Serikali ijaribu sera ya madaraka mikoani, yaweza kabisa kuibadili nchi yetu ndani ya kipindi kifupi

Richard

JF-Expert Member
Oct 23, 2006
14,939
20,400
Makamu mwenyekiti yupo ziarani mikoa ya magharibi mwa Tanzania, ambapo tayari kapita Kagera na mkoa mpya wa Geita.

Hapo Kagera kakutana na mkuu wa mkoa bwana Chalamila ambae juzi kaongea maneno ambayo yamekosa mwongozo wa kitaaluma kwa kujaribu kulinganisha uwezo wa kuongea lugha ya kiingereza kwa wakazi wa mkoa huo na kasi ndogo ya maendeleo.

Akiwa mkoani Geita ndugu Kinana amemshauri waziri wa madini bwana Biteko kuhakikisha mkoa huo wajengwa kufikia hadhi ya juu kwa kuzingatia kwamba mkoa huo ndipo kunapotoka madini ya dhahabu.

Lakini CCM lazima itambue kuwa kuchelewa kwa kukua kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi khasa mikoani pamoja na mengine, kwachangiwa na viongozi wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa maendeleo kushindwa kutekeleza sera na uboreshaji wa miradi ya maendeleo kwasababu asilimia kubwa ya mapato yaenda serikali kuu.

Nadhani umefika wakati serikali kupitia bunge ijadili na kupitisha sheria ya madaraka mikoani ambayo itasaidia mikoa na wilaya kuwa huru zaidi kupamnga shughuli za maendeleo ambazo haziingliani na sera za taifa kwa ujumla.

Hii pia huitwa ni demokrasia katika eneo lako yaani "local democracy" ambapo kwa kuanzia wananchi waweza kuchagua mameya wa mji au manispaa badala ya kikao cha madiwani. Kuendeela kuwa na mameya ambao wanakuwa wanawajibika kwa madiwani ni kuendeleza mianya ya upigaji na kutowajibika.

Mameya wakiwa ni wa kuchaguliwa waweza kuwa ni msaada mkubwa kwa viongozi wa serikali katika mikoa hivyo kushauriana katika kuleta maendeleo khasa shughuli za kiuchumi, ujenzi wa miundombinu kama barabara safi na shughuli zingine za kibiashara.

Kwa mfano Geita waweza kuwa mkoa kamili wenye kila kitu, wenye miundombinu imara kama barabara zilojipanga uzuri na pia kuwa na ramani inoeleweka ya mipango miji. Mji wowote ule ili ukue kiuchumi wahitaji pia kutoa huduma. Huduma ambazo zaweza kutolewa na mji au manispaa (kama ukijengwa uzuri) ni pamoja na uzoaji taka, huduma za usafiri, barabara na magari ambazo huenda sambamba na maegesho na utoaji vibali vya maegesho, mipango miji, huduma za biashara na mambo mengine kama hata kusimamia mazingira.

Haya yote si masuala ya kisiasa bali ni masuala yanohusu jamii husika katika eneo maalum kama mkoa Wilaya na manispaa.

Suala la uchaguzi wa mameya na madiwani ni suala muhimu sana ambalo ndilo litatathmini uwezo wao katika kuleta maendeleo kwenye maeneo yao. Wananchi hawawezi kumchagua diwani ambae ni mpigaji au mhuni tu wa barabarani bali ni mtu ambae akitamka maneno ya kutafuta maendeleo humaanisha.

Nafahamu kuna TAMISEMI ambayo ipo ofisi lakini kuhusu hii TAMISEMI nitazungumzia masuala mawili ya mapato na ajira.

TAMISEMI hutangaza mapato ya kila mwaka kupitia waziri wake lakini je, haya mapato hupangwa kwa kutumia vigezo vipi?

Kama kuna asilimia fulani (ambayo ni kubwa ) yapaswa kubaki mikoani ambako ndipo mapato hayo yatokea. Hivyo fedha za mapato hayo ndizo zitalipa walimu, wauguzi na madaktari pamoja na watumishi wa serikali katika mikoa.

Lakini hapohapo mikoa hiyo hutakiwa kuwa na vyanzo vyake vyenyewe vya mapato ambavyo ndivyo vitasaidia shughuli za kuboresha mazingira yake kama barabara na kadhalika. Sera ya madaraka mikoani itaipa mikoa hiyo uwezo wa kutumia hizo fedha zitokanazo na vyanzo vyake ilivyobuni kutumika ndani ya mikoa hiyo bila kwanza fedha hizo zote kwenda makao makuu na kisha kurudi mikoani kulingana na bajeti ilopangwa.

Kwa mfano mikoa ikiwa na huduma za maegesho katika baadhi ya kata fedha hizo ni mapato yake ya ndani na hapo ndipo ukosekanaji wa huduma zingine kama barabara katika maeneo mengi kuwepo.

Suala jingine ni la ajira abalo ndilo lapigiwa kelele kila kukicha ambapo kuna kundi kubwa vijana ambao wanahitimu katika vyuo mbalimbali kisha kuishia katika fani au tasnia ambazo zinawadidimiza kiuchumi.

Madaraka mikoani itaruhusu mikoa kubuni mazingira mazuri ya kuwezesha biashara kubwakubwa kama maduka makubwa kujengwa, maduka ya mitaani katika miji (town centres) na kuw atayari kuwavutia makampuni makubwa ya nje kuja kuwekeza ndani ya mikoa hiyo.

Sera ya madaraka mikoani haitakuwa ni kuachia mikoa kuamua kila kitu bali ni masuala muhimu kwa ajili ya eneo husika na kwa kuzingatia mahitaji ya mikoa badala ya kuamuliwa kutoka TAMISEMI.

