Kumbukumbu ya Ramadhani - Sehemu ya 2

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,265
KUMBUKUMBU YA RAMADHANI 2

MFUNGO WA RAMADHANI NA SIKUKUU YA EID MBALI NA NYUMBANI NA KWINGI DUNIANI

Mombasa, Kenya 1990s


Hii mbali na nyumbani nimemwibia gwiji wa fasihi, Shafi Adam Shafi.
Adam Shafi ameandika kitabu, ‘’Mbali na Nyumbani.’’

Ukisoma kitabu hiki utapata hisia mtu anakuwaje akiwa mbali na kwao.

Mombasa si mbali na Dar es Salaam kiasi cha kumtia mtu unyonge ikiwa ataifunga Ramadhani katika mji huo na sababu ni kuwa hawezi kujihisi upweke.

Miaka mingi nyuma nilifunga Mombasa.

Wakati wa kufungua mwadhini ulipokaribia nikawa najisogeza katika msikiti wa jirani kwa kufungua na kusali sala ya Maghrib kisha nitafute hoteli ya kwenda kufuturu.

Nilikuwa nakwenda Mombasa mara nyingi kiasi nikawa nafahamika katika barza moja Mwembetayari.

Barza hii ilikuwa barza ya wanachama wa chama fulani cha siasa na kila nikipita pale husimama kusalimiana na jamaa na wao wataniuliza habari za TZ kama jamaa wa Kenya wanavyopenda kuita Tanzania.

Basi nilipopita barzani jamaa wakanizuia wakaniambia nisubiri tufungue pamoja kisha sote tutaelekea msikitini.

Nilichoshuhudia pale siku ile kinilishangaza sana.
Nilikuwa sijaona popote pale.

Ilipopigwa adhana zikawekwa ‘’snacks’’ kilima cha sambusa, kababu, jelebi na mapochopocho mengine na chupa za juisi.

Kwa kweli vitu vilikuwa vingi kiasi nikajiuliza baada ya hawa jamaa kula kiasi hiki watakwenda kweli majumbani kwao kufuturu?

Cardiff, Wales 1992

Niko Uingereza Ramadhani imenikuta katika nchi na mji ambao Waislam ni wachache sana.

Ilikuwa ikifika wakati wa kufungua naingia unyonge mkubwa sana.
Dar es Salaam Ramadhani ni ‘’funfair,’’ wakati wa kufungua na kabla yake.

Nakumbuka nyumbani.

Misikiti inakuwa na watu wengi na wafanya biashara hasa akina mama wanaleta kila aina ya vyakula kuuza nje ya misikiti kuanzia mishikaki, sambusa, kababu na kila aina ya juisi.

Hapa Uingereza hakuna kitu.
Wala huwezi kuhisi kuwa ni Ramadhani.

Nikawa nakumbuka nyumbani Msikiti wa Mtoro kuna darsa ya tafsiri ya Qur’an niliyokuwa sikosi kuhudhuria akisomesha Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo, mwanafunzi wa bingwa wa tafsir, Mufti Sheikh Hassan bin Ameir.

Msikitini petu Cardiff hakuna darsa labda kwa kuwa msikiti ulikuwa ukisaliwa zaidi na wanafunzi.

Huu msikiti zamani ilikuwa ni kanisa Waislam wakauziwa na wao wakageuza kanisa kuwa msikiti ukapewa jina ''Darul Isra.''

Msikiti ulikuwa ukiendeshwa na Wapakistani na kwa kujua kuwa msikiti ule ni wa wanafunzi walikuwa wanatoa futari ya biriani matunda na juisi kila siku.

Wanafunzi kutoka kila pembe ya ulimwengu tunafuturu hapo.

Nyumbani nilikotoka biriani si futari lakini niliipenda futari ya biriani mchele wa basmati kwa nyama ya kondoo.

Siku ya Eid imefika.
Ikanijia hamu ya kwenda kusali Msikiti wa Regent Park London.

Huu ni msikiti mkubwa na maariufu sana Uingereza.
Natokea Cardiff.

Sikujua kuwa London kuna misikiti wamefunga tofauti na Cardiff.

Nikakuta msikiti lango kuu limefungwa na kuna tangazo kuwa siku hiyo si siku ya Eid wao watasali Eid siku ya pili, kesho yake.

Niliingiwa na majonzi.
Nilishangazwa kuona kuwa hata huku kuna tatizo la mwezi.

Nikiwa nimezubaa pale msikitini akatokea kijana mmoja wa Kinigeria akaniuliza kama ningependa kwenda msikiti mwingine kusali.

Yule kijana akaniambai kuwa White Chapel Mosque, East London wanasali Eid.

Tukaondoka tukapanda bus kuelekea East London.

East London ni sehemu ambayo kuna jamii kubwa sana ya Wahindi na wengi ni Waislam.

Basi letu lilipoanza kukaribia mitaa ya East London na ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kufika nikaanza kuona watu wamevaa kanzu na mavazi nadhifu ya Eid wakiashiria kuwa walikuwa wanaharakia misikitini kusali Eid watoto wadogo na wakubwa mitaa yote imepambika kwa shamra shamra za sikukuu.

Ilinijia kama vile niko Dar es Salaam mitaa ya Jamhuri karibu na misikiti ya Kitumbini, Sunni na Ibadh.

Nikasali sala ya Eid hapo White Chapel Mosque na baada ya sala sikufanya haraka ya kuondoka kurejea Cardiff nikawa natembea kuangalia mandhari ya East London.

Nikapata hoteli wanauza chai na sambusa na kabab na baadae mchana nilirejea hoteli ile kupiga biriyani.

Hoteli zote ni za Wahindi.
Jioni jua linazama nikapanda treni kurudi nyumbani Cardiff.

Stori hii ya sala ya Eid bado haijesha.

Nilirudi tena London mwaka unaofuata 1993 nikasali Eid Kubwa Regent Park Mosque bila ya kupanga nikitokea Le Havre na Paris nikakatiza English Channel na kuja London.

Allah ni mwingi wa rehema.

Itaendelea…

1710328088989.png

Darul Isra, Cardiff
1710328186350.png

Regent Park Mosque, London

Sehemu ya kwanza soma Kumbukumbu ya Mwezi wa Ramadhani1: Darsa la Tafsiri ya Qur'an la Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom