Shangwe Ayo: Kuhusu Toto Afya Kadi, Serikali Isicheze na Afya Zetu

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540

Toto afya kadi au bima ya afya kwa wote; Serikali isitafute njia ya mkato kulinda afya zetu​

Utangulizi

Katika mjadala unaoendelea nchini kuhusu hatima ya Toto Afya Kadi baada ya kauli za Serikali kusitisha huduma hiyo (iliyolewa mwezi Machi, 2023) na hivi karibuni kutangaza utaratibu mpya wa upatikanaji wake (kupitia shuleni) Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea msimamo wake kwamba tunapitia changamoto hizi kutokana na Serikali kuamua kukwepa jukumu lake la kugharamia huduma za afya au kutokuwa na lengo la kuboresha na kuweka usawa wa upatikanaji wa huduma hizo kwa wote.

Mfumo wa sasa wa kugharamia huduma ya afya umeachwa kwenye mabega ya mwananchi kwa asilimia 100 kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya. Serikali haijihangaishi kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya afya kwa usawa unaozuiliwa na gharama kubwa na kukosekana kwa mfumo endelevu wa kugharamia na kupanua wigo na uwezo Serikali.

Tutegue tatizo la afya za wananchi

Huduma mbovu za Afya ni chanzo kikubwa cha umasikini wa Watanzania. Kwa mujibu wa tafiti za Benki ya Dunia, watanzania wengi wapo juu kidogo au chini kidogo ya mstari wa umasikini. Wakipata changamoto za afya walio juu ya mstari wa umasikini hurudi chini na walio chini huenda chini zaidi. Bima ya Afya ni nyenzo muhimu sana kuzuia watu kutumbukia kwenye umasikini. Mfumo wetu wa Bima ya Afya wa sasa ni mfumo wa kitabaka ambao unatoa huduma kulingana na uwezo wa mtu badala ya kulingana na mahitaji yake. Suala hili limekua likipigwa danadana kila mwaka.

Bajeti ya Serikali ya mwaka huu 2023/24 haijalitazama tatizo hili na kutenga fedha ili kuweka mfumo mzuri na endelevu wa kufadhili Bima ya Afya kwa Watanzania wote. Sisi, tumekuwa na msisitizo wakati wote wa kuitaka Serikali kuwekeza fedha kwenye Mfumo utakaoimarisha afya ya watanzania kwa kuwezesha kugharamia matibabu kwa watu wote nchini bila kuweka matabaka.

Mfumo ambao tumekuwa tukipendekeza ni ule wa Bima ya Afya iliyotoka na Mfumo wa Hifadhi ya Jamii. Tunataka mfumo unaomfanya mtu alipe bima kulingana na uwezo wake lakini apate huduma kulingana na mahitaji yake. Hali ya sasa katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa umekuwa ukitegemea uwezo wa kifedha wa Mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa.

Hali ya watanzania kwa Mujibu ya takwimu rasmi zinaonyesha kama ifuatavyo;

  • Ni Watanzania watu wazima milioni 1.8 tu ndio wapo kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii (NSSF na PSSSF) wanaohudumiwa na bima ya afya.
  • Watanzania milioni 7.4 wapo juu kidogo ya mstari wa umasikini ambao wengi wao wapo kwenye sekta isiyo rasmi
  • Watanzania milioni 8 wapo chini ya mstari wa umasikini ambao baadhi yao wapo kwenye mfumo wa kunusuru kaya masikini (TASAF)
Pendekezo la ACT Wazalendo ni kutaka mfumo wa hifadhi ya jamii upanuliwe kutoka kwenye kundi dogo la watu wazima milioni 1.8 hadi milioni 18.2 ili kuhakikisha watanzania wote wanakuwa na bima ya afya.

Hivyo basi, mapendekezo ya ACT Wazalendo kuhusu mfumo endelevu wa Hifadhi ya Jamii utakaofungamanisha na Bima ya Afya kwa Wananchi wote ni yafuatayo;

  • Kwa wananchi ambao sasa ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii ambao ni milioni 1.8 Serikali ichukue asilimia 20 ya michango yao kwenye mifuko ya NSSF au PSSF kwenda kwenye skimu ya bima ya afya. Badala ya kukatwa michango mara mbili
  • Kwa wananchi ambao wapo kwenye sekta isiyo rasmi ambao wana vipato vya kuweza kuchangia (watanzania milioni 7.4). Serikali itoe motisha kwa kuwachangi shilingi 10,000 na wananchi kuchangia shilingi 20.000 kutoka sehemu ya vipato vyao kwa mwezi.
  • Kwa wananchi ambao ni masikini zaidi (watanzania milioni 8) Serikali iwachangie kwa silimia 100 kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii
Kupitia pendekezo letu Serikali kitakwimu tunaenda kuwa na matokeo yafutayo.

  • Jumla ya Watanzania watu wazima Milioni 17.2 watakuwa wanachama wa Hifadhi ya Jamii na moja kwa moja watanufaika na fao la skimu ya bima ya afya.
  • Watanzania milioni 61 watapata bima ya afya kwa kanuni ya kawaida ya mchangiaji mmoja na wategemezi watano (Mwenza na wanufaika).
  • Skimu ya hifadhi ya jamii itakuwa na jumla ya Shilingi trilioni 8.5 kwa mwaka kwa mchanganuo ufuatao;
  • Shilingi trilioni 2.7 kutoka kwa wanachama wa sasa waliopo kwenye mfuko ya hifadhi ya jamii.
  • Shilingi trilioni 2.9 kutoka wanachama wanaojiungwa kwa mfumo wa hiyari (wanachama milioni 8.4)
  • Shilingi trilioni 2.8 kutoka kwa wanachma wanaochangiwa asilimia 100 na Serikali (Watanzania milioni 8-TASAF)
  • 20% ya michango ya hifadhi itaenda kugharamia bima ya afya ambayo ni shilingi trilioni 1.7
  • Kati ya michango yote Serikali kupitia kuchangia makundi yote mawili ya itatumia shilingi trilioni 3.88 kila mwaka.
Kwa hiyo, ili kutekeza hili Serikali inapaswa kutenga fedha sawa na 2.5% ya Pato la Taifa kuweza kuhudumia Mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa wote ambao una Fao la Matibabu kwa wanachama wake. Kwa Mfumo huu kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya

Hitimishio.

Kutoa huduma ya afya kwa vifurushi au kudhibiti huduma zinazotolewa na Bima ya Afya kwa kuweka madaraja, kupandisha gharama, kuondosha baadhi ya huduma (Magonjwa ya moyo, saratani, ini, sukari na hata huduma za operesheni za uzazi) na kuzuia matumizi kwa baadhi ya hospitali haisaidii kujenga taifa badala yake itaenda kuumiza wananchi hasa wenye vipato vya chini.

Ni muhimu kwa Serikali kufikiria Mfumo utakaoimarisha afya ya watanzania na kuwezesha kugharamia matibabu kwa watu wote kwa kutoa jawabu la kuimarisha afya na kukabiliana na changamoto za gharama za matibabu. Sisi tumeona mfumo huo ni mfumo wa hifadhi ya jamii kwa watu wote kama tulivyofafanua hapo juu.

Serikali lazima ishiriki kuhudumia na kugharamia afya za Watanzania kwa kutumia kodi zetu. Afya sio bidhaa kuuzwa kama shati sokoni mwenye nacho ndio anunue na asiyenacho aangamie.



Imetolewa na;
Ndg. Shangwe Mike Ayo
X: @ayo_shangwe
Naibu Waziri Kivuli Ofisi ya Rais-Mipango, Uwekezaji na Hifadhi ya Jamii
ACT Wazalendo.
22 Septemba, 2023
 
Kumbe jamaa wamekwapua mabilioni kwenye mfuko halafu wana tubebesha wananchi. Ccm bila kuwatia adabu hakuna maendeleo kwenye hii nchi. Yaan wamefikia mahali hata afya zetu wana zifanyia biashara? Mambo ya aibu kabisa.
 
Back
Top Bottom