SteveMollel
JF-Expert Member
- Jul 12, 2015
- 8,768
- 25,089
Simulizi:- "Intelijensia inapokutana na nguvu ya upande wa pili wa dunia.
BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA.
Biashara kubwa ya magendo inafanywa na watumishi wa serikali akiwemo Bwana Malale aliyeshawishiwa na wenzake kwasababu ya ukata. Pale biashara hiyo inapobumburuka, Bwana Malale anahaha kutafuta msaada kwa wenzake waliomshawishi bila ya mafanikio. Mwishowe anauwawa ili kuficha siri.
Kifo hiki kinaleta utata, kinaleta kisasi bandia. Kinamvumbua wa aliye nyuma ya pazia – Baradhuli mwenye mikono yenye nguvu.
Baradhuli mwenye mikono mirefu. Baradhuli mwenye mikono ya chuma. Ni mpaka pale akionja kifo tu, ndipo dunia itakuwa salama tena.
RATIBA YA SIMULIZI: Kila siku usiku saa tatu usiku. Nitaituma mwanzo mpaka mwisho hapahapa.
*****
SURA YA KWANZA:
Dar es Salaam, miaka ya karibuni.
Jua lilikuwa njiani kukomaa. Sauti za magari zilinguruma zikijaza pande zote nane za jiji la Dar – jiji karimu kwa joto na karaha za usafiri.
Wakati ikiwa ni saa tano tu iliyo njiani kuitafuta saa sita iwe mchana, tayari maeneo ya Mbezi beach mpaka Mwenge palishatapakaa foleni ya kushiba ikisababishwa na ajali mbaya iliyotokea maeneo ya Kawe darajani kati ya magari manne binafsi na bodaboda.
Kutokana na ukubwa wa foleni hiyo isiyoleta matumaini ya kusonga, watu wengi wakashuka kwenye magari yao binafsi na kuketi nje ama basi watembee kupunguza uchovu. Abiria wengi wa madaladala nao wasiwe nyuma, wakaradhi washuke kutembea ama kunyoosha viungo vyao; hali hiyo ikapelekea barabara kufurika watu kana kwamba kuna maandamano ya kisiasa.
Katika msururu huo wa magari, binafsi na daladala, yakiwa yamejipanga kutengeneza umbo la nyoka mkubwa, miongoni mwa daladala mojawapo la Mwenge-Tegeta lililokuwepo maeneo ya Makonde, upande wa kushoto dirishani aliketi mwanadada mmoja mweupe.
Alikuwa mwembamba mno kwa umbo akibarikiwa uso mrefu wenye paji kubwa, macho rangi ya kahawia, mdomo mweusi na nywele ndefu nyeusi ti ila zilizonyimwa taratibu ya kuvutia.
Msichana huyo alikuwa anatizama nje kupitia dirishani macho yake yakionyesha ametekwa kitafakuri. Mara zingine alitikisa kichwa chake mdomo ukionekana unateta jambo ambalo halikupata kusikika na mtu mwingine yeyote ndani ama nje ya gari.
Zilipita dakika kadhaa mwanamke huyo akadondosha chozi asioneshe kujali. Chozi hilo likishuka, ghafula akapiga yowe kali na kuwashitua abiria waliosalia chomboni.
“Niache!” Alifoka. “Niache, si’ mimi!”
Alihangaika huku na huko kama aunguzwaye na moto, watu wote garini wakamtizama. Ana nini huyu?
Hakukoma, aliendelea kujirusharurusha huku na huko akijibamiza mpaka pale alipovunja kioo na kujijeruhi vibaya, damu zilimchuruza kichwani kama maji.
Wanaume wawili garini walijitolea kumtuliza lakini hawakufanikiwa, walizidiwa nguvu wakarushwa mbali mhanga akaendelea kujiadhibu kwa kujibamiza; damu zikimmwagika, mdomowe bado ukilalama sio yeye na anakufa!
Isichukue muda mrefu, mwanamke yule akalala chini na kutulia tuli. Abiria walimsogelea wakamtazama.
Amekufa? Damu bado ziliendelea kuchuruza kichwani kwake na kutapakaa garini. Dereva alitikisa kichwa chake akatoa mlio wa kuita paka.
“Mkosi gani huu!” Alilaumu.
“Huyu mwanamke kapatwa na nini?” Aliuliza kana kwamba kuna ajuaye kwa undani kilichojiri. Swali hilo likazua mzozo kila mtu akajaribu kueleza anavyofahamu yeye: wengine wakasema ana mapepo, wengine wakahukumu alikuwa na msongo wa mawazo kwa hoja kwamba tangu apande gari alionekana ana mawazo mengi.
Ila kwa muda huo kondakta alikuwa kimya akiutathmini mwili wa mwanamke huyo. Na baada ya sekunde chache alikumbuka jambo.
“Huyu mdada alipandia gari maeneno ya Mbuyuni. Nakumbuka wakati anasimamisha gari alikuwa anakimbia akitazama nyuma. Sijui kuna mtu alikuwa anamkimbiza, sifahamu!”
Kauli hiyo ya konda ikazidi kuleta mkanganyiko. Walimpekua yule dada mifukoni wakakuta kitambulisho kilichomtambulisha kama karani wa kampuni ya Kim na Kamugisha (K&K) inayopatikana maeneo ya Kunduchi Beach karibu na shule ya Bahari. Abiria mmojawapo alijaribu kupiga namba elekezi iliyoainishwa kitambulishoni, ikapokelewa.
Alifafanua juu ya dhamira ya simu yake, akapewa ahadi ya hilo jambo kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi. Baada ya muda kidogo gari la wagonjwa likiwa linapata taabu kukatiza pembezoni mwa barabara ya lami, likafika eneoni na kumchukua mlengwa kwa msaada wa maelekezo ya abiria.
Lilitokomea upesi likirudi Tegeta. Tungeweza kubashiri lilikuwa laenda hospitali ya IMTU. Lilikakata kona na kupenya penya mithili ya panya. Likiwa limekaribia kuwasili kwenye hospitali hiyo iliyopo karibu na hayo maeneo, ghafula likapoteza muelekeo baada ya kujaribu kujinusuru kukumbana uso kwa uso na bodaboda iliyokuwa inakuja kwa kasi.
Dereva alishindwa kumudu gari hilo hatimaye likavamia gari lingine.
Watu wote ndani ya gari la wagonjwa walifariki papo hapo!
NINI JAMBO NYUMA YA PAZIA?
***
SURA YA PILI:
Dar es Salaam, miaka kadhaa nyuma:
Mida ya mchana ilipofika, Marietta, msichana mwenye miaka kumi, mrefu na mwenye uweusi wa kung’aa, alitoka eneo la shule akijirudisha nyumbani. Alikuwa amechoka kwa mujibu wa mwendo wake. Alitembea kigoigoi akiburuza miguu. Aliufungua mlango kivivu akaingia ndani.
Cha kwanza kufanya ikawa kuita:
“Mamaaa!”
Aliijitupia kochini. Alinyamaza kwa muda kidogo kusikilizia majibu lakini hakusikia kitu.
Alinyanyuka akaenda jikoni moja kwa moja mpaka kwenye masufuria aliyoyafungua na kutizama kama kuna chochote kitu. Hakukuwa na lolote, pakavu. Alisonya akaelekea chumbani, akajilaza kitandani na sare zake za shule tumbo likinguruma kwa njaa.
Wazo lilimjia, alinyanyuka akafuata jokofu kutizama kilichomo ndani, lakini bado majibu yakawa yaleyale, hakukuwa na kitu chochote cha kutia mdomoni. Alivuta mdomo akajipiga mapaja. “Jamani! Aaah! Tokea jana mi s’jala. N’taishije sasa? ... Nasikia njaa!” Alifoka.
Aliifuata simu ya mkononi maeneo ya kabatini akaweka namba na kuziita. Baada ya muda kidogo …“Mama! ... Mi nasikia njaa, mbona chakula hamna sasa? ... We unakuja saa ngapi? ... Upo ospitali? ... Sasa mimi je? ... Mi siwezi kuvumilia mama … Njaa inauma!”
Simu ikakata. Alijaribu kupiga tena, mara hii akaambiwa salio halitoshi. Aliitupa simu chini akarukia kochi na kuanza kulia. Hakunyamaza mpaka pale usingizi ulipomtwaa. Alilala kwa masaa mawili akaja kurupushwa na sauti za kilio tokea nje. Sauti mojawapo aliitambua ni ya mama yake, haraka akalifuata dirisha na kuchungulia.
Aliona gari moja kubwa: Toyota Prado nyeusi, pamoja na mzee mmoja mnene mwenye kiwaraza akiwa kamshikilia mama yake aliyekuwa analia. Alitoka nje upesi akitwaliwa na hofu. Alimuuliza mamaye kwanini analia lakini hakupewa jibu, wala yule mzee mwenye kiwaraza, kwa jina Mtemvu, hakumsemesha. Alikuwa bize akimbembeleza mama yake wakielekea ndani.
“Pole, shemeji. Yote ni mipango ya Mungu.” Mtemvu alifariji. Mama Marietta, ama Bernadetha kwa jina, akamjibu kwa kilio cha nguvu ambacho kilichukua muda kukoma. Marietta naye alilia asifahamu anacholilia ni nini.
Bernadetha aliingizwa ndani bado akiendelea kulia na Marietta naye akifichwa kilichojiri…Ndani ya muda mchache watu walijaa kwenye nyumba hiyo kila mmoja akimnyookea mama Marietta na kumpa mkono wa pole.
Hapo ndio Marietta akafahamu nini kilichojiri – Baba yake, bwana Malale, aliyekuwa amelazwa kwa miezi kadhaa, amefariki dunia. Alilisikia hilo kwenye kinywa cha mmoja wa waombolezaji waliofika nyumbani kwao. Basi huo kwake ukawa muendelezo wa yeye kulia, akijumuisha na njaa aliyokuwa anasikia hapo awali, ambayo kwa dakika kadhaa ilikoma.
