Ndugu Kasori,
iii) Katika makala yako umejitahidi kumtenga Lowasa na Kikwete, huku ukijua wazi kuwa Lowasa asingefika alipofika na pengine asingefanya aliyoyafanya bila kubebwa na Kikwete. Sasa nakuuliza, huoni kwamba na wewe unaingia kwenye kundi hilohilo la wakwepa ukweli? Hebu nitoe wasiwasi. Hivi karibuni familia na watu waliokuwa karibu na mwalimu Nyerere wanafanya bidii kuwa karibu na Kikwete kwa kumuonyesha kwamba yeye ni tofauti sana na wengine. Kwa kufanya hivi wamekuwa wakiwashambulia viongozi waliostaafu au ambao wameng'oka madarakani. Sasa hebu nitoe wasiwasi, je nitakuwa nimekosea nikisema kuwa kuna kajitahada mnakokafanya kakujipendekeza kwa Kikwete ili mrudi kundini? Je, na nyie mnajaribu kukwepa ukweli?
iv) Hili ni la kwetu sote watanzania. Kuna tabia ambayo tumeijenga ambayo pia imethibitika kwenye makala ya ndugu Kasori. Nayo ni kuogopa kuwasema viongozi wetu wakiwa madarakani lakini mara wanapoondoka ndipo tunapata nguvu za kuwabebea mabango. Tulifanya hivi kwa Mkapa; tulimsifia sana Mkapa akiwa madarakani na wana CCM kama Kasori waliandaa kila aina ya makongamano na maandamano ya kumpongeza kuanzia lile la kumpongeza kwa kufanikisha nchi yetu kufutiwa madeni pale Ubungo Terminal hadi lile la kumpongeza kukuza uchumi pale Mnazi Mmoja. Na tena Butiku na Mwalimu Nyerere Foundation walimsifu sana Mkapa wakati ule angali akiwapa pesa za kuendesha foundation. Lakini mara alipotoka, tulimrushia mawe mpaka huwezi kuamini kwamba ni yuleyule. Sasa tunafanya yaleyale kwa Lowasa. Wana CCM hawa hawa wanaomchamba Lowasa leo baada ya kutoka madarakani ndio hawahawa ambao walikuwa hawachoki kutukumbusha ujemadari wa Lowasa alipokuwa waziri mkuu.
Na sasa tunamkwepa Kikwete, tunasubiri tuje tumvurumshie matope akitoka madarakani.Tafsiri ya yote haya ni maneno mawili kwa kiswahili: Woga na Unafiki. Wenzetu hawafanyi hivi. Wenzetu wanashughulika na viongozi wao wakiwa madarakani, hawahangaiki na wastaafu. Ndivyo walivyofanya kwa Blair kuhusu vita ya Iraq na sasa wameachana naye baada ya kuondoka na wana-deal na Gordon Brown. Ndivyo walivyofanya na wanavyoendelea kumshughulisha George Bush kuhusu Iraq lakini wataachana naye mara baada ya Rais mwingine kuapishwa hapa January 2009.
Ukweli ni kwamba tunaelekeza nguvu zetu pasipo. Lowasa tulishindwa kumshughulisha alipokuwa kwenye madaraka. Tutamchukia na kumsuta sana sasa hivi lakini ukweli ni kwamba hili halitabadili kitu madamu yeye sasa hana alichoshikilia ambacho kinatusaidia au kutuathiri sisi kama taifa. Ushauri wangu ni kwamba tushughulike na waliopo madarakani. Na wito wangu mkubwa zaidi ni kwamba tushughulike na Rais Kikwete na serikali yake. Ninachosema ni kwamba tufike mahala watanzania tuache woga na unafiki.
Hongera Ndugu Kasori kwa makala yako.