Mwezi February niliweka hapa taarifa ya Mwalimu mmoja mkoani Arusha ambaye ana astashahada ya ualimu (Teaching Certificate), Bachelor Degree ya Ualimu (B.A with Education), Postgraduate Diploma in Special education (aliyoipata huko Norway) na Masters Degree ya usimamizi wa Elimu (Master of Education - Planing &Administration).
Lakini Mwalimu huyo amekuwa akilipwa mshahara wa certificate na bado anafundisha MAGAZIJUTO darasa la 3B.
Nilimuandikia Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe.Silinde Ernest David kumuomba mambo mawili. Moja huyo mwalimu abadilishiwe muundo wa mshahara ili alipwe kwa viwango vya Mwalimu mwenye degree, na pili kama ikipatikana nafasi Mwalimu huyo aondolewe shule ya msingi apelekwe sekondari au vyuo vya kati akatumike vizuri. Kumuacha msomi kama huyu kuimba mabata madogo madogo ni matumizi mabaya ya rasilimali.
Napenda kutoa mrejesho kwamba Mhe.Silinde alilifanyia kazi suala hilo, aliwasiliana nami, baadae akawasiliana na Mwalimu huyo pamoja na uongozi wa Halmashauri anayofanyia kazi. Tayari amebadilishiwa muundo wa mshahara, kwa sasa analipwa kwa kiwango cha mwalimu mwenye degree. Pia Silinde ameahidi kufanyia kazi suala la kuhamishiwa vyuo vya kati. Amesema kwa sasa hakuna nafasi lakini zikipatikana Mwalimu huyo atapewa kipaumbele.
Nitumie fursa hii kumpongeza Mhe.Silinde kwa kuchukua hatua kwa haraka. Pia aendelee kugusa maisha ya watumishi wengine wa wizara yake hata wale ambao hawapati fursa ya kusemewa kama huyu. Hongera Silinde. Tutawapongeza mnapofanya vizuri, na kuwakosoa mnapoboronga. We give credit where credit is due.
Mawaziri wengine pia waige hili. Zile zama za kuogopa kufanyia kazi matatizo yanayoibuliwa na upinzani zimepitwa na wakati. Mama amesema tufungue ukurasa mpya kwa maslahi ya watanzania wote.!
GJ Malisa