Watu walizidi kufurika kwenye makazi hayo, wengi wakija na magari yenye plate number: STK ama DFP. Maturubai yaliletwa uwanjani yakafungwa na viti vya plastiki navyo waombolezaji wapate kukaa. Michango ya mamilioni ilitolewa.
Siku iliyofuata mtoto wa kwanza wa marehemu mwenye miaka ishirini na tatu, kwa jina Miraji, alirejea nchini akitokea India alipokuwa akisomea udaktari. Kwa mujibu wa Imani za wafiwa, marehemu akazikwa siku hiyohiyo.
Kijikao cha familia kiliitishwa kikiundwa na watu watano: mke wa marehemu: Bernadetha, mtoto mkubwa wa marehemu: Miraji, pamoja na kaka na dada wa marehemu.
Waliketi sebuleni nyuso zao zikitandazwa na huzuni.
Waliswali kikao kikafunguliwa na kaka wa marehemu, bwana Tahid. Mbaba mwenye mwili mpana na ngozi nyeupe pe!
“Natumai tu salama salmini baada ya kutoka katika shughuli pevu hapo jana na hata juzi. Ningependa kuchukua nafasi hii sisi kama familia kujulishana hasa ni nini kitakachofuata baada ya mwenzetu, mwanafamilia mwenzetu kutwaliwa na mwenyezi Mungu.
Kama tunavyofahamu, japokuwa kulikuwa na matatizo ya hapa na pale yaliyopelekea mwenzetu kutengwa na jamii, vilevile kusalitiwa na muajiri wake, serikali, sisi katika muda huu ndiyo yatupasa tuwe zaidi ya kitu kimoja.”
Akaweka kituo. Alisafisha koo akaendelea:
“Basi kutokana na hali iliyopo sasa, makubaliano na maagano yetu kama familia yatakuwa hivi: nyumba ya marehemu itakuwa chini ya mkewe na wanawe.
Mwanaye mkubwa atabaki nyumbani kwasababu hakuna pesa ya kusoma huko nje tena, wote tunafahamu kwamba bwana Malale alifilisiwa kila kitu pamoja na miradi yake yote na serikali. Kwahiyo sisi kama ndugu tutachukua jukumu la kuchangia familia kwa kile chochote kitakachopatikana pale patakapokuwa na muhitaji. Nadhani tumeelewana.”
Hoja zilizosemwa na bwana Tahid hazikupingwa na yeyote kikaoni. Wote waliafiki makubaliano hayo. Bernadetha alitizama chini machozi yakaanza kumbubujika tena upya. Miraji alimbembeleza akimtaka anyamaze asije mkufuru Mungu, mama akainua uso wake wenye uchovu akisema:
“Yupo wapi huyo Mungu, mwanangu? Baba yako alikuwa anafanya kazi kama punda, si Mungu wala serikali yake ilimuona. Pesa ilikuwa shida. Hamkusoma wala kula vizuri. Angefanyaje na yeye ni baba?
Alirubuniwa akajiingiza kwenye biashara za magendo - hakuwa na namna. Na hapo ndio maisha yalibadilika, mkasoma na kula vizuri. Lakini ndivyo havikudumu wakamuabisha, wakamdhalilisha na mwishowe kumuua kabisa!”
“Usikufuru, shemeji.” Bwana Tahid alimkatiza. “Yote hiyo ni kazi ya Mwenyezi Mungu. Wote tunajua ya kwamba mdogo wangu aliumwa.”
“Aliumwa?” Mama Marietta aliwaka. “Kuumwa gani kule? Ameumwa baada tu ya kuvamiwa hapa nyumbani na kupuliziwa madawa yaliyomfanya awe hoi kwa kuzidiwa.
Kama haitoshi hata huko hospitali wakaendelea kuisaka roho yake kwa udi na uvumba tukawa tunahama hospitali kila baada ya siku chache lakini bado haikusaidia. Majibu yake yalionyesha ameuwawa kwa sumu lakini hakuna aliyejali! Hakuna!”
Mama Marietta alikabwa na kilio, alishindwa kuendelea. Alinyanyuka akajiendea zake chumbani na kujifungia nyuma akiacha mzozo ukizizima.
“Alichokisema mama ni kweli bam’kubwa?” Miraji aliuliza.
Tahid alishusha pumzi yake ndefu mithili ya kuli aliyetua mzigo kisha akatizama chini. Shangazi, dada wa marehemeu, akateka zamu na kusema:
“Mwanangu, usijali ya Mungu mengi. Mama yako kwa sasa hayuko sawa. Ni vyema tukamuacha tu, mdomo wake unasukumwa na uchungu alio nao.”
Jibu hilo halikuonekana kumkosha Miraji – halikukunjua uso wake uliokunjamana. Aliminya lips akarusha macho yake kando. Kichwani sauti ya mama yake ilikuwa nzito kuliko zile hoja nyepesi alizopewa na ndugu.
***
Muendelezo soma hapa