Serikali imesema kuanzia Julai Mosi itaanza kutoa mafunzo kazini, ikiwamo mbinu za ufundishaji wa somo la hesabu.
Hatua hiyo ni baada ya Serikali kubaini kuwa kuna walimu hawamudu kufundisha baadhi ya mada katika somo hilo.
Pia ili kuboresha ufaulu wa somo hilo watachapa na kusambaza vitabu kwa wanafunzi wote wa sekondari, kuwatia moyo wanafunzi kupenda hesabu, kuhuisha na kuanzisha vituo vya kujifunza kwa walimu.
Hayo yalisemwa katika uzinduzi wa kampeni ‘KiuHisabati Ubungo’ iliyozinduliwa na mbunge wa jimbo la Ubungo ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo.
Kampeni hiyo ililenga kuhamasisha ufaulu wa somo hilo katika mitihani ya kitaifa, hususan kidato cha nne.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu alisema kuboresha elimu ya sekondari ni moja ya mikakati yao katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Alisema katika mikakati hiyo, wanatarajia kufanya mambo manne, ikiwamo kutoa mafunzo kazini kwa walimu wote wa hesabu juu ya mbinu bora za ufundishaji somo hilo.
“Tutawafundisha mbinu bora za ufundishaji darasani na jinsi ya kuwasaidia wanafunzi wenye uelewa mdogo, tutachapa na kusambaza vitabu vya hesabu kwa wanafunzi wote wa sekondari ili kila mmoja awe na chake ili aweze kufanya mazoezi nje ya masomo,” alisema.
Alisema pia watafufua na kuanzisha vituo vya kujifunza vya walimu kuanzia ngazi ya tarafa na sehemu ambayo kata ni kubwa vitapelekwa huko, ili walimu wawe na sehemu ya kwenda kujifunza mada ngumu na kubadilishana mbinu za ufundishaji.
“Kuhamasisha wanafunzi kupenda hesabu pia ni moja ya mambo ambayo tutayafanya na tutaangalia namna ya kuwapa motisha walimu watakaokuwa wanafanya vizuri,” alisema Ummy na kuongeza kuwa Serikali imegundua kuwa wanafunzi wanafeli hesabu kwa mtazamo kuwa ni ngumu.
Chanzo: Mwananchi