utambuzi wa nguvu hizi, ukimtazama tu unamjua ndiyo maana nilikwambia vile,” alisema yule mwanamke na kuzidi kunishangaza.
Kitu alichokisema sikuwa nimewahi kukisikia sehemu yoyote, nikabaki nimepigwa na butwaa, akaendelea:
“Japokuwa watu wengi huwa hawaelewi kuhusu aura kwa hiyo hawajui umuhimu wa kuishi kitakatifu hata kama huna dini, siyo kitu cha mchezomchezo. Aura ya mtu huanza kuishi kabla mtu hajazaliwa na huendelea pia mpaka mtu anapokufa. Ndiyo maana mtoto anapokaribia kuzaliwa, tafiti zinaonesha kwamba huwa ana uwezo wa kuelewa kinachoendelea kwenye ulimwengu wa nje.
“Hii ni kwa sababu tayari mwili wake ambao hauonekani unakuwa umeshaingia kwenye ulimwengu wa kawaida. Akishazaliwa, huwa inatakiwa mwili wake halisi uungane na hii aura na hiyo hufanyika katika kipindi cha siku arobaini tangu mtoto azaliwe ndiyo maana kuna tamaduni nyingi kwamba mtoto anatakiwa kuanza kutolewa nje baada ya siku arobaini kwani pale inakuwa tayari aura yake na mwili halisi vinakuwa vimeungana hivyo anakuwa na kinga dhidi ya mambo mabaya yasiyoonekana kwenye ulimwengu wa kaiwada.
“Hiyo pia hutokea pale mtu anapokufa ambapo nafsi inapotengana na mwili, aura huwa inaendelea kuishi mpaka baada ya siku arobaini ndiyo nayo hutoweka, ndiyo maana pia huwa kuna tamaduni za kufanya arobaini ya marehemu kwani pale ndiyo uhai huwa unakuwa umefikia mwisho.”
Maelezo hayo yalinifanya nikune kichwa kwani siyo siri yalikuwa yamenichanganya sana akili. Ni mambo ambayo sikuwahi kuyasikia kabla lakini kwa jinsi alivyokuwa akiyafafanua, ilionesha dhahiri kwamba ni kweli. Hata mimi sikuwahi kupata jibu la kwa nini mtoto anatakiwa atolewe nje baada ya siku arobaini tangu azaliwe na kwa nini mtu akifa, msiba huwa unahitimishwa baada ya siku arobaini.
“Lakini mamdogo…”
“Usiniite mamdogo, ningependa zaidi uniite kwa jina langu halisi ambalo ni watu wachache huwa wanalijua. Nina majina mengi lakini jina langu halisi ni Junaitha,” alisema huku akiinuka pale alipokuwa amekaa.
“Hakuna cha lakini… punguza wanawake ili aura yako ing’ae na kukuongezea nguvu, mimi sijui nina mwaka wa ngapi simjui mwanaume,” alisema huku tayari akiwa amesimama, akanipa mkono kama ishara ya kutaka anisaidie kuinuka.
Nilibaki kumtazama tu usoni, mambo mengi yalikuwa yakipita ndani ya kichwa changu.
“Mbona unanitumbulia macho? Amka twende ukaoge, bado kuna kazi kubwa leo,” alisema yule mwanamke, nikampa mkono, akanishika na kunivuta kidogo, nikasimama.
“Halafu inatakiwa pia uwe makini na vyakula unavyokula, inaonesha mwili wako hauna uzito unaotakiwa, hata hao wanawake unaotembea nao hovyo huwa unawaridhisha kweli? Wanaume wa siku hizi wana tatizo kubwa la upungufu wa nguvu za kiume, na wewe usije kuwa miongoni mwao,” alisema huku akitabasamu.
Japokuwa mwenyewe alichukulia kama masihara lakini kwa hulka za kiume, niliona kama amenidharau sana. Maneno yake ni kama yalikuwa yakihitaji nifanye kitu fulani kumthibitishia kwamba sikuwa mtu wa mchezomchezo bali mwanaume niliyekamilika.
Nilipounganisha na tukio la yeye kunibusu kwenye midomo yangu wakati akinipongeza, akili nyingine zilianza kupita ndani ya kichwa changu.
“Kwa hiyo unaishije bila mume?”
“Kwani wewe unapata faida gani kubadilishabadilisha wanawake?” aliniuliza swali juu ya swali ambalo lilinifanya nijiulize sana kwa nini alikuwa akinikomalia kuhusu suala la mimi kuwa na wanawake wengi. Elimu aliyonipa ilikuwa imetosha kunifanya nijitambue lakini kwa nini alikuwa akiendelea kuulizauliza kuhusu mimi kuwa na wanawake? Sikupata majibu.
