SEHEMU YA 36:
“Nimekuelewa,” mume wangu alikuwa mpole kama kanyeshewa mvua.
“Na sitaki kusikia ujinga huu tena!”
“Sawa baba,” mume wangu alijibu ameinama kama kondoo.
Baada ya kusema yale alinigeukia mimi niliyekuwa nimewapakata wanangu. “Samahani sana mama kwa yote yaliyotokea, kwa nini ulikaa nayo haya muda mrefu kwa nini hukuja mapema mwanangu? "
“Baba nilichanganyikiwa.” "Pole sana mama, lakini nimeisha mjua mchawi wa ndoa yako. Niliyasikia nakayadharau kumbe yalikuwa na maana yake. Leo ndio nimesadiki mvunja nchi ni mwananchi... Mwanangu rudi kwako nakuhakikishia nitakuwa na wewe muda wote," baba mkwe alikata mzizi wa fitina.
"Asante baba kwa kuliona hilo, ni mengi sikujua kumbe yote ningeyaleta kwako."
"Mwanangu yote nayajua niliwaonya, kumbe walifanya mambo yao kwa siri, sasa nasema kwanza sipendi kuongea mengi...Mama niache niongee na hawa washenzi wa tabia kapumzike nje na wanao."
Nilitoka nje na kuwaacha mume wangu na wazazi wake kwenye kikao cha dharura. Baada ya nusu saa mume wangu aliondoka bila kuniaga. Baada ya muda niliitwa na baba mkwe na kunieleza:
"Mama nimemtuma akarudishe vitu vyako ndani na kisha auondoe ule uchafu ili urudi chumbani kwako, pole sana mwanangu. Lakini kwa nini hukuja kunieleza mapema?" baba mkwe alirudia swali lake la awali.
"Kutokujua baba." Nilishinda ukweni mpaka jioni na kufuatwa na dereva wetu Salumu, aliyenichukua na kunirudisha nyumbani kwangu. Njiani Salumu aliniuliza maswali:
“Mama mbona mpaka sasa sijui, kwani kuna nini?”
“Kwani vipi Salu?”
“Asubuhi aliondoka na kuonesha kuna tatizo baada ya kuingia yule mwanamke. Huwezi kuamini muda mfupi aliishaanza kuwa kero. Mchana aliporudi baba na nilishangaa kuona vitu vya yule mwanamke vilivyoingizwa asubuhi vikitolewa ndani na kupandishwa kwenye gari na wote kuondoka.
“Baada ya muda walirudi wifi zako na kupanga vitu ndani kisha nao wakaondoka ndipo nilipoambiwa nikufuate kwani kuna nini?”
“Utajua tu Salumu, usiwe na haraka.”
Salumu aliliponifikisha nyumbani, niiingia hadi chumbani na kukuta vitu vyangu vimerudishwa bila kupangwa. Niliingia kazi ya kuvipanga na kugundua vitu vyangu vingi vimechukuliwa, lakini sikujali sana.