Sumaye amtetea Nape
na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameeleza kushangazwa na kushtushwa na uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana la Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa kumpokonya uanachama wake, Nape Nnauye.
Sumaye amesema anakusudia kueleza dukuduku lake hilo kuhusu uamuzi huo wa UVCCM wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) inayokutana mjini Dodoma leo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka mjini Dodoma anakohudhuria kikao hicho cha NEC, Sumaye alisema uamuzi wa kumwadhibu Nape wakati akiwa mgombea wa uenyekiti wa UVCCM unaweza kutafsiriwa kuwa ni jitihada za makusudi zilizofanywa na maadui zake kisiasa.
Alisema Baraza Kuu la UVCCM liliingia kwenye kikao hicho likiwa na mambo mawili, mosi kupitisha majina ya wagombea walioomba uteuzi wa nafasi za juu za uongozi wa jumuiya, Nape akiwa mmoja wao, na pili, kushughulikia kauli ya Nape dhidi ya tuhuma alizozitoa kuhusiana na mradi wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya UVCCM, kwamba ulikuwa na harufu ya ufisadi.
"Mimi sina hakika sana na haya ninayoyasoma kwenye vyombo vya habari, lakini kama baraza lingeamua kujadili majina, basi lingeshughulika na majina ya wagombea tu, na kama lingetaka kujadili kauli ya Nape kuhusu tuhuma alizotoa, basi lingefanya hivyo, kwani unapozichanganya hoja zote kwa wakati mmoja, lazima watu watahoji, kama ilivyo sasa," alisema Sumaye.
Alisema baraza lilikuwa na uwezo wa kuijadili kauli ya Nape kuhusu ufisadi na kumwita ajieleze, lakini lilisubiri kwa makusudi kuileta hoja hiyo wakati wa kujadili majina, huku likijua fika kuwa yeye ni mmoja wa wagombea.
Akifafanua, alisema ni makosa kwa baraza kumshughulikia kwa tuhuma alizozitoa wakati anagombea, kwani uamuzi huo unaweza kutafsiriwa kuwa umefanywa kwa makusudi na wabaya wake kisiasa.
Alisema hata Mwalimu Nyerere wakati wa utawala wake, mara nyingi alisisitiza kuwa kama kuna mwanachama ana makosa, ni bora ahojiwe na kuadhibiwa na vikao husika, lakini si busara kusubiri wakati wa uchaguzi, ndipo madhambi yake yaibuliwe.
"Ninavyoongea na wewe hapa, ndivyo nitakavyoongea ndani ya kikao cha NEC leo kwa masilahi ya chama chetu, kwani tuna dhamana ya kukilinda na kukitetea," alisema Sumaye kwa kujiamini.
Mbali ya kubeza hatua zilizochukuliwa na UVCCM dhidi ya Nape, Sumaye ambaye ndiye waziri mkuu pekee aliyedumu kwa vipindi viwili mfululizo vya miaka 10, alieleza kusikitishwa kwake na kauli zinazotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba kuhusiana na uamuzi huo.
"Kama kweli Makamba amesema yanayosemwa kwenye vyombo vya habari, maana wakati mwingine magazeti yetu yanaongeza chumvi, lakini kama ni kweli, nadhani hizo si kauli za mtu anayepaswa kuwa kiongozi wa chama chetu," alisema Sumaye bila kutaka kuingia kwa undani juu ya suala hilo.
Vyombo kadhaa vya habari vimemkariri Makamba akisema kwamba, uamuzi wa UVCCM wa kumfuta uanachama wake Nape, hauwezi kuhojiwa na mamlaka yoyote nyingine nje ya jumuiya hiyo ya CCM.
Kauli hiyo ya Sumaye inakuja ikiwa ni siku moja tu baada ya waziri mkuu mwingine mstaafu, Cleopa Msuya, kukaririwa akieleza kushangazwa na uamuzi huo wa UVCCM kumvua uanachama Nape.
Msuya ambaye naye ni mjumbe wa NEC alikaririwa akisema kwamba, uamuzi wa Baraza Kuu la UVCCM kumvua uanachama wake Nape ulifanywa katika mazingira ya jazba.
Kwa mujibu wa Msuya, hakutegemea kabisa kusikia kwamba uamuzi wa namna hiyo ungechukuliwa na vikao vya CCM ya sasa yenye dhamira ya dhati ya kujenga demokrasia ya mtu kutoa maoni.
Kwa maoni yake, Msuya alisema sababu zilizoelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Francis Isaac, kuhusu kupokonywa uanachama kwa Nape akidaiwa kusema uongo, ni nyepesi na hazina uzito unaostahili.
Msuya alieleza kushangazwa kwake na uamuzi wa UVCCM kumpokonya uanachama badala ya kumsimamisha uanachama na kutoa fursa kwa vikao vya juu viamue kuhusu majaliwa ya kijana huyo.
Malumbano hayo yanakuja siku takriban nne sasa tangu Nape alipovuliwa uanachama akituhumiwa kusema uongo wakati alipopinga mkataba wa ujenzi wa jengo la UVCCM na hivyo kwenda kinyume cha Kanuni za 17 (C) na18 (B) za jumuiya hiyo ya CCM.
Isaac aliyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na kutoa tuhuma nzito kwa viongozi wa juu wa UVCCM, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UVCCM, Edward Lowassa, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Emmanuel Nchimbi, Isaac mwenyewe na aliyekuwa Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Amos Makala, wote akiwahusisha katika kashfa ya mradi huo.
Isaac alisema licha ya adhabu hiyo, baraza limependekeza kwa chama chao kumvua nyadhifa zote za uongozi alizonazo Nape katika ofisi ndogo ya makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam, uamuzi ambao una nafasi ndogo ya kupata baraka za vikao vya juu vya chama hicho.
Kwa sababu hiyo, iwapo uamuzi wa kumvua Nape uanachama utabakia pasipo kutenguliwa, basi anaweza akajikuta akipoteza sifa za kuendelea kuwa mjumbe wa NEC ya CCM, ingawa nafasi zake nyingine za kimamlaka ndani ya chama hicho hazitokani moja kwa moja na kuwa mwanachama wa UVCCM.
Hata hivyo habari zaidi kutoka mjini Dodoma zinasema kuwa, hoja ya Nape, inaweza kuigawa NEC leo kutokana na misimamo tofauti ya wajumbe.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima mjini Dodoma, unaonyesha kuwa kuna wajumbe wanaounga mkono uamuzi wa baraza na kumwona kama Nape amekiuka maadili ya chama kwa kutoa siri za vikao na maoni nje, badala ya kufanya hivyo ndani ya vikao vya chama.
Pia wapo wajumbe waliobeba misimamo kuwa Nape ameonewa na hata kuishawishi NEC kwa hoja ili iweze kutengua baadhi ya maamuzi ya UVCCM.
Jana jioni Kamati Kuu (CC) ambayo pamoja na mambo mengine ilitarajia kuijadili hoja ya Nape, ilikuwa ikiendelea na kikao chake kilichoanza saa 10 jioni, chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Nape amekuwa katika mjadala mzito katika uchaguzi wa UVCCM, kutokana na hatua yake ya kulipua kile kinachoonekana kuwa bomu la ufisadi linalohusu mradi wa ujenzi wa jengo la makao makuu ya umoja huo.
Kwa mara ya kwanza, Nape alitoa hoja yake hiyo saa chache tu baada ya kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo inayompa fursa mshindi kuwa mjumbe wa vikao vya kimaamuzi vyenye nguvu kubwa ndani ya chama hicho tawala, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).