SoC03 Uchambuzi juu ya uwajibikaji katika kupunguza ongezeko la taka za plastiki

Stories of Change - 2023 Competition

vholl2000

Member
Nov 8, 2011
11
10
1686128618603.png
Tarehe tano mwezi wa sita kila mwaka ni siku ambayo dunia nzima inaazimisha siku ya mazingira. Mwaka huu 2023, siku hii imebeba kauli mbiu “ Pinga uchafuzi wa plastiki”.Nyaraka hii itaangazia athari za plastiki katika mazingira na afya, pamoja na uwajibikaji kwa wananchi,serikali,mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na viwanda vinavyozalisha plastiki kwenye suala zima la kupunguza na kuondoa kabisa matumizi ya plastiki yasiyo ya lazima katika mazingira yetu.

Tatizo la plastiki ni tatizo la kidunia na ni tatizo ambalo haliwezi kutatuliwa na mtu mmoja au kikundi au nchi fulani bali kwa pamoja dunia nzima inatakiwa kupambana na janga hili kwa sababu athari za plastiki kwa nchi moja huamia nchi nyingine.

Athari za plastiki
Kulingana na utafiti uliofanywa na (Thang, D) unaonesha kuwa, nchi ambazo zinapakana na bahari zilizalisha tani bilioni 2.5 za taka za plastiki na tani milioni 275 za plastiki zilitelekezwa kama uchafu wa baharini ambapo tani milioni 8 ziliingia baharini. Plastiki yoyote inachukua zaidi ya miaka 20-500 kuoza .Plastiki inapovunjwa vunjwa vipande vidogo vyenye urefu usiozidi milimita tano huingia baharini kwa urahisi , chembe hizi “microplastic”, zinapoingia baharini, pamoja na plastiki nyingine zinaliwa na viumbe hai kama samaki, samaki wanavuliwa na kuliwa na binadamu matokeo yake binadamu wanakula plastiki kupitia samaki.

Plastiki inasababisha vifo kwa viumbe hai wa baharini pamoja na wanyama wa kufugwa kama ng’ombe na mbuzi.Kwa mujibu wa “ripoti ya ukaguzi wa udhibiti wa taka za plastiki Tanzania” ya mwaka 2022, iligundulika kuwa tani milioni 150 za taka za plastiki zilionekana kwenye vyanzo vya maji,ripoti hii inaonesha pia utafiti uliofanyika Mwanza katika ziwa Victoria, asilimia ishirini (20%) ya samaki aina ya sangara na tilapia waliochunguzwa walionekana kuwa na chembechembe za plastiki.

Kemikali zinazopatikana kwenye plastiki zinaweza kusababisha magonjwa ya kansa pamoja na kulete mabadiliko ya homoni na hivyo kuathiri mfumo wa uzazi. Jamii zinazoishi karibu na maeneo yanayozalisha plastiki na maeneo taka za plastiki zinapohifadhiwa wanaweza kupata athari zifuatazo; kuzaa watoto njiti, watoto wenye uzito mdogo, asma, lukimia kwa watoto, na kansa ya mapafu.

Plastiki hii inapoingia ardhini inaondoa rutuba katika udongo na kusababisha ukame na ukosefu wa mvua . Tanzania inategemea Kilimo kwa asilimia kubwa na kilimo chetu kinategemea udongo wa asili pamoja na mvua. Pia ukame unaweza kusababisha ukosefu mkubwa wa maji katika vyanzo vya maji.

Nani awajibishwe?
Njia mojawapo wa kumaliza janga la Plastiki katika dunia ni kuwajibisha wahusika wote katika mzunguko mzima wa plastiki.Watungaji na watekelezaji wa sera na sheria wana takiwa kuwajibika na kuhakikisha ongezeko la plastiki katika nchi linapungua kwa kutunga sheria ya kukataza “plastiki zinazotumika mara moja tu” mfano mirija ya plastiki, chupa za plastiki zinazotumika mara moja na kutupwa, vibebeo vya plastiki ambavyo pia hutumika mara moja na kutupwa, vifungashio vya chakula (disposable) ambazo pia hutumika mara moja na kutupwa. Watekelezaji wa sera na sheria zilizopo wanapaswa kufuatilia sheria zilizowekwa kuhakikisha zinafuatwa kikamilifu.

Kuna umuhimu pia wa serikali kupunguza kodi kwa wazalishajii na waingizaji wa vifungashio mbadala wa plastiki na kuongeza kodi kwenye vifungashio vya plastiki ili viwe na urahisi wa bei au viwe vinatolewa bure na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.Hii itafanya wafanyabiashara wengi kuchagua vifungashio mbadala kama vile vifungashio vya glasi, ngozi,box,mbao (bamboo) na nguo na hivyo kuinua uchumi wa mtanzania badala ya kufaidisha wazalishaji wa plastiki ambao kwa wingi wao hawatoki nchi kwetu.

Serikali inashauriwa kuhimiza jamii kutumia mfumo wa taka sifuri ambao unalengo la kupunguza taka zinazoenda kwenye madampo, mfumo huu unatoa fursa za kibiashara kupitia taka. Mfumo huu unahimiza utenganishwaji taka majumbani na ujegwaji wa vizimba vilivyotengwa vya kuhifadhi taka katika mitaa, taka hizi zitahifadhiwa kulingana na aina ya taka mfano taka ozo (mabaki ya chakula), taka hatarishi, taka za kurejerezwa na taka zinginezo ambapo hizi taka zinginezo zitapelekwa dampo. Mfumo huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mlundikano wa taka kwenye madampo, lakini pia utatoa ajira kwa vijana na kina mama.Mfumo huu unahimiza matumizi tena “RE-use” kwa bidhaa za plastiki, mfano ndoo iliyochakaa badala ya kuitupa itatumika tena kupandia maua, matairi ya magari yaliyotumika yatatumika tena kupambia bustani n.k

Jamii inatakiwa iunge mkono jitihada za serikali kwa kukataa kutumia plastiki, kama watu 100 tu kwa siku wakikataa kutumia plastiki za mara moja (disposable) biashara hiyo itakuwa ngumu na hivyo wafanyabiashara kulazimika kutafuta mbadala. Jamii ikiongeza thamani kwenye vyombo vya glasi na asili, vibebeo vya ukili, nguo, ngozi na kuamua kutumia hivyo kwa wingi, wafanyabiashara watahamisha mwelekeo wa biashara zao.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utetezi wa mazingira yanapaswa kupaza sauti kwa pamoja na kutoa uelewa kwa jamii juu ya athari za matumizi ya plastiki katika afya, mazingira na uchumi wa nchi.
Mashirika haya yanapaswa pia kuhimiza jamii kutumia mbadala wa vifaa vya plastiki kwa kuwajengea uwezo jamii katika elimu na mitaji ili biashara ya vifungashio na vibebeo mbadala wa plastiki vienee kwa wingi.

Plastiki ambazo hazina umuhimu na zinagharama kwa mlaji si lazima kuzalishwa. Viwanda vya vinywaji baridi vihifadhi vinywaji kwenye vifungashio vya glasi ambavyo mlaji atarudisha na kupewa bidhaa nyingine. Makampuni ya maji ya kunywa yaanzishe mfumo wa kuuza maji kwa kutumia mashine za maji barabarani badala ya kuhifadhi maji kwenye plastiki, hii pia itapunguza sana gharama za maji ya kunywa na hivyo kuwezesha watu wote kutumia maji ya kunywa yaliyosafi na salama, lakini pia itapunguza sana matumizi makubwa ya mkaa kwa kuchemshia maji ya kunywa.

Viwanda vitumie teknolojia ambazo ni rafiki kwa mazingira katika kuzalisha bidhaa. Viwanda na makampuni viondoe ubinafsi na kuunga mkono jitihada za serikali kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Kwa kumalizia, Jitahada za kupunguza na kuondoa kabisa matumizi ya plastiki hazitofanikiwa iwapo hakutakuwa na uwajibikaji. Uwajibikaji unatakiwa kufanywa na mzunguko mzima wa waandaaji, wazalishaji, watumiaji, waidhinishaji na wenye mamlaka kuhusiana na bidhaa za plastiki. Kama kila mmoja atafanya kwa nafasi yake tutaokoa kizazi kijacho.
Tazama video hapa (Mali ya UNEP)

CHANZO
Thang D, 2019 Overview of Marine Plastic Debris in Vietnam in Relation to International Context.

The Negative Effects Of Plastic On The Environment

A report of the controller and auditor general of the united republic of Tanzania, march, 2021​
 
Back
Top Bottom