Serikali yakana kupokea barua ya Mkurugenzi Jatu kukiri Mashtaka

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
1683549837680.png

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33) umeileza mahakama kuwa bado haujapata barua ya mshtakiwa huyo kuomba kufanya majadiliano na makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri mashtaka yanayomkabili.

Gesaya anakabiliwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu.

Katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 8 ya mwaka 2023, anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha haramu.

Aprili 24, 2023, wakati kesi hiyo ilipotajwa, mshtakiwa huyo kupitia kwa mmoja wa mawakili wake, Nafikile Mwamboma, aliieleza mahakama hiyo kuwa amemwandika barua DPP akiomba kufanya majadiliano na makubaliano ya kukiri makosa ili apunguziwe adhabu.

Hata hivyo leo Mei 8, 2023, wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kujua maendeleo ya mchakato huo wa majadiliano na makubaliano na DPP, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Agnes Mtungija ameileza Mahakama hiyo kuwa bado hawajapata barua hiyo ya mshtakiwa.

Wakili wa mshtakiwa huyo, Kung'e Wabeya amesisitiza kuwa tayari walishaandika barua hiyo na kuiwasilisha ofisini Kwa DPP.

Hivyo Wakili wa Serikali, Mtungija ameiomba mahakama wapewe muda ili wafuatilie barua hiyo kwa DPP kujua hatima yake.

Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate anayesikiliza kesi hiyo katika hatua ya awali ya uchunguzi wa kesi hiyo, amekubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na akaelekeza upande wa mashtaka kufuatilia barua hiyo kama imeshafika kwa DPP, na akaahirisha kesi hiyo hadi Mei 22, 2023.

Kesi hiyo imesikilizwa wakati mshtakiwa akiwa rumande katika gereza la Keko, huku akiunganishwa na mahakama kwa mawasiliano kielektroniki ya video (video conference).

Mshtakiwa huyo yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika shtaka la kwanza, Gesaya anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.1 bilioni kutoka Saccos ya JATU.

Anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya JATU kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la pili anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es Salaam, akiwa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa JATU SACCOS, alijihusisha na muamala wa Sh5.1 bilioni.

Anadaiwa kuwa katika nyakati hizo alihamisha fedha hizo kutoka katika akaunti ya JATU SACCOS iliyopo Benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya JATU PLC liyopo katika Benki ya NMB tawi la Temeke.

Anadaiwa kutenda kosa hilo wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

MWANANCHI


Pia soma:

 
Back
Top Bottom