ScanLink likitoka Mwanza kuja Dar lapinduka Gairo - Morogoro

na Joseph Malembeka, Morogoro

WATU wanane wamefariki dunia na wengine 52 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Scanlik.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 5:30 asubuhi katika Barabara ya Morogoro-Dodoma.

Katika ajali hiyo, basi hilo likiwa katika Barabara Kuu ya Morogoro-Dodoma, lilipinduka katika eneo la Magubike, Dumila wilayani Kilosa na kusababisha vifo vya watu hao.

Basi hilo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda jijini Mwanza, na lilikuwa likiendeshwa na Clement Lumola (47).

Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema basi hilo lilipofika sehemu hiyo, liliacha njia na kupinduka mara kadhaa.

Ingawa polisi inaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo, lakini baadhi ya majeruhi walisema ilitokana na mwendo kasi wa dereva, ambaye baadaye alishindwa kulimudu basi hilo na kuacha njia kisha kupinduka.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendegu, alisema kuwa ingawa ajali hiyo ilitokana na utelezi wa barabara, lakini mwendo kasi wa basi hilo umechangia kutokea kwa ajali hiyo.

Alisema pia ajali hiyo ilitokana na uchakavu wa basi lenyewe pamoja na matairi yake.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Thobias Andengenye, miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo, imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Morogoro.

Aliwataja waliofariki kuwa ni pamoja na mtoto wa miezi sita, Kwiumba Sengeti, wanaume watatu na wanawake wanne ambao majina yao bado hayajafahamika.

Baadhi ya waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni pamoja na askari wa JWTZ, Luteni 9712 Alistin Mwatambila (32) wa kikosi cha 82 KJ Shinyanga, MT. 87806 Abdarhaman Mohamed (26) wa kikosi 262 KJ Tabora, Rukia Haji (27) wa Ihumo, Rukia Haji (2) wa Ihumo, Kessy Philipo (32) wa Msamvu Morogoro, Ummy Deus (27) wa Zanzibar, Ayubu Joseph (1 ½) wa Zanzibar, Emmanuel Tengo (54) wa Shinyanga, Anjelina Kihunga (80) wa Kilombero, Figenia Mkongwa (62) wa Arusha, Paulo William (43) wa Dar es Salaam, Faustin Msuka (27) wa Mbezi, Dar es Salaam, A. 9670 CPL Yahaya Jumanne (39) wa Lushora, Shinyanga na Hassan Juma (25) wa Dar es Salaam.

Wakati huo huo, ajali nyingine ilihusisha basi la Kampuni ya Al-Hushoom Investment, lenye namba za usajili T 252 AED, lililokuwa likitoka Morogoro kwenda Dodoma, ambapo liligongana uso kwa uso lori namba T 981 AYF na tela T194AYK, kutoka Dodoma kwenda Morogoro katika eneo ambalo ajali ya kwanza ilitokea.

Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa basi la Al- Hushoom Investment ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, akishangaa basi la Kampuni ya Scanlink lililopinduka. Hata hivyo hakuna aliyepoteza maisha katika ajali hiyo.


SOURCE: Tanzania Daima August 27, 2009
 
Ndugu zangu je mliona zile tairi za hilo bus zilivyokwisha? ni mambo ya ajabu kweli vyombo vyetu vya usalama wa barabara kuruhusu gari ambalo halina viwango vya kutembea barabarani na kuliruhusu kufanya kazi ya kubeba abiria alafu nini matokeo yake? watu wamepoteza maisha na taifa linazidi kuangamia kwa kukosa nguvu kazi
 
Back
Top Bottom