WABUNGE CCM WAFURAHIA ONGEZEKO LA POSHO
Wakati Shibuda akiwashambulia viongozi wake, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesherehekea kupandishwa kwa posho zao, wakidai kuwa wao ni watu wenye heshima ya mbunge wanaostahili kuishi na kufanya kazi katika mazingira mazuri na salama. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Mlaki, alipongeza uamuzi huo kwa madai kuwa hutumia fedha nyingi awapo Dodoma kuliko anayolipwa na Bunge. Alisema nyumba aliyopanga huko Dodoma hulipa kodi ya sh 350,000 kwa mwezi, ingawa anaitumia kwa muda mfupi tu, hivyo fedha nyingi zinapotea bure. "Mafuta tunayopewa ni kidogo, fedha za madereva haziwatoshelezi, hivyo ni lazima nihakikishe dereva awapo Dodoma anaishi vizuri na kumlipia chumba kizuri…naupongeza uamuzi huu wa serikali," alisema.
Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, alisema mbunge si mtu binafsi, bali ni taasisi hivyo kama taasisi inahitaji fedha za kujiendesha.Simbachawene ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, alisema shughuli za mbunge si kama za mkulima, mfanyabiashara au mtu yeyote yule, hivyo zinahitaji kuenziwa na kuheshimiwa kwani hufanya shughuli nyingine za hatari ambazo zinaweza kuhatarisha maisha yao. "Kama unasafiri kikazi, unahitaji usafiri mzuri, sehemu nzuri na salama ya kulala lakini mazingira salama zaidi kwa kuwa tunafanya kazi za hatari, tunakemea maovu na maovu hayo hufanywa na watu wenye uwezo, hivyo tunahitaji ulinzi wa kutosha. "Haiwezekani mbunge akalala nyumba ya wageni ya sh 5,000 au umkute anakula gengeni, lakini wakati mwingine watu wanatufuata wanahitaji misaada, fedha ni hizo hizo," alisema.
Aliwafananisha wabunge na wanafunzi 12 wa Yesu Kristo, kwa madai kwamba alipokuwa akiambatana nao haikumaanisha kuwa aliwadharau Wakristo wengine na kuwapenda wao tu, hivyo hata wabunge kuongezewa posho haimaanishi Watanzania wengine wanadharauliwa. Kwa mujibu wa Simbachawene, wabunge wa Tanzania ndio wanaolipwa posho ndogo sana ikilinganishwa na wale wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nao wabunge wa vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi walisema nyongeza hiyo si mbaya, lakini wakaishauri serikali kufanya uwiano wa nyongeza za posho kwa mihimili mingine ya dola, vinginevyo nchi haitatawalika. Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa, alisema gharama za kuishi Dodoma ni kubwa na kwamba hadhi ya wabunge wa Tanzania ni tofauti na wabunge wa nchi nyingine hasa za Afrika kimasilahi. Alisema mbunge ni kioo cha jamii, hivyo aliwashangaa baadhi ya watu kuhoji nyongeza zao badala ya kuhoji vitu vya msingi. "Mbona wafanyakazi wengine kama wakurugenzi wanalipwa fedha nyingi sana, lakini haihojiwi na isitoshe fedha zetu zinarudi kwa wananchi hao hao. Mjadala huu una lengo la kuchonganisha wabunge na wananchi wao," alisema. Hata hivyo alisisitiza kuwa kupanda kwa maisha si kwa wabunge tu, bali hata na wananchi wengine, hivyo suala la kupandisha posho, mishahara na marupurupu liangaliwe kwa upana wake.
Mbunge wa Uvinza, David Kafulila, alisema ipo haja serikali ikaongeza viwango vya mishahara na posho nyingine kwa mihimili yote ya dola, yaani Bunge, Mahakama na serikali. "Suala hili liangaliwe kwa watumishi wote. Maisha magumu si kwa wabunge tu. Kuwe na mfumo mzuri wa kurekebisha mishahara kwa mihimili yote si Bunge pekee…Tanzania hakuna uwiano wa mishahara kwa mihimili hii," alisema. Kafulila alisema wabunge wanapo pa kusemea katika kudai masilahi yao, lakini wafanyakazi wengine hawana, hivyo aliishauri serikali kuandaa mfumo mzuri.