SEHEMU YA 60
“Hali ya baba Jacky siyo nzuri.” Nilimjibu nikiwa nimeinama mkono kwenye paji la uso huku machozi yakiendelea kunitoka bila kumuangalia. Nilijishangaa jinsi nilivyoumizwa na ugonjwa wa mume wangu.
“Tuendelee kumuombea,” shoga yangu alinieleza kwa sauti ya upole.
“Mmh!” niliguna huku nikitosa kitambaa na kupenga kamasi zilizoanza kunichuruzika, pamoja akili yangu haikuwa kurudi kwa mume wangu.
Lakini bado nilimtambua kama mzazi mwenzangu ambaye alikuwa muhimili wa wanaye, pamoja na yote aliyoyafanya haikubadilisha wanangu kuwa siyo wanaye.
Siku ile tulikaa mpaka saa moja usiku bila kula tukiwa nje ya chumba cha wagonjwa mahututi mpaka alipokuja daktari mwingine tofauti na yule wa kwanza na kutueleza kwa pamoja.
“Jamani, kwa vile hali ya mgonjwa si ya kubadilika mara moja, mngekwenda kupumzika nyumbani ili kesho mje kumuona.”
Baada ya kusema vile mimi na baba mkwe tulitazamana kutafuta jibu la pamoja.
“Mama, nina imani daktari tumemsikia, tukapumzike ili kesho tuje tena,” bamkwe alisema.
“Sawa baba.”
Tulikubaliana kurudi nyumbani, tukiwa tunatoka baba mkwe ambaye alikuwa mnyonge alisema kwa sauti ya kukwaruza.
“Nimeamini mshahara wa dhambi mauti. Kama angekuwa na wewe haya yangemfika, sijui nitamfanya nini mke wangu na wanawe kama mwanangu atakufa?” baba mkwe alisema kwa uchungu kitu kilichozidi kuumiza moyo wangu. “Baba usiseme hivyo, hatutakiwi kumkatia tamaa bali tuendelee kumuombea.”
“Ni kweli, ILA haya ni malipo aliyoyafanya japo sehemu kubwa imechangiwa na mama yake na wadogo zake kuingilia ndoa yenu.”
“Baba yameishapita, tuangalie tutamsaidia vipi ndipo tujue waliosababisha wanafanywa nini.”
“Yaani wee acha tu, kila ni..niki..ku..ku,” baba mkwe hakuimaliza alianza kulia.
Pamoja na kuwa kwenye wakati mgumu, lakini nilijitahidi kumtuliza baba mkwe ambaye niliamini alikata tamaa kwa hali ya mwanaye.
“Baba inauma lakini tusimkatie tamaa, bado baba Jacky ana nafasi ya kuendelea kuishi.” “Ni kweli mama, kukuacha wewe alipoteza mwanamke wa kweli na kukikimbilia kifo.”
“Baba kuugua siyo kifo,” niliendelea kumpoza baba mkwe.