“Mbona unakuwa mkali sana kwangu Junaitha? Au kuna kitu nimekuudhi?”
“Ndiyo umeniudhi, kwa nini kijana mtanashati kama wewe usitafute mwanamke mmoja tu anayejitambua ukatulia naye?” nilijikuta nikishindwa kujizuia, nikaangua kicheko kwani tayari nilishaanza kupata picha ya kilichokuwa kikiendelea ndani ya kichwa chake.
“Kwa hiyo unanidharau si ndiyo? Yaani mi naongea mambo ya maana wewe unacheka,” alisema, akatoka na kuniacha nimesimama palepale, nikiwaangalia wale waliokuwa wamelala juu ya zulia, kila mmoja akiwa hajitambui kwa uchovu.
“Hebu njoo huku,” nilisikia sauti ya Junaitha ikitokea chumbani kwake, harakaharaka nikatoka pale na kuelekea kule sauti ilikokuwa inatokea.
“Ingia tu mlango upo wazi,” alisema, nikageuka huku na kule kwanza kwa sababu sikuona kama ni heshima kwa mtoto wa kiume kuingia chumbani kwake, hasa ukizingatia ukweli kwamba alikuwa amenizidi sana umri. Nikapiga moyo konde na kuingia ndani ya chumba hicho cha kisasa kilichokuwa na vitu vingi vya thamani.
“Chukua taulo pale kabatini ingia bafuni ukaoge,” alisema akiwa amekaa juu ya kitanda kikubwa cha kisasa akihangaika kufungua zipu ya gauni alilokuwa amevaa, nikaelekea pale kwenye kabati aliponielekeza, nikachukua taulo na kuanza kuelekea kwenye lile bafu la ndani kwa ndani kule chumbani kwake.
Nililazimika kuingia na nguo zote bafuni kwani nilikuwa naona aibu kuvua hata shati mbele ya macho yake.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 52


ILIPOISHIA:
Lakini ni hapo pia nilipokumbuka ile ajali nyingine ya bodaboda niliyoisababisha na pia nikakumbuka kisanga cha dereva wa Bajaj aliyekuwa akipaki jirani na hapo kwa akina Rahma na jinsi nilivyomkomesha asubuhi hiyo. Sikujua kama amesharudi au la na sikujua siku atakaponiona tena atasema nini.
Nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo, nilisikia mlango ukifunguliwa, Rahma akaingiza kichwa na kuchungulia ndani, macho yangu na yake yakagongana.
SASA ENDELEA…
“Togo!” aliita Rahma kwa sauti ya udadisi huku akiingia ndani na kuurudishia mlango taratibu, nikakaa vizuri kumsikiliza maana nilikuwa najua kabisa kwamba alikuwa na maswali mengi ya kuniuliza kutokana na mabadiliko makubwa niliyokuwa nayo kwa siku kadhaa zilizopita.
“Najua kwamba nalazimisha mapenzi kwako, najua kwamba unajisikia aibu kuwa na mpenzi ambaye amekuzidi umri na najua pia kwamba kama isingekuwa mimi kukuanza usingekuwa na mawazo yoyote ya kutoka kimapenzi na mimi kwa sababu hunipendi,” alisema Rahma kwa sauti ya kulalama mno, akionesha kuwa na maumivu makali ndani ya moyo wake.
“Leo nataka uniambie jambo moja tu, nimechoka kuteseka kimapenzi, kwa kipindi chote tangu nikiwa msichana mdogo nimekuwa nikijitunza na kujiheshimu sana, sasa isiwe kwa sababu nimetokea kukupenda basi ukaanza kunitesa kwa makusudi na kunidhalilisha, nataka uniambie kwamba hunitaki ili nijue moja,” alisema Rahma, safari hii machozi yakiwa yanamchuruzika na kulowanisha uso wake mzuri.
Nilijisikia kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wangu kwa jinsi Rahma alivyokuwa akilalamika na kulia kwa sababu yangu. Rahma hakustahili kulia kwa sababu yangu kwa sababu maskini ya Mungu hakuwahi kunifanyia jambo lolote baya na ndani ya kipindi kifupi tu nilichokaa naye, alinionesha mapenzi ya dhati kabisa kutoka moyoni mwake.
Mimi pia sikuwa mtu wa kujihusisha na mambo ya mapenzi na Rahma ndiye aliyekuwa mwanamke wangu wa kwanza tangu nipate akili za kikubwa, na kipindi hichohicho pia nikakutana na Isrina, kwa hiyo siyo kweli kwamba nilikuwa nikimtesa kwa makusudi.
“Naongea na wewe, nataka uniambie jambo moja tu,” alisema Rahma na safari hii, alinishika mkono wangu na kuuvuta. Katika hali ambayo hakuna aliyetegemea, alinishika pale nilipokuwa nimeifunga ile hirizi, nikamuona akishtuka na kunitazama usoni.
“Hiki ni nini?” aliniuliza na kabla sijajibu chochote, tayari alishanifunua mkono wangu na kwa kuwa nilikuwa nimevaa shati la mikono mifupi, aliweza kuiona vizuri ile hirizi.
”Hiki ni nini Togo? Si naongea na wewe?” alizidi kunibana lakini sikuwa na majibu, akazidi kunitumbulia macho.
“Samahani, nitakufafanulia baadaye, kuna jambo nilikuwa naomba unisaidie kwanza,” niliongea kwa sauti ya upole.
“Jambo gani?”
“Naomba kachukue pini uje unisaidie kunitoa miiba miguuni,” nilisema huku nikiinua nyayo zangu na kumuonesha Rahma, akazidi kushtuka maana nilikuwa na miiba mingi niliyoikanyaga kule Mlandizi wakati nikikimbia lile sakata, tena nikiwa mtupu.
Licha ya mshtuko alioupata, Rahma alitoka na muda mfupi baadaye, alirudi akiwa na beseni dogo, wembe, pini, spirit, mafuta na sabuni. Nilichokuwa nampendea Rahma, alikuwa akinijali sana, yaani hakuwa tayari kuona nasumbuliwa na kitu chochote, alikuwa na mapenzi ya dhati kwangu ingawa ndiyo hivyo tena, tayari kikwazo kikubwa kilikuwa kimeingia katikati yetu.
“Hii miiba umeikanyaga wapi yote hii jamani Togo!” aliniuliza wakati akinisafisha miguu, tayari kwa kazi ile. Alinimwagia ‘spirit’ kwa wingi, jambo lililonifanya nisikie maumivi makali kuliko kawaida. Alianza kunitoa mwiba mmoja baada ya mwingine na baada ya karibu nusu saa ya maumivu makali, tayari alikuwa amemaliza. Akanisafisha upya na kunipaka mafuta.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikisikia maumivu, hata kusimama sikuweza, nikajilaza vizuri huku nikimshukuru sana kwa wema wake. Alitoa vile vifaa, aliporudi alikuja na kifungua kinywa, akakaa pembeni ya kitanda na kuanza kunisihi ninywe chai.
“Halafu mbona una chale nyingi hivi mwilini? Na zote zinaonesha ni mbichi kabisa,” alihoji Rahma na kuzidi kunikosesha raha, hata chai yenyewe ikawa hainyweki tena. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya tangu nianze yale mambo nikwepe kukaa naye karibu maana nilihofia mambo kama hayo.
Ilibidi nivungevunge tu, nikawa nataka kubadilisha mada lakini bado aliendelea kuniganda kwa maswali ambayo yalizidi kunikosesha amani ndani ya moyo wangu.
“Ni kweli kwamba wewe ni mchawi?”
“Mimi? Masihara hayo Rahma, mimi na uchawi wapi na wapi?”
“Mbona yule Dick dereva Bajaj anasema usiku umemuwangia kichawi na asubuhi ameamka na kujikuta yupo Kimara na alikuwa anakuota wewe? Na hiyo hirizi ni ya nini?” Rahma aliniambia kitu kilichonishtua sana, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
“Amesemaje?”
“Anasema eti wewe ulimtishia na usiku alipoenda kulala, ndiyo umemtokea na kumbeba kichawi na Bajaj yake mpaka Kimara, ameshtuka na kujikuta amelala kwenye usukani,” Rahma alizidi kusisitiza, ikabidi nicheke ili kumhadaa.
“Huyo atakuwa mwendawazimu, sijui chochote anachokisema.”
“Kwani jana usiku ulikuwa wapi?”
“Si nilikuwa nimelala jamani?”
“Mbona nilikuja kukuangalia huku chumbani sikukuona na hata chakula cha usiku hukula?”
“Nilitoka kidogo na baba yangu na baba yako, tulikuwa hukohuko tulikoenda, tulirudi mapema tu mbona?”
“Mh! Na asubuhi pia ulikuwa wapi maana nilikuja pia kukuchungulia nikamuona mdogo wako amelala peke yake.”
