OFISI ZA C.T.I (Safe house)-IRINGA
Wapelelezi wa C.T.I walikuwa wanaendelea na kazi mbalimbali ndani ya ofisi hizi. Wapelelezi hawa ukiachana na wale waliokuwa nje ya ofisi hii kikazi, walikuwa wakifanya uchambuzi wa taarifa mbali mbali ambazo zingesaidia upatikanaji wa ufumbuzi juu ya kesi hii iliyowafanya wawepo hapa Iringa.
Ndani ya ofisi binafsi ya mkurugenzi wa C.T.I pia kulikuwa na watu wawili tu waliokuwa bize sana.Watu hao ni mkurugenzi Eliakim Makassy na 'field agent' Paul. Mbele yao kulikuwa na makabrasha kadhaa ambayo walikuwa wakiyafanyia uchambuzi wa hali ya juu.
Makabrasha haya yaliletwa na 'field agent' Paul kutoka nyumbani kwa waziri wa ulinzi aliyetoroka nchi.Wakati kikosi maalum cha C.T.I kilipofanya upekuzi katika nyumba ya waziri huyu msaliti,Paul aligundua uwepo wa makabrasha haya ambayo aliyatilia shaka na kuamua kuyachukua kwa kificho cha hali ya juu.
Kutilia mashaka makabrasha haya kulitokana na namna ya muonekano wake na mahali yalipohifadhiwa. Paul aliyaona makabrasha haya yakiwa katika kikabati maalum kilichofungwa kwa namba za siri ambacho kilikuwa kimepachikwa ukutani na kufunikwa kwa picha kubwa iliyoonesha wanyama mbalimbali.Kama si uzoefu wa kazi ya ushushushu basi isingekuwa rahisi hata kuhisi kuwa nyuma ya picha ile pangeweza kuwa na kitu kimefichwa.Alipofanikiwa kukifungua kikabati kile kwa kukiharibu, ndipo ndani alifanikiwa kukuta makabrasha yale. Alipo taka kujaribu kujua kilichoandikwa katika nyaraka zilizokuwa ndani ya makabrasha yale ndipo alipogundua kuwa mambo yaliyoandikwa mule yaliandikwa kwa maneno ya kificho (codes).Hapo ndipo alipoamua kuyabeba makabrasha yale hadi kwa mkurugenzi mkuu wa C.T.I bwana Makassy.
"Mzee, katika kupekua pekua na kutafiti hapa na pale, nimefanikiwa kuwa hiki kilichoandikwa kwa maneno ya kificho(codes) yawezekana ni mipango haramu ambayo magaidi walitaka kutekeleza kwa kushirikiana na msaliti huyu. Lakini pia kuna majina ambayo nadhani ni ya watu mbali mbali ambao nao wanahusika na uovu huu ambao nao majina yao yameandukwa kwa maneno kificho.Ila pia nimegundua kuna kitabu wenyewe wanakiita 'book of codes au master codes' ambacho kina ufunguo wa maneno siri yaliyoandikwa katika makabrasha haya.Kama tutakipata kitabu hiki basi tunaweza kuwajua wabaya wetu na wasaliti wa nchi hii wote".Aliongea Paul kisha akatulia kidogo na kuendelea kuongea.
"Na kitu cha mwisho nilichoweza kukigunduani kwamba kitabu hicho yaani 'book of codes' kwa sasa kiko mikononi mwa mtuhumiwa wetu namba tatu.Namaanisha John Karobota".Alimalizia kuongea Paul.
"Duh.Safi sana.Pamoja na kuwa huyu jamaa kakimbia nchi lakini bado umeweza kung'amua mambo mengi sana ambayo yanazidi kuleta mwanga katika kesi hii.Sasa wacha mimi niendelee kuwasiliana na maajenti walio Mbeya ili tujue tunaendelea vipi na kazi hii".Aliongea mkurugenzi wa C.T.I kwa kumalizia, Paul akaaga na kutoka katika ofisi hiyo kuendelea na majukumu mengine.
**************************************************************************************************
MAHALI FULANI MKOANI MBEYA
Mick-Reuben na Clara walikuwa ndani ya gari mpya aina ya Subaru nyeusi mali ya C.T.I. Gari hili walilipata katika uwanja mkubwa ulio katika ofisi za TAZARA. Waliletewa gari hili na afisa upelelezi kutoka katika idara ya intelijensia ya kijeshi (Military Intelligence) au kwa kifupi M.I.
Gari hii aina ya SUBARU, lililoboreshwa kwa kuwekewa mfumo wa kompyuta uliounganishwa na mifumo ya ki-intelijensia ya C.T.I, ndilo lililosugua lami ya barabara hii pasipo huruma. Ajenti Clara alikuwa akishughulika na kompyuta huku Mick akiendesha gari kwa kasi kubwa. Sasa waliikuwa wamefika Inyara, eneo ambalo kuna kituo kikuu cha polisi cha Inyara pamoja na ofisi za TAZAMA (bomba la mafuta linalohusisha Tanzania na Zambia). Walikuwa wanaelekea Chimala, kufanyia kazi taarifa muhimu walizopewa na Devi masaa kadhaa nyuma.
SAA CHACHE NYUMA.
Mara Mick alipowasiliana na C.T.I masaa kadhaa nyuma na kuwasilisha pendekezo lake la kutaka waziri wa ulinzi kuwekwa kizuizini ili ahojiwe na kuhusika na mtandao wa kigaidi, Mick na Clara waliendelea na mahojiano na kijana Devi kuhusiana na mambo mengi tu.
Mahojiano yao yaliwawezesha kupata namba ya simu ya James Peter, aliyekuwa mlinzi wa waziri wa ulinzi aliyetoroka.Ajenti Clara akaiunganisha namba hii na programu maalum ya kijasusi ya kompyuta kisha akaipiga namba ile. Namba ilipopokelewa, Clara akaongea na aliyepokea namba ile kwa dakika moja huku akijitahidi kurefusha maongezi hadi pale dakika moja ilipotimia.
Wakati Clara akiongea na simu hii kwa kupitia 'earphones' alizovaa , mikono yake ilikuwa bize katika kompyuta iliyokuwa mbele yake.Kompyuta hii ilionesha ramani ya dunia na 'icon' fulani iliyokuwa inaonesha kuwa mpokeaji alikuwa katika nchi ya Tanzania.Clara akai-zoom ramani ya Tanzania na icon ile ikaonesha mpokeaji yupo ndani ya mkoa wa Mbeya.Clara aka-zoom tena ramani ile na kubonyeza hapa na pale, ramani ikabadilika na kuonesha picha za 'satelite'.
Katika picha hii ya satelite, Clara aliweza kuona mpokeaji wa simu ile aliipokea akiwa yupo Chimala, nyuma ya milima mirefu iliyo umbali wa kilomita tano kutoka ilipo barabara ya Lami.Clara aliyafanya yote hayo katika dakika moja.
Kilichomshtua Clara katika picha hii aliyoiona ni mazingira ambayo aliyepokea simu (James Peter) alikuwepo kwa mujibu wa 'satellite image'.
"Mick nadhani unapaswa kuona hii"Clara alimgutusha Mick ambaye alikuwa akifanya mawasiliano ya hapa na pale.
Mick akasogea Pale alipokaa Clara na kutazama kilichoonekana katika kompyuta.Naam.Hata Mick alishtuka.
Walichokiona ilikuwa ni kama kambi kubwa la jeshi lililozungushiwa ngome kubwa.Limetumika neno 'ni kama' kwa kuwa hadi wakati huo hakuna aliyeweza kuthibitisha kuwa kweli ni kambi la jeshi au siyo.Hii ni kwa kuwa, katika kambi za jeshi zote ambazo hata wananchi wa kawaida wanazifahamu zilizopo ndani ya mkoa, hakuna hata kambi moja ambalo lipo upande huo na mahali hapo ambapo Picha ya 'satelite' ilionesha.
Mara baada ya Mick kuona jambo hilo kengere ya hatari ililia kichwani mwake.Hakuhitaji kumuuliza mtu yeyote ili kupata usaidizi wa kutambua kwamba kuna jambo hatari linaloendelea katika kambi hilo kama lilivyoonekana kwa msaada wa picha za 'satellite'.
Mick akapitisha maamuzi fulani fulani kichwani mwake.Kwanza kabisa, kwa kusaidiwa na Clara, Mick alifuatilia kwa undani picha zile za 'satellite'. Katika kufuatilia huko, Mick aligundua mambo mengi yaliyokuwa katika picha hizo.Aliweza kuhisi kuwa yawezekana kambi hiyo inaandaa wapiganaji ambao serikali haiwatambui. Mick alijaribu kuunganisha doti mbili tatu za mlolongo wa mambo mbali mbali yaliyotokea tangu alipoanza kufuatilia kesi hii na kung'amua kuwa, uwepo wa ngome kama inavyooneshwa na picha hizi za satellite,yawezekana ndiyo palipo na fumbo kubwa sana ambalo bado lilikuwa halijafumbuliwa. Fumbo la magaidi waliovamia msafara uliokuwa unamsafirisha gaidi Omar Al-Mahmood, walitokea wapi ndani ya nchi hii na walitokomea kwenda wapi mara baada ya tukio hili.
Mick aliweza kuhisi haya kwa ushahidi wa kimazingira alioupata katika picha hizo mara baada ya kukuza picha hizi kwa ku-zoom na kuona vizuri kwa ukaribu zaidi.
Hisia zake zilipata uhakika zaidi na kubadilika kuwa ukweli mara baada ya kufanya mawasiliano na mamlaka kadhaa zinazohusika na mambo mbalimbali yakiwamo ya usalama wa nchi ya Tanzania. Mawasiliano yote aliyoyafanya yalimuhakikishia kuwa hakuna anayefahamu kuhusiana na uwepo wa ngome hiyo.Kwa maana nyingine kwa kutofahamika na mamlaka ilimaanisha kuwa ngome hiyo ipo kinyume na sheria.Hivyo basi hii ilimuhakikishia Mick kuwa hii inaweza kuwa ngome ya adui anaowatafuta.
"Clara tunakwenda Chimala muda huu mamaa ". Mick aliongea.Kisha akawasiliana na watu fulani ambao dakika kumi na tano baadaye walifika eneo alilokuwapo na kumchukua Devi na kuondoka naye kwenda kumuhifadhi mahali 'salama'.
**************************************************************************************************
Sasa Mick na Clara walikuwa wanaelekea eneo linaloitwa Igurusi, umbali wa kilometa chache tu kabla ya kufika kati kati ya mji mdogo sana wa Chimala.Ilikuwa saa 12:00 jioni. Wakati wote chuo mawasiliano yaliendelea kati yake yeye na mkuu wa idara ya C.T.I , Makassy.
"Mick, nakupa ruhusa ya kuongoza kikosi maalum cha ECS (Ellite Combat Squad) ambacho nitakituma kwako masaa kadhaa yajayo.Pia utapata usaidizi wa kutoka kwa 'field agents' wenzako pamoja na vikosi vingine vya 'back up' kadri ya itakavyohitajika.Kazi yako ni kuwakamata wakuu wa ngome hiyo wote utakaowapata na watakaoshindikana kuwakamata unaruhusiwa 'kuwadondosha'. Kazi yako nyingine ni kuhakikisha unapata kitu kinachoitwa 'book of codes'. Hatujui bado kama ni kitabu kweli au ni neno la fumbo tu.Lakini ni muhimu sana kupata kitu hicho kwa kuwa ndiyo kitafichua waovu wote waliotaka kuichafua serikali tukufu ya taifa hili lililotukuka la Tanzania"Alitoa maagizo haya Makassy kwa kupitia kifaa cha mawasiliano ambacho Mick alikivaa sikioni mwake.
"Sawa mkuu.Kama mambo yatakwenda sawa basi leo hii tuta funga ukurasa huu wa kesi hii ya hawa magaidi."Alijibu Mick huku akiendelea kuendesha gari kwa spidi kali.
Wakati yote hayo yakiendelea,Clara alikuwa bize akitumia kompyuta yake kuendesha 'DRONE'(ndege ndogo isiyo na rubani ambayo huendeshwa kwa kompyuta) ambayo ilifungwa kamera maalum inayoweza kurekodi hata katika giza nene la usiku wa manane.Clara aliielekeza ndege hiyo katika ngome ambayo waliigundua masaa machache yaliyopita ili aweze kukusanya taarifa za ki-intelijensia za kutosha na kwa ukaribu zaidi. Sasa ilikwishatimu saa kumi na mbili na dakika ishirini na tano na giza lilikwishaanza kutanda. Mick na Clara nao ndiyo walikuwa wamewasili katika kituo cha mabasi cha Chimala, na sasa walikuwa wanakatisha katika barabara moja ya vumbi upande wao wa kulia tayari kwa kujiandaa na kazi kubwa waliyokuwa wanaitegemea kuwa itawajia mbele yao wao na idara nzima ya C.T.I.
CHIMALA
Chimala ni jina la sehemu ya wilaya ya Mbalali mkoa wa Mbeya.Kutoka Mbeya mjini hadi Chimala kuna umbali wa kilomita zaidi ya sabini. Chimala ni sehemu ya bonde la Usangu,bonde maarufu sana kwa kilimo cha mpunga.
Zaidi ya haya yote, Chimala imetawaliwa na milima mingi sana.Milima midogo kwa mikubwa kidogo.Kwa sababu hiyo mtu akiwa eneo la Chimala hawezi kuona mbali zaidi kwa kuwa kila akigeuka ataona milima tu.
Kwa Mick haikuwa mara ya kwanza kufika Chimala.Kwa mara ya kwanza alifika miaka kadhaa iliyopita,wakati alipokuwa akisomea shahada ya kwanza chuo kikuu cha Dar es salaam, kozi ya Geology Engineering. Kama ilivyo kawaida ya wanafunzi wa vyuo vinavyofundisha kozi hii ya Geology katika ngazi ya shahada au hata stashahada, kufika Chimala ilikuwa ni jambo la lazima.
Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dar es salaam na Dodoma na wale wa stashahada wa Chuo cha Madini Dodoma walifika Chimala walipokuwa wakihitimu mwaka wa kwanza na mwaka wa pili(kasoro wanafunzi wa chuo cha madini Dodoma ambao walifika Chimala mara moja tu) kwa ajili ya mafunzo ya kutengeneza ramani za ki-jiolojia kwa vitendo wakati wa mafunzo kwa vitendo.
Kwa hiyo Mick naye wakati alipokuwa akisoma kozi hiyo pale chuo kikuu cha Dar es salaam, naye aliwahi kufika Chimala mara mbili.Wakati alipohitimu mwaka wa kwanza wa masomo na wakati alipohitimu mwaka wa pili kwa ajili ya mafunzo ya ukusanyaji wa data za kijiolojia na hatimaye kutengeneza ramani ya jiolojia.
Sasa alikuwa akienda Chimala kwa mara ya tatu.Tofauti na nyakati zingine alipoenda kwa sababu ya kujifunza kwa vitendo kozi ya 'geology' au kwa kiswahili 'utafiti wa miamba na madini' aliyokuwa anaisomea, safari hii alikwenda mahali pale kwa sababu ya kazi maalum. Ilikuwa ni kazi ya mapambano na hatimaye maangamizi ya ngome ya maadui kadri ya alivyoelekezwa na mkuu wake wa kazi bwana Eliakim Makassy.
**************************************************************************************************
Saa mbili usiku,Ajenti Mick na Ajenti Clara walikuwa wamepaki gari lao aina ya subaru katika viwanja vya mnadani huko Chimala.Macho yao yalikuwa katika kompyuta .Clara alikuwa akitumia kompyuta kuongoza ndege moja ya rangi nyeusi sana isiyo na abiria (Drone) kwa kasi kubwa sana. 'Drone' hiyo iliyofungwa kamera ya kisasa iliyo na uwezo wa kurekodi hata katika giza,iliweza kurusha video ilizorekodi moja kwa moja katika kompyuta ile ya Clara na katika kompyuta ya mkurugenzi Eliakim Makassy, katika ofisi yake binafsi ndani ya C.T.I. Wafuatiliaji wa video hiyo ya moja kwa moja, walikuwa ni Ajenti Paul na Makassy mwenyewe.Kutoka ndani ya ofisi ya C.T.I ni wao wawili tu walifuatilia video hiyo tena kwa siri kubwa kwa kuwa bado walihisi uwepo wa wasaliti kutoka ndani ya Idara.
"Nadhani sehemu nzuri kuingilia ni hapa nyuma ya ngome.Mimi naona kama ndipo pana ulinzi dhaifu."Aliongea Clara huku akionesha kwa kidole katika kioo cha kompyuta kutoka katika video ile ya moja kwa moja iliyorekodiwa na 'drone'.
"Naona kuna uwigo wa umeme katika ukuta wa ngome.Hebu tafuta Chanzo cha umeme kinachotawanya umeme katika ngome."Alizungumza Mick.
Kwa kutumia kompyuta ile,Clara aliiongoza 'drone' ile kufanya 'survey' katika ngome ile.Akaishia sehemu ambayo panaonekana transfoma moja kubwa na makorokoro kibao ya umeme.
"Nadhani ni hapa".Aliongea Clara.
"Kweli.Hapo panaweza kuwa ndiyo chanzo cha umeme.Hawa jamaa inaonekana wanatumia umeme aina mbili tofauti.Kuna umeme wa TANESCO na huu mwingine wa jenereta.Hebu endelea kuchunguza zaidi."Aliongea Mick.
Clara aliendelea kuongoza 'Drone' ile kwa umakini wa hali ya juu.'Survey' iliendelea kufanyika katika ngome yote.
"Hebu acha hapo".Mick alimwambia Clara.Clara akabonyeza hapa na pale katika kompyuta, 'drone' ikasimama hewani mahali fulani.Katika video iliyorekodiwa na kurushwa moja kwa moja, lilionekana jengo moja ambalo kwa kulitazama tu basi mtu yeyote angeweza kuhisi kuwa ni makazi ya kuishi mtu mwenye heshima kubwa ndani ya ngome hiyo.Pengine mtu wa cheo cha juu zaidi katika ngome hiyo.Nyumba iliyoonekana ilikuwa ya hadhi ya juu sana.
"Hebu iweke 'drone' katika kona ambayo itaweza kurekodi vizuri huo mlango wa mbele wa nyumba hiyo".Mick alitoa maelekezo ambayo yalifuatwa na Clara mara moja.
Kutoka katika video ile ya moja kwa moja,mbele ya nyumba hiyo kulikuwa na geti dogo la chuma likifuatiwa na mlango uliotengenezwa na mbao za mti wa mninga.Geti hilo la chuma lilikuwa limefunguliwa ila mlango wa mbao ulikuwa umefungwa huku funguo zikining'inia katika tundu la kitasa kwa upande wa nje.
Funguo kuning'inia nje ya mlango ilikuwa na maana sana kwa upande wa Mick.Labda inawezekana mtu aliyeingia ndani ya nyumba hiyo alisahau kuchomoa ufunguo huo baada ya kufungua mlango,hivyo bila shaka atarudi kuuchukua ufunguo huo mara tu atakapokumbuka.
Na kweli ikatokea hivyo kama Mick alivyoongea.Dakika tano baadaye,mlango ule ulifunguliwa na mtu mmoja akatokea nje na kuanza kuuchomoa ufunguo ule.Tena kwa bahati nzuri mtu huyo alikaa katika kona nzuri ambayo ikawa rahisi kwa kamera iliyo katika 'drone' kuweza kumrekodi vizuri.
"Hebu 'zoom' sura ya huyo jamaa."Mick aliongea mara baada ya kuiona sura ya mtu yule kwa mbali.Clara akafanya kama alivyoagizwa.Zaidi ya hapo ,Clara akaipakua picha hiyo na kuipakia katika programu maalum ya kompyuta ya kufananisha sura.
Kabla hata dakika moja haijaisha, neno 'match found 99.7%' likaonekana katika kompyuta ile.
"Bingo".Mick alisikika akisema kwa bashasha.
Uhakika ulikuwa umepatikana.Mtu aliyeonekana alikuwa ni James Omolo Ekeni.Hapo moja kwa moja ikawa imejulikana kuwa kwa asilimia mia ni kweli adui zao wapo pale.
"Mkuu tumewapata kwa uhakika".Aliongea Mick mara baada ya kukiruhusu kifaa alichovaa sikioni upande wa kulia kufanya kazi yake.
