SEHEMU YA 30
“Faraji ni nani?” askari akauliza kwa ukali, hakuta kumsikiliza yule mwenyekiti. “Huyu hapa” mke wangu akawaonyesha wale polisi kwa kunisonta. “Mkamateni,” amri ikatoka. Nikakamatwa na polisi.
Nilipotaka kujieleza kwa wale mabwana, sikupewa nafasi hiyo, waliniburuza kwa nguvu hadi nje. Mtoto wangu mdogo akaanza kulia tena kwa uchungu.
Niliingizwa kwenye gari la polisi kama gaidi, kisha safari ya kituo cha polisi cha Oystabay ikaanza, nilijisikia uchungu sana kwa kile kilichokuwa kikinitokea. Nilijikuta namchukia sana mke wangu. Hasira dhidi yake ikawa kubwa.
Baada ya kufikishwa kituoni, sikuchukuliwa maelezo yoyote zaidi ya kutakiwa kuvua mkanda na viatu, pamoja na kukabidhi vitu vyangu, kisha nikaingizwa selo.
Tangu nizaliwe sikuwahi kuingia ‘lockup’ na sikudhani kama siku moja ningeingia sehemu mbaya kama ile. Mule ndani kulikuwa kunanuka mkojo na hewa ilikuwa nzito sana. Chawa na kunguni lile lilikuwa ni zizi lao.
Nikiwa mule ndani, nikaamini muda si mrefu marafiki na jamaa wangekuja kuniwekea dhamana endapo wangepata taarifa juu ya maswahibu yale.
Nusu saa ilipita bila kuona dalili zozote za kuchomoka, nilimwita askari aliyekuwa kaunta nikamwomba anisaidie kufanya mawasiliano na moja ya marafiki zangu ili wajue nipo kwenye madhila.
“Hata kama akipatikana mtu wa kukuwekea dhaman, kwa muda huu siyo rahisi kutoka,” yule askari aliniambia. “Kwa nini?”
“Ni utaratibu tu, usiku huwa hatutoi dhamana.” “Kwa hiyo nitalala humu hadi asubuhi?” “Ndio maana yake.” “Mungu wangu,” nilimaka.
Hata hivyo kabla sijawasiliana na jamaa yangu kwa ajili ya kumpa taarifa za kukamatwa kwangu, mwenyekiti wa mtaa alifika.
Aliomba kuzungumza na mimi, kisha akasogea katika geti. “Kesho utaachiwa…” aliniambia. “Kweli leo haiwezikani?”
“Ndio, dhamana mara nyingi zinatolewa mchana sio usiku, vinginevyo labda tutumie njia za panya” alisema, nikamwelewa hapo lazima rushwa utumike. “Haina shida we waulize wanataka kiasi gani.” “Basi subiri kidogo,” aliniambia.
Akatoka na kwenda kuzungumza na polisi, sikujua alimkabili nani ila muda mfupi badaye akarudi. “Jamaa wanasema wanataka laki moja.” “Haina neno, pesa siyo tatizo, ninachotaka ni kutoka