“Hukuangalia vizuri, nilikuwepo,” nilizidi kutetea uongo wangu. Niliona Rahma akinyamaza kimya, nikajua lazima atakuwa amejiongeza mwenyewe na kupata majibu kichwani mwake maana hakuwa mtoto mdogo.
Alichoniambia kuhusu yule dereva Bajaj kilinikasirisha sana, hasa kusikia kwamba alikuwa akinitangazia mbovu mtaani kwamba eti nimeenda kumuwangia, nikajikuta hasira juu yake ziki kuongezeka. Hata hivyo, kuna mambo bado yalikuwa yananitatiza kichwa.
Nilikutana na huyo dereva Bajaj nje, akiwa ameshaamka mwenyewe na akielekea kwenye kituo chao, iweje aseme kwamba nilimfuata usiku? Ina maana muda ule nakutana naye mwenyewe alikuwa anajua yupo ndotoni? Ni kweli kwamba fahamu zake zilimrudia akiwa Kimara, pale nilipomuacha baada ya Bajaj yake kuishiwa mafuta?
“Kwa nini hutaki tena kukutana kimwili na mimi? Ndiyo masharti yenu mliyopewa?” rahma aliniuliza swali ambalo sasa lilinipa picha kwamba alikuwa anaelewa kila kitu kinachoendelea, ikabidi niwe mkali maana kama ningeendelea kumchekea, angeendelea kuniingia.
“Kwa hiyo na wewe unaamini kwamba mimi ni mchawi si ndiyo? Umefikia hatua ya kunikosea heshima kiasi hicho?”
“Ooh! Samahani Togo, naomba unisamehe tu bure, basi yaishe baba’angu,” alisema Rahma huku akinisogelea na kunibusu, machozi yakiwa yameshaanza kumlengalenga. Japokuwa nilikuwa najua kwamba siruhusiwi kabisa kukutana tena kimwili na Rahma, sikuwa na namna yoyote ya kumtuliza na kumuondolea huzuni ambayo sasa ilikuwa ikijionesha waziwazi kwenye uso wake.
“Na mimi si tayari nimeshakuwa na nguvu za ziada? Chochote kitakachotokea nitapambana kuhakikisha namuokoa, kwanza akina baba hawawezi kukubali kuona akipatwa na jambo baya wakati uwezo wa kumsaidia wanao,” nilijisimea moyoni na ghafla nikajikuta nikipata ujasiri mkubwa ndani ya moyo wangu.
Nilimvutia Rahma kwenye kifua changu, kumbe na yeye ni kama alikuwa akisubiri tu nifanye hivyo kwani naye alinikumbatia kwa nguvu huku akiendelea kulia kwa kugugumia ndani kwa ndani.
“Kwa nini unanifanyia hivi Togo? Ina maana nimekosea kukupenda?” alisema huku machozi yakizidi kumtoka, nikaanza kumbembeleza huku nikimfuta machozi, nikimchombeza kwa maneno matamu, zoezi hilo lilienda sambamba na kupashana misuli, tayari kwa mpambano wa kukata na mundu.
Je, nini kitafuatia? Usikose
 
SEHEMU YA 53


“Kwa nini unanifanyia hivi Togo? Ina maana nimekosea kukupenda?” alisema huku machozi yakizidi kumtoka, nikaanza kumbembeleza huku nikimfuta machozi, nikimchombeza kwa maneno matamu, zoezi hilo lilienda sambamba na kupashana misuli, tayari kwa mpambano wa kukata na mundu.
SASA ENDELEA...
Sijui baba alijuaje kinachotaka kufanyika kule chumbani kwani wakati tukiwa kwenye maandalizi ya mwishomwisho kuelekea kwenye mpambano huo wa kirafiki, kila timu ikiwa imekamia mchezo, tulishtuka baada ya kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu, Rahma akakurupuka na kuvaa nguo zake harakaharaka, mlango ukawa unaendelea kugongwa kwa nguvu.
Ilibidi na mimi nivae zangu na kwenda kufungua, baba akaingia mzimamzima akiwa ameongozana na baba yake Rahma.
“Kuna nini kinachoendelea hapa,” baba aliuliza huku akitazama huku na kule. Hali aliyoikuta mle ndani, ilitosha kutoa majibu juu ya kilichokuwa kikitaka kufanyika, nikavaa sura ya ‘ukauzu’ na kumjibu:
“Rahma alikuwa ananitoa miiba miguuni.”
“Miba gani?” baba aliniuliza kwa ukali, ikabidi niinue nyayo zangu na kumuonesha, wote wawili wakanisogelea na kuanza kunitazama kwa makini. Niliona wametazamana kisha wakapeana kama ishara fulani.
“Rahma nenda kwa wenzako jikoni, kesi yako itaamuliwa na mama zako,” baba yake Rahma alisema kwa sauti ya chini, harakaharaka Rahma akasimama na kutoka, huku akionesha dhahiri jinsi alivyokuwa na hofu ndani ya moyo wake.
“Najua unampenda binti yangu Togo, lakini nakuomba sana mwanangu, ukifanya naye mapenzi tutampoteza, yeye si miongoni mwa jamii yetu na mwili wake hauna kinga yoyote, hebu zingatia sana ninachokwambia, nakuomba usimguse,” baba yake Rahma alizungumza kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo mkubwa.
Tofauti na baba ambaye kila akiongea alikuwa akifokafoka, baba Rahma alikuwa akizungumza kwa utaratibu sana na nikajikuta nikimuelewa sana.
Jambo ambalo nilishindwa kulikataa ndani ya moyo wangu ni kwamba nilikuwa nikimpenda sana Rahma kwa hiyo akili za harakaharaka zilianza kunituma kufikiria namna ninavyoweza kukivuka kikwazo kilichokuwepo kati yetu kwani kiukweli sikuwa tayari kumpoteza.
“Kwa hiyo na yeye akiwa miongoni mwetu tutaruhusiwa kuoana?” niliuliza swali ambalo liliwafanya baba na baba Rahma watazamane kwa sekunde kadhaa.
“Lakini si unajua kwamba mwenzako anasoma na siku chache zilizopita mama yake alikuwa akifuatilia mambo ya chuo?”
“Hata akimaliza hakuna shida,” nilijibu huku nikiwa na wasiwasi na atakachokisema baba.
“Wewe mtoto mpumbavu sana, yaani umeshupalia kabisa, ina maana hujui kama nyie mmeshakuwa ndugu? Halafu hiyo michezo ya mapenzi umeianza lini wakati wewe bado mdogo?”
“Lakini baba mimi nampenda Rahma.”
“Unampenda? Unajua maana ya kupenda wewe? Toka lini wewe ukampenda mtu? Hebu toa wendawazimu wako hapa, yaani badala uelekeze nguvu kwenye ulimwengu mpya tuliokufunulia unaanza mambo yako ya mapenzi hapa, una akili wewe?” baba alinifokea.
“Hapana, huna haja ya kuwa mkali mzee mwenzangu,” baba yake Rahma alimkatisha baba kisha akanisogelea pale nilipokuwa nimekaa.
“Unampenda kwa kiasi gani?”
“Nampenda sana baba.”
“Lakini nyie mmeshakuwa ndugu?”
“Mbona undugu wetu siyo wa damu?”
“Kama kweli unampenda, nakuomba uzingatie nilichokwambia, hayo mengine tuachieni sisi wazazi wenu,” baba yake Rahma alisema kwa upole. Ilihitaji ujasiri mkubwa kuzungumza mambo yale mbele ya baba lakini kwa kuwa baba Rahma alikuwa mwelewa, na mimi nilijikuta nikipata nguvu.
Majibu aliyonipa, yaliufanya moyo wangu ufurahi sana, nikajiapiza kwamba sitakutana naye tena kimwili kwa kuhofia kumpoteza lakini nikawa nafikiria mbinu nyingine mbadala na harakaharaka akili zangu zilinituma kutafuta muda wa kutosha wa kukaa na Rahma na kumweleza ukweli kuhusu mimi, baba na baba yake na mwisho nimshawishi na yeye ajiunge kwenye jamii yetu.
Tayari nilishaanza kuona dalili za ushindi, tabasamu pana likachanua kwenye uso wangu, hisia tamu zikawa zinapita kwenye mishipa yangu huku nikivuta picha ya miaka kadhaa baadaye, nikiishi na Rahma kama mume na mke halali.
“Kilichotuleta hapa siyo hiki tulichokuwa tunakizungumza,” baba yake Rahma alivunja ukimya, baba akawa anatingisha kichwa kukubaliana naye huku akiwa amenitolea macho ya ukali.
“Leo umefanya kitu cha ajabu sana na kama isingekuwa nguvu za ziada kutumika, ungeweza hata kuuawa kule Mlandizi, kama hiyo haitoshi umesababisha majanga mengine ambayo hayakuwepo kwenye ratiba, umesababisha yule dereva wa bodaboda amepoteza maisha,” alisema baba yake Rahma, kauli ambayo ilinishtua kuliko kawaida.
Kilichonishtua zaidi ni kusikia kwamba yule dereva wa bodaboda amekufa, moyo ulishtuka kuliko kawaida.