"Safi sana vijana wangu kwa kazi nzuri mliyoifanya.Sasa kazi inayofuata ni kuhakikisha yeye na wenzie wanajuta kuingia katika nchi yetu."Ilisikikasauti ya Makassy kutoka upande wa pili.
"Sasa mkuu, mimi nadhani sasa ututumie vikosi vya mapambano muda huu ili ikiwezekana kesho usiku tukapambane nao hukohuko.Usiku huu nitafanya tathmini ya makadirio kisha nitakuambia unitumie kikosi cha askari wangapi."Aliongea Mick.
"Sawa Mick.Ukinipa tathmini yako usiku huu,basi kikosi kitawasili huko kabla hakujakucha."Alizungumza Makassy.
"Halafu nikuombe kitu kingine. Kesho tutakapoanza mapambano, nitaomba utuunganishe moja kwa moja na idara nzima ya C.T.I. Yaani wana idara wote watuone moja kwa moja.Hapo nadhani ndiyo itakuwa karata nzuri na ya mwisho ya kumkamata msaliti wetu."Aliongea Mick.
"Nimekuelewa vizuri Mick.Nawatakia maandalizi mema iki kesho tuweze kufunga kazi hii."Aliongea Makassy kisha akakata mawasiliano.
Kisha Makassy akafanya mawasiliano na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania bwana George Katumba na kumjulisha yote yaliyojiri.
Wakati huo huo Gari aina ya Subaru lililowabeba Mick na Clara lilichanja mbuga kuelekea Eneo la tukio.Kilomita moja kabla ya kufika ngomeni,gari hilo liliingizwa porini na kwenda nyumabya mlima mmoja mrefu.Hapo Mick alishuka na hemabna vifaa kadhaa zikiwamo silaha mbali mbali kisha akatengeneza hema mahali hapo kwa ajili ya kulala usiku huo.Clara akaondoka na gari kurudi Chimala mjini kwa ajili ya kusubiri na kutoa maelekezo ya moja kwa moja mara kikosi maalum cha E.C.S(Elite Combat Squad) kitakapowasili. Sasa kazi iliyoanza ilikuwa inaelekea kuisha.UKURASA WA GAIDI ULIELEKEA KUFUNGWA.
**************************************************************************************************Saa kumi na moja alfajiri, Mick alilifunga hema lake na kulitelekeza sehemu iliyojificha hapo hapo porini.Kisha akapandisha mlimani juu kabisa na kutafuta mahala ambapo pamejificha vizuri, mahali ambako pamejificha vizur, mahali ambako hata adui angetumia kiona mbali, au darubini, bado asingeweza kumuona. Aliendelea kuchunguza ngome ile ambayo ilikuwa umbali wa kilomita moja na kadhaa kwa kupitia kiona mbali cha kisasa kabisa.
Wakati mwingine, Mick alitumia bunduki kubwa ya kudungulia kupitia kiona mbali kilichofungwa katika bunduki hilo.
Wakati huo alikwishavaa sare maalum za kikosi cha E.C.S(Elite Combat Squad) zilizojumuisha gwanda nyeusi, kofia ngumu yenye uwezo wa kuzuia risasi iliyokuwa ya rangi nyeusi pamoja na buti za kisasa za kijeshi nyeusi.
Zaidi ya hayo, kifurushi cha sare za kikosi maalum cha E.C.S(Elite Combat Squad) pia kilijumuisha bastola aina ya beretta iliyofungwa lenzi na tochi,kisu maalum cha mapigano kikiwa ndani ya ala yake, pingu nane za plastiki, mabomu matatu ya kurusha kwa mkono, mkasi mdogo maalum kwa kukata nondo na nyaya zote, miwani maalum ya kuona gizani pamoja na bunduki ya kisasa kabisa aina ya M4A1 ikiambatana na Magazine yake inayobeba risasi nyingi tu pamoja na uwezo wa kurusha makombora.
Helikopta na magari ya mapigano ya Kikosi cha E.C.S, vilikuwa vimefungwa na bunduki aina ya FN MINIMI, silaha ya kisasa kabisa.
Nb:Group la whatsapp ni Tsh 2500/= huko utapata simulizi bila kikomo
Wasiliana nami kwa 0758573660