Riwaya ya Mbali na Nyumbani ya Adam Shafi

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
21,305
24,193
January 22, 2013

RIWAYA: MBALI NA NYUMBANI mwandishi Shafi Adam Shafi

Kwa Mukhtasari Tunachangamkia kuchapishwa kwa Mbali na Nyumbani, tawasifu ya mwandishi maarufu wa Zanzibar Adam Shafi, anayejulikana zaidi kama Shafi Adam Shafi.

Ipo haja kubwa sasa kwa waandishi kujitolea kuandika tawasifu zao au wasifu. Vile vile kuandikwa kwa wasifu wa watu wengine unasisitizwa hapa.

mbalinanyumbani-jalada-shafi.jpg


Mchapishaji: Longhorn (K) Limited

Mwaka wa Uchapishaji: 2012

Mhakiki: Ken Walibora
Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita yametokea machapisho mengi sana ya bunilizi katika Kiswahili hasa nchini Kenya. Kipindi hiki muhimu kimeshuhudia waandishi wakongwe na chipukizi tumbi nzima kuchapishiwa kazi zao kwa wingi zaidi kuliko kipindi chochote kingine katika historia ya fasihi ya Kiswahili.

Yamkini ongezeko hili la machapisho ya Kiswahili linatokana na ukweli kwamba wachapishaji wamezinduka ghafla kutambua kwamba lina faida pia soko la vitabu vya Kiswahili, lugha ambayo umaarufu wake unakua kwa mapana na marefu kote duniani na hasa nyumbani Afrika Mashariki na Kati. Sababu nyingine ni kuibuka kwa watu wengi wanaokiteua Kiswahili kama nyenzo yao ya kuzibebea kazi zao za kibunifu badala ya Kiingereza au lugha nyingine yoyote.

Lakini hii haimaanishi kwamba kwa ubora na wingi machapisho ya Kiswahili kwa sasa yako sawa na ya Kiingereza. Ni kweli kwamba fasihi ya Kiswahili inajishajiisha kuchuana vilivyo na fasihi ya Kiingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika hasa katika tanzu zake za kibunifu, lakini sivyo ilivyo katika simulizi zinazohusu maisha halisi, tanzu zile ambazo nitaziita uandishi maisha, kama vile tawasifu, shajara, wasifu, n.k.

Tangu gwiji - au tumwite baba wa fasihi ya kisasa ya Kiswahili, Shaaban bin Robert alipotunga wasifu wa mwimbaji wa taarab, Wasifu wa Siti Biti Saad, na tawasifu yake mwenyewe, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, kumekuwapo na kazi chache sana za Kiswahili katika ulingo wa simulizi za maisha halisi.

Hiyo ndiyo maana tunachangamkia kuchapishwa kwa Mbali na Nyumbani, tawasifu ya mwandishi maarufu wa Zanzibar Adam Shafi, anayejulikana zaidi kama Shafi Adam Shafi. Kwa hakika tawasifu ya Shafi huenda ikawa ndiyo tawasifu yenye ujasiri zaidi na iliyotungwa kwa usanifu na usanii mkubwa zaidi katika kanzi nzima ya fasihi ya Kiswahili.

Tawasifu hii imejikita kwenye maudhui ya maisha ugenini, jasira za ujana, na msako wa elimu pamoja na motifu ya safari. Ni tawasifu yenye kuvutia mno na ambayo ina uwezo wa kuleta mapindukizi makubwa katika uwanja wa uandishi maisha wa Kiswahili.

Angalao kwa mara ya kwanza tunakumbana na tawasifu iliyosheheni ucheshi lakini ambayo haizingatii majisifu ya mwandishi wala jaribio la makusudi ya kuficha udhaifu wake. Aidha tawasifu hii haikupi maelezo makavu ya tarehe, mambo hakika, na tarakimu huku mwandishi akijisifusifu kama ambavyo twaona kwenye tawasifu chapwa nyingi zilizoko kwenye rafu za vitabu kote kote duniani.

Mbali na Nyumbani inadhihirisha ubora wa kiujumi na hutoa raha kamili kuisoma. Hata hivyo, yamkini ubora mkubwa zaidi wa tawasifu hii kuhusu safari ugenini, humo katika uwezo wake wa kutuonyesha mengi kuhusu hali ya binadamu na kufundisha bila kuhubiri kwa kumshikia msomaji mtutu wa bunduki na kumlazimishia maoni yasiyopindika.

Shafi si mgeni katika ulingo wa fasihi ya Kiswahili. Ingawa si mwandishi wa vitabu vingi kama mathalani Shaaban Robert, K. W. Wamitila na Said A. Mohamed, ameandika riwaya nne za kutajika,yaani; Kuli, Kasri ya Mwinyi Fuad, Haini, na Vuta N'kuvute. Riwaya ya Haini ambayo ni nusu-tawasifu na ile ya Vute N'kuvute ndizo labda kazi zake bora zaidi.

Katika Mbali na Nyumbani, kama ilivyo katika kazi zake nyinginezo, ni msomaji hana budi kumakia umbuji wa lugha ya Shafi, umbuji unaomwezesha kuchonga sanamu yake mwenyewe kwa ajili ya hadhara kutoka kwenye maisha yake ya faragha na kuifanya tawasifu yake kuwa na ubora utakaokiuka vizazi. Kadhalika Shafi anafanikiwa kucheza na kutatiza mpaka mwembamba uliopo kati uhalisia na ubunifu.

Shafi anaelezea jinsi alivyopatwa na maradhi ya kutaka kusafiri kutoka kwao alikozaliwa na kulelewa. Wasomaji wengi ambao wamewahi kutamani kutoka kwao watajitambulisha na hali hiyo iliyomkumba mwandishi. Vyombo ya bahari vilivyotia nanga bandarini Zanzibar ndivyo vilivyochochea roho ya jasira na hamu na ghamu ya Shafi kutaka kuhujuru kwao.

Mafunzo ya ualimu

Alipokuwa mvulana mdogo akikaa ufukweni mwa bahari na kuvitazama vyombo hivyo na mabaharia walioingia na kutoka. Kukaa kwingi ufukweni kulimpatisha adhabu kali kutoka kwa babake ambaye akihofia usalama wa mwanawe. Baadaye maishani, Shafi aliachia katikati mafunzo ya ualimu kwenye chuo cha ualimu Zanzibar na kuanza safari ya kwenda kusoma Misri bila hata kuwaarifu wazazi wake.

Zanzibar ilikuwa katika minyonyoro ya ukoloni wa Uingereza wakati huo, naye akitarajia kupata elimu kwengineko mbali na nyumbani. Pitapita zake za kwenda Misri zinampitisha Kenya, Uganda, na Sudan ambapo mara kadha alikuwa akienda na kurudi au kurudishwa nyuma kutokana na vikwazo safarini.

Shafi anaelezea visa vingi vya kushangaza kukiwemo kufanya kazi ya kondakta kwente basi la Mawingo Bus lililohudumu kati ya Bungoma na Kisumu, uhusiano wake wa mapenzi haramu na wanawake Bungoma na Khartoum na kufungwa jela Uganda Kaskazini n.k. Hadithi ya maisha yake inaishia mpomoko pale ambapo anajikuta kwenye kambi ya siri ya mazoezi ya kijeshi nchini Msiri ili kuipindua serikali ya Mkoloni Zanzibar, badala ya chuo kikuu kusomea elimu aliyodhamiria.

Aidha anaporejea kwao nyumbani anakuta kwamba hana fursa ya kutumia mafunzo ya kijeshi aliyoyapata Misri kwa vile Uhuru unapatikana mara moja bila yeye na wapiganaji wenzake kuhusishwa kwenye mapigano.

Ilmuradi mwandishi anaandika kuhusu makosa yake na taksiri zake kwa ujasiri wa kustaajabisha. Mfano ni masimulizi yake kuhusu wanawake aliofanya nao ngono nje ya ndoa na mara nyingine akiwa mwenyewe kakirimiwa na maimamu msikitini. Lakini tawasifu ya Shafi sio tu masimulizi kuhusu uhusiano wa kimapenzi na wanawake; inazungumzia kwa mapana na marefu awamu ya maisha ya kujasiria kwingi ujanani. Inajumuisha matamanio yake, matumaini yake, mashaka yake, kutamauka kwake, huku akisaka elimu ya chuo kikuu isiyofikiwa katika Afrika iliyokuwa inatawaliwa na Wakoloni.

Elimu kama kiini cha msako wa msimulizi inafanana na tawasifu nyinginezo za Kiafrika kama vile ile ya Leonard Kayira, I Will Try, ambapo mwandishi anaondoka kwao Nyasaland, (siku hizi Malawi) ili kwenda kutafuta elimu ya juu Marekani. Maudhui ya elimu kama kani ya ukombozi yanajirudia tena katika tawasifu ya Shafi nayo ni muhimu katika uelewa wetu wa mkutadha wa Zanzibar kihistoria na mapambano ya kibinafsi ya mwandishi mwenyewe kujinusuru kutokana na madhila yaliyoletwa na ukoloni.

Kwa hiyo tawasifu hii, ni zaidi ya hadithi ya mtu mmoja. Katika safari zake zote, Shafi anaandamana na vijana wenzake wanaotamani kupata nafuu maishani nje ya mawanda yao ya kinyumbani. Kwa maana hiyo basi, tawasifu hii ni ni hadithi ya wengi, kama zilivyo tawasifu nyingi za Kiafrika.

Kichocheo kikubwa

Kama mwaka 2010 ulishuhudia kuchapishwa kwa Dreams in a Time of War, labda kazi bora zaidi ya Ngugi wa Thiong'o, basi 2012 ulioshuhudia kuibuka kwa Mbali na Nyumbani ambayo ni kichocheo kikubwa katika uandishi maisha wa Kiswahili. Kwa maoni yangu kwa kuandika Mbali na Nyumbani, Shafi kutoa changamoto kwa waandishi wenzake pia kugeukia maisha yao halisi kama mada ya uandishi na ubunifu wao.

