Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,997
" border="0">
Sijui ni kitu gani kinaendelea; hatushindanishi hoja tena, hatupingani kwa hoja tunaanza kushindanisha umati. Kwamba ni mwanasiasa gani anapata watu wengi na ni mwanasiasa gani hapati watu wengi kwenye mikutano yake. Kwamba kwa kuangalia umati wa watu kwenye mikutano tunaamua ni yupi anakubalika na yupi hakubaliki na hivyo tunachagua nani wa kumfuata na nani wa kutomfuata?
Fikiria habari inaletwa kuwa kuna mkutano wa CHADEMA mahali ambao utahutubiwa na viongozi fulani. Kwa haraka watu wanataka "waone picha". Utasikia mtu anakimbia na kusema "nitawaletea picha hivi punde". Na kweli watu wanasubiria kuona picha "za mkutano" zilivyo na watu nyomi. Sasa kwa vile mkutano unaweza kuwa na watu wengi kweli basi baadhi ya watu wanajisikia furaha kuwa CDM imepata watu wengi.
Upande mwingine nao ni vile vile. Kiongozi wa CCM anaenda kufanya mkutano au kundi la viongozi wanaenda kufanya mkutano na wao wanafanya haraka kuleta picha. Na kama taarifa za kuwa watu wanakusanywa na mabasi nazo ni kweli basi na CCM nao wanataka kuwa na 'watu wengi' kwenye mikutano yao. Hivyo, picha itafanyiwa haraka kuonesha kuwa "hata" kwenye mikutano ya CCM watu wengi wanakusanyika.
Na katika sehemu zote mbili picha haziwezi kunoga bila watu (mamia au maelfu) kuvaa nguo za rangi za chama. Na kwa hivi tunaamua ni hali gani ya kisiasa iliyopo. Na pamoja na rangi sasa wapiga picha wetu (ambao wengi nao wana maslahi na vyama husika) hawapigi picha za kuonesha upande mbaya kwani wote watatafuta sehemu ambapo watapiga picha kuonesha umati. Na tunapoona umati kuna kitu kinatufanya tujisikie vizuri kuwa kwa kweli mambo siyo mabaya; tunashindanisha umati.
Lakini jingine ambalo nalo nimeliona na linaendelea kuonekana ni kuwa tunashindanisha nani anazungumza vizuri na kwa ukali wa maneno au kwa mwamko na jazba ya kutufanya tuamini kuwa ni mzungumzaji mzuri. Hivi majuzi kijana mmoja aliniuliza kuhusu kiongozi mmoja wa chama cha upinzani na kuniambia "anajua kujenga hoja" na kuwa "ni mzungumzaji mzuri". Nilimuuliza kijana huyo kijana juu ya hoja zinazotolewa na kiongozi huyo na kijana akashindwa kuelezea isipokuwa kuzirudia hoja zilivyo. Nilipoanza kuonesha fallacy za hoja hizo kijana wa watu akaona kama najaribu kumtusi huyo kiongozi!
Tunawaangalia wanasiasa wetu na kuwasikiliza wanavyozungumza majukwaani na kufurahia jinsi wanavyozungumza kwa ukali, kwa mbwembwe na kwa kuonesha wana uchungu sana. Sasa hili linanoga zaidi kama linafanyika kwenye umati mkubwa basi sauti, mbwembwe na mwamko wa umati unatufanya tulinganishe vyama hivyo hivyo. Sasa utaona CCM na wenyewe wakisimama majukwaani wanazungumza kwa ukali na kwa mbwembwe huku wakishangiliwa - wengi tunakumbuka Mr. Kudadadeki!
Sasa hakuna ubaya kuwa na umati wa watu na wala hakuna ubaya wa watu kuzungumza kwa mbwembwe na kwa jazba. Lakini kuna tatizo kama hatujui kusikiliza hoja zinazotolewa na kushindanishana kwa hoja, kwa sera, kwa mitazamo na kwa maono. Kuna faida gani watu kubishana nani amezaa na nani au nani ni fisadi kama hatusikii tofauti ya sera, mitazamo, maono na mwelekeo wa vyama vyetu vya siasa.
Binafsi ningependa kusikia CCM ikitetea sera zake na mafanikio yake na kueleza kwanini sera zake ziendelee kutumika nchini. Lakini kwa vile ninaamini sera hizo zimeshindwa kuliongoza taifa letu ningependa kusikia zaidi CDM wakizikosoa sera hizo na kutueleza wao wangefanya nini tofauti. CDM haipaswi kutuambia nyumba iliyojengwa na CCM ni mbovu na kuwa mafundi waliotumika ni wabovu na kuwa haiwezi kuhimili mafuriko au matetemeko. Watu wanachotaka kusikia ni kuwa wao wakiibomoa hiyo nyumba watajenga nyumba ya aina gani ambayo itakuwa tofauti na ile ya CCM?
Na sisi wananchi, wanachama na mashabiki wa vyama vyetu tuanze kukataa kuambiwa stori za kusemezana na kurushiana vijembe; tudai hoja. Tudai kusikia mwelekeo mpya wa taifa letu; tuulize "wanafanya nini" ama "watafanya nini". Kwa CCM ni rahisi kwani wao wanahitai kuulizwa "kwanini hawajafanya x,y" kwa sababu wao wako madarakani. wanatakiwa wajibu - siyo wasema "mbona". CDM wasiachwe waendelee kusema "waone wanafanya x,y" tunataka wao nao wasema watafanya nini? Watuambie ubaya wa sera za CCM na matokeo yake na uzuri wa sera zao.
Lakini tusipoanza kudai haya na kuyaoana haya tutaendelea kuletewa picha, tutashangilia na kufurahia na kujisikia vizuri. Na kwa kadiri inavyoonekana picha zitazidi kuletwa za kila aina huku watu wakibishana ni yupi ana picha nzuri. Silly Politics. Picha zitufanye tuhoji 'walisema nini"? "Je kilichosemwa kina ukweli"? "Je kilichosemwa kina makosa gani?". Picha ziwe alama za kutuelekeza kwenye maswali ya hoja na tupate majibu. Sasa watu wanatuwekea picha mtu akivikwa mgololo au amekaa mezani halafu haisemwi kimezungumzwa nini wanafikiria watu watahisi kwa kutumia njia ya mnunurisho kujua kilichosemwa.
Tusiridhike na picha, turidhishwa na hoja.
Hoja zijibiwe kwa hoja.