“Kibaya zaidi umesababisha watu hapa mtaani waanze kututilia mashaka, kwa nini umeenda kumroga huyo kijana dereva wa Bajaj hapo nje? Hujui kama ni hatari sana watu kujua kama unajishughulisha na haya mambo ya giza? Mtoto mpumbavu sana wewe,” baba aliongezea kwa ukali, nikajiinamia kwani kiukweli nilikuwa nimefanya makosa makubwa.
“Lakini nilikuwa nataka kujifunza,” nilijibu kwa sauti ya chini, baba yake Rahma akaniambia kwamba mambo hayo huwa hujifunzi kama unavyojifunza mambo mengine, bali kuna utaratibu wake.
Akaniambia kwamba nilichokifanya kilikuwa makosa makubwa kwa watu wa jamii yetu na kama zilivyo sheria, yeyote anayeenda kinyume lazima akumbane na rungu la Mkuu. Kauli hiyo ilizidi kunitisha moyoni mwangu, nikajaribu kuvuta taswira ya Mkuu, yule kiongozi wa watu wa jamii yetu, hofu ikazidi kunijaa.
“Ili kumfurahisha, inabidi usiku wa leo ufanye juu chini nyama zipatikane, tukifika tutaenda kukuombea msamaha na kwa kuwa utakuwa na mzigo, bila shaka atakupa adhabu ndogo, kinyume na hapo anaweza hata kuamuru uliwe nyama ukiwa hai,” alisema baba yake Rahma, nikajikuta nikitokwa na kijasho chembamba.
Baba Rahma aliniona hali niliyokuwa nayo, akaniambia nisijali watanisaidia lakini kitu cha kwanza, ilikuwa ni lazima nikatoe sadaka ya kitu ninachokipenda zaidi, nje ya familia yangu.
Sikumuelewa kauli yake hiyo, akanifafanulia kwamba wanaposema kitu, kwenye imani yao wanamaanisha mtu kwa hiyo ilikuwa ni lazima nimfikirie rafiki yangu ninayempenda zaidi ambaye ndiye angetolewa kafara usiku ili mimi nisamehewe na Mkuu kwa kitendo changu cha kwenda kwenye msiba wa mtu ambaye tumemla nyama na mimi ndiye niliyesababisha kifo chake.
“Mimi sina rafiki hapa mjini, kwanza sijazoeana na mtu yeyote,” nilijitetea, baba akaniambia kwamba anawajua marafiki zangu wengi tu Chunya.
“Sasa nitaendaje Chunya?”
“Hutakiwi kuhoji kwa sababu hakuna kisichowezekana, unachotakiwa ni kututajia mtu, vinginevyo wewe ndiyo utaaliwa leo,” baba alisema, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
Nimewahi kusikia kwamba wachawi huwa na kawaida ya kuwatoa kafara watu wao wa karibu na ndiyo maana watu wakishajua kwamba wewe ni mchawi wanajitenga na kukuogopa sana lakini nilikuwa naona kama ni hadithi za kufikirika tu, lakini sasa yalikuwa yamenifika.
Ni kweli nilikuwa na marafiki wengi wanaonipenda kule nyumbani Chunya lakini sikuwa tayari hata kidogo kuona mtu yeyote asiye na hatia anapatwa na matatizo kwa sababu yangu. Nilijikuta nikijilaumu sana kwa upumbavu wangu wa kutaka kwenda kujionea mwenyewe kilichotokea kule Mlandizi.
“Tunasubiri jibu lako,” baba alinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 54

ILIPOISHIA:
Ni kweli nilikuwa na marafiki wengi wanaonipenda kule nyumbani Chunya lakini sikuwa tayari hata kidogo kuona mtu yeyote asiye na hatia anapatwa na matatizo kwa sababu yangu. Nilijikuta nikijilaumu sana kwa upumbavu wangu wa kutaka kwenda kujionea mwenyewe kilichotokea kule Mlandizi.
“Tunasubiri jibu lako,” baba alinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
SASA ENDELEA…
“Lakini baba…”
“Lakini nini? Hakuna mjadala, kinachotakiwa hapa ni utekelezaji tu,” alisema baba na kunitishia kwamba endapo sitatoa majibu, kwa kuwa yeye anawafahamu marafiki zangu, atapendekeza jina lolote.
Kwa mara nyingine nilikuwa nimeingia kwenye mtego hatari wa kutaka kupoteza maisha ya mtu asiye na hatia kwa sababu ya uzembe wangu. Nilijisikia vibaya sana, nikashindwa kuzuia machozi yasiulowanishe uso wangu.
“Hata sisi mwanzo tulikuwa kama wewe, utazoea tu,” alisema baba yake Rahma. Sikujua ni nini hasa kilichotokea kwenye akili za baba na baba yake Rahma mpaka wachukulie kitendo cha kukatisha maisha ya mtu asiye na hatia kuwa cha kawaida kiasi kile.
Baada ya kulumbana kwa muda mrefu, baadaye niliamua kusalimu amri, nikamtaja rafiki yangu kipenzi, Sadoki. Kilichosababisha nikamchagua Sadoki, ni kwa sababu dakika za mwisho, urafiki wetu ulikuwa umeingia dosari baada ya siku moja kumkuta akishirikiana na watu wengine kumteta baba yangu kwamba alikuwa mchawi.
Kwa kipindi hicho, nilikuwa bado sijajua ukweli kwamba baba ni mchawi au mganga kwa sababu mara zote nilizokuwa namuuliza alikuwa akisema kwamba yeye ni mganga na wala si kweli kwamba anajihusisha na mambo ya kishirikina kwa hiyo yeyote niliyemsikia akizungumza mabaya ya baba, alikuwa akigeuka na kuwa adui yangu.
Siku nyingi zilikuwa zimepita tangu siku tulipotaka ‘kuzichapa’ maana baada ya kumkuta akimsema vibaya baba, nilimjia juu sana, kama isingekuwa watu wazima waliokuwa jirani nasi, huenda tungepigana na kuumizana sana.
Hata hivyo, tukio hilo moja halikuharibu ukweli kwamba tulikuwa marafiki wakubwa kwa sababu nakumbuka mara kwa mara alikuwa akija kwetu, na mimi nilikuwa nikienda kwao. Kwa kifupi ni kwamba ukiachilia mbali hiyo dosari ndogo iliyotokea, tulikuwa tumeshibana kisawasawa.
Baada ya kumtaja jina, sikuweza kuendelea kukaa mle chumbani, nilitoka na kwenda bafuni huku nikichechemea, nikajifungia na kuanza kulia kwa uchungu, baba na baba yake Rahma wakabaki chumbani kwangu wakiendelea kujadiliana mambo yao. Nililia mpaka macho yakawa mekundu kabisa, nilimuonea huruma Sadoki, nilimuonea huruma mama yake na wadogo zake.
Walikuwa wakimtegemea kwa sababu baba yao alifariki wakiwa bado wadogo kwa hiyo baada tu ya kumaliza shule ya msingi, Sadoki alikuwa akienda kufanya vibarua kwenye machimbo ya dhahabu na fedha kidogo alizokuwa akizipata ndizo zilizokuwa zikiihudumia familia yao.
Nikiwa bado naendelea kulia kule bafuni, baba alikuja kunigongea, ikabidi ninawe uso harakaharaka, nikatoka huku uso wangu nikiwa nimeuinamisha. Tulirudi chumbani kisha akaanza kunipa maelekezo kwamba usiku wa siku hiyo tunatakiwa kusafiri kuelekea Chunya.
“Tukifika, inabidi twende mpaka nyumbani kwa huyo rafiki yako, kuna dawa utaitega mlangoni, asubuhi akiwa anatoka anatakiwa airuke, akishairuka tu kazi itakuwa imekwisha.
“Sasa tutaendaje Chunya na kufanya hivyo unavyosema kabla hakujapambazuka?” niliuliza kwa sababu kama ni mabasi, muda huo tusingeweza kupata la kwenda Mbeya na hata kama lingepatikana, tusingewahi kama baba alivyokuwa anasema.
“Hutakiwi kuhoji sana, sikiliza kwa makini ninachokueleza,” baba alinikatisha, akaendelea kunipa maelezo ya namna ya kukamilisha zoezi hilo ambayo kwangu yalikuwa yakiingilia sikio la kushoto na kutokea la kulia.
Sikuona sababu yoyote ya kumuadhibu Sadoki kwa makosa ambayo nilikuwa nimeyafanya mwenyewe, nikajikuta nikijihisi hatia kubwa mno ndani ya moyo wangu. Basi tuliendelea kuzungumza pale, kisha baba akaniambia nijiandae kwa safari.
Walitoka na kuniacha nimejilaza kitandani, machozi yakaanza kunitoka tena na kwa sababu nilikuwa nimejilaza kwa kutazama juu, yalikuwa yakichuruzika kupitia kona za macho yangu mpaka kichwani na kupotelea kwenye shuka lililokuwa limetandikwa pale kitandani.
“Hivi ndiyo nimeshakuwa mchawi?” nilijiuliza swali kama mwendawazimu. Ni mimi ndiye niliyekuwa na shauku kubwa ya kuwa na nguvu zile za ajabu lakini sijui ni kutoelewa au ni kitu gani, ndani ya muda mfupi tu nilishaanza kuhisi kwamba pengine nimebeba mzigo mzito ambao sina uwezo nao. Zile kauli za baba akinikebehi kwamba bado nina akili za kitoto zikawa zinajirudia ndani ya kichwa changu.
Niliendelea kutafakari kwa kina na baadaye usingizi mzito ulinipitia, nikiwa usingizini nilianza kuota ndoto za ajabuajabu na kusababisha niwe nashtuka mara kwa mara. Baadaye ndoto hizo zisizoeleweka zilikoma, nikalala mpaka majira ya saa mbili za usiku nilipokuja kuzinduliwa na sauti ya baba aliyekuwa akiniita, nikakurupuka na kuamka.
“Umeshajiandaa?”
“Ndiyo,” nilimjibu huku nikijifikicha macho na kujinyoosha. Ukweli ni kwamba sikuwa nimejiandaa chochote.
“Haya nifuate.”
“Lakini bado sijala.”
“Utaenda kula mbele ya safari,” alisema baba huku akinihimiza nisimame. Nilishuka kitandani, miguu ikawa inauma sana hasa kwenye nyayo kutokana na majeraha ya ile miiba niliyotolewa na Rahma. Ilibidi nijikaze kisabuni kwa sababu ni mambo ambayo nilijitakia.
Tulitoka mpaka nje bila kuonekana na mtu yeyote, tukamkuta baba yake Rahma amesimama mlangoni, akionesha kwamba alikuwa akitusubiri. Alinipa kofia kubwa na kuniambia niivae, sikumuelewa kwa sababu gani amefanya vile. Tulitoka, mimi nikiwa katikati na kwenda hadi pale kwenye maegesho ya Bajaj, tukaingia kwenye mojawapo na baba yake Rahma akampa maelekezo dereva kwamba atupeleke Mwenge.
Sikuwa napajua Mwenge zaidi ya kupasikia tu, ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini baba yake Rahma alinipa ile kofia kwa sababu japokuwa nilikuwa nimeivaa, na kuziba sehemu kubwa ya uso wake, wale madereva Bajaj walikuwa wakinitazama kama wanaotaka kuhakikisha kama ni mimi kweli au laah!
Sikuwajali zaidi ya kuwadharau kwa sababu sasa nilikuwa na uwezo wa kumfanya mtu yeyote ninavyotaka mimi. Bajaj ilianza kukata mitaa na baada ya muda, tuliingia kwenye barabara ya lami iliyokuwa na magari mengi.
Safari ikaendelea mpaka tulipofika mahali kwenye mataa yenye mwanga mkali ambayo licha ya kwamba ilikuwa ni usiku, yalikuwa yakiangaza sehemu yote, watu wakiendelea na shughuli zao utafikiri ni mchana.
Tulishuka kwenye Bajaj huku nikishangaa huku na kule, moyoni nikawa najisemea ‘mjini kuzuri sana’. Tukaanza kuvuka barabara mbili pana ambazo katikati zimetenganishwa na bustani ya maua.
Kiukweli kama ningekuwa peke yangu, nisingeweza kuvuka kwa sababu kulikuwa na magari mengi mno, nikawa naung’ang’ania mkono wa baba Rahma maana baba naye alionesha kuwa na mchecheto.
Tulivuka salama mpaka upande wa pili ambako tulipanda magari mengine yanayoelekea Kunduchi. Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu, safari ikaanza mpaka tulipofika Kunduchi, tukashuka kwenye gari na kuanza kutembea kwa miguu. Sikuwa najua tunaelekea wapi, baada ya muda tukatokezea kwenye makaburi yaliyokuwa karibu na bahari.
“Haya ni makaburi ya Wagiriki, ni ya zamani sana na hapa ndiyo hutumika kama njia ya kuingia na kutoka kwenda sehemu yoyote,” baba yake Rahma alinielekeza kwa sauti ya upole, tukaingia mpaka katikati kabisa ya makaburi hayo, mahali palipokuwa na mti mkubwa wa mbuyu.
“Tunaenda Chunya, hutakiwi kwenda kinyume na maelekezo tunayokupa, ukifanya uzembe tu, kitakachokutokea ni juu yako,” alisema baba kwa sauti ya msisitizo, nikawa natingisha kichwa kukubaliana naye. Tulikaa chini na kuweka kama duara hivi, tukashikana mikono kisha nikaambiwa nifumbe macho.
Je, nini kitafuatia?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom