SURA YA TISA*
(MSIMU WA 02)
Wiki moja ilipita.
Inspekta alikuwa ameketi kwenye kiti kirefu cha bar akinywa mvinyo kwa mtindo wa tarumbeta. Macho yake yalikuwa mekundu na ni kama vile alikuwa amezama kwenye lindi la fikra. Alimaliza chupa nzima, akaagiza chupa nyingine, nayo akamaliza yote. Akiwa anakunywa chupa ya tatu, Kaguta alitokea eneo hilo akaungana naye.
“Aisee, Vitalis, haya madude yatakugarimu. Acha kuyaendekeza sana, unadhani hii ni suluhisho?”
Kimya. Inspekta alipeleka mdomo wa chupa kinywani akapiga mafundo kadhaa. Kaguta alimpokonya inspekta chupa akaiweka kando.
“Hapana, inatosha.”
Kaguta alimgeukia dada muuzaji akamuuliza;
“Dada amekunywa ngapi huyu?”
“Mbili, hiyo ya tatu.”
Kaguta akatahamaki. Alinyanyuka akalipia kisha akamnyanyua inspekta na kumburuta kwenda ndani ya gari.Moja kwa moja walielekea nyumbani kwa inspekta, inspekta akajilaza kwenye kochi. Kaguta aliwasha runinga akawa anatizama.
“Ni wakati wa kutulia huu ndugu yangu. Najua una mawazo sana, ila yasiwe kigezo kwako kulowea kwenye ulevi.”
Kaguta alitema cheche. Inspekta hakusema jambo. Alikuwa ametulia kimya tu. Ghafla, aliamka akaketi kitako huku akitoa macho yake.
“Vipi!” Kaguta alishangaa.
“Barua!”
“Barua imefanya nini?”
Inspekta hakujibu. Haraka aliinuka akaelekea kufuata dustbin yake na kuanza kuokoteza vipande vya barua alivyovichana chana. Alivikusanya vyote akarudi sebuleni na kuviweka juu ya meza. Akawa anavitizama kwa umakini zaidivile vipande vilivyounda bahasha kuliko vile vya barua.
Baada ya muda aligundua jambo.
“Kaguta. Embu sogea karibu.” Inspekta aliita. Kaguta alisonga karibu na kutizama vipande vya bahasha alivyovipanga inspekta. Akafungua kinywa;
“Haya si maandishi? Au macho yangu?”
“Ndio. Umeona yameandikwa nini? Mimi sikuyaona kabisa.”
“Rosemath Stationary.” Kaguta alisoma maneno yale huku akiyafuatisha na kidole kisha wakatizamana na inspekta kwa macho yaliyobebelea kiulizo.
“Ndio nini?” Kaguta aliuliza.
“Hii bahasha ilikuwa imebebelea ujumbe nilioachiwa na wauaji siku waliyomuua mke wangu na mwanangu. Hii stationary itatusaidia kuwapata.”
“Una uhakika gani tukiipata hiyo stationary tutawapata?”
“Kuipata hii stationary ni hatua ya kwanza kuwatia nguvuni. Amini hivyo.”
“Sawa. Kwahiyo tunaenda kuitafuta saa ngapi?”
“Saa hii.”
“Acha masihara wewe! Na ulivyo chakari hivyo, uende na nani?”
“Nani kakuambia nipo chakari?”
“Kwani mpaka niambiwe. Si naliona mwenyewe hapo. Pumzika tutafanya hiyo kazi kesho.”
“Hapana! Hapana Kaguta! Siwezi nikakaa hapa bila ya kufanya lolote. Roho ya mke wangu na mwanangu inanidai.”
“Basi fanya hivi. We pumzika, acha mimi niende.”
“Uende mwenyewe? Hapana!”
“Acha ubishi basi ndugu yangu. Huniamini?”
“Nakuamini.”
“Sasa shida nini? … Acha niende. Wewe pumzika, nitakuletea feedback.”
Inspekta hakutia neno lakini uso wake ulionyesha kama vile hakuridhika pamoja kwamba ulisadifu uchovu wa kilevi.
