Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

Simulizi: Baradhuli mwenye mikono ya chuma

Kitu cha ukweli hicho mkuu nakupa big up sana
 
***SURA YA ISHIRINI***



(MSIMU WA 02)





Ndani ya asubuhi ya saa mbili na nusu, Kaguta akawasili kwenye nyumba ya inspekta Vitalis Byabata. Alipiga honi akatoka mama Miraji, ama Bernadetha kwa jina alilopewa na wazazi wake. Wakasalimiana kwa bashasha la furaha kisha Kaguta akamuulizia inspekta.



“Hayupo, ametoka muda si mrefu. Nilidhani mmewasiliana.”
“Hapana. Atakuwa kaenda wapi?”
“Ameniaga anaenda hospitali kwenda kumuona dokta Rajesh Deepti wa Royal Hospital.”
“Kuna tatizo lolote?”
“Hapana. Ni ameenda kufanya tu upelelezi wake. Dokta Rajesh ndiye alikuwa daktari wa mume wangu, na yeye ndiye alikuwa anaujua ukweli wote kuhusu kifo cha mume wangu kabla ya kuupotosha umma kwa sababu zisizojulikana.”
“Sawa. Vipi mtoto ameenda shule? Yani leo nilipitiwa na usingizi kama mzoga.”



Bernadetha alicheka kidogo kisha akajibu;



“Usihofu. Vitalis ameenda naye alipoamka tu asubuhi.”
“Afadhali. Sasa acha mie niende huko hospitali nikaonane naye.”
“Safari njema.”
Kaguta aliwasha gari, ila kabla hajasogea, Jombi alitokezea tokea ndani.
“Aaaah bwana Kaguta, kweli unataka uondoke hata hatujasalimiana?”



Kaguta alicheka kwanza ndio akajibu.



“Aisee. Samahani sana ndugu yangu. Si unajua tena, haraka haraka! Vipi lakini?”
“Safi tu. Wewe je?”
“Aaah … Nipo njema tu!”
“Nadhani sasa ni bora ukashuka unywe chai kabisa.” Bernadetha alishauri.
“Najua hujatia chochote mdomoni, Kaguta. Wala usifikirie kunipiga sound zozote.” Bernadetha alisisitizia. Kaguta akabakia bila ya maneno, alishuka akaungana na Jombi na Bernadetha wakaenda ndani.



Huko ndani ya Royal hospital kwenye sakafu ya tano, Vitalis alikuwa mbele ya mlango mpana ulioandikwa jina la Doctor Rajesh Deepti. Chini ya jina hilo kulikuwa na ratiba ya maonano, Vitalis aliitizama kisha akagonga mlango.




“Who is it?”



Sauti iliuliza ikitokea ndani. Vitalis hakujibu. Alitulia kama vile hakusikia hilo swali.



“Ingia.”




Vitalis akafungua mlango na kuingia ndani.




“Nani wewe? Taka nini hapa jaona ratiba ka mlango?” Mtabibu aling’aka.


Vitalis aliketi taratibu kisha akamtizama daktari aliyekuwa na uso na nywele za kihindi usoni akiwa na miwani ya macho.




“Naitwa Inspekta Vitalis Byabata.” Inspekta akaonyeshea kitambulisho chake. “Nina maongezi na wewe.”
“Maogezi bhanaa … Taka nini kwangu?”
“Unamjua huyu?” Vitalis alitoa picha ya Malale akamuonyeshea mtabibu. Mtabibu akashtuka.
“Sijui mimi!”



Vitalis akatabasamu kwa dharau.




“Mbio zako hazitokupeleka popote, dokta. Ni bora ukaeleza ukweli bila shuruti.”
“Kweli gani nataka phephe? … Sijui kitu. Toka kwa ofisi yangu bhana niko bhize. ”




Vitalis alinyanyuka akaufuata mlango akaufunga na komeo. Mtabibu Rajesh akawahi kuchukua simu yake ya mezani, kabla hata hajasema lolote, Vitalis akawa tayari ameshamfikia na kumpokonya simu kisha akatoa bunduki yake na kumuonyeshea.




“Kwanini uliongopa juu ya kifo cha Malale?”



Uso wa Vitalis ulibadilika na kuwa mchungu ghafula, hakuonyesha masikhara hata punje. Rajesh alikuwa mpole ghafla, macho yalimtoka na pumzi yake ilikuwa inapanda na kushuka kwa haraka.




“Usiniue, takwambia … takwambia kila kitu!”
“Sema kabla sijakupa tiketi chap ya kwenda jehanam!”
“Nilitumwa! Kama singalifanya. Ingeniua!”
“Nani?”
“Temvu … Temvu na wenzhake.”
Vitalis alishusha mkono wake wenye bunduki akaketi.
“Si nimeshaambia wewe. Nenda bhasi.”
“Inabidi twende wote kituoni. Una mashtaka ya kujibu.”
“Hapana! Hapana kwenda kituoni mimi.”
“Embu tusipotezeana muda bwana mzee. Simama twende kituoni, si mpaka tulazimishane.”




Japokuwa Vitalis alitia msisitizo, Rajesh hakuwa tayari kwenda popote. Ilibidi nguvu itumike. Vitalis alimnyanyua mtabibu kwa nguvu kwa mtindo wa kukwida akamburuzia mpaka mlangoni.




Akiwa katika purukushani ya kutaka kuufungua mlango, Vitalis akaona kitu kiunoni mwa mtabibu baada ya shati la mtuhumiwa wake kupanda. Aliona tattoo! Tattoo ile ile ambayo yeye anayo ikiwa imefunikwa na shati lake la kitenge.





“Umenidanganya, sio? Wewe ni nani?”




Vitalis aliuliza kwa sauti ya kufoka. Huku akimuonyeshea bunduki mtabibu Rajesh.



“Si ameshaambia wewe. nini taka kwangu?”
“Wewe ni mfuasi wa Mr Kim. Si ndio? … Hiyo tattoo umetoa wapi?”




Rajesh akashikwa na kigugumizi. Alichomekea shati lake akatengenezea miwai yake iliyokaa upande.




“Taka nini kwangu phephe?”
“Jibu swali langu, upesi!” Vitalis aliamuru. Kufumba na kufumbua, Rajesh alinyanyua mguu wake wa kuume akatandika mkono wa Vitalis uliobebelea bunduki. Bunduki ikarukia kando. Haraka kama upepo, Rajesh akaruka teke na kumsigina Vitalis kifuani, Vitalis akadondokea chini kama fuko la marando. Rajesh akavua koti lake la utabibu akaliweka juu ya meza.



“Si unataka vita, acha uipate sasa.”




Alisema Rajesh tena kwa lafudhi nzuri tu tofauti kabisa na ile ya mwanzoni aliyokuwa anaigiza.



Vitalis alichumpa kwa kutumia mikono yake akanyanyuka na kumtizama Rajesh. Wote wakakunja ngumi kwa mtanange.




Rajesh alirusha teke akiwa hewani, Vitalis akakwepa, lle kujiweka tu sawa, zikarushwa ngumi zingine mbili za haraka, Vitalis akaipangua moja na kuikwepa nyingine ambayo ilienda na kurudi kama kiwiko haraka kikambatua inspekta kichwani. Rajesh akatabasamu. Vitalis akaguna.




“Umemaliza?” Vitalis aliuliza. Vuup! Likaja teke lingine likifuata tumbo la Vitalis, Vitalis akajiweka ubapa haraka, teke likapita kama gari moshi. Rajesh alipolirejesha teke lake kwa mfumo wa goti, Vitalis akadaka goti lile na kulisukumia kando. Rajesh akaja tena kwa pupa, mara hii akitishia kurusha teke la mguu wa kulia ingali anataka kuleta la kushoto.




Vitalis akamtangulia Rajesh hatua mbele, akauwahi mguu ule wa kushoto kwa kuukanyaga kama mtu anayepiga breki ya gari na ule wa kulia uliokuwa unatishia akaudaka na kuurejesha chini.




“Kuna jipya? Au nianze na mimi kushambulia?”




Vitalis aliuliza. Upesi, Rajesh akachukua waya wake wa vipimo uliokuwa mezani akautuma umchape Vitalis usoni. Bahati haikuwa yak wake kwani Vitalis aliinama, waya ukapita kisha akapiga ngumi mkono wa Rajesh mbele kidogo ya kwapa, Rajesh akapigwa na ganzi paaap! Waya ukadondoka chini.





“Mi naona twende tu kituoni. Tunachoshana hapa!”




Vitalis alisema huku akitengenezea shati lake na kuigiza kama mtu afutaye vumbi. Rajesh alimtizama kwa hasira, akajaribu tena kushambulia kwa kupiga sarakasi atue na miguu kichwani mwa Vitalis, ila haraka mikono yake ikatenguliwa na miguu ya Vitalis akadondoka chini!




Vitalis akasonya kisha akaanza kuifuata bunduki yake. Alipoikota na kuiweka kiganjani akasikia mlio mkali wa kioo. Alipotizama, hakumuona tena Rajesh! Haraka akakimbilia dirishani kuchungulia, akamuona Rajesh kwa chini akiyoyoma.





“Shit!”




Vitalis alifoka. Alipepesa pepesa macho yake huku na huko ndani ya ofisi, akaona simu kubwa LG nyeusi akaitwaa na kuiwasha. Ubaya akashindwa kutambua pattern iliyowekwa, ila hakuiacha, aliiweka mfukoni akaondoka zake. Baada ya dakika ishirini akawa yupo nyumbani. Alikutana na Bernadetha ama mama Miraji akamueleza kila jambo alilokumbana nalo huko.




“Kama ilivyokuwa msaada wa Jombi kwa Miraji. Daktari naye aliwasaidia wakina Mtemvu ili wamalizane wenyewe kwa wenyewe bila wao kujua. Nimeona ile tattoo kiunoni mwake, ina maana ni mfuasi wa bwana Kim.”



Alisema Vitalis kwa kujiamini.




“Mmmh … huyu bwana Kim ananitisha kusema ukweli. Inspekta, najua kwako ni vigumu, ila kama waweza naomba uachane naye tupate kuishi maisha yetu tu ya kawaida. Ni kama vile tunapambana na bahari, ni mkubwa mno.”
“Hapana, mama. Siwezi kumuacha. Embu fikiria ni wangapi amewaumiza kwa biashara zake haramu? … Vijana wengi huko mitaani wanakufa kwasababu yake. Nchi yetu i mashakani na dhambini kwa ajili yake. Najua yeye ni goliath ila nasi tutajitahidi tuwe Daudi.”
“Sawa. Nakuombea kila siku Mungu akupe salama. Sitaki kukupoteza, kila unapotoka na kurudi nyumbani salama ni ahueni kwangu.”
“Nashukuru sana kwa kujali. Umekuwa mama yangu wa pili sasa.”




Bernadetha alicheka kidogo akamtizama Vitalis.



“Kujali ni jukumu mojawapo la mwanamke.”




Vitalis akatabasamu na kutizama chini. Kwa muda usiopungua wala kuzidi dakika mbili kukawa kimya. Vitalis alimtizama Bernadetha machoni, naye Berna akafanya vivyo hivyo. Ni kama vile kuna kitu walikuwa wanakiona sisi tusikione. Vitalis alinyanyua mkono wa kuume wa Bernadetha akaushika kama vile anataka uvalisha pete. Aliupeleka mkono huo kinywani akaubusu. Bernadetha akatabasamu.





“Nashukuru kwa yote unayonifanyia.” Vitalis alisema kwa sauti ya chini. Bernadetha hakusema jambo, aliacha macho yake makubwa yaseme kila kitu kwamba anafurahi kusikia vile. Labda ndio kilikuwa kipindi muafaka naye akajihisi mwanamke tangu mumewe afariki.




Kwa muda wakaendelea kutizamana wasione lolote linaloendelea ulimwengu mwingine. Huko nje ya nyumba, Kaguta aliwasili. Alikuwa amewekelea earphone masikioni kichwa chake kikidunda kama kitenesi. Alipopanda kibarazani kabla hajagonga mlango macho yake yaliruka ndani, na humo akamuona Vitalis akiwa na Bernadetha katika mkao ule wa mtizamano. Kaguta akatabasamu, na bila ya kusema lolote akageuza na kunyata taratibu akaondoka eneo lile.






Vitalis aliuteka mkono mwingine wa Bernadetha akaushikilia, sasa mikono yote akawa nayo. Taratibu akapeleka mdomo wake kinywani mwa Bernadetha akambusu mwanamke pap na kuacha kama vile alikuwa anataka kusikilizia mtendwa atasemaje.





Bernadetha akawa kimya zaidi alitabasamu. Vitalis akapeleka tena mdomo wake kwa Bernadetha, Bernadetha akaupokea mdomo wa Vitalis kwa kuufunda. Ila mara wakasikia mlango wa chumbani unafunguliwa, zoezi lao likakomea hapo. Punde Jombi akawa amefika sebuleni na kusalimia.





“Hivi mnajua leo ni siku ya ripoti ya Miraji?”



Jombi aliuliza. Vitalis na Bernadetha wakatizamana. Bernadetha akatabasamu.




“Najua. Naenda huko jioni hii. Acha nikajiandae.” Bernadetha alisema kisha akatoka na kuelekea jikoni akawaacha wanaume wale wawili watete mawili matatu. Vitalis akamueleza Jombi yale yaliyotukia hospitali. Jombi akaonekana kushtushwa na taarifa hizo.
“Bwana Rajesh ni coordinator wa bwana Kim kwa wahindi wote walipo hapa nchini. Kumpata kwake ni mojawapo ya hatua japo ya mbali ya kumpata bwana Kim.”
“Una maanisha nini kusema coordinator wa wahindi.”
“Ni hivi, kila race iliyopo nchini ina coordinator wake, ama tuseme muwakilishi kwa mr Kim. kwa watu weusi, coordinator ni bwana Isaac Makongo. Kwa wahindi ni huyo, Rajesh Deepti. Na kwa wazungu ni bwana Wayne Ford. Si rahisi kuwapata hao watu. Wana viapo vya binafsi.”
“Unaweza ukaniambia nitawapata wapi?”
“Kusema ukweli, sijui. Hawana makazi ya kudumu yanayojulikana. Ni watu wa kuhama hama pia kusafiri huku na kule.”




Inspekta alishusha pumzi ndefu akashika tama. Ni wazi aliona kuna mlima mkubwa mbele yake anaotakiwa kuusogeza. Kazi haikuwa nyepesi hata punje. Alinyanyuka akaaga, akaenda kuoga kisha akashika tanakilishi yake na kuitia modem, akaanza kuperuzi mtandaoni.




Aliandika jina kamili la bwana Kim na kubonyeza kitufe cha kutafuta, paap majibu kadhaa yakaja. Bwana Kim akatambulishwa kama mfanyabiashara mkubwa wa mambo ya mawasiliano kwa kupitia kampuni yake ya Bartel yenye makao yake Barmuda.



Zaidi ya hapo, picha mbalimbali za bwana Kim zikarushwa na hata makampuni ambayo ana ubia nayo, hadi ambazo ameweka hisa zake kwa wingi; makampuni ya vinywaji laini, makampuni ya bidhaa za wanawake, makampuni ya kilimo na kadhalika. Mitandao ikaendelea kumwaga maneno juu ya bwana Kim kuwa ni mfanyabiashara mkubwa na mwenye nguvu katika bara la Afrika na Amerika ya kaskazini.





Inspekta aliporidhika na taarifa alizozipata, akafunga tanakilishi yake na kujilaza kitandani. Alikuja kuamshwa baadae na sauti ya Kaguta. Ilikuwa ni jioni, jua limeanza kupoteza nguvu zake. Inspekta alinyanyuka akaenda sebuleni kukutana na Kaguta ambaye alikuwa amekaa na Jombi kwenye kochi. Wakasalimiana na kujuliana hali, Kaguta akaanza kueleza alichokipata toka kwa Sandra, mpaka kumtambulishwa kwake kwa bwana Isaac Makongo.





Inspekta na Jombi wakashtushwa na taarifa za bwana Makongo, nao huo ukawa mwanya mzuri kwao kuanza kumtafuta mtuhumiwa wao huyo baada ya inspekta naye kueleza ni wapi alipogumana nalo hilo jina.




“Kwa mujibu wa maelezo ya Sandra, Isaac Makongoanaishi kurasini, nyumba namba 898. Picha zake hizi hapa. Anapendelea sana kutizama mpira, na maeneo yake ni Samaki Samaki mbezi beach.” Kaguta alimwaga maelezo huku akiwa kazitandaza picha juu ya meza.
“Basi hatuna tena muda wa kupoteza, nadhani ni muda wa kuanza kufanya kazi. Tupange ni jinsi gani tunaweza kumpata huyu wakala haraka iwezekanavyo.” Inspekta alisihi.
“Kweli, ila inabidi tuwe waangalifu mno. Huyu mtu si wa kawaida.” Jombi naye akasisitiza.
“Kabisa!” Kaguta akadakia na kuendeleza maneno, “Inabidi tuanze pole pole. Kesho kutakuwa na mechi kubwa ya UEFA, najua hatokosa maeneo yake hayo. Alimradi najua sura yake, nitamfuatilia. Niacheni hiyo kazi.”
“Hakuna shida. Ila hakikisha unatupasha kila kinachotukia huko.” Inspekta alisema.
“Nitafanya hivyo.” Kaguta akamtoa hofu.
“Mbali na hayo, kuna baadhi ya taarifa nimezipata toka mtandaoni; makazi ya bwana Kim.” Inspekta alieleza. Jombi akatikisa kichwa chake huku akipunga mkono kama vile mtu anayeaga,
“Hakuna kitu cha ukweli huko. Hakuna mtu anayejua makazi ya bwana Kim hata wafanyakazi wake. Mitandao yenyewe haina data halisi juu ya huyo bwana.”
“Sasa ni wapi tutapata taarifa zake?” Inspekta akauliza.
“Ni kuzitafuta tu. Otherwise hakuna lolote.” Jombi alishauri. Inspekta na Kaguta wakawa kama wamekamatwa na kabutwaa.
“Kwanza, hakuna aneyejua sura halisi ya bwana Kim. Sura ambazo zimewekwa mitandaoni si za kwake, ni bandia na za kutengenezwa. Ni watu wachache mno wanaomjua the real Kim, watu wake wa karibu mno, kama vile familia yake.”
“Sasa hata hiyo familia yake tutaikotea wapi?” Kaguta aliuliza.
“Hapo ndipo kwenye shida. Kama nilivyosema mwanzo. Hakuna mtu anayejua haswa maelezo ya karibu ya bwana Kim. Ni kazi ya kutafuta hayo.”
“Hakuna linaloshindikana. We shall do it.” Inspekta Vitalis alisema kwa kujiamini. Kaguta akatikisa kichwa kumuunga mkono.
Baada ya muda mfupi, simu ya inspekta ikaita. Alipigiwa na Bernadetha, alipokea akaweka simu sikioni;
“Hallo … Hospital? … Haya sawa, nitakuwa hapo muda si mrefu.”



Simu ilipokata akawatonya wenzake;




“Miraji ameruhusiwa kutoka. Inabidi niende nikamtoe, si unajua tena mambo ya utaratibu.”
“Twende!” Kaguta akatamka.
“Na mimi naomba niende.” Jombi naye akatia neno. Wakajiandaa na kujipakia kwenye gari, wakaelekea hospitali na kurudi na Bernadetha pamoja na Miraji. Miraji alionekana kuchoka. Macho yake yalikuwa yanafunguka na kufunga. Ni kama vile alikuwa amelemewa na usingizi mzito.
“Daktari amesema anahitaji mapumziko. Asifanye kazi yoyote ngumu kwa sasa zaidi ya mazoezi madogo madogo.” Bernadetha alilonga.




Jombi akishirikiana na inspekta Vitalis wakamshusha Miraji na kumpeleka moja kwa moja kitandani kwenye chumba alalacho Jombi.




“Mungu mkubwa. Sikujua kama kuna siku mwanangu atatoka hospitali.” Bernadetha alisema kwa tabasamu.
“Atapona tu, na atarudi katika hali yake.” Inspekta akamtia moyo mwanamama.

*****

☆Steve
 
***SURA YA ISHIRINI NA MOJA***





(MSIMU WA 02)





Wakati saa ya ukutani inatamka ni saa moja kasoro tano tu, Inspekta Vitalis alikuwa tayari yupo sebuleni akiwa kavaa shati la kitenge na suruali nyeusi ya kitambaa.




Ilipohitimu tu saa moja kamili, Marietta akatoka chumbani akiwa kavalia sare za shule akaenda kukutana na inspekta sebuleni. Punde, mama mtu, Bernadeta, naye akatoka akiwa kajitanda khanga. Walisalimiana na inspekta kisha wakaagana.




“Leo una ratiba gani, baba?” Bernadetha aliuliza na uso mkarimu.
“Nampeleka mwanangu shule.” Inspekta akajibu na tabasamu kisha akamtizama Marietta.
“Baada ya hapo?”
“Baada ya hapo, narudi nyumbani.”
“Mmmh … Unaniongopea.”



Inspekta alitabasamu kisha akambeba Marietta.




“Kuna sehemu hivi nitapita. Kuna kakazi kadogo nataka kukamalizia.”
“Utarudi saa ngapi?”
“Mapema tu. Nitampitia na mtoto.”
“Haya sawa. Kazi njema.”
“Ahsante. Kwaheri!”




Inspekta alifungua mlango akatoka nje na Marietta aliyemshusha chini wakawa wanatembea. Mpaka wanapotelea, Bernadetha alikuwa ameshika mlango akiwatazama kwa macho yaliyojaa tenzi ya furaha. Taratibu chozi likamshuka. Akalifuta huku akitabasamu. Alifunga mlango akarudi ndani na kuanza kufanya kazi za hapa na pale; kuosha vyombo, kufagia, kudeki na kuandaa chai.





Wakati saa ya ukutani ikitamka ni saa tano kamili, inspekta alikuwa yupo kituo kikubwa cha polisi ofisini kwake, akiwa anaandika maelezo kwenye faili moja lililobebelea maandishi makubwa yasomekayo; MTEMVU’S CASE kwa rangi nyekundu. Pembeni ya meza yake, kulikuwa na kikombe cheupe kilichobebelea kahawa nyeusi ifukayo moshi. Mara kwa mara wakati anaandika, akawa anapeleka kikombe kile cha kahawa mkononi na kuria mafundo kadha wa kadha.





Alipomaliza kuandika. Alivuta tanakilishi iliyokuwepo mezani kwake akaandika jina la Isaac Makongo na kuanza kuperuzi. Majibu yakaja na picha pia kwamba ni mfanya biashara mkubwa asafirishaye nyama za kusindika nchi za nje, lakini pia ni mchezaji mpira mkongwe aliyewahi kuiwakilisha nchi vizuri kimataifa kwa kuchezea klabu kubwa duniani ya Ajax ya uholanzi na Marseille ya ufaransa.




Wakati inspekta Vitalis akiendelea kuperuzi, kwa kupitia dirisha la ofisi yake tunamuona mwanaume mmoja mwenye mwili mnene akitoka kwenye ofisi ilyopachikwa kibandiko kilichosomeka; OCD. Mwanaume huyo alipoufunga mlango sauti ikazalishwa na kufika masikioni mwa inspekta Vitalis ambaye aliacha kidogo kutazama skrini ya tanakilishi yake na kurusha macho huko.





La haula! Akamuona mtu anayemperuzi; bwana Isaac Makongo. Inspekta hakuamini, alitizama picha za kwenye mtandao kisha akarudisha tena uso wake kwa mtuhumiwa wake, bahati mbaya hakumuona tena, alikuwa ashapotea eneo la mlangoni mwa OCD. Inspekta akanyanyuka haraka akatoka ofisini kwake na kuelekea nje, huko akakuta gari moja aina ya Suzuki vitara nyeusi yaondoka.




Inspekta alipepesa macho yake huku na huko akaona pikipiki ya polisi. Alirudi ofisini haraka akakwapua ufunguo kwa mwenzake akapanda pikipiki na kuanza kufuatilia gari lile Suzuki Vitara kwa nyuma taratibu.




Baada ya mwendo wa dakika kumi, Suzuki ikapaki hoteli moja kubwa. Isaac akashuka na kuingia ndani. Inspekta naye akafanya hivyo, akapaki pikipiki yake na kuingia ndani. Bahati mbaya hakumuona tena bwana Isaac. Alitumia kitambulisho chake cha polisi kupita kila eneo lakini hakufanikiwa. Isaac hakuwepo kabisa kila eneo.






Inspekta alitoka ndani ya hoteli na kwenda nje kwa mlengo wa kumngoja mlengwa wake atoke. Ajabu, hata gari la mtuhumiwa wake hakulikuta. Alimwendea mlinzi akamuuliza. Mlinzi akamuambia hilo gari limetoka muda mrefu tu. Inspekta akashika kiuno huku akitoa macho yake kama ndubwi. Alimezwa na butwaa. Hakuelewa kilichojiri. Alipanda pikipiki akarudi kituoni akaenda kuonana na OCD.





“Samahani, mkuu. Kuna mwanaume ametoka ndani ya ofisi yako muda si mrefu, amevalia suti na miwani ya macho. Naweza nikamjua ni nani?”
OCD alishusha miwani yake akamtizama inspekta.
“Kwani kuna tatizo, inspekta?”
“Hamna, nahisi nimemfananisha hivi …”
“Na nani? Ulimuonea wapi?”
“Aaahm … Ni kwanba kuna kesi fulani hivi naifuatilia. Na kuna mtu mithili yake ndio mana nikauliza.”



OCD alikunja sura yake kidogo akalaza mgongo wake kwenye kiti chake kirefu na kumtizama Vitalis kwa sekunde kadhaa kisha akafungua mdomo;
“Anaitwa Isaac Makongo, ni mfanyabiashara.”
“Hakuna kingine unakijua zaidi ya hapo?”
“Hapana. Wewe je?”
“Hamna.” Inspekta alijibu kisha akanyanyuka. “Nashukuru, mkuu. Naomba niende.” Inspekta alisema kisha akajigeuza kuufuata mlango. Aliposhika kitasa, OCD akamuita. Inspekta akageuka.
“Naomba ulete hapa hilo faili la kesi ya Isaac.”
“Unasema?”
“Hiyo ni amri. Lete hapa hilo faili la kesi ya Isaac, upesi!” Uso wa OCD uligeuka na kuwa wa mbogo. Inspekta akashangazwa na hiyo hali.
“Unasubiri nini? Kalete!”




Inspekta aliendea ofisi yake akapekua na kumletea OCD faili jingine. OCD akalipokea na kuliweka juu ya meza yake.




“Kesi hii imeshafungwa. Rasmi.” OCD alisema huku akimtizama inspekta Vitalis. Inspekta hakusema jambo, alitoka akarudi ofisini kwake akiwa na sura ya mawazo. Alishika tama akiwa amewekea ndita. Kwa muda kama wa dakika kumi na tano akawa anaatafakari. Mwishowe alizima kila kitu akatoka ofisini.




****

☆Steve
 
***SURA YA ISHIRINI NA MBILI***




(MSIMU WA 02)







Ndani ya usiku wa saa nne maeneo ya Samaki Samaki Mbezi beach makonde, Kaguta alikuwa yumo hapo akiwa amekaa kwenye kiti kirefu mbali kidogo na runinga kubwa. Watu walikuwa pomoni wakiwa wameshikilia vinywaji vyao walivyokuwa wanavipeleka vinywani huku macho yao yakipewa ajira ya kutizama kioo kikubwa kilichokuwa kinaonyesha mechi ya nusu fainali ya kombe la UEFA kati ya Juventus na Altetico Madrid.





Macho ya Kaguta yalikuwa yanatizama huku na kule kumtafuta bwana Isaac Makongo. Hakuwepo katika lile eneo, ila baada ya dakika kadhaa akafika akiwa katika mwendo mkali. Tukio lake la kwanza kulifanya ilikuwa ni kutizama dakika ngapi za mpira zimempita kisha akaagizia kinywaji na kuketi vizuri aufaidi mchezo.





Kwa dakika kama tano, Kaguta akamsoma bwana Isaac Makongo anashaingilia timu gani. Alipogundua hilo, taratibu akajisogeza karibu na mlengwa wake akaanza na yeye kushangilia kwa pupa timu ile ile anayoishangilia bwana Isaac.




“Funga haoo mbwa! Leo Juventus wataisoma nambaa!” Yalikuwa maneno ya Kaguta. Aliendelea kushangilia na kushangilia. Taratibu Isaac akaanza kumuongelesha.
“Umeona pale … Daah yani asingemkata angefunga! Alafu refa kanyamaza. Fala kweli!” Isaac alitupa lawama.
“Kweli. Hawa wanabebwa!” Kaguta akaunga mkono hoja.





Mchezo ukaendelea. Bwana Isaac akijua kapata mshabiki mwenzake aliyekuwa anamshirikisha mara kwa mara kwenye kila tukio linalotokea uwanjani. Ulipofika muda wa mapumziko, Isaac alitoka akafuata gari lake. Kaguta akamuita mhudumu;




“Mambo?”
“Poa!”
“Naweza nikapata grants ndogo?”
“Ndio!”
“Naomba basi.”



Mhudumu alienda akarudi na alichotumwa.




“Ahsante. Mbona unaonekana umechoka mpendwa?”




Mhudumu alitabasamu pasipo kutia neno.




“Naitwa Erick, mwenzangu unaitwa nani?”
“Naitwa Salome.”
“Wow! Una jina la mama yangu!”
“Kweli?”
“Ndio. Pole mama kwa kazi.”
“Ahsante.”
“Sasa unaonaje ukapata na wewe moja mbili tatu? … Siwezi nikakaa hapa nakunywa wakati mama yangu amejikunyata tu.”
“Ahsante. Nashukuru.” Salome alisema kwa tabasamu nene.
“Naomba basi uniletee na maji ya kunywa.” Kaguta aliagiza tena. Mhudumu akashika njia kwenda kufuata maji, Kaguta akamsindikiza kwa macho yaliyokita maeneo ya kiunoni na makalioni.
“Mungu wetu mkubwa jamani, khaa! Wote huo wa kwake?” Kaguta alijisemesha na kutabasamu mwenyewe kisha akajilamba kama vile mtu aliyetoka kula chakula kitamu. Muhudumu aliporudi, akamtaka wakae pamoja.
“Niko bored hapa kwa kweli. Naomba basi kampani, mama yangu.”
‘Tatizo boss. Akiniona nimekaa atakasirika.”
“Usijali, nitaongea naye.”




Salome akaketi pembeni ya Kaguta na kuagiza kinywaji aina ya savanna. Wakawa wanapiga soga za hapa na pale na Kaguta ambaye kwa muda alisahau kama mechi inaendelea na mlengwa wake amesharudi.





“Yani wewe bwana unan’chekesha kweli!” Salome alisema huku akicheka kwanguvu.
“Kweli nakuambia. Mie dada yangu alikuja kuomba kazi hapa wakamkatalia katakata kwa kuwa si mzuri. Miguu imeelekea kusi-kaskazi!”
“Mmmh labda kama kuna vigezo vingine, si hiko. Mbona tuliokuwepo hapa ni kawaida tu.”
“Wa kawaida? … Nani kasema? Yani hapa natamani nikuagiza tena nikuone tu unavyotembea.”




Salome akaangua kicheko.




“Wapi bwana. Kawaida tu!”
“Agiza! … Agiza! Mbona umemaliza alafu upo kimya, mama?”




Salome akaagiza tena Savanna nyingine. Taratibu zikaanza kumuingia kichwani. Kaguta naye akazidisha maneno kumsifia mwanamke kama vile anaoga na mafuta ya nazi ananawia uso maziwa fresh. Mwanamke akaanza kurembua na kurembua. Cheko mia nane.




Kaguta alipokuja kushtuka, bwana Isaac Makongo hakuwepo. Watu ndio walikuwa wanatawanyika mechi imekwisha. Kaguta akanyanyuka na kwenda kutizama parking, loh! Hata gari la Isaac halikuwepo. Alijilaumu kwa kutukana matusi mbalimbali. Aliamua kurudi ndani na kuendelea na Salome ambaye alimng’ang’ania mpaka wakaondoka wote kama fidio la siku yake aliyoipoteza kizembe.





Siku iliyofuata akakutana na wenzake; Vitalis na Jombi akawaeleza kilichotokea. Naye Inspekta Vitalis akaeleza ilivyotokea baada ya kumuona bwana Isaac Makongo kituoni, wakashangazwa na mfanano wa matukio hayo.





Hapo ndipo Kaguta akakumbuka kauli ya Sandra … “Hakuna chochote mtakachofanikiwa mkiwa na hizo chapa. Kila mnalopanga mtatanguliwa hatua tatu mbele.” Kabla Kaguta hajawaambia wenzake chochote, simu ya inspekta Vitalis ikatetema. Ujumbe uliingia ukitokea namba mpya. Vitalis aliufungua akausoma;




“Acheni kupoteza muda wenu, ndugu zangu. Nadhani sasa ni wasaa wa kujenga taifa letu.”



Aliwaonyeshea wenzake huo ujumbe, wote wakawa wanajiuliza swali la nani kautuma ujumbe ule na ulikuwa una maana gani. Punde, sauti ya Miraji ikasikika toka chumbani;
“Sitaki! Sitaki nasema!”




Ghafla Miraji akaja sebuleni akiwa anapepesuka na mama yake anajitahidi kumsimamisha. Aliwatizama inspekta na Kaguta kwa ghadhabu akaropoka;




“Siwezi nikaishi na hawa mbwa! Nataka kwenda kwetu, sasa hivi!” Macho yake yalikuwa yanavuja machozi na uso wake ulikuwa umefungamana na hasira. Hakusubiri hata jibu, akaanza kuufuata mlango na mwendo wake wa kusuasua. Mama alimshika mkono, Miraji akautoa na kumsukuma mama mbali kisha akaendelea kuufuata mlango. Aliposhika tu kitasa, akadondoka chini kama mzigo puuh!




“Mungu wangu mtoto wangu!” Bernadetha alilalama huku akiweka mikono yake kichwani. Vitalis alimbeba Miraji akamuweka kwenye gari wamuwaishe hospitali. Kaguta akashika usukani, Jombi akaachwa atizame nyumba.




Hazikupita dakika kumi, Kaguta akaingiza gari hospitalini. Vitalis alimbeba Miraji wakamuingiza mpaka ndani wakapokelewa na kitoroli cha wagonjwa kikambeba Miraji mpaka chumba ambacho Miraji aliingia, wengine wakazuiwa.




“Ngojeni hapa.” Dokta alisema kisha akaenda ndani kumuhudumia mgonjwa. Inspekta, Kaguta na Bernadetha wakaketi kwenye benchi kungoja majibu. Uso wa Bernadetha ulieleza hofu, machozi yalikuwa yanamtiririka, alilaza kichwa chake kwenye mkono wa inspekta, inspekta akamfuta machozi na kiganja chake akimtaka aache kulia.
“Nilijua amepona sasa. Sikutegemea kama atarudi tena hospitali mapema hivi.” Bernadetha alisema kwa sauti nyong’onyevu.
“Usihofu. Atapona na tutaondoka naye.” Inspekta Vitalis alisema kwa kujiamini. Kaguta naye alimwaga tabasamu kuonyesha matumaini.




Baada ya muda wa dakika ishirini, daktari akaja kutoa majibu.




“Uti wake wa mgongo bado haujatengemaa, kusimama na kutembea kunakuwa shida, lakini pia hata fahamu zake zinakuwa na kasoro ndogo ndogo mara zingine. Ila yupo sawa, na mnaweza mkaondoka naye. Hakikisheni apate mapumziko zaidi na mazoezi ili kurudufu afya yake kwa haraka.”




Baada ya hapo, Miraji akachukuliwa na kurudishwa kwenye gari. Gari lilipowashwa Miraji akamwambia mamaye;



“Nipeleke nyumbani. Sitaki kwenda na hawa watu.”





Mama hakuzozana, akamtaka tu waende kwa inspekta ili wamchukue Marietta alafu waende nyumbani.Miraji akakubali. Marietta alienda kuchukuliwa kisha gari likaelekea nyumbani kwa wakina Miraji. Walipofika, inspekta alitaka kumsaidia Miraji kutembea, Miraji akakataa. Hakutaka ashikwe na yeyote isipokuwa mama yake.




“Nitakuona lini tena, anko?” Marietta alimuuliza inspekta. Inspekta akatabasamu na kuchuchumaa wakawa sawa kimo.
“Utaniona mara nyingi tu, umesikia?”
“Ndio.”
“Haya, usiku mwema eenh …”




Maerietta alitabasamu akaenda ndani, akamuacha mama yake na inspekta Vitalis wamesimama karibia na mlango.




“Samahani kwa yote yaliyotokea, Vitalis.” Bernadetha alisema huku akimtizama inspekta Vitalis machoni. Inspekta alitabasamu kama vile hakuna lolote liendealo, akamkumbatia Bernadetha na kumnong’oneza;
“Usijali, nipo sawa. Naelewa.”
Bernadetha alimkumbatia inspekta Vitalis kwanguvu akamwambia;
“Nitakumiss sana. Naomba uwe unakuja kun’tembelea.”
“Nitakuja. Kamwe usitie shaka juu ya hilo.”




Baada ya hayo maongezi, inspekta Vitalis na Kaguta wakaaga. Walimuacha Bernadetha pale pale mlangoni machozi yakimtoka. Baada ya gari kutokomea, ndipo Bernadetha akaingia ndani.





“Sasa itakuaje, Vitalis?” Kaguta aliuliza.
“Kuhusu nini?”
“Mama Miraji.”
“Sijui. Nilikuwa tayari nimeshamzoea.”
“Usihofu. Yule mtoto ana kimuhe muhe. Akitulia atajua jinsi maisha yanavyokwenda.”
“Natumai itakuwa hivyo.”




Inspekta hakusema tena neno lingine mpaka anafika nyumbani kwake. Yeye na Kaguta walishuka wakaingia ndani, wakaendeleza kikao chao pamoja na Jombi.





“Kuna jambo moja alipata kunambia Sandra juu ya hizi chapa. Alinambia hakuna kitu tutakachofanya kikafanikiwa tukiwa nazo. Kila tutakachopanga tutanguliwa hatua tatu mbele.” Kaguta alimwaga maneno.
“Tutatanguliwa na nani?” Inspekta Vitalis aliuliza.
“Hakuna mwingine, ni jitu la kuangamiza.”



Inspekta alitulia macho yake yakionyesha anatafakari, baada ya sekunde nne akalipuka na hoja;
“Kumbee! Ina mana hata kule kisiwani ilikuwa ni vivyo hivyo, sio?”
“Ndio!” Kaguta akajibu.
“Sasa tunafanyeje?” Inspekta aliuliza. Wote wakamtizama Jombi kama vile ndiye aliyekuwa na majibu.
“Sijui cha kufanya!” Jombi alijipambanua. “Ni vyema sasa tumegundua kumbe twakimbiza kivuli.”
“Kuna haja ya kuondoa haya matattoo!” Inspekta alisema kwa uso mkakamavu.
“Tutaondoaje sasa?” Kaguta na Jombi wakauliza.
“I must figure the way out of this! … Lazima nitapata njia.”
“Haya. Utakapopata, usisite kutujulisha na sisi.” Kaguta alisihi, kikao kikafungwa wakaenda kulala.



Asubuhi na mapema, inspekta Vitalis aliamka na kwenda kazini. Alipofika alifungua droo yake akatoa faili lililoandikwa MTEMVU’S CASE kwa wino mwekundu, akalifungua na kulitizama kwa dakika kadhaa akitizama picha za matukio mbali mbali.





Aliliweka faili juu ya meza, akawasha tanakilishi yake na kwenda moja kwa moja kwenye faili ya kesi ya Mtemvu, akafungua na kuanza kuongezea baadhi ya taarifa mpya. Wakati anafanya hivyo, dirisha lake linalotizamana na la OCD likamteka akili.





Alimuona OCD anaongea na simu huku akiwa ameshikilia mkononi lile faili alilompatia kwa kulaghai ndimo lina kesi ya bwana Isaac Makongo. Baada ya OCD kumaliza kuongea na simu, aliliweka lile faili kwenye mkoba wake na kuanza kupanga panga makabrasha mezani. Wakati wote huo, inspekta akawa anatizama kwa umakini.




Masaa yalipita, inspekta akaendelea na kazi zake na mara moja moja kwa kuibia ibia akawa anatizama dirisha la mkuu wake. Alimaliza kazi yake ila hakutaka kuondoka. Alitulia kwenye kiti chake akawa anamtizama OCD kila anachokifanya. Ilipofikia mida ya saa nane za mchana, OCD akafungua ofisi yake na kutoka mkononi akiwa kabebelea ule mkoba aliloweka faili. Inspekta Vitalis naye alitoka ofisini kwake, taratibu akawa anamfuatilia OCD kwa nyuma.





OCD alipanda gari lake, akaondoka kituoni. Inspekta Vitalis alichukua pikipiki ndogo ya polisi akawa anamfuatilia OCD kwa mbali. Gari la OCD lilisimama eneo moja la kiwanja, baada ya muda mfupi likaja gari lingine, Suzuki Vitara nyeusi, na kupaki karibu na gari la OCD, OCD akafungua mlango wa gari lake akatoka na ule mkoba akaingia ndani ya gari lililokuja. Ilichukua dakika kumi OCD kurudi kwenye gari lake na kuondoka, nalo Suzuki Vitara liliwashwa na kuondoka. Inspekta Vitalis akaanza kulifuatilia Suzuki Vitara kwa mbali.



******

☆Steve
 
nawaza kwa sauti umri wa inspector na mama miraji.....

ni watu wazima nahisi lkn hamu hainaga mwenyewe

Kitu cha ukweli hicho mkuu nakupa big up sana

Hadithi Kali kwelkwel

Mkuu SteveMollel hongera kwa kazi nzuri nilianza kuipitia hii kitu "BARADHULI MWENYE MIKONO YA CHUMA" jana mida ya saa 3 usiku yaan kila nilipomaliza sehemu moja ndipo nilizidi kushawishika kuendelea na sehemu iliyofuata mpaka saa 9 usiku ndipo nikamaliza na kulala
*Mtiririko wa matukio ukopoa
Ila matukio ya mauaji na uchawi wa kutisha i real enjoy it!
*Wahusika umewachora vizuri but huyu Jombi rafiki wa Miraji ilikuwaje asifunguliwe mashtaka dhidi ya mauaji aliyoyafanya
*Pia hongera kuhusu mauzauza ya kile kisiwa cha Bagamoyo inasemekani si pahala pa mchezomchezo
Aysee endelea kutupia mzigo mkuu

Hatari mkuu
Haya nshafika.


☆Steve
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom