Serikali na Matumizi ya Programu za Udukuzi na Upelelezi: Ongezeko la Tishio kwa Ulinzi wa Faragha na Haki za Binadamu

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
Programu za upelelezi na udukuzi.jpg


Serikali nyingi duniani zinaongeza matumizi ya udukuzi kufanikisha shughuli zao za upelelezi. Hata hivyo, nyingi hutumia udukuzi huo kwa siri na bila msingi wa wazi wa kisheria. Hata katika kesi ambapo serikali zinajaribu kuweka uwezo huo katika sheria, mara nyingi hufanya hivyo bila kuweka kinga na usimamizi unaofaa kwa shughuli za upelelezi chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Udukuzi unaweza kuwa na vitisho vikubwa zaidi tofauti kwa faragha na usalama wetu. Kwa sababu hizi, hata pale ambapo serikali zinafanya upelelezi kwa shughuli halali kama vile kukusanya ushahidi katika uchunguzi wa jinai au ujasusi, mara nyingi hawawezi kuthibitisha kuwa udukuzi kama njia ya upelelezi ni unafuata sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Stori ya Pegasus

Mnamo mwezi wa Julai 2021, mtandao wa uandishi wa habari wa uchunguzi uitwao Forbidden Stories ukiungwa mkono na shirika la Amnesty International, ulichapisha habari kuhusu matumizi ya programu ya Pegasus ambayo ilivuta masikio ya wengi duniani kuhusu suala lililojadiliwa kimataifa kwa miaka mingi - yaani kuenea kwa zana za udukuzi zinazolenga na kufanya upelelezi wa siri kwenye vifaa vya kidigitali.

Ingawa zana hizi zilitangazwa kutumiwa kupambana na ugaidi na uhalifu, mara nyingi zimekuwa zikitumiwa vinginevyo, ikiwa ni pamoja na kukandamiza maoni au mitazamo ya wale wanaofikiri tofauti na mamlaka, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, viongozi wa upinzani na watetezi wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa orodha iliyovuja ya namba za simu zaidi ya 50,000 za walengwa wa upelelezi na uchunguzi wa simu zilizoathiriwa, mwaka 2021 takribani waandishi wa habari 189, watetezi wa haki za binadamu 85, wanasiasa na maafisa wa serikali zaidi ya 600, ikiwa ni pamoja na mawaziri, na mabalozi walilengwa. Uchunguzi pia ulifichua udukuzi kwa majaji, mawakili, madaktari, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanazuoni. Kampuni ya NSO Group, ambayo inatengeneza na kuuza Pegasus, ilikiri kwamba wateja wake wanawalenga watu 12,000 hadi 13,000 kila mwaka.

NSO iliripoti kuwa miongoni mwa wateja wake ni zaidi ya mawakala wa serikali 60 katika nchi 45. Siku chache kabla ya kuibuliwa sakata la Pegasus, kampuni za Citizen Lab na Microsoft zilitoa ripoti iliyoelezea jinsi programu nyingine ilivyotumiwa na serikali kuwalenga watetezi wa haki za binadamu, wapinzani, waandishi wa habari, wanaharakati na wanasiasa. Mnamo Novemba 2021, kampuni ya mitandao ya kijamii ya Meta ilitangaza kuwa imedhibiti taasisi saba zilizowalenga watu kupitia mtandao katika nchi zaidi ya 100. Kampuni hiyo pia iliwajulisha watu takriban 50,000 ambao waliaminiwa kuwa walilengwa na shughuli hizo.

Udukuzi na Haki ya Faragha

Kupata udhibiti kamili wa simu au kompyuta kunawafanya wadukuzi kupata picha kamili ya maisha ya wale wanaolengwa na udukuzi huo. Udukuzi pia unaweza kupata ufikiaji wa vifaa vingine vya kiteknolojia vinavyovaliwa (kama vile saa za mkononi), au magari ambavyo vinaweza kutoa taarifa za afya ya mtu au eneo alilopo, inasema Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyopewa jina Haki ya Faragha katika Zama za Kidigitali.

Vifaa vilivyotengenezwa na kamera au maikrofoni, kama spika za smart au televisheni, pia vinaweza kuwa zana za udukuzi za sauti na video. Kuingilia miundombinu ya watoa huduma kunaweza kuwezesha ufikiaji wa kiasi kikubwa cha taarifa kuhusu maelfu ya wateja, ikiwa ni pamoja na mawasiliano yao, taarifa za maeneo waliopo.

Udukuzi wa vifaa vya mawasiliano binafsi unakiuka haki ya faragha na unaweza kusababisha ukiukwaji wa haki nyingine mbalimbali. Kuingilia vifaa vya mawasiliano vya kidigitali kunawapa wadukuzi nafasi ya kufikia historia ya mambo ambayo mtumiaji wa kifaa hicho ametafuta mtandaoni. Inaweza pia kuwapa ufahamu wa namna walengwa wanavyofikiri, pamoja na mitazamo yao ya kisiasa na kidini, hivyo kuingilia uhuru wa maoni na mawazo. Operesheni za udukuzi zinaweza kuwaathiri sana kisaikolojia waathirika na familia zao.

Udukuzi na Uhuru wa Habari

Udukuzi umehusishwa na kukamatwa na kushikiliwa kwa watetezi wa haki za binadamu na wanasiasa, huku baadhi yao wakiripotiwa kuteswa au kuuawa.

Kuwalenga waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa zana za udukuzi kunasababisha ukandamizaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari, hasa kwa sababu vyanzo vya habari vinaweza kuogopa kugundulika na kisha kushambuliwa. Matokeo yake ni kuhatarisha utawala wa kidemokrasia. Kwa maneno ya Mahakama Kuu ya India katika uamuzi wake wa hivi karibuni juu ya matumizi ya programu ya Pegasus, udukuzi ni "shambulio dhidi ya jukumu muhimu la ulinzi wa umma la vyombo vya habari."

Udukuzi na Michakato ya Haki

Udukuzi pia unaweza kuathiri vibaya michakato ya haki. Kupata ufikiaji wa kifaa kunaweza kuwezesha mdukuzi sio tu kuona maudhui ya kifaa hicho na mwingiliano wake na vifaa vingine, lakini pia kubadilisha, kufuta au kuongeza mafaili. Hivyo, inawezekana kughushi ushahidi ili kumtia hatiani au kumtishia mtu. Zaidi ya hayo, programu za udukuzi zinaweza kuathiri si tu walengwa wa operesheni za udukuzi, bali pia kila mtu anayewasiliana na watu hao.

Hata hivyo, mashirika ya haki za binadamu na wataalam wameonya kuhusu programu hizo kwa miaka mingi. Baraza Kuu na Baraza la Haki za Binadamu wameeleza mara kwa mara kuwa nchi wanachama wanapaswa kujizuia kufanya ufuatiliaji (surveillance) usio halali au usio wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kupitia njia ya udukuzi.

Juhudi Zinazotakiwa

Nchi zinapaswa kuunda sheria madhubuti na kanuni zinazolinda faragha na haki za binadamu katika muktadha wa matumizi ya programu za udukuzi. Sheria hizo zinapaswa kuweka mipaka wazi kwa upelelezi wa serikali, kuhakikisha uwazi, uwajibikaji, na uwepo wa kinga za kutosha kwa watu wanaolengwa.

Lakini pia, jumuiya ya kimataifa inahitaji kushirikiana katika kukabiliana na matumizi mabaya ya programu za udukuzi. Hii inaweza kujumuisha ushirikiano wa kimataifa katika kuanzisha viwango vya kimataifa na kanuni za faragha na usalama wa mtandao, na kushirikiana katika kuchunguza na kuwajibisha serikali zinazokiuka haki za faragha.

Uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu za demokrasia. Ni muhimu kuunga mkono na kulinda uhuru huu ili kuruhusu uchunguzi huru na uwazi wa matumizi ya programu za udukuzi na kusimamia serikali. Kwa kufuata hatua hizi, tunaweza kuchukua hatua madhubuti dhidi ya matumizi mabaya ya programu za udukuzi na kulinda haki za faragha za watu.

Kabla ya kufunguliwa kwa RightsCon, mkutano kuhusu haki za binadamu katika zama ya kidigitali, ambao umefanyika San José, Costa Rica, mwaka huu, Rasha Abdul Rahim, Mkurugenzi wa Amnesty Tech, alisema: "Serikali duniani kote lazima zichukue hatua za kuzuia makampuni yanayotengeneza programu za upelelezi zisizokuwa na maadili kuuza bidhaa zao, na kuzuia simu zisigeuzwe kuwa silaha.”
 
Udukuzi ulianza zamani sanatangia pale binadamu waliposimika utawala juu ya jamii zake yote hii Ni juu ya hofu ya kupinduliwa na kuwatafuta wasaliti wa tawala zao. Kadri teknolojia inavyoendelea udukuzi umekuwa ukikuwa kwa kasi sana. Kwa mdukuzi ni ngumu kupata taarifa azitakazo tu bila kuingilia faraga za anayedukuliwa maana teknolojia inakusanya taarifa zote na kazi ya kuchambua na kuchakata ni juu ya mdukuzi ili kupata zile taarifa azitakazo. Ni kutokuwa na uwaminifu tu juu ya baadhi ya wenye majukumu hayo kuvujisha taarifa za faragha za watu wanaowafuatilia. Hapa ndipo uvunjifu wa haki za binadamu unapoanzia.
 
Udukuzi ulianza zamani sanatangia pale binadamu waliposimika utawala juu ya jamii zake yote hii Ni juu ya hofu ya kupinduliwa na kuwatafuta wasaliti wa tawala zao. Kadri teknolojia inavyoendelea udukuzi umekuwa ukikuwa kwa kasi sana. Kwa mdukuzi ni ngumu kupata taarifa azitakazo tu bila kuingilia faraga za anayedukuliwa maana teknolojia inakusanya taarifa zote na kazi ya kuchambua na kuchakata ni juu ya mdukuzi ili kupata zile taarifa azitakazo. Ni kutokuwa na uwaminifu tu juu ya baadhi ya wenye majukumu hayo kuvujisha taarifa za faragha za watu wanaowafuatilia. Hapa ndipo uvunjifu wa haki za binadamu unapoanzia.
Ni balaa
 
Nakumbuka Kuna kiongozi mmoja was taifa letu alikuwa hana break, ye alikuwa anawachana mawaziri wake kuwa wanavyotongozana na kupigiana simu za umbea kumnanga ye anajua🤣🤣
That was unethical as a leader anayepokea taarifa za taifa zima. Sasa sijui nia yake ilikuwa kutengeneza hofu kwa subordinates wake😆😆
 
Back
Top Bottom