Ni dhahiri hiyo yote yahitaji fedha nyingi ambazo zitatumika kujenga miji hiyo kwa kuwa na barabara nzuri, taa za bararani jambo ambalo pia litapelekea kupynguza vitendo vya kihalifu ambavyo huchangiwa sana na hali ya kutokuwepo kwa taa za barabarani. Kutokana na upangaji wa bajeti zao mikoa itaweza kuishawisi serikali itoe fedha zaidi ili miradi hiyo iweze kukamilika.

Serikali ikiruhusu madaraka mikoani kwanza itapunguza safari zake kuzunguka mikoani humohumo kwa manung'uniko khasa ya wakati huu kuhusu suala la tozo yamezidi kiwango nahali ya hewa si nzuri. Tozo ni suala ambalo serikali yenyewe imezembea kwa kushindwa kubuni njia sahihi za kukusanya mapato na kuwaachia wafanyabiashara kuendelea kukwepa kodi na kukazania kupandisha bei ya bidhaa kwa minajili ya kujipatia faida kubwa ndani ya muda mfupi.

Pili, kitendo cha CCM kutumia rasilimali na fedha za walipa kodi wachache au fedha ambazo wamejikusanyia kabla kufanya ziara za mikoani katika kipindi hiki kigumu ambacho kila mwananchi alalamika hali ngumu ya uchumi ni ufujaji ambao watakiwa kukemewa na viongozi wake akiwemo mzee Kinana.

Mkoa au wilaya na manispaa zikiweza kufanikisha kujenga misingi na mazingira mazuri ya ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi hiyo huwezesha hata masuala kama kubuniwa na kutengenzwa ajira mpya, biashara nyingi kukua mikoa kushamiri na hatimae taifa kwa ujumla kukua kiuchumi au kuboreshwa zaidi.

Hivyo basi kwa mtazamo wangu naona kwamba wakati umefika sasa kwa serikali ya CCM kufikiria juu ya suala la kuwa na sera ya madaraka mikoani ili kuwaachia viongozi wenye maono, ubunifu na uthubutu kuamua na kupanga masuala muhimu ya kimaendeleo katika maeneo yao.

Pia hata kukiwepo na mabadiliko ya katiba ya nchi, suala la madaraka mikoani litapaswa pia kuzingatiwa kwa maana ya kutaka kuirudisha nchi yetu katika utawala bora wenye manufaa kwa kila mtanzania.
 
Naheshimu sana mawazo yako ILA huo mfumo ndio uliokuwepo kabla JPM hajabadilisha na kuleta huo wa sasa kwamba pesa yote inakusanywa kwenda hazina na kurudishwa mikoani kwa ajili ya maendeleo.
MADARAKA YALIKUWA MIKOANI NA PESA WALIKUWA NAYO TATIZO WATZ SISI NI WEZI SANA NA WABINAFSI MNO.
ACHA HIVYO HIVYO TULIPOTOKA TUNAPAJUA VIZURI.
 
Nadhani umefika wakati serikali kupitia bunge ijadili na kupitisha sheria ya madaraka mikoani ambayo itasaidia mikoa na wilaya kuwa huru zaidi kupamnga shughuli za maendeleo ambazo haziingliani na sera za taifa kwa ujumla.
Serikali ya majimbo ndio suluhu ya kudumu.

kila kitu kuhodhiwa na serikali kuu (mpaka uteuzi wa viongozi wa mikoa na wilaya sio sahihi wala haki kwa wananchi wa mikoa husika)
 
Ni wazo zuri , Ila njia nyingine Tunaweza kuweka mfumo wa kikanda mfano Kanda ya Kaskazini ambapo kutakuwa na Gavana mwenye madaraka na baraza lake la wawakilishi kama vile Zanzibar, kwa kila kanda na hapo maendeleo yataenda kwa kasi na kutakua na ushindani. Nafikiri kwa uwezo wetu kiafrika Nchi ni kubwa sana , Haiwekani Nchi ndogo kama Rwanda ifanye vizuri kwa kila kitu . Tukiacha madaraka wenye Kanda tutaboresha kwani kila kanda itahitaji kuwa na Chuo kikuu chake, hospitali kubwa ya rufaa, Mji wake mkuu , Viwanja vya mpira na ligi yake ndogo n.k n.k
 
Natamani siku moja nishuhudie utawala wa serikali za majimbo

Kila jimbo liwe na bendera yake, coat of arms,motto, gavana, etc
Bendera na vitu ulovitaja hapana.

Nikisema madaraka mikoani ni kwamba mikoa kupewa uwezo wa kisheria kusimamia maendeleo yake kulingana na mapato inayopata.

Mapato yanokusanywa ni asimilia kiasi fulani ndo huenda serikali kuu.

Meya ndie mwenye mamlaka ya kupanga maendeleo ya mji au jiji lake kupitia baraza lake la madiwani.

Pia kwa kushirikiana na wabunge wa mkoa husika kupanga mipango ya maendeleo.
 
Serikali ya majimbo ndio suluhu ya kudumu.

kila kitu kuhodhiwa na serikali kuu (mpaka uteuzi wa viongozi wa mikoa na wilaya sio sahihi wala haki kwa wananchi wa mikoa husika)
Hatuhitaji serikali za majimbo ila madraka mikoani ili mikoa hiyo iwe huru kupanga mipango ya maendeleo katika mikoa hiyo kulingana na hali ya mikoa kiuchumi, kimazingira na kijiografia.
 
Back
Top Bottom