***SURA YA ISHIRINI NA NANE***
(MSIMU WA 02)
Mlango wa nyumba ulipofunguliwa, Miraji na Jombi walirusha macho yao wote kuona nani anaingia. Hakuwa mwingine bali Bernadetha, mama Miraji, aliingia ndani akatengeneza tabasamu usoni.
“Mnaendeleaje?”
“Safi tu. Vipi huko utokako?” Miraji aliuliza.
“Kwema tu.”
“Kweli?”
“Ndio. Kwema.”
“Sidhani kama ni kwema. Gauni lako lina damu.”
Bernadetha akashtuka kusikia hivyo, alitizama gauni lake kwa chini kweli akaona alama za damu. Macho yakamtoka.
“Mama, hakuna haja ya kunidanganya. Najua umetoka kwa inspekta. Vipi ana jeraha?”
Bernadetha alishusha pumzi ndefu akatikisa kichwa chake kama mtu akubaliye jambo. Akasema:
“Ndio, ana jeraha. Umefurahi?”
Hakusubiria jibu. Alienenda zake kwa mwendo wa haraka kuelekea chumbani. Miraji na Jombi wakamsindikiza kwa macho mpaka anazama.
“Naomba niondoke, Miraji. Inaelekea kuna tatizo huko nyumbani.”
Jombi aliaga. Miraji akanyanyuka na kumtoa mpaka nje.
“Kwaheri, Jombi.”
“Kwaheri. Hakikisha unazingatia na kuyatafakari yale niliyokuambia.”
“Sawa.”
Jombi alishika njia akaondoka. Miraji alirudi sebuleni akajilaza kwenye kochi. Baada ya muda mama yake akaja na simu na daftari akaketi papo, akawa anapiga mahesabu ya biashara zake. Kwa muda kama dakika kumi, hakuna aliyeongea na mwenzake mpaka pale mama alipofunga daftari lake la mahesabu.
“Mama, mbona umetoa picha ya baba sebuleni?” Miraji aliuliza. Mama akamtizama bila ya kumjibu, akaendelea kubofya simu yake.
“Mama, nimeuliza. Mbona umetoa picha ya baba sebuleni?”
“Kwani umeona leo?”
“Ndio, nimeona leo haipo.”
“Embu wacha nikuulize. Hii nyumba ya nani?”
“Ya kwetu.”
“Ulitoa hata sumni kuijenga?”
“Si alijenga baba yangu.”
“Mpumbavu wewe! Funga bakuli lako. Kwa kazi gani ya maana aliyokuwa nayo baba yako ajenge nyumba kama hii peke yake? Hii nyumba tumejenga mimi na baba yako, tukijibana na kujinyima kadiri tulivyoweza. Baba yako amefariki, hii nyumba ni ya kwangu, usinipangie nini cha kufanya. Umesikia?”
“Mama, jua mimi ni mwanao …”
“Kama ungekuwa unalijua hilo, ungekuwa na adabu na mimi. Umekuwa mtoto wa ajabu sana. Adabu huna, unanipandishia sauti kama vile unaongea na housegirl. Umekuwa wa kunchagulia wapi pa kwenda, kipi cha kuongea. Nikitoka uniulize nikirudi uniulize, naishi mahakamani?”
“Mama nafanya yote hayo kwa ajili yako.”
“Nimekuomba? Wakati unaumwa umelala kitandani hujielewi kwa lolote, nani alikuwa ananilinda? Mimi sio dada yako, mama yako!”
“Mama yote hayo ni kwa ajili ya …”
“Funga mdomo wako! Ishia hapo hapo.”
Macho ya Bernadetha yalikuwa mekundu. Alifura kama simba aliyejeruhiwa. Alikuwa anahema juu juu. Alikwapua daftari lake kama kibaka akarudi chumbani.
Zilipita siku tatu mwisho wa wiki ukabisha hodi. Bernadetha akatimiza ahadi yake kwa mwanae, Marietta, aliongozana naye kwenda kumtembelea inspekta Vitalis. Huko wakamkuta inspekta akiwa amekaa kwenye kiti cha matairi, Jombi akiwa ndiye dereva wake akimpeleka huku na huko.
“Hukuenda hospitali, Vitalis.” Bernadetha alitamka akiwa na uso usio na utani.
“Ndio, sikwenda.”
“Kwanini?”
“Nimeshindwa kwenda.”
“Umeshindwa? … Kivipi?”
Inspekta Vitalis hakupewa muda wa kujibu, Marietta alikuja haraka akitokea nje akamrukia Vitalis.
“Mariettaaa, si nimekuambia uncle anaumwa? Nenda nje kacheze.” Bernadetha alifoka. Marietta akasimama na kunywea ghafla.
“Muache bana. Njoo Marietta.” Vitalis alimvuta Marietta akamshika mkono. Marietta akamuangalia Vitalis kwa tabasamu.
“Utapona lini uncle uje kwetu?” Marietta aliuliza.
“Muda si mrefu napona. Ila ukitaka nipone haraka uwe unakuja kun’tembelea.”
“N’takuja kila siku.”
“Nitafurahi kweli. Haya shika hii kanunue chocolate. Si unapenda chocolate?”
“Ndio.”
“Haya kanunue.”
Inspekta Vitalis alitoa elfu moja mfukoni akampatia Marietta. Marietta alishukuru kisha akatoka ndani akawaacha Bernadetha na inspekta Vitalis. Wakaendelea kuteta:
“Tokea nimetoa taarifa kazini hakuna lolote ambalo nimefanyiwa. Hakuna hatua yoyote ambayo wameichukua. Sina pesa, Bernadetha.”
“Una uhakika taarifa imewafikia?”
“Exactly. Nimepiga mpaka na simu, wameishia kunipatia kiti tu cha matairi.”
“Labda wapo kwenye process. Nina uhakika watafanya jambo, Vitalis.”
“Lini? Hali yangu haisubiri.”
“Naamini hawatokuacha. We usichoke kuwasumbua kuwapa taarifa.”
Kinyume kabisa na alivyosema Bernadetha, majuma yakazidi kukata bila ya inspekta Vitalis kupokea mkono wowote wa msaada toka kazini kwake.
Mara kwa mara Bernadetha alikuwa anakuja kumuona na kumjulia hali, vile vile Kaguta. Hata inspekta alipokwenda kazini akiwa kwenye kiti cha matairi, hakuna alichoambulia zaidi ya ahadi tu. Mwishowe alikata tamaa. Kama haitoshi, akatumiwa barua ya kufukuzwa kazi.
“Siwezi amini kama haya ndio malipo ya kazi yote ile niliyofanya.” Vitalis alimwambia Kaguta kwa sura ya uchungu.
“Nilijitolea kwa hali na mali kupambana na kutimiza majukumu yangu, leo hii naishia kuwa fukara kilema?” Vitalis alitabasamu huku akitizama chini. Kaguta akamshika bega na kumpa moyo:
“Yote ni maisha, Vitalis, usinononeke sana. Mimi nipo, hakuna litakalo kwenda kombo.”
Vitalis akageuka mlevi. Kila siku alitaka aletewe pombe na Kaguta, na hata pale ilipokosekana kabisa alidiriki kumtuma Jombi kiroba hata cha mia tano apate kunywa.
Hakuweza kulala akiwa na akili timamu bali pombe. Hakuwa na hamu ya kula, Bernadetha alijitahidi kumpikia ila akiondoka tu, anaacha papo hapo. Hata afya yake ikaanza kuzorota. Miguu yake ikalemaa kabisa kutokana na kutokula wala kutotaka kufanya mazoezi. Hakuwa tena Vitalis yule, bali Vitalis aliyekuwa hajipendi wala kujijali tena.
“Naomba ukakae nae, hakuna tena jinsi. Yupo stressed sana, hali yake inaweza ikawa mbaya zaidi.” Kaguta alimwambia Bernadetha. Bernadetha alitizama chini kama mtu anayefikiria, uso wake ulikuwa umenyong’onyea mno. Alinyamaza kwa muda kidogo machozi yakambubujika.
“Nitajitahidi kulifanyia kazi, Kaguta.”
“Please. Vitalis anakuhitaji sana kwa sasa.”
“Nitajitahidi Kaguta.” Bernadetha alisisitizia. Kaguta alinyanyuka akaaga. Bernadetha akabaki mwenyewe sebuleni na uso wake uliopoa. Kwa muda wote waliokuwa wanaongea na Kaguta Miraji alikuwa ametega sikio mlangoni akisikiliza.
Kaguta alipoondoka, Miraji akafungua mlango na kwenda kumkuta mama yake sebuleni. Aliketi kando akamtazama mama yake aliyekuwa anabubujikwa na machozi, akamshika mkono.
“Mama.” Miraji aliita. Mama akageuza uso na kumtizama.
“Mara yangu ya mwisho kukuona katika hali uliyopo ni kipindi kile baba alipokufa. Haukuwa na raha. Ulikonda kwa mawazo. Hukutaka kuongea na mtu yeyote zaidi ya kulia kila uchwao. Na yote hayo ni kwakuwa ulimpoteza mtu uliyempenda. Siwezi kukuona ukipitia katika hali ile kwa mara ya pili kwa mana najua jinsi ninavyojisikia nikikuona hivyo. Nakuomba futa machozi mama. Nenda kapiganie maisha ya unayempenda.”
Miraji alisema kwa sauti ya chini na punde machozi yalimtoka. Mama yake alimtizama huku naye machozi yakimbubujika. Alimvuta mwanaye akamkumbatia kwanguvu na kumwambia:
“Ahsante. Wewe ndiye Miraji niliyekumis kwa muda wote huo tangu ulipodondoka.”
Miraji alitabasamu, akasema:
“Nisamehe mama kwa kukatili moyo wako kwa muda wote huo. Sasa naelewa ni jinsi gani Vitalis anamaanisha kwako.”
Alimfuta machozi mama yake kwa kutumia vidole vyake, akamwambia:
“Nenda mama.”
Mama akamjibu:
“Nataka twende wote.”
Miraji akatikisa kichwa.
*****
☆Steve