***SURA YA ISHIRINI NA TANO***
(MSIMU WA 02)
“Sijajua mpaka sasa. Kuna jambo lipo nyuma ya pazia.”
“Na inatulazimu kuling’amua. Pia umeona namba 898?”
“Nimeiona.”
“Itakuwa ina maanisha nini?”
“Sijajua. Ila si unajua nyumba ya bwana Isaac Makongo ina namba 898?”
“Ndio. Kuna kitu pia katika hiyo namba.”
Baada ya dakika ishirini na tano wakawa tayari wameshawasili jiji la Dar es salaam. Bakari alishushwa wakina inspekta wakaelekea mpaka nyumbani kwa Bernadetha.
“Karibuni!” Bernadetha aliwakaribisha kwa tabasamu pana.
“Ahsante!”
Waliketi kwenye viti inspekta Vitalis akamueleza Bernadetha yaliyotokea. Zaidi inspekta Vitalis akamtaka Bernadetha ahamie kwake kwa usalama. Jambo hilo likawa gumu.
“Mwanangu Miraji hataki kabisa hata uongelewe humu ndani. Inakuwa ugomvi kabisa, sembuse kuja kukaa kwako.”
“Mueleze hali halisi. Muambie mpo hatarini.”
“Sidhani kama itaweka mabadiliko yoyote. Anawahesabu nyie kama wauaji wa baba yake, hapo ndipo ugumu unakuja. Ila nitajitahidi sana kumueleza.”
“Sawa. Itakuwa vyema.”
“Vipi Kaguta, mbona mkono wako una bandeji?”
Kaguta akaeleza yaliyotukia. Bernadetha akachukua wasaa wake kumpa huduma ya kwanza kama ile aliyompa inspekta Vitalis kisha akamtaka Kaguta asifunge hilo jeraha. Baada ya hapo, wakina inspekta waliaga. Bernadetha aliwatoa mpaka nje, akamkumbatia inspekta Vitalis na kumbusu shavuni.
“Utakapohisi tatizo, nipigie immediately. Na usisahau kumsalimia Marietta akirudi.” Inspekta Vitalis alimwambia Bernadetha. Bernadetha akatikisa kichwa kukubali alichoambiwa. Mpaka wanaume wanatokomea na gari lao, Bernadetha akawa yu kibarazani anawatizama. Chozi lilimshuka akalipangusa na kiganja chake.
Alitizama chini akajigeuza na kurudi ndani. Kumbe wakati yupo hapo kibarazani Miraji alikuwa anamchungulia dirishani. Baada ya mama kuingia ndani, Miraji alifunga dirisha lake akajilaza kitandani akarusha macho yake darini kama mtu anayewaza jambo.
Katikati ya mida ya saa mbili za usiku, Bernadetha alikuwa na wanawe: Marietta na Miraji wakiwa wanapata chakula kwa pamoja. Kulikuwa ni kimya kati yao kwa muda wa dakika kadhaa, vijiko tu na sahani ndivyo vilikuwa vinapiga makelele. Miraji alimtizama mama yake, akamtizama na mdogo wake, Marietta, kisha akaamua kuufungua mdomo kwa kuuliza:
“Mama, mbona siku hizi hauna raha?”
Bernadetha alimtizama Miraji akatabasamu kiuongo.
“Kwanini unasema hivyo mwanangu? … Nipo sawa tu.”
“Hapana. Mara kwa mara nimekuwa nikikuona unaketi nje peke yako, unadondosha chozi. Umekuwa ni mtu wa kuketi kiupweke. Umekuwa ukichelewa kulala na hata mara nyingine kulala sebuleni. Nini tatizo, mama?”
Bernadetha aliyafichama yote yaliyosemwa na Miraji kwa tabasamu pana lililojaza uso wake. Akasema:
“Mwanangu, hakuna lolote. Labda kwa kuwa hujaniona kwa muda.”
“Mama, kwani uncle Vitalis amesema anakuja lini?” Marietta aliingilia kwa kuuliza.
“Atakuja tu.”
“Lini? Mi nimemkumbuka. Basi twende kwake.”
Marietta alizidi kusisitiza. Bernadetha akamtizama Miraji kwa jicho la tahadhari, Miraji hakusema jambo, aliendelea tu kula kama mtu ambaye hajasikia lolote.
‘Tutaenda tu, usihofu mwanangu.” Bernadetha alimwambia Marietta, Marietta akatabasamu na kuendelea kula. Miraji alipomaliza alinyanyuka akaondoka zake kwenda chumbani.
Baada ya muda mfupi, Marietta naye alinyanyuka akaenda kuoga na kulala, alibakia Bernadetha peke yake sebuleni akiwa anatizama runinga. Mara simu yake ya mkononi iliita na kutetemeka, akainyakua toka mezani na kuitizama, akaona ujumbe toka kwa inspekta.
“Helo … Umelala?”
Bernadetha akatabasamu na kubonyeza vitufe vya simu kujibu.
“Hapana, nipo tu natizama televisheni.”
“Upo salama?”
“Am ok. Wewe?”
“Nipo salama. Jus missin yu.”
Bernadetha alitabasamu tena, kisha akajibu:
“Me too.”
“Unakuja lini kuniona?”
“Nadhani wknd hii. Marietta pia anataka kukuona.”
“Nimemmis sana. Karibuni.”
“Ahsante. Mkono wako unaendeleaje?”
“Naendelea vyema tu. Upo na nani hapo?”
“Mwenyewe. Wewe je?”
“Nipo mwenyewe pia.”
“Wapi?”
“Chumbani. Naona nyumba imekuwa kubwa mno. Nakumiss kweli.”
“Sana?”
Marietta alituma ujumbe huku aking’ata lips zake. Bahati mbaya hakujibiwa. Alikaa dakika kama tano bila ya majibu. Simu ilikuwa imekata mtandao. Alitoka nje akanyanyua mkono wake kutafuta mtandao bila ya mafanikio.
Hata pale mtandao uliporudi hakuona ujumbe mwingine, alienda chumbani kwake akalala ila kila muda akawa anahisi sauti ya ujumbe kuingia ila alipotizama hakuona kitu, mwishowe usingizi ulimpitia akajikuta asubuhi simu yake ikiwa imejaa jumbe nyingi toka kwa inspekta Vitalis. Akatabasamu na kuanza kuzijibu kabla ya kufanya kitu kingine chochote.
****
☆Steve