IRINGA
SAFE HOUSE
Hadi kufikia siku iliyofuata asubuhi, idara yote ilikuwa imehamia Iringa katika moja ya nyumba ambazo inazimiliki Tanzania. Katika mikoa yote iliyo jirani na mikoa iliyo mpakani mwa nchi,C.T.I ilimiliki nyumba moja kama hii. Kwa kuwa mkoa wa Mbeya unapakana na nchi ya Malawi na Zambia, nyumba ilijengwa katika mkoa jirani wa Iringa.
Kiuhalisia si kwamba nyumba ilikuwa mpya. Nyumba ile ilikuwa imefanyiwa ukarabati kutoka kuwa ghala la chakula na kurekebishwa kuwa jumba la kisasa sana.Jumba hili lilikuwa na vyumba kadhaa vya kulala pamoja na ofisi kubwa na ofisi ndogo ndogo pamoja na vitu vingine vingi sana.Hata namna ya kuingia katika nyumba ile haikuwa kazi nyepesi. Kulikuw na vitasa vya kisasa katika nyumba hii ambavyo vilihitaji namba ya siri, alama za vidole pamoja na mtazamo wa mboni ya jicho ili kufungua.Walio weza kuingia ndani ya nyumba hii ni wale wahusika tu. Hawa ndio pekee ambao teknolojia inayohusika kwa sababu za usalama katika nyumba hii ilikuwa imelishwa taarifa zao.
Maajenti wa idara hii ya CTI,walikuwa wamekusanyika katika ofisi kubwa ya pamoja wakifanya hili na lile pamoja na kupanga hiki na kile ili mradi kuweka mambo sawa.Chumba hiki cha ofisi, kilikuwa kimetawaliwa na kompyuta kadhaa zilizounganishwa kwa utaalamu wa hali ya juu huku zikitumia 'soft wares' za kisasa kabisa zinazohusika na kazi hii ya upelelezi. Yaani kwa kifupi kazi ilikuwa inaanza kuoamba moto rasmi wakati huu.
********************************************************
"Clara, hebu jaribu ku-hack mfumo wa kamera za CCTV za jeshi kikosi cha jkt Mafinga uangalie kilichorekodiwa kwa muda wa wiki moja nyuma kabla ya tukio kutokea." Aliongea Mick na kusikika kwa ajenti Clara upande wa pili kupitia kifaa cha mawasiliano alichokivaa sikioni.
"Ok acha nifanye yangu ".Alijibu Clara kutoka upande wa pili na kisha sauti ya vitufe vya kompyuta ikaanza kusikika ikibonyezwa bonyezwa kwa kasi ya ajabu.
Wakati huu ambao wawili hao walikuwa wanawasiliana, Clara alikuwa yupo ofisini wakati Mick yupo msituni,mahali ambapo palitokea tukio siku mbili tatu nyuma.Tukio lililosababisha wanaidara wa C.T.I kujikuta wana jukumu zito la kufanya mara baada ya kuwa na majukumu ya kawaida tu kwa muda mrefu.
Tangu asubuhi,wakati idara yote ya C.T.I ilipokuwa imewasili katika eneo hili, Mick alikwenda mahali pale na kuanza kazi yake eneo la tukio mara moja.Akiwa amekwishapata taarifa za awali za nini kilichojiri,moja kwa moja Mick alijua ni wapi pa kuanzia. Alikumbuka moja ya kauli mbiu ya idara yake iliyosema "katika tukio lolote, ni vizuri na lazima upelelezi uanzie eneo la tukio kwa sababu ndiyo mahali pekee ambapo utapata ushahidi au fununu zitakazokupeleka kwenye ushahidi". Na ni ukweli mtupu unaoongelewa katika kauli mbiu hii.Idara yoyote ya usalama duniani inapofanya upelelezi wa tukio fulani,ni lazima itafika eneo la tukio kwa sababu ya mambo mawili.Ushahidiau fununu au kama mataifa ya magharibi yaliyotufundisha mambo haya wanavyosema kwa lugha yao 'either clue or evidence'.
Kwanza kabisa baada ya kufika eneo la tukio,ajenti Mick alimuhoji mmoja wa askari waliokuwa wanalinda eneo hilo.Wakati alipomuhoji,Mick aliweza kung'amua kuwa magaidi wale walikhwapo muda mrefu,pengine masaa mawili matatu kabla ya msafara kupita na kushambuliwa.Aling'amua kuwa magaidi wale walikuja kwa pamoja eneo hilo na kisha wakatawanyika kila upande nyuma ya misitu ya eneo lile la tukio na ndiyo maana ilikuwa vigumu kupambana nao.Pia alihisi,kwa jinsi eneo lilivyokuwa msituni basi magaidi hawa yawezekana waliletwa eneo lile kwa usafiri fulani mahali pale.Kwa maelezo ya askari aliyehojiwa Mick ,aliweza kung'amua upande ambao inawezekana ndiko magaidi wale walikoikia kabla ya kutawanyika kuzingira eneo lote.
Ndiyo.Ilikuwa ni rahisi kwa Mick kung'amua mambo haya kutokana na maelezo ya askari yule wa weledi wa E.C.S waliokuwa chini ya C.T.I ambaye alikuwa miongoni mwa askari waliokuwa wakilinda eneo lile la tukio ili ushahidi usipotee.Kilichopelekea askari yule kutoa maelezo kwa kina ni kwa kuwa pia alikuwa ni miongoni mwa askari waliosindikiza msafara uke uliovamiwa.Askari yule alimueleza ajenti Mick upande ambao risasi nzito zaidi kutoka kwa adui ziliwashambulia.Na ni upande huo huo ambako upinzani mkubwa ulitokea kuliko upande wowote.Mick aliposikia hayo aliweza kuhisi kuwa yawezekana upande huo ndiko upande ambao adui walikuwa wengi zaidi.Pia yawezekana risasi nzito kwa maelezo ya askari,zilitokea katika bunduki nzito nzito zilizofungwa katika magari ya adui.Basi kwa kusikiliza hayo na kuyachambua kichwani Mick aliuhisi upande huo na kuanza kufuatilia,akitokea barabara ya lami na kuingia msituni.
Mick alipasua msitu na kuukabili hadi kilometa moja na nusu msitu ukipoishia. Wakati huu wote,alikuwa anafuata njia za vumbi ambazo zilitawaliwa na tope katika msimu huu wa mvua Akitumia gari alilokabidhiwa,aina ya Range rover sport nyeusi iliyong'ara sana,Mick alifuatisha barabara ya vumbi iliyokuwa inapita nyuma,upande wa pili wa msitu huu kwa umbali wa kilomita moja tena. Kama ingepigwa picha kutoka juu sana,ama kama ilivyoonekana kwa picha za satelite, barabara hii ilikuwa upande wa pili wa msitu huu wa 'mipaina' ikionekana kwenda ki-msambamba na barabara ya lami.
Kilomita moja mbele ,Mick aliweza kung'amua alama za matairi ya magari zinazoingia msituni.Kilichompa dukuduku zaidi kuwa huenda hicho ndicho alichokuwa ankitafuta,ni kuwa alama zile zilizojichora katika tope zilionesha kuwa magari zaidi ya nane yalipita eneo hili na kuchepuka kuingia msituni.Alama hizi zilinoga zaidi eneo la miti michanga ambapo miti ilikanyagwa sana.Akiwa ameshuka kutoka garini,kwa miguu yake Mick alipasua pori na kuanza kufuatilia matairi hayo huku bastola yake aina ya bereta ikiwa kiunoni na ile ndogo ya 'colt 45' ikiwa imepachikwa katika soksi mguu wa kulia.Kufuatilia huku kulimpeleka hadi mita 300 ndani ya msitu ule,eneo ambalo alama za matairi ya magari yale ziliishia.Hapo Mick aliona kitu ambacho kilimuhakikishia kuwa adui walifikia katika eneo hili na kisha kutawanyika.Eneo lilikuwa limetawaliwa na maganda ya risasi kwa uwingi hasa. Maganda ya risasi kutoka katika bunduki nzito nzito yalikuwa yametawanyika katika eneo hili.Bunduki ambazo aidha zilikuwa zimefungwa kwenye magari au hata kama zilibebwa na magaidi wale basi wasingeweza kutembea nazo kwa umbali mrefu kutoka katika gari kutokana na uzito wake.Hili nalo lilizidi kumthibitishia kuwa hapa ndipo maadui walifikia nakutawanyika kufanya mashambulizi.
Baada ya kujihakikishia kwa hili,Mick alirudi katika gari lake na kuanza kufuatilia alama zile.za magari zilizokatisha msituni na kuishia mahali alikokuta maganda ya risasi mengi,upande zilikotokea kabla yakukatisha porini hapo.
Akiwa anaendesha gari lake huku akifuatilia alama za matairi za magari haya mahali zilikotokea, alama hizi zilimpeleka kilomita nane mbele,mahali ambako barabara hii ilipita nyuma ya kambi la jeshi la kujenga taifa.Kambi ya Mafinga.
Hapa Mick aliona alama za matairi zikiwa zimechepuka kidogo na kisha mbele kurudi usawa wa mwanzo.Alama hii ilikuwa ni ya matairi ya gari dogo.Mick alipaki gari pembeni, akashuka na kuchuchumaa kuangalia kwa umakini alama zile huku akionekana kutafakari jambo.
"Hapa yalipita magari madogo mawili na makubwa au labda malori sita.Kati ya haya magari makubwa kulikuwa na magari aina ya TATA mawili, IVECO mawili na ISUZU mawili.Hapa alama za matairi zinazoonekana kwenda pembeni kidogo nakisha kurudi usawa wa mwanzo na kutengeneza 'curve', kuna gari moja kati ya magari makubwa lilipaki kando na kisha kuendelea na safari,labda kuna jambo wahusika walifanya nje ya gari."Aliwaza ajenti Mick ndani ya kichwa chake.Kisha akageuka nyuma na kuona ukuta wa fensi upande wa nyuma wa kambi hilo ulivyo mrefu.Kisha baada ya ukuta huo kwa ndani kulikuwa na msitu wa miti mingi aina ya milingoti na miti ya matunda mingi. Majengo hayakuonekana labda utumie kiona mbali kutokana na msitu ulivyoshona mahali hapo,hivyo Mick akatambua kuwa si rahisi kwa walio ndani kujua nini kinaendelea nje.Lakini alipokaza macho vizuri, aliona kamera za CCTV zilizofungwa kwa juu katika jengo hilo ambapo kama si utaalamu na uzoefu wa kazi yake pengine asingeziona.
Na hapo ndipo alipowasiliana na ajenti Clara ili amsaidie kwa utundu wa kompyuta kuingilia mfumo wa kamera hizi na ikiwezekana kuibia mambo yaliyorekodiwa nyakati za tukio lile lilipotokea.
Mara baada ya kuwasiliana na ajenti Clara,Mick alirudi katika gari lake na kuendelea kufuatilia alama za matairi alizokuwa anazifuatilia tangu mwanzo.Alifuatilia zilikotokea kabla ya eneo hili alikotoka.Mbelealimaliza eneo la usawa wa jeshi.Mbele kidogo ya hapo alikutana na magari yanayobeba mbao yakitokea katika upande mmoja wa barabara hii ya tope na kwenda porini kwa kufuata barabara nyingine.Hii barabara iliyofuatwa na malori haya na ile inayotoka nyuma ya jeshi zimeunganishwa kwa barabara moja huko zilikotokea.Kwa sababu hiyo ikawa siyo rahisi kwa Mick kuweza kuendelea kung'amua alama zile za matairi alizokuwa anazifuatilia kwani zilichanganyika na alama za matairi za malori yale naa pengine zilifutwa kabisa na kubaki alama za malori yale.
Akiwa amekata tamaa ya kufuatilia kile alichokuwa anakifuatilia,akaona si vibaya akiuliza kitu kutoka kwa bwana mmoja aliyekuwa akibadilisha tairi katika roli lake lililokuwa tupu.Bwana huyu alionekana kama ndiye dereva wa gari lile na kwa upande ambao gari lake lilitazama,ilionekana kuwa ndiyo anaenda kufuata mzigo wa mbao.
"Samahani braza".Mick alianzisha mazungumzo na dreva yule ambaye ndiyo kwanza alikuwa amegundua kuwa kuna mtu nyuma yake.
"Bila samahani kaka sijui nikusaidie nini".Alijibu kwa staha dreva yule hasa kutokana na unadhifu wa huyu mgeni wa ghafla(Mick).Ama kwa hakika jinsi dreva huyu alivyoongea kwa adabu ungeweza kudhani kuwa madreva wa malori ni watu wa staarabu sana.Lakini kumbe...........
"Hivi ni kwa nini mnapita njia ndefu na malori yenu. Mbona kuna njia fupi hii inayopita nyuma ya jeshi au wajeda wanamaindi nini.?" Alihoji Mick.
Yule dreva aliyeulizwa swali hili akamuangalia Mick usoni kwa sekunde kadhaa kwa kukereka kisha akafungua mdomo wake.
"Hivi blaza mbona unapenda kusumbua watu kwa maswali ya kiboya.Mi nilikuona kama mstaarabu kumbe hovyo tu.Au tuseme hujui kusoma.Pita uone utakavyo chezea vitasa hadi ujinyee".Alijibu kwa jazba dreva yule huku akinyoosha kidole mahali fulani kama vile anataka Kumuonesha Mick kitu fulani upande wa kushoto kwake.
Mick alipogeuka kutazama upande ule ndiyo kwanza aliona kibao kilichoandikwa " ILANI. NI MARUFUKU KUPITA BARABARA HII NYUMA YA KAMBI.UKIPATIKANA UTAONA CHA MOTO."Kibao kile kilijieleza.
"Bas poa blaza.Shika hii ya maji."Aliongea tena Mick huku akimkabidhi dreva yule noti tatu za shilingi elfu kumi kumi.Ustaarabu wa dreva yule alioonekana nao mara ya kwanza ukarudi tena wakati huu alipokuwa akipokea fedha hii na kushukuru huku akiwa kama haaminikama kuulizwa swali moja tu la kipuuzi ambalo amejibu kwa jazba kumempa pesa yote hii kabla hata ya mchana.Tabasamu lilichomoza usoni mwa dreva huyu ambaye sekunde chache zilizopita alimjibu Mick kwa ghadhabu.Ama kweli pesa ni sabuni ya roho.
"Hawa madreva wa magari makubwa sijui wana matatizo gani.Yaani akili zao wanazijua wenyewe".Aliwaza Mick wakati akiwa amerudi ndani ya gari lake.
"Lakini mbona mimi nimepita barabara ile na nimeshuka na kukaa zaidi ya dakika ishirini bila kubugudhiwa na mtu.Au kamera zimekufa."Alijiuliza Mick.Alihisi taa nyekundu kuwaka kichwani mwake.Yeye kama mwana usalama yeyote,alihisi kuwepo kwa mchezo mchafu.Ndiyo.Kwa nini kamera ziharibiwe.Kwa nini magaidi walipita njia ile.Alipojaribu kuunganisha mambo haya,Mick alihisi kuwa kuna jambo limejificha nyuma yake,hii haikuwa 'Coincidence'.
Mick aliendesha gari lake kurudi ' safe house' huku akiwaza jambo hili na lile.Mwisho aliamua kuwa muda utatoa majibu muafaka wa maswali aliyojiuliza kichwani mwake,japo muda hausubiri mtu.