***SURA YA SABINI NA MOJA***
(MSIMU WA 02)
Hamilton, Bermuda: Saa kumi na mbili asubuhi.
Stanis alitizama saa yake ya mkononi mara mbili kisha akatizama kushoto na kulia kwake. Ni kama vile abiria anayesubiria ‘treni’ la mwendo kasi akiwa anadhani aidha litakuwa limemuacha. Hakutulia.
Dakika kumi mbele akaungana na wanaume wanne: Gog, Fraud, Nun na Adrian. Bila ya kupoteza muda wakaanza kujongea kuelekea upande wao wa kaskazini.
“Wengine wapo wapi?”
“Wametangulia.” Fraud alijibu. “Tumeona kuongozana kwa wingi itapelekea kugundulikana kwa urahisi.”
“Ila hayo hayakuwa makubaliano yetu.” Stanis alitamba. “Sikupanga twende wote ila kuna baadhi tu ya mambo ningependelea kuyaweka sawa.”
“Kwani kutakuwa na shida yoyote kubwa kwa wao kutokuwepo hapa muda huu?” Gog aliuliza.
“Inaweza ikawepo, inategemea na huko tuendako.” Stanis akajibu.
“Ila sisi tupo, unaweza tu ukatujuza hayo mambo.” Gog alipendekeza. Stanis akatikisa kichwa chake.
“Tuachane nayo. Tuzingatie tu yale tuliyoyapanga awali.”
Walitembea kwa muda wa dakika ishirini kamili mpaka kufikia kwenye jengo lao la kazi. Palikuwa kimya na tulivu. Wakati wanaingia, Stanis aliwatizama wenzake na kuwapa ishara ya ngumi akinong’oneza:
“Kama tulivyokubaliana.”
Gog na wenzake wakamuacha Stanis aende mbele wakati wao wakijigawa kushoto na kulia kwenda kukutana na wengineo ambao walikuwapo kwenye mkutano siku iliyopita.
Stanis asiwe na hofu bali papara, akatembea akiwa amepachika macho yake kwenye mlango wa ofisi ya Kim. Hatua zake ndefu zilimuwia muda mfupi tu kumkutanisha na mlango huo ambao aliugonga kistaarabu, akatulia kusikiliza majibu.
“Ingia!”
Sauti toka ndani ikamkarimu. Alitabasamu kwanza kabla hajazungusha komeo na kuzama ndani alipomkuta Kim akiwa ameketi kwenye kiti chake kikubwa akibembea kwa kwenda kushoto na kulia.
“Karibu, Stanis. Vipi mbona mapema hivi?” Kim aliuliza na uso wenye hamu ya kufahamu. Kabla Stanis hajajibu, Kim alidaka simu yake ya mezani akamuita mhudumu.
“Kuna jambo nimekuja kumalizana na wewe.” Stanis aligamba.
“Jambo lipi tena hilo? Kuna lolote jipya?” Kim aliuliza.
Kabla Stanis hajajibu, mhudumu akaingia ndani akibebelea vikombe viwili ya kahawa. Alivisambaza vikombe hivyo kisha akaondoka zake.
“Fukuza uchovu na kahawa, Stanis.” Kim alimkaribisha mgeni wake baada ya kunywa mafundo mawili.
Stanis akanyanyua kikombe apeleke kinywani, ila alipofikisha nusu safari akashindwa. Alisikia maumivu makali ya kichwa akarejesha kikombe mezani.
“Vipi, kuna tatizo?” Kim aliuliza akitabasamu.
Stanis alinyanyua mkono wake akitaka kumkamata Kim, lakini zoezi lake hilo likashindikana haraka. Kichwa kilimgonga mithili ya nyundo akabaki akilaumu huku akipapasa papasa kichwa chake mithili ya mama kipofu anayejitahidi kumgundua mwanaye kwa kutumia viganja.
Kadiri muda ulivyozidi kusogea, maumivu yakazidi.
“Stanis … Stanis … Stanis. Unadhani ni rahisi kiasi hiko? Yani ulale tu na kuamka utake kunipindua? Unajua ni kwa nguvu gani nilitumia kujenga hiki unachokiona sasa? Unajua imenigharimu kiasi gani kuwepo hapa? … Hakika nakwambia, njia zangu si rahisi hivyo. Kiatu changu ukitumbukiza mguu basi hautoweza kuunyanyua.”
Maneno hayo yalikuwa kama mwangwi kwenye masikio ya Stanis, aliyasikia yakijirudufu kana kwamba yumo ndani ya chungu. Hata macho yake sasa hayakuona vema, yalimuona Kim wakiwa wanne tena akielea elea kama mtu anayeogelea.
“Nini kinatokea?” Stanis alijiuliza akitetema maneno kama ‘teja’.
“Unasema?” Kim aliuliza akijinywea kahawa.
“Nini … nini kinan’tokea mwilin … mwangu.” Stanis aliongea kwa shida. Si kichwa kilikuwa kinauma sasa bali kilikuwa kizito kama vile amebebelea kichwa cha gari moshi.
“Pole sana. Ulikosea. Kaa ukijua siku zote waweke marafiki zako karibu, ila maadui zako karibu zaidi. Nilitambua wewe ni adui yangu tokea siku ya kwanza ulipokuja ofisini kwangu kulaumu. Niliona ndani ya macho yako ari na matamanio makubwa, hivyo nikakuweka karibu zaidi nijue kila unalofanya, kila ulipo. Hatimaye kama unavyoona, nimefanikiwa.”
Kim alikunywa fundo moja la kahawa kisha akanyanyua mkonga wa simu yake na kupiga simu, punde Fraud na Gog wakaja ofisini.
“Mpelekeni anapostahili. Nina maongezi naye baadae.”
Fraud na Gog wakambeba Stanis kwa kumburuza mpaka kwenye chumba kimoja kilichojitenga kikitawaliwa na giza totoro. Humo wakamrushia Stanis na kuufunga mlango.
***
Masaa kadhaa huko nyuma …
“Nimekuja kukufikishia habari kama ulivyoniagiza, mkuu. Leo pia anataka tukutane naye.” Gog alisema kwa kujiamini akimtizama Kim.
“Unataka tufanye nini? Sema nasi tutafanya … tummalize?” Fraud aliuliza. Kim akatikisa kichwa.
Aliwatizama kwanza wanaume wake wa kazi, Gog na Fraud kisha akasema:
“Hapana. Nataka nimmalize kwa mikono yangu mwenyewe. Fanyeni kama aliyowaagiza, ila hakikisha na mimi nasikia kila kitu kwenye hayo maongezi.”
Kim alifungua droo akatoa kifaa kidogo rangi ya zambarau akamkabidhi Gog. Gog na mwenzake wakanyanyuka na kuaga. Nje wakakutana na Nun na Adrian walioongozana nao mpaka kwa wenzao wengine walioongea nao kwa dakika kadhaa kabla ya kukubaliana jambo kwa kutikisa vichwa vyao na kupeana mikono.
Baadae jua lilipozama na hata kusahau lilipotokea, wanaume hao wakaongozana kwenda kukutana na Stanis maeneo ya ufukweni. Hapo wakati wote wakiwa wanalonga, Kim akawa anasikia kila jambo kwa kifaache.
Stanis asiwe na hili wala lile, aliagana na wenzake akaenda. Wenzake walizunguka nyuma na kukutana. Gog akawasiliana na Kim.
“Nadhani umesikia yote yaliyopangwa, mkuu.”
“Nimeyasikia yote. Umefanya kazi njema, kapumzike sasa tukutane kesho.”
“Sawa, mkuu. Ila unaonaje tukarahisisha kazi zaidi?” Aliuliza Gog kabla hajamuelewesha Kim nini wamedhamiria kufanya.
Baada ya maongezi hayo, Gog alimteua Fraud kwa ajili ya kazi ya ziada. Alimpatia chupa kubwa ya kijani akisema:
“Hakikisha anakuwa salama. Ulisikia mkuu anataka ammalize kwa mkono wake mwenyewe.”
Wakati wenzake wanaelekea kwenye makazi yao, Fraud akashika njia kwenda kwa Stanis. Kwa kunyata na kwa uangalifu mkubwa alifuata dirisha la chumba alalacho Stanis akapulizia dawa humo taratibu akiwa amejifunga kitambaa kuziba mdomo na pua.
****
☆Steve