Wito huu unawaendea wote walio hai kama vile Said A. Mohamed, Mohammed S. Mohammed, John Habwe, Bitugi Matundura, Hezekiel Gikambi, Mwenda Mbatia, Timothy Arege, Omar Babu, Clara Momanyi, na Wamitila nami pia. Ipo haja kubwa sasa kwa waandishi kujitolea kuandika tawasifu zao au wasifu. Vile vile kuandikwa kwa wasifu wa watu wengine unasisitizwa hapa.

Wasifu wa Sheikh Ahmed Nabhanny uliotolewa hivi karibuni ni mfano bora wa aina ya tungo za uandishi maisha ambazo Kiswahili kinazihitaji. Ni matumaini yangu kwamba wasifu wa marehemu Shihabdin Chiraghdin ulioandikwa na kuchapishwa hivi karibuni na bintiye kwenye Kiingereza utatafsiriwa kwa Kiswahili pia. Hiyo ni mojawapo wa njia za kukiwezesha Kiswahili kuchuana barabara na Kiingereza katika ulingo wa fasihi katika eneo la Mashariki na ya Kati Afrika.

Mimi mwenyewe nimetunga tawasifu yangu yenye kichwa, Nasikia Sauti ya Mama: Tawasifu ya Maisha Utotoni, na ambayo nimempa mchapishaji. Nimeitika wito pasi ya kuitwa kwa vile nimeiandika kabla ya kusoma Mbali na Nyumbani. Labda siku moja nayo itachapishwa na kusomwa na wengi. Vyovyote viwavyo, kwa Mbali na Nyumbani, Adam Shafi ametuzindua na kutuonyesha njia ya kuandama. Shime Waswahili, mpo?

Ken Walibora ni profesa mwandamizi wa fasihi ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani


kwalibora@yahoo.com

Chanzo: Ujasiri wa kujimulika katika uandishi wa Kiswahili - MAKALA - swahilihub.com

 
Nimependa kiswahili cha Ken Walibora. Ni bahati mbaya kuwa kiswahili asili yake Tanzania lakini tunazidiwa na Kenya. Kenya wanasherehekea kuchapisha vitabu vingi wakati Tanzania wachapishaji wanakufa mmoja mmoja kutokana na kukosa soko la kazi zao ambalo mara nyingi ni mashule. Hii imetokana na mitaala ya kipumbavu iliyoanzishwa na profesa Jumanne Maghembe na ufisadi wa kiuchumi na kimawazo. Wakati wa Mwalimu Nyerere uandishi ulitukuzwa. Chini ya Kikwete unatukuzwa ufisadi, sanaa, wizi, ukihiyo na upuuzi mwingine mwingi hadi elimu inazidi kuzikwa ikiwa hai. Sintoona ajabu siku moja shule na vyuo vyetu vikianza kuagiza vitabu vya kiada vya fasihi ya kiswahili toka Kenya. Ni aibu na pigo kwa taifa linalojivunia kuwa chanzo cha kiswahili.
 
img_30651.jpg

Kasr ya Mwinyi Fuad, toleo lake la kwanza kabisa, lilitolewa pia na TPH mwaka 1978. Kitabu hiki kimeshatafsiriwa katika Kifaransa, jambo linaloonyesha namna mwandishi huyu Adam Shafi Adam anavyosifika duniani.

img_30661.jpg

Kuli, kilichotolewa mwaka 1979 (TPH) na 2005 na Longhorn, ni moja ya vitabu maarufu vya mwandishi Adam Shafi Adam ambavyo vimempatia sifa ya kuiangalia jamii yake kwa macho ya darubini kali ya kimaendeleo.

Source: KITABU KIPYA CHA GWIJI WA FASIHI YA KISWAHILI- ADAM SHAFI KIMETOKA « kitoto
 
Kwa wale tuliosoma enzi mpaka utawala wa awamu ya kwanza (Rais Nyerere) unaishia, vitabu ilikuwa ni MUST; si unajua tena enzi hizo mambo mengi yalikuwa hakuna; hakuna TV, Video labda CINEMA tu tena unaenda ukumbini.
Huenda upeo wa ufahamu unapungua kwa kiasi kikubwa kwa sasa maana watu na TV, watu na simu, hivi tumeshajiuliza kwa nini wazazi makini wanasimamia watoto wao na muda wa kuangalia TV? Labda ndio maana katika jamii yetu tuna baadhi ya watu (sijui ni wangapi) walioenda shule ila wana UVIVU WA KIFIKRA?
Enzi zile sikumbuki vizuri kana ni msingi au sekondari niliposoma kitabu hiki, "KULI" we acha tu ilikuwa ni kama unawatch movie (hiyo kwa jinsi ya kiakili), tena ilikufanya kujiuliza na kudadavua na kuwa naTAFAKURI kwa upana kuhusiana na maudhui husika wakati huo
 
Najivunia kukutana na ngumu huyu wa Riwaya Tz,
Alinifunza mengi sana na kunifanya niwe mpenda riwaya na fasihi kwa ujumla.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom