***SURA YA ISHIRINI NA TISA***
(MSIMU WA 02)
Bernadetha pamoja na familia yake walihamia kwa Vitalis. Kwa sababu ya kipato, Bernadetha alilazimika kutumia vyeti vyake vya taaluma kutafuta kazi ya unesi hospitalini. Alipata kazi, sasa ikamlazimu biashara yake ya kuuza vitenge amkambidhi mwanae,
Miraji, aendeleze nayo, wakiwa pamoja na Jombi wakajitolea kufanya biashara hiyo, yote hayo yakiwa yamelenga kukuza kipato kwa ajili ya kumsaidia Vitalis. Baada ya muda wa wiki mbili Vitalis alipelekwa hospitalini, Bernadetha akawa anamuhudumia huko. Mara kwa mara Kaguta alikuwa anakuja kumjulia hali rafikiye hospitalini, pamoja na Jombi na Miraji.
Siku moja wakati Bernadetha akiwa anaongea na Vitalis kwenye kitanda cha hospitali, alikuja mwanaume mmoja mnene aliyevaa shati jeusi na suruali ya bluu ya jeans akamuita Bernadetha nje. Bernadetha akabadilika sura kwa kunyong’onyea, alimuaga Vitalis na kwenda nje.
“Sasa inakuaje lile ombi langu. Tangu umepata kazi umen’sahau kabisa na unajua usingeipata bila yangu.” Sauti ya kiume ilisikika.
“Najua. Ila tafadhali naomba muda.” Sauti ya Bernadetha ilivuma.
“Mpaka lini sasa?”
“Muda si mrefu. We nivumilie tu.”
“Nataka kesho unipe jibu langu.” Sauti ya kiume ilisema kisha punde Bernadetha akarudi ndani ya chumba alicholazwa Vitalis. Hakujua kama Vitalis kasikia kila kitu.
“Nani huyo?”
“Aah jamaa fulani hivi … mkurugenzi wa hospitali.”
“Anasemaje?”
“Alikuwa ananikumbushia tu baadhi ya majukumu.”
Vitalis hakuuliza tena. Waliendelea na habari zingine. Siku iliyofuata Kaguta alikuja kumjulia hali Vitalis, Vitalis akamueleza juu ya saga la mkurugenzi wa hospitali na Bernadetha.
“Nataka umfanyie kazi huyo mbwa. Haraka iwezekanavyo.” Vitalis alimwambia Kaguta. Kaguta akatabasamu na kuuliza:
“Lishakwisha hilo, kuna lingine?”
Vitalis alitabasamu akasema: “Hakuna mkuu.”
Kaguta akatabasamu.
Kesho yake asubuhi Kaguta akiwa kavalia miwani ya macho, suti nyeusi matata na tai, mkononi akiwa kashikilia briefcase alienenda mpaka mapokezi akapokelewa na mwanadada mwembamba mweupe.
“Naweza nikakusaidia?”
Kaguta alimtizama yule mdada na macho nje ya miwani, akasema:
“Sorry, My name is Peltridge Allan from Detroit, USA. I want to see your manager.”
Kaguta alinena kwa lafudhi ya muamerika mweusi. Macho yake yalikuwa yanaonyesha kujiamini na akiamini kile anachokinena. Mdada wa mapokezi alimtizama mwenzake aliyekuwa naye kwenye chumba, akamwambia:
“Leo tumepata muamerika, mweh!”
Kaguta alitabasamu kidogo kisha akaurudisha uso wake katika hali ya u-serious. Mdada wa mapokezi alimtizama kisha akamuelekeza:
“Just take this corridor till you see a door with a badge written ‘manager’. There you are.”
Kaguta alitabasamu, akatikisa kichwa chake kimaridhiano.
“Thanks madam.”
Alisema kisha akashika njia ya korido, lakini mara akarudi mapokezi.
“Sorry, madam. May I have your phone number if you don’t mind?”
Mdada wa mapokezi alitabasamu na kumwangalia mwenzake kwa macho yenye jazba la furaha, alichana karatasi haraka toka kwenye counter book lililokuwepo mezani akaandika namba yake na kumkabidhi Kaguta.
“Here it is.”
Kaguta alitabasamu ishara ya shukrani alafu akaondokaze.
“Sasa wewe Rhoda, umechana kitabu cha wageni jinsi ulivyokuwa huna akili!”
“Aaah bwana! Ulitaka nilaze damu tena. Watu tunatafuta fursa.”
“Nani kakuambia huyo mkaka anakutaka?”
“Hujaona alivyokuwa ananitizama? … hehehe! Kalaghabao dada. Nitaenda zangu America we uendelee kusugua gaga manzese.” Alijinadi mdada wa mapokezi, ama Rhoda. “Na hapa akitoka tu huko namwambia anibip. Yani nishajiona Amerika mie. Mungu mkubwa jamani!”
Mwenzake na Rhoda alibinua mdomo akaendelea na kazi yake ya kupanga panga mafaili.
----
Ngo! Ngo! ngo!
“Welcome!”
Mlango ulifunguliwa na Kaguta akaingia.
“Habari yako?” Kaguta alisalimu.
“Njema tu, naweza kukusaidia?”
“Unaweza haswaa kunisaidia.” Alisema Kaguta huku akiketi kwenye kiti. Mkurugenzi aliacha shughuli zake akamtizama. Kaguta alitoa kitambulisho chake akamuonyesha mkurugenzi. Mkurugenzi alitizama kitambulisho na macho yake ndani ya miwani kisha akatabasamu.
“Nikusaidie nini, afande?”
Kaguta alibinua mdomo, akanyanyua briefcase yake na kuiweka mezani. Alipofungua alitoa faili moja rangi ya kahawia likiwa limeandikwa na wino mweupe, ‘SENSITIVE CASE’. Alilifungua na kulipitia kwa haraka haraka kisha akamuuliza mkurugenzi:
“Mzee, bila ya kupoteza muda. Una kesi ya kujibu.”
Mkurugenzi alitambaa na uso wa shaka. Aliubandua mgongo wake kitini akauliza:
“Kesi gani afande?”
Kaguta alitoa miwani yake akaiweka mezani.
“Tangu mwaka jana. Tangu lini mkurugenzi?”
“Mwaka jana.”
“Haswaa. Tangu mwaka jana hii hospitali chini ya uangalizi wangu. Umeona hapo?” Kaguta alionyesha mojawapo ya picha ya jengo la hospitali likiwa kwenye ukarabati wa wodi ya wanawake.
“Ndio, nimeona afande.”
“Sawia. Nimekuwa nikitembelea hii hospitali mara kwa mara na ungependa kuniuliza kwasababu gani, sio?”
“Ndio, afande. Kwasababu gani?”
“Ni kwasababu ya ukuaji wa urasimu hasa kwenye hizi hospitali binafsi. Unamjua huyu?”
Kaguta alionyeshea picha ya Bernadetha kwa kufungua upande wa pili wa faili. Mkurugenzi akaguguma na kifuache.
“Ndio, namjua. Ni mfanyakazi wa hapa.”
Kaguta alifunga faili kisha akamtizama mkurugenzi machoni kwa dakika bila ya kusema jambo.
“Kwani kuna nini, afande?”
Kaguta hakusema kitu, aliendelea kumtizama mkurugenzi na macho sh’takizi kwa dakika moja nyingine. Hatimaye mkurugenzi akapakua mdomowe:
“Afande, sijamaanisha. Nilikuwa namtania tu nipime msimamo wake.”
“Eti enh? … Ulijua haitojulikana, sio?”
“Hapana, afande. Nani kakuambia? Yeye au?”
“Camera yangu niliyoipachika kwenye korido na pia ofisini kwako, haisemi hivyo, mkurugenzi.”
“Umeweka lini camera ofisini kwangu?”
“Rudi kwenye mada, mkurugenzi. Hiyo ni kazi yangu.”
Mkurugenzi alishusha pumzi ndefu akatizama meza yake. Ni kama vile hakuwa na la kunena. Alifungua droo yake akatoa bahasha ya kaki na kuiweka mezani kisha akaitelezesha kumfuata Kaguta.
“Chukua hiyo basi, afande. Yaishe.”
Kaguta alivuta ile bahasha karibuye akatoa marker pen na kuiandika kwa juu, ‘USHAHIDI WA HONGO’. Macho yakamtoka mkurugenzi.
“Una kesi mbili sasa za kujibu, mkurugenzi.”
Mkurugenzi alitota jasho. Akabanwa na kigugumizi.
****
☆Steve