SoC01 Sababu 3 za Waokota Chupa za Plastiki kuonekana kama wana Magonjwa ya Akili

Stories of Change - 2021 Competition

Ambakucha

JF-Expert Member
Aug 16, 2019
277
445
1678076_Single-use-plastic-bottles-.jpg


Ni hakika kwamba, kwa miaka ya karibuni, kila Mtanzania mwenye akili timamu na ukamilifu wa kujitegemea, kama siyo mfanyakazi wa kuajiriwa au mfanyabiashara, lazima aisumbue akili yake ili kujua nini atafanya aweze kuingiza kipato kitakachomfanya kuishi kwa chakula na mahitaji mengine.

Ndiyo maana siku hizi, idadi ya Watanzania wanaojishughulisha na ujasiriamali imezidi kuongezeka ili tu kwenda sanjari na onyo la maandiko lisemalo; ASIYETAKA KUFANYA KAZI NA ASILE.

Wengi wamegundua miradi mbalimbali, mikubwa kwa midogo. Yenye hadhi na isiyokuwa na hadhi, kikubwa ni 'mkono uende kinywani.'

Hata hivyo, baadhi ya miradi imekuwa ikizua utata wa usahihi wake na uhalali. Moja ni mradi wa ujasiriamali wa kuokota makopo na chupa tupu za plastiki ambapo wajasiriamali wake wamekuwa na mwonekano wa kama wagonjwa wa akili (vichaa).

Linalowashangaza wengi ni kwa sababu gani waokota makopo wengi, badala ya kuonesha mabadiliko ya biashara yao hiyo kwa mwonekano nadhifu, wao wamekuwa wakionekana kama wana matatizo ya afya ya akili.

Ikumbukwe biashara hii hufanywa na wajasiriamali, hasa vijana ambao wamejitoa kujiajiri kwa kuokota chupa za plastiki au makopo mengine chakavu na kuweka kweye mifuko ya viroba (salfeti) wakipita mitaani kuendelea kutafuta bidhaa hizo na kwenda kuziuza sehemu husika hivyo kujipatia pesa za kujikimu.

MASWALI YANAYOSUMBUA VICHWA

Baadhi ya watu waliyozungumza na mwandishi wanahoji, kwa nini vijana hao wakianza kazi hiyo huwa katika mwonekano wa binadamu wenye akili timamu , wasafi, wazuri na wamenawiri. Lakini baada ya kuanza kuokota bidhaa hizo, huanza kuonekana kama hawana akili timamu au wavuta bangi huku wengine wakidhaniwa ni vibaka?

Utafiti unaonesha kwamba, muda mchache baada ya kuanza kuokota chupa za plastiki na makopo hayo, vijana hao huanza kujiweka mbali na usafi hususan kufua nguo, kuchana nywele na hata kujijali katika mambo mengine yanayomtambulisha binadamu kwamba, yuko na akili timamu kutokana na mazingira ya kazi.

SABABU 3 ZATAJWA

Mwandishi wa mahala haya amezungumza na baadhi ya wazee wa kimila kutoka baadhi ya makabila nchini, ambao wengi wao walifanana ufahamu wao kwenye sababu ya kwanza.

1. NI BIASHARA YENYE 'MKONO WA LAANA'

Wazee hao, kwa nyakati tofauti walisema kuwa, shughuli ya kuokota chupa tupu za plastiki au makopo ni nzuri kama nyinginezo lakini haiwezi kuwa nzuri kwa wahusika kwa sababu 'ina laana' ya kitambo!

“Tangu zamani za kale, mtu, hasa kijana, akilaaniwa na wazazi wake, baba au mama, alikuwa anapata matatizo ya afya ya akili na kuanza kuokota makopo mitaani mpaka majalalani ambako ndiyo makazi makubwa ya watu wenye magonjwa ya akili.

“Na hiyo haikuishia zamani tu, hata sasa, kijana akifanya matendo ambayo, wazazi wake hawakubaliano nayo na akionywa bila kusikia utawasikia watu wanasema ‘utaokota makopo.’ Yaani utalaanika," anasema James Kileo, mkazi wa Holili, Rombo Kilimanjaro.

Mzee Mhagama Matayo, mkazi wa Keko, Dar na mwenye asili ya Mkoa wa Ruvuma, yeye anasema:

"We waangalie hata wakipita mitaani watu wanawaona kama wamerukwa na akili. Lakini ukiongea nao ni watu timamu kabisa. Ukweli ni ile laana ya kuokota makopo bado inaishi. Hapa wazee wenzangu wa kimila tumwombe Mungu kwa ajili yao kwani kazi wanayoifanya ni halali ila tu ina mkomo mbaya tangu kale."

2. CHUPA ZA PLASTIKI NA MAKOPO HUPATIKANA MAJALALANI AMBAKO NI MAKUTANO WA KILA UCHAFU WA BINADAMU

Aidha, wazee wengine waliyozungumza na Mwandishi wanasema kwamba, makopo hayo, hasa chupa za plastiki hupatikana kwenye mazingira machafu kama vile majalalani, sehemu za kutupa taka nyingine chafu, hivyo imekuwa rahisi kwa vijana wanaookota makopo na wao kuwa wachafu kwa sababu ya mazingira

"Unategemea lini kumkuta fundi makenika kuwa msafi kama daktari wakati majukumu yake ni lazima alake kwenye vumbi," anahoji mzee Ally Mshamu, mkazi wa Mkuranga, Pwani.

3. KISAIKOLOJIA WAOKOTA MAKOPO WANAAMINI WANADHARAULIWA

Hamis Hussein na Bahati Liwalo, ni vijana wanaopita mitaani wakiokota makopo kwenye maeneo ya Buguruni jijini Dar, wanasema kuonakana kwao wachafu, hawana akili timamu, wanavuta bangi ni kwa sababu ya mtazamo hasi wa jamii.

"Mfano mdogo tu. Ukipita mtaani huku umebeba fuko, mtu anakuita uende kwenye eneo analotupia taka ukachukue chupa za plastiki, lakini anakwambia lazima uondoke na uchafu wake mwingine.

"Sasa huo uchafu mwingine, unaweza kukuta mna pedi za hedhi, pampasi zilizotumika na watoto, mabaki ya chipsi na uchafu mwingine mbaya. Kisa tu anakupa chupa za plastiki. Kwa kweli huwa tunaumia mioyo," anasema Liwalo.

Kwa maelezo hayo ya Liwalo, Hamis yeye ambaye anakaribia kufunga ndoa na Mwajabu Jumaa, akasema, jamii imekuwa ikiwadharau kwa kuwaona waokota chupa hawako timamu wakati siyo kweli. Aliitaka jamii kubadili mtazamo kuhusu wao kwa vile wana akili timamu na wanaendesha maisha kama wahasibu.

KAZI ZA CHUPA ZA PLASTIKI

Inaelezwa kuwa, chupa za plastiki hurudishwa viwandani kutengenezwa bidhaa mbalimbali, zikiwemo chupa zenyewe, CD zinazobeba picha za sinema (filamu) pia hutengeneza bidhaa nyingine za plastiki kama bakuli na ndoo.
 
Mahitaji ya chupa yapo.....

Wanunuzi wanazihitaji......

Ni biashara.....

Wanangu waendelee kusebenza nazo tu kwani huko tuendako mpaka GRADUATES watajiunga nasi majalalani.....

#KaziIendelee
 
Jamii forum wameandaa,
shindano la kuandika stori kuhusu jamii, afya, uchumi, michezo nk washindi wanapata zawadi wa kwanza million 5 wa pili million 3, na wa tatu million2
Shindano hilo limeanza lini na litafikia tamati lini?
Nina stori yangu (ukweli mtupu) ya safari yangu ya kutoka Cabo del gado mpaka Mpaka Maputo, na kutoka Maputo kurudi tena Cabo del gado.
Kutoka Maputo mpaka Cabo del gado sikulipa hata nauli, utaamini.

Natamani nikutane na mwandishi mzuri nimuhadithie ili aandike story tupige pesa.

Ndani ya story hiyo utapata kujua yanayo wakuta vijana wengi wanao zamia kwenda south africa (japo mimi lengo lilikua sio kwenda Sauth Africa)
 
Shindano hilo limeanza lini na litafikia tamati lini?
Nina stori yangu (ukweli mtupu) ya safari yangu ya kutoka Cabo del gado mpaka Mpaka Maputo, na kutoka Maputo kurudi tena Cabo del gado.
Kutoka Maputo mpaka Cabo del gado sikulipa hata nauli, utaamini.

Natamani nikutane na mwandishi mzuri nimuhadithie ili aandike story tupige pesa.

Ndani ya story hiyo utapata kujua yanayo wakuta vijana wengi wanao zamia kwenda south africa (japo mimi lengo lilikua sio kwenda Sauth Africa)
Wacha were😋naanza kuipenda story Kabla sijaujua mkasa
 
Hakuna cha ukichaa hapo wala nini, ni wanajitoa ufahamu tu ili wawe huru…. wakute kwenye mzani ndo utajua hujui.
Hivi kilo ya chupa inaweza kua kiasi gani?
Kipindi nakua nilikua na tabia ya kuokota siso na shaba.
Nashukuru baba yangu alikua mkali sana, kunasiku alinikamata mitaa ya Sudan (Temeke) alitembezea kichapo kutoka hapo Sudan mpaka home Tandika.
Tangu hapo niliacha tabia ya kuokota okota.

Lakini kipindi kile Shaba kilo ilifika mpaka 7000, kwa umri wangu ilikua ni pesa nyingi, hiyo ni 2001.

Nikiwa darasani nilikua nawaza siso na shaba tu, nilikua naiona saa 8 iko mbali.

Dah, watoto wa uswahilini tumepitia mbali sana.
 
Hivi kilo ya chupa inaweza kua kiasi gani?
Kipindi nakua nilikua na tabia ya kuokota siso na shaba.
Nashukuru baba yangu alikua mkali sana, kunasiku alinikamata mitaa ya Sudan (Temeke) alitembezea kichapo kutoka hapo Sudan mpaka home Tandika.
Tangu hapo niliacha tabia ya kuokota okota.

Lakini kipindi kile Shaba kilo ilifika mpaka 7000, kwa umri wangu ilikua ni pesa nyingi, hiyo ni 2001.

Nikiwa darasani nilikua nawaza siso na shaba tu, nilikua naiona saa 8 iko mbali.

Dah, watoto wa uswahilini tumepitia mbali sana.

Sijui bei yake kwa kweli. Hivi, hizo siso ni nini?
 
Back
Top Bottom