SALAMU KUTOKA KUZIMU
SURA YA NNE II
"Umesema u nani wewe?".
"Naitwa Joram Kiango".
Inspekta Mkwaju Kombora hakuyaamini masikio yake. Jina la Joram Kiango lilikuwa maarufu kichwani mwake kama mbwa anavyoifahamu harufu ya chui. Mzee huyu alimfahamu vyema Joram. Yule kijana machachari aliyefanya mengi dhidi ya wahujumu uchumi na majasusi hatari ambao jeshi la polisi lilielekea kukata tamaa. Yule kijana nadhifu sana, mpole sana, mwenye nguvu na akili. Si huyu mzee aliyesimama mbele yake katika vazi la Kiarabu, akiwa amevaa kanzu nyeupe, kapiga kilemba, mwenye ndevu nyingi, uso uliofunikwa na miwani na mkononi kashika fimbo ambayo ilimsaidia katika mwendo wake wenye dalili zote za udhaifu wa kizee,
"Joram?", Inspekta Kombora akauliza tena.
"Naona huniamini kwa vile hujanifahamu Inspekita", ilisema sauti ambayo Kombora alielekea kuifahamu kwa mbali,lakini sura haikuwa ya Joram.
"Pengine niondoe miwani na haya madevu ya bandia ili uweze kunitambua". Madevu yakatolewa na miwani ikavuliwa, Uso ulisimama mbele yake ukitabasamu, Alikuwa ni Joram Kiango halisi ambaye Inspekta Kombora alimfahamu vyema.
"Nini sasa unafanya Joram?", alishangaa Inspekta Kombora. "Mchezo huu una lengo gani?".
"Siyo mchezo inspekta. Niko kazini. Unionavyo hapa mimi ni marehemu. wapo watu wameniua. Nataka niendelee kuwa marehemu ili...
Inspekta Kombora alimkatisha na kumwekea mkono begani huku akisema, "Sikia Joram. Kama ni mzaha subiri nitakapokuwa huru ndipo utakapoufanya tena mchezo wako, tucheke pamoja. Kwa sasa niko katika mkasa mzito ambao unaweza kuhatarisha usalama wa jiji endapo mtu huyo mwenye roho ya kinyama hatapatikana".
Habari hiyo ikamvutia Joram. "Mtu gani?", Joram alihoji mara moja.
"Hujasikia tu? Nadhani wewe hupitwi na neno".
"Kusikia?".
"Kuhusu msichana huyo aliyeuawa kikatili kuliko ilivyowahi kutokea. Polisi wamefanya kuokota viungo vyake kimoja baada ya kingine ndipo ukapatikana mwili mzima wa marehemu. Mtu aliyefanya mauaji hayo ni mnyama zaidi ya wanyama wengine wa kawaida. Mtu mwenye kumchinja msichana mrembo kama yule".
"Sijakupata Inspekta, yaani..." kisha Joram akapunguza kasi kuhoji kuhusu tukio hilo kwa kituo. Inspekta Kombora akamweleza yote kuhusu tukio zima lilivyotokea usiku huo huko Mburahati.
Hakukuwa na sababun za kuupeleka mwili huo hospitali", Inspekta Kombora aliongeza. "Viongo vyote vya marehemu vimeletwa hapa katika chumba cha maabara. Kama utapenda kutazama vitu vya kutisha unaweza kwenda maabara, inatisha sana".
"Nitapenda kumwona tafadhali".
Inspeta Kombora akaiacha ofisi yake na kumuongoza Joram kuelekea maabara ambako alifungua friji na kutoa kichwa cha msichana mrembo. Joram alikitambua kichwa hicho kuwa cha Waridi. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alihisi machozi yakimdondoka. Aliyafukuza macho hayo kwa tabasamu huku akinong'ona kama mtu anayesali. "Ni Waridi! Mungu akurehemu. Naamini ni mapenzi yako kwangu ambayo yamekufanya ustahili adhabu hiyo ya kinyama. Naahidi nitakulipia kisasi".
Sala hiyo ilimfikia Inspekta Kombora. Akamgeukia Joram kwa mshangao na kusema, "Kumbe unamfahamu msichana huyu? Tafadhali turejee ofisini ili unisimulie kuhusu mkasa mzima ulivyotokea".
"Sijawa na cha kusimulia", Joram alijitetea. Hata hivyo alilazimika kusimsimulia Inspekta Kombora yote aliyoyajua. Alieleza jinsi alipomwona Waridi kwa mara ya kwanza pale baa akiwa ametegwa kwa sumu iliyokusudiwa kumwua yeye. Akaeleza pia yaliyotokea katika chumba ambacho waridi aliandaliwa kwa sumu ile ile ili amnyweshe Joram kwa hila. Ambacho Joram hakueleza ni jinsi alipofika hapo kabla ya wakati na kubahatisha, ingawa kwa taabu, kumwona mwuaji yule akitoa maelezo kwa Waridi. Hilo aliliacha ili apambane nalo binafsi. Hakupenda kuwaachia polisi ambao aliamini wangeweza kuharibu mapngo wake wa kumtia mikononi mwuaji.
"Ina maana binti huyu marehemu ndiye yule msichana aliyetoroka hospitali baada ya kuokotwa kando ya baa", Joram akatikisa kichwa kukubaliana na swali la Inspekta Kombora.
"Ndiye. Basi anastahili kifo cha aina hiyo. Kwa nini hakutoa taarifa polisi, tungeweza kumsaidia. Alishirikiana na wahalifu kuandaa njama za kufanya uhalifu".
"Inawezekana au isiwezekane", Joram alijibu kwa mkato. "Aweza kuwa alilazimika au kulazimishwa. La muhimu sasa ni kumpata huyo mwuaji".
"Ndio... apatikane haraka. Wewe humjui?".
Joram alikanusha. "Angalia bwana mdogo. Ninavyookufahamu mimi bila shaka wajua mwengi zaidi ya haya uliyonieleza. Nawe kama uonavyo hawa ni watu hatari kuliko unavyofikiri. Usiwachukulie mzaha, Ucheze nao kama ilivyo kawaida yako".
"Kawaida yangu sina mzaha wa mwuaji Inspekta", Joram alijibu. "Tena naamini kuwa nitawafikisha mikononi mwako mapema zaidi. Ninayo nafasi nzuri sana. Sasa hivi wao wanadhani kuwa nilikunywa ile dawa na sasa niko mahututi au marehemu tayari. Imani hiyo itawafanya wapate jeuri ya kuendelea na mipango yao kama walivyokusudia. Nataja kujua lengo lao, wanakusudia kufanya nini, na watu hawa ni akina nani, baada ya kufahamu hivyo nitawaleta mikononi mwako.
"Kazi hiyo ndiyo iliyonifanya nijibadili kuwa katika hali hii Inspekta. Nimeona nitoweke machoni