SoC03 Selo/Lokapu Haziwezi Kuwa Safi Ikiwa Dar es salaam Inanuka

Stories of Change - 2023 Competition

UMUGHAKA

JF-Expert Member
Sep 1, 2021
2,157
10,718
Mwaka 1993,Wilaya ya Musoma (Mjini) kwa Mara ya kwanza iliweza kuwa Mji uliokuwa ukiongoza kwa Usafi nchini Tanzania,baada ya hapo imebaki historia na sifa zote kuanzia hapo ilijichukulia mji wa Moshi unaopatikana Kaskazini mwa Tanzania, Mkoani Kilimanjaro.
Siku zote unapokuwa mtu wa kwanza darasani ni lazima kuhakikisha unaendelea kusoma kwa bidii ili uendelee kuishikiria nafasi ya kwanza,tofauti na hapo utashangaa unarudi nyuma kwasababu ya dharau,kujikweza na kudhani wenzio ni wajinga wasiokuwa na akili.Alichokifanya Musoma miaka hiyo anapambana sana kukirejesha lakini ni kama kushika shuka kukiwa kumepambazuka kwani kuna mjanja kutoka kaskazini ameamua kushikiria kwa nguvu zote alichonacho asije kukiachia kwa wengine.

Siku kadhaa zimepita nimewasikia viongozi wa kiserikali wakisema kunahitajika nguvu kutoka serikalini kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuzifanya Selo zisiwe sehemu mbaya hadi kuiletea sifa mbaya Serikali pamoja na jeshi la polisi lenyewe!.Kitu walichosahau hawa viongozi wetu ni kwamba,Nzi huwa hatoki chooni na kuelekea nje bali huanzia nje na kuelekea chooni ambako harufu ya vinyesi huwavutia.

NINI MAANA YAKE?

Hatuwezi kuzifanya Selo zikawa safi wakati huohuo Mji mkuu wa Kibiashara nchini Tanzania ukiwa unanuka uchafu na harufu kali za vinyesi za kuchukiza,ili kuzifanya selo zetu za polisi ziwe kivutio kwa watalii wavunjao sheria ni lazima kwanza Dar es salaam iwe safi.

Tangu nimekuwa mtu mzima ninayejitambua sijawahi kuona au kusikia kwenye vyombo vya habari hata kwa bahati mbaya mji/jiji la Dar es salaam likitangazwa likiongoza kwa usafi nchi Tanzania,ingawaje mwaka 2018 lilikuwa ni miongoni mwa majiji 10 yanayosifika kwa usafi Barani Afrika.Nilipoona wataalamu wa mazingira wameliorodhesha jiji la Dar es salaam kama jiji namba 9 kwa usafi Afrika ndipo nilipopata mashaka na hao wataalamu,kama ni kweli basi ukiondoa hayo majiji yenye “Unafuu” miji mingine iliyobaki Afrika Inanuka.

NINI KIFANYIKE KUONDOA KERO YA UCHAFU ULIOKITHIRI DAR ES SALAAM NA KUWA JIJI LINALOONGOZA KWA USAFI SI KWA TANZANIA TU BALI AFRIKA NZIMA?.

1.USIMAMIZI MKALI WA SHERIA

Hakuna mwanadamu mwenye kichwa ngumu kama muafrika,bila sheria kali/ngumu zinazohusu mazingira serikali haiwezi kufanya lolote kuhusu usafi wa mazingira.Yawezekana sheria kali zipo lakini wasimamizi wa sheria hizo ndiyo wakawa na kichwa ngumu,kazi yao ni ulaji wa kodi za watanzania huku wakisema “Kila mtu atajua mwenyewe”.
Hizi kama sheria kali kweli zipo inakuwaje watu wanatupa Taka ovyo na kitapisha vyoo ovyo na hakuna hatua zinazochukuliwa?,Je sheria ndizo zina mapungufu au wasimamizi wa sheria ndiyo kichwa ngumu?
Napendekeza sheria(By laws) ifanyiwe maboresho na itamke ya kwamba nyumba au mtu yeyote atakayekamatwa akitupa taka au uchafu kiholela atapigwa faini isiyopungua laki moja ikiwa na pamoja na kufanya usafi wa mazingira mahali atakapopangiwa na viongozi wa eneo husika kwa kipindi kisichopungua wiki moja.
Lugalo pale huwezi kuona uchafu kwasababu wanasimamia sheria na ukikaidi ni kipigo na utafanya usafi bila kupenda,Akili ya Muafrika kutoka Tanzania bila kufanya kama wafanyavyo watiifu wa sheria kutoka Lugalo hatuwezi kufanikiwa kamwe.

2.KONDAKTA NA DEREVA WA DALADALA (HAWA NI WATU MUHIMU)

Ukiingia kwenye Daladala utakuta kuna dust bin kwa ajili ya uchafu,hii iliwekwa kwa makusudi ili abiria akimaliza kunywa juisi,mo energy,maji ya chupa,biscuits ama ndizi basi yale maganda au chupa ziwekwe kwenye hiyo dust bin.Kwakuwa kuna watu akili zao zina makengeza,pamoja na kuiona dust bin lakini wakimaliza kutumia hizo bidhaa wao hufungua vioo na kutupa nje uchafu huku wakijiona wameyapatia maisha kumbe ni ujinga wa kiwango cha kimataifa.
Hapa Napendekeza ya kwamba Makondakta na Madereva wote wa Daladala zote za jiji la Dar es salaam wapewe maelekezo ya kwamba iwapo abiria atapanda kwenye gari akatumia bidhaa yake na uchafu akatupa nje basi hilo litapigwa faini ya Tsh 50,000/= na itabidi hilo gari ligeuzwe likaukote huo uchafu ili liendelee na safari.
Kama Ngorongoro,Serengeti na hifadhi nyingine hii mbinu imefanikiwa hapa mjini haiwezi kushindikana;Kondakta na dereva hawatokubali kupigwa faini kwasababu ya abiria asiyekuwa na akili timamu,pia hata abiria nao watakuwa wakali kupotezewa muda wa kurudi walikotoka ili kuokota uchafu uliotupwa na abiria asiyetaka kufuata sheria.
Hii ikiingia kwenye akili kwa muda wa mwezi mmoja hili jiji hakika litakuwa safi.

3.HABARI ZA ONYO NA TAHADHALI KWENYE VYOMBO VYA HABARI.

Hapa napendekeza manispaa na serikali kutumia nguvu ya vyombo vya habari kuhabarisha Umma wa wakazi wa Jiji la Dar es salaam ya kwamba utokapo nyumbani kwako hakikisha ukifika mjini hautupi uchafu kwasababu ukidakwa utashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,Jambo lolote linahitaji elimu hivyo kila mwisho wa habari kwenye vyombo vya habari kuwe na dakika 5 za Tangazo kuhusu kutupa taka na faini zake zinazo ambatana na sheria kali.

4.MAPIPA/DUST BIN ZA TAKA NYEPESI

Dar es salaam nzima sijaona mapipa ya takataka nyepesi,hatuwezi kuwa tunaimba kila siku tutunze mazingira halafu hata vyombo vya kutupa taka hakuna,nilitegemea Kariakoo yote kuwe na mapipa ya uchafu kila mahali ili kupunguza uchafu.Kama tuko makini nadhani mapipa ni jambo la msingi sana.

5.MIGAMBO WABADILISHIWE MAJUKUMU

Migambo wa nchi hii wamekuwa wakichukua majukumu ya TRA pamoja na POLISI,sidhani kama ndivyo sheria zinavyosema,mimi ninavyofahamu Mugambo ni Jeshi la Akiba,hivyo basi migambo wapewe kazi ya kusimamia usafi ndani ya jiji badala ya kukimbazana na wafanyabiashara kila siku utadhani wao ndiyo maofisaa wa TRA,yaani leo mfanyabiashara anamuogopa Mgambo kuliko askari polisi.
Napendekeza hawa migambo wapewe majukumu mapya ya kusimamia usafi na kuwakamata wale wote watupao taka ovyo na napendekeza wavae kiraia ili iwe rahisi kuwasaka vichwa ngumu hadi pale hili somo la usafi litakapoingia ingia vichwani mwa wajinga.

6.CAMERA ZA USALAMA.

Kupitia Kamera za kuzuia uhalifu zitazofungwa hapa Mjini ndizo hizo hizo zitatumika kuwabaini watupaji wa Takataka mjini ili washughulikiwe kwa mujibu wa sheria,pia kutakuwa na ukaguzi wa Mara kwa mara wa nyumba kwa nyumba na kuona mifumo ya maji taka pamoja na uchafu vinapelekwa wapi!.
Kama nchi nyingine zimeweza Tanzania haiwezi kushindwa,nafahamu watu wapo vichwa ngumu lakini mbele ya sheria kali vichwa vitakuwa laini tu kama kumsukuma mlevi.

MWISHO

Kila mmoja awajibike katika kuhakikisha Dar es salaam inakuwa safi,wasimamizi wa sheria wahakikishe wanatimiza wajibu wao bila upendeleo na wananchi pia wanahakikishe wanafuata sheria za utunzaji wa mazingira ili kuilinda Dar es salaam isije geuka Dampo mithili ya Pugu Kinyamwezi.

DAR ES SALAAM NI KIOO CHA NCHI IKING'AA NA TANZANIA IMENG’AA.
 
Back
Top Bottom