Leo hii sijui hii nchi inaendeshwa na consensus ya nani tena.
Mzee Mwanakijiji! heshima mbele mkubwa wangu. Bado nchi yetu inaendeshwa kwa amri kutoka Washington. Umesahau malengo ya milenia na uchafu mwingine? si sera tu, kibaya zaidi, hata baadhi ya sheria zinazoendesha nchi zinatungwa kwa msukumo kutoka nje, na wananchi wanalazimishwa kuzikubali na kuzitii.
Si unakumbuka 2006/2007 Serikali ya Denmark kupitia kwa balozi wake Carsten Pedersen, ilisitisha msaada wa zaidi ya shilingi bilioni 3.16 kwa serikali ya Tanzania mpaka hapo serikali ya Tanzania ingepeleka Muswada wa rushwa Bungeni. Si unajua fedha (si msingi bali ni matokeo ya maendeleo). Hoops! Nimekosea, fedha ndiyo msingi wa maendeleo. Hivyo, Serikali ya Tanzania ilifyata mkia na kupeleka Muswada wa rushwa Bungeni.
Ni kipindi hicho hicho ambapo, Wabunge ambao ni (wawakilishi wa wananchi) Hoops! ambao ni wawakilishi wa vyama vya siasa, ambavyo ndivyo vinawakilisha wananchi, waliikaba koo Serikali iweke wazi mikataba ya madini ili angalau waisome tu. Si unajua ati kazi yao ni kuisimamia na kuiwajibisha Serikali kwa niaba ya nani tena? Serikali iliwakejeli na kusema mikataba ni siri. Mmmh! jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Sasa utasimamia na kuwajibisha wakati uko gizani? Wawakilishi wakitaka chochote wanatoka kapa, lakini Mzungu akitaka chochote kinafanyika.
Unakumbuka mkutano wa IMF uliofanyika Dar mwaka jana, ambapo kimwana wa CNN aliwauliza wajumbe wa mkutano walioamini kuwa amri kutoka Washington sasa basi. Rais Kikwete alinyoosha mkono, lakini Waziri wake wa Fedha, machale yalimcheza na kuuchuna (alijua ni usanii). Haya bana, swali la pili (kimwana naye..mmmh), sasa Rais Kikwete hutapokea tena amri kutoka Washington (Manake watoa amri wamevurunda uchumi wao), una mawazo/mikakati gani ya kuendesha nchi? Rais wetu alijibu kuwa ataendelea kufanya vilevile, yaani anavyofanyafanya, yaani yaani, si unajua tena kiaina?
Nawashangaa Wabongo wanaodai Rais wetu ni "kigulu na njia". Sasa afanye nini nchini wakati sera na sheria za kuendesha nchi zinasukumwa kutoka nje?
Alafu hawa "viongozi bora" kabla hatujawachagua wanasema ni "vichwa kweli kweli" yaani ni "moto" wa kuotea mbali kwa "mawazo na ubunifu" wao. Tena wengine tunawajua ni wajinga tu, lakini nasikia siku wanapochanguliwa/teuliwa kuwa "viongozi bora", basi akili, busara, PHD na nini tena... vyoote vinawaangukia papo kwa papo. Lakini wanapotakiwa kutuliza bori na kuchanga bongo zao hizo ili kubuni mbinu, sera, dira na mikakati kabambe ya kutukwamua, wanaona maluilui na kukimbilia Washington kwa akina IMF, WB, WTO na kadhalika, ati kuhemea.
Tukiwauliza mmeleta nini kutoka Washington? Hawasemi, ila tunaona watu wanahamishwa kutoka katika ardhi zao ili kuwapisha "wawekezaji". Yaani mambo yaleyale ya Abushiri. Tofauti ni kwamba Abushiri hakuwa na PHD. Pia Abushiri hakwenda Washington. Umesahau hivi majuzi, Rais Obama alimsifia Rais Kikwete kuwa anafanya kazi nzuri isiyo kifani, kama ambavyo Rais Reagan na Bush walivyomsifia Rais Mobutu kuwa ni mfano wa kuigwa Afrika. Si unajua Wamarekani hawana rafiki yakhe. Wana maslahi. Ukitaka fedha, watakupa. Ukitaka mabomu watakuvurumushia. Ukitaka misifa, watakumwagia kebekebe, ilimradi tu wametimiza haja yao.
Tuliambiwa kuwa mnaona! Obama kamsifia Kikwete, sasa wawekezaji watanyesha Tanzania kama mvua za masika. Hata hivyo, baada ya Kikwete kumpa kisogo tu Obama, Serikali ya Obama imetoa ripoti kwa Wamarekani na dunia nzima kuwa "aka ka nchi ka Tanzania kanakoongozwa na Kikwete kananuka rushwa". Hivi vilemba vya ukoka bwana! lakini vinalipa, si unajua wabongo kwa kubabaika. Juzi anti yangu ananipigia simu kuwa Kikwete na Obama pete na kidole. Na huu ni msimu wa uchaguzi. Na kale ka asilimia sabini ketu kanako fuata upepo, mmmh! yetu macho.
Anyway, Haya masharti ya IMF ambayo Bo Karlstrom alitaka kumuingiza mkenge Nyerere ni upuuzi mtupu. In fact, Rais Mwinyi aliyakubali yote na mengine ya ziada -kama cost-sharing katika elimu na afya. Walimpa dose ya kuvizika kabisa viwanda na mashirika ya umma, kuididimiza elimu na idara ya afya. Hiyo dose iliitwa SAPs - Structural Adjustment Programs.
Of course, hata kilaza anajua kuwa unaposhusha thamani ya shilingi wakati unaagiza malighafi na mafuta kutoka nje, unavizika viwanda, siyo unavifufua. Unapokata mipango ya elimu na kupunguza fedha za kununua vifaa vya mahabara, vitabu vya ziada na kiada, mishahara ya waalimu na kadhalika, unakuwa umewekeza katika bora elimu na siyo elimu bora. Matokeo yake, ama unakuwa na asilimia kubwa ya wanafunzi wanaopata zero, au unakuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma wala kuandika.
Dira ya Azimio la Arusha inasema kuwa mtu anaweza kutetea haki zake bara-bara kama haki hizo anazijua, na anazijua sheria zinazomlinda kitaifa na kimataifa. Ndiyo maana ukatoka mkakati wa Msoma (Azimio la msoma)-Elimu kwa wote. Matunda yake yalionekana na matunda ya SAPs tunayaona leo.
Nasikia Obama anarudisha mikopo ya wanafunzi serikalini kutoka katika mabenki binafsi. Sasa Serikali itaimiliki kwa asilimia 100 na itapanua wigo wa kuwasomesha Wamarekani wasiyo na uwezo bure. Sisi tunaambiwa hatuwezi kuwasomesha watu wetu bure kwa sababu inabidi fedha inayopatikana baada ya kukusanya kodi iende kulipa madeni. tena madeni mengine tulikopa kutunza vyura vya Kihansi. Yaani watu wasiende shule ili vyura wapone.
Unakumbuka miaka ya 2000, nchi masikini zililalamika kuwa masharti ya SAPs yalizitia kilema cha maisha na kudai yaondolewe. Well, February 2003 na March 2005, nchi tajiri zilikutana na kupitisha maazimio ya Rome 2003 na Paris 2005 ili kupunguza makali ya masharti. Rais Mkapa alimtuma Kikwete (waziri wa mambo ya ndani-wakati ule) atuwakilishe. Hayo maazimio hayatekelezwi na bado wanaendeleza ubabe tu mpaka hapo tutakapo damka kutoka usingizini.
Azimio la Arusha ilikuwa dira, kama vile ngazi ambayo mtu anaweka ukutani ili imwezeshe kufika paani. Katika msukosuko wa upepo, anakuja Mzungu, tena yuko paani, anakwambia itupe hiyo nganzi nitakutupia kamba alafu nikuvute. Ukiiangalia ngazi unaona imebuniwa na mswahili mwenzako na kamba imebuniwa na mzungu, tena yuko paani unapotaka kwenda. Unaitupilia mbali hiyo ngazi na kubakia kubembea kwenye kamba. Mzungu anavuta kidogo alafu anaiachia unadondoka puu!. Anakwambia kabla ujaishika tena kamba, nitupie hilo embe, unamtupia, nitupie Hindi la kuchoma, unamtupia na yeye anakula. Na hivi ndivyo wanavyotufanya. Nasi tunashangilia Hoyeeeee!
😎