Sehemu ya 90.
"Kaka, kaka mbona wanapakia jeneza kule?"
Nilishtuka kusikia hivyo, nikamuuliza.
"Una uhakika?"
"Nimewaona mwenyewe kaka, hakika ya nini?" alisema akihema wakati ameshafika.
Nilimshika ili kumtuliza kutokana na hali aliyokuwa nayo. Lakini alitulia akidai kuwa, yeye mawazo yake yalikuwa kwamba wameliiba jeneza nililokuwa nalitengeneza baada ya mimi kwenda mahali, lakini alipoliona akapata nguvu.
"Liko hivi hivi kama hili kaka," aliniambia.
Akashangaa imekuwaje sasa, watu waliokuwa wameagiza jeneza pale kwangu, wakalisubiri kwa muda mrefu, sasa inakuwaje waonekane wakiliingiza jeneza jingine ndani ya gari, wamelitoa wapi?
"Tunaweza kwenda kuwaona wote?" nilimuuliza mdogo wangu.
"Twende sidhani kama watakuwa wameondoka," alisema huku akiangalia kwa macho yenye woga.
"Au labda walipoona tunachelewa waliamua kununua jingine lililokwishatengenezwa nini?" mdogo wangu aliniuliza akijishika mikono.
"Wawe wamenunua kwa wapi?" na mimi nilimuuliza kwa sababu katika eneo lile hakuna mtu aliyekuwa akitengeneza majeneza zaidi yangu.
Tulirudisha mlango. Na mimi ndiye niliyerudishia mlango, kisha tukaenda wote hadi barabarani ambako hatukukuta wale watu wala dalili za kuwepo kwao.
"Lakini walikuwepo kaka," alisema mdogo wangu akidhani labda nitapunguza kumwamini baada ya kutowaona wale watu.
"Au tuulizie watu kama wamewaona wakiondoka?" aliniuliza mdogo wangu.
"Hakuna haja," nilimjibu.
Kisa cha mimi kumjibu hivyo ni kwamba, katika hali niliyokuwa nayo moyoni sikuwa napenda kuwajulisha watu mambo makubwa na mazito yaliyokuwa yakinitokea.
Nilimwona mdogo wangu akiangalia angalia chini nikajua alikuwa akiangalia sehemu ambazl labda alama za tairi za gari zingeonekana.
"Ona kaka, ona tairi si hizi?" aliniambia akiangalia bado chini.
Lakini njia ile ilikuwa na magari kila wakati japo si sana. Kwa hiyo haikuwa lazima tairi ziwe za gari hilo walilokuwa wakilitumia wale watu.
Nilimsihi tuondoke licha ya kwamba ufumbuzi ulikuwa hajapatikana.
Je nini kitaendelea?