Serikali yasaini mkataba wa trilioni 10

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,128
SERIKALI kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imesaini mkataba wa miaka 25 wa kutafuta gesi asilia na mafuta utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 10.

Mafuta na gesi vitatafutwa chini ya bahari mkoani Mtwara kwa kuzingatia sheria za Tanzania bara.

Waziri wa Nishati na Madini,William Ngeleja na Mkurugenzi wa ufundi wa kampuni ya Ophir, Jonathan Taylor wameasani mkataba huo leo jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Ophir itafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya BG group.

Ngeleja amesema,mkataba huo ni wa kihistoria na kwamba,baada ya kuhakikisha gesi na mafuta vimepatikana unaweza kuongezwa hadi miaka 45 kwa kuzingatia mazingira ya wakati huo.

Amesema,mkataba huo utakaoanza kutekelezwa wakati wowote kuanzia sasa ni wa kihistoria kwa kuwa,hakuna mradi uliowahi kuwekezwa kwa gharama hizo.

Kwa mujibu wa Ngeleja, Serikali ya Tanzania na kampuni ya Ophir wamekubaliana kuzingatia maslahi ya wananchi.

“Mkataba huu wa dola bilioni saba ambao ni sawa na shilingi Trilioni 10 ni wa gharama kubwa ambayo haijawahi kuwekezwa kwa kiasi hicho tangu wawekezaji waanze kufanya shughuli za utafuaji gesi asilia na mafuta ambapo katika sehemu hizo kuna dalili za mafanikio” amesema Waziri Ngeleja

Amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeupitia mkataba huo na pia Serikali imepata ushauri kutoka kitengo cha sheria cha Jumuiya ya Madola.

Ngeleja amesema, iwapo utafutaji huo utafanikiwa, wameweka kipaumbele kutumia gesi na mafuta katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea ili kuboresha Kilimo,ujenzi wa viwanda vya sementi pamoja na gesi asilia kutumika kuzalisha umeme.

Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dismas Fuko, amesema, wawekezaji wanamiliki kwa asilimia 80 na Serikali ina asilimia 20 ya kazi hiyo ya kutafuta mafuta na gesi.

Taylor amesema,watanzania zaidi ya 2,000 watapata ajira katika shughuli za ujenzi zitakazoanza hivi karibuni na pia idadi kama hiyo pia inatarajiwa kuajiriwa wakati wa utafutaji ukianza.
 
Back
Top Bottom