***SURA YA SITINI NA SABA***
(MSIMU WA 02)
Masaa matano mbele wote wakiwa wamedidimia ndani ya usingizi mzito, wanaume wasiopungua kumi na mbili wakiwa vifua wazi, wamebebelea mishale, mikuki na mapanga, waliwazingira katika hali ambayo hakuna sauti yoyote ilisikika – kama mizuka.
Wanaume hao walikuwa wamejichora chora michoro ya ajabu miilini mwao. Si kaptula wala suruali walivaa, bali ngozi zilizofungiwa vema viunoni mwao vipate kuwasitiri nyeti. Miguuni walikuwa peku. Kwenye mapaja ya mikono yao ya kushoto walifunga kamba isipokuwa mwanaume mmoja tu ambaye yeye pekee ndiye aliyevalia kofia kubwa la manyoya kichwani, shingoni akivalia cheni ya mifupa.
Mwanaume huyo alikuwa ana macho makubwa meupe yaliyokodoa. Aliwatizama wenzake akapandisha kichwa, wote wakasogea zaidi wakinyanyua mikono yao kana kwamba wanataka sasa kushambulia ndani muda mfupi ujao. Kabla hawajatimiza adhma, Vitalis alishituka usingizini mithili ya mtu aliyeona mzimu.
Alihema kama mbwa mwitu akitizama pande zake zote pasipo kuona kitu. Hakukuwa na lolote isipokuwa giza tu. Hakutosheka, alinyanyuka akatembea hatua kadhaa kila upande kabla hajarudi alipokuwa ameketi na kuanza kupekenyua mkoba mmoja uliokuwa kando, akatoa sindano.
Alishusha pumzi ndefu. Alipapasa papasa mkono wake wa kulia maeneo ya mkunjo akitafuta mshipa wa damu, taratibu akapeleka hapo sindano na kujidunga kwa uangalifu mkubwa wa vidole vyake kwenye uhakiki.
Alirudisha sindano mkobani, akajaribu kujilaza tena. Isichukue muda mrefu, akasikia sauti ya majani yakimwendo. Alikaa kitako akatizama tizama, mwishowe alipuuzia akaacha usingizi umbebe.
Watu wale waliokuwa wanataka kuvamia walikaa umbali wa mita kadhaa wakitizama yote anayofanya Vitalis. Japokuwa kulikuwa na giza totoro, kwao haikuonekana shida, walimuona vema Vitalis akihangaika hangaika mpaka pale alipoamua kujilaza.
Mwanaume yule mwenye shungi la manyoya alipiga kamluzi kadogo, wote wakaondoka eneo hilo wasijulikane hata wapi walielekea.
Masaa yalisonga, jua likachomoza. Kaguta alikuwa wa kwanza kuamka kabla ya yeyote. Alijikongoja akaenda baharini kupata maji, baada ya muda mfupi aliungana na Bakari na Miraji majini. Sandra naye na Bernadetha wasichukue muda wakaamka wakatengenezea kuni na kuwasha moto kwa ajili ya kuandaa chai. Muda wote huo, Vitalis alikuwa bado yu usingizini. Tena si usingizi mwepesi, bali ule wa kukoroma hoi bin taabani.
Sandra alimtizama Vitalis akamwambia Sandra:
“Sandra, unadhani ni kawaida?”
“Nini?” Sandra alijibu kwa kuuliza.
“Vitalis kulala mpaka saa hizi wakati yeye ndiyo huwa wa kwanza kuamka kila siku?”
“Labda kachoka. Kazi ya jana ilikuwa pevu.”
“Sidhani. Mbona wenzake wamekwisha amka? … huwa ikifika saa kumi na moja tu, Vitalis anaamka. Haijalishi amefanya kitu gani jana yake.”
“Kwahiyo wewe unahisi nini?”
Bernadetha alirusha macho yake vema akaona mkoba mmoja uliokuwa karibu na Vitalis ukiwa wazi. Alinyanyuka upesi akafuata mkoba huo alioutwaa na kutizama ndani. Akaona sindano tupu.
“Nilijua tu.” Alijisemea mwenyewe. Alichuchumaa akapachika kiganja chake kwenye paji la uso la Vitalis.
“Mmmh … wa moto.” Akasema tena. Alimtizama Vitalis kwa macho ya huruma, akatikisa kichwa.
“Nini kimetokea Vitalis? …” Alinong’oneza. Mara Vitalis akakurupuka. Bernadetha alimshika mabega akimtuliza.
“Tulia Vitalis … tulia, tupo hapa. Tupo wote.”
Vitalis alishusha pumzi akatizama chini. Bernadetha akamuuliza:
“Imekurudia jana, sio?”
Vitalis akatikisa kichwa kukubali.
“Ulijis’kiaje?”
“Nilihisi kuna watu wamekuja kutuvamia … nilisikia sauti za ajabu na vishindo vyao vikisogea tokea mbali. Nilipoamka sikukuta yeyote. Ila bado nilikuwa nasikia sauti … sauti kana kwamba wanatembea.”
“Haukuwaona kabisa?”
“Sikuwaona! Labda kwasababu sikugeuka mnyama kabisa. Niliwahi kujidunga sindano ndipo nikapata ahueni. Nikalala.”
“Pole sana. Ila upo sawa sasa.”
Alisema Bernadetha kwa tabasamu la matumaini. Vitalis alishika kichwa akalalama:
“Kichwa kinanipasua.”
Bernadetha akamlaza akimwambia:
“Pumzika. Mwili wako umetoka kwenye kazi kubwa ya kurudi kwenye hali yake.”
Vitalis akajilaza tena.
Bernadetha alinyanyuka akamrudia Sandra. Alimueleza yale yote aliyoyasikia toka kwa Vitalis, na kipindi wanapata chai akawaeleza na wanaume: Kaguta, Bakari na Miraji juu ya habari hizo.
Walipomaliza kunywa chai, Kaguta aliwaaga anaelekea bara kuleta mahitaji yaliyopungua, akilenga kwenda mapema hiyo ili awahi kurudi waendeleze zoezi lao la ujenzi lililokomea jana. Bakari alimpatia Kaguta tanakilishi pamoja na simu akazitie moto huko penye umeme.
Kaguta aliwasha boti akaondoka zake, baada ya nusu saa akakanyaga ardhi ya jiji la Dar es Salaam. Alipeleka simu na tanakilishi sehemu za kutia moto kisha akaelekea maeneo ya soko la kariakoo ambapo ndipo anachukulia mahitaji yake.
Hakuwa na papara, kwakuwa alilazimika kungoja vifaa vile vya umeme alivyovipeleka vipate moto, basi akaamua kutafuta mahali atulizane kidogo akinywa vitu vyake.
Akielekea kwenye mgahawa mmoja hapo hapo maeneo ya Kariakoo, alikatiza eneo la magazeti aoshe macho kwa kufahamu yanayoendelea ulimwenguni. Hapo vichwa viwili vya magazeti vikamteka fahamu:
MAJAMBAZI YATOROKA KIJASUSI!
MAJAMBAZI WAUA MAGEREZA NA KUTOKOMEA!
****
☆Steve