Kaguta alisimama na kuaga akaelekea kwenye gari lake. Aliwasha gari na redio juu. Huku mziki ukitwanga alipata kujongea kwenda aelekeapo. Ndani ya dakika chache, alikuwa tayari ameshafika eneo la Rosemath stationary; jengo kubwa jeupe lenye kuta na milango ya vioo. Kaguta alishuka akatengenezea vizuri koti lake na kuingia ndani baada ya kusukuma mlango wa kioo.
Ndani ya jengo la Rosemath stationary kulikuwa kumetapakaa hali ya hewa ya kiyoyozi. Wahudumu walikuwa watatu wote wakiwa wanawake warembo waliovalia sare za makoti meusi na suruali za vitambaa. Mashine za kuchapisha na kufyatulia kopi zilikuwa zimejaa zikirandana na tanakilishi mpakato na zile za mezani. Kwenye ukuta, kulikuwana runinga kubwa isiyo na kisogo ikionyesha video za miziki mbalimbali.
Kaguta alisogelea mezani akakaribishwa na tabasamu pana la mwanadada;
“Karibu.”
“Ahsante.”
Kaguta alirusha macho yake kutizama huku na kule juu ya mashelvu huku aking’ata lips yake. Aliporudisha macho yake kwa mhudumu alitabasamu akauliza;
“Kama vile nimewahi kukuona sehemu?”
Mwanadada alitabasamu na kubinua mdomo wake.
“Wapi?”
“Maeneo ya Mwenge.”
“Mwenge kwa nyuma hivi kwenye mwamvuli?”
“Ndio.”
“Labda, huwa napandia daladala hapo asubuhi.”
“Unapanda daladala? Aaah bwana ofisi yote hii?”
“Ha ha ha! Kwani ya kwangu? Si nimeajiriwa tu hapa.” Mhudumu alisema kwa sauti yake nyororo. Mteja mwingine aliingia na kuelekea mahali alipo Kaguta na mhudumu.
Mhudumu alisogea kidogo kumsikiliza. Kaguta alipepesa macho yake kwa chini akaona kibandiko kidogo chenye kipini kikiwa kimeandikwa Sandra. Kilikuwa ni kibandiko cha kuweka kifuani kwa ajili ya kujitambulisha kwa wahudumu. Kaguta alitabasamu akatoa ulimi wake nje na kujilamba kisha akakaa tenge kumngojea mhudumu amrudie baada ya kumaliza kumuhudumia mteja aliyeingia karibuni.
“Kwani huwa unakuja saa ngapi kazini niwe nakupitia?” Kaguta alimpokea mhudumu kwa swali. Mhudumu alitabasamu akatengenezea nywele zake ndefu zisimkere.
“Wala! Nashukuru sana.”
“Karibu, Sandra.”
Mhudumu alitoa macho kumtazama Kaguta; “Umejuaje jina langu?”
Kaguta alitabasamu akatikisa kichwa kama vile mtu anayesikitia jambo. Alilamba lips zake akamtizama mhudumu machoni.
“Si nilikuambia nakujua. Wewe ndio hunijui. Anyway, naomba unitolee kopi kitambulisho changu hiki nataka nikasajili line.”
Kaguta alitoa kitambulisho cha mpiga kura pamoja na elfu kumi akamkabidhi Sandra.
“Kutoa kopi shingapi?”
“Mia mbili tu.”
“Haya nitolee basi kopi mbili.”
Sandra alifuata mashine ya kutolea kopi akaweka kitambulisho cha Kaguta na kuamrisha mashine ifanye kazi. Kaguta alimtizama Sandra kwa macho ya matamanio. Sandra alikuwa na mvuto, si tu wa sura bali wa umbo pia. Nyonga zake zilikuwa nyembamba wakati mapaja yake yakiwa ya kujaa na mwenye kalio la wastani. Alipomaliza kutoa kopi, alimrudia Kaguta akiwa kashikilia chenji mkononi.
“Hii hapa.” Sandra alitoa kopi pamoja na kitambulisho. Baada ya hapo akatoa na chenji.
“Hapana! Utakunywa soda hiyo.” Kaguta alimwambia Sandra. Kabla Sandra hajatia neno, Kaguta alikuwa tayari ameshatoka ndani ya jengo. Alifuata gari lake akajiweka ndani akatizama jengo la Rosemath kwa muda kidogo kisha akapotea eneo lile.
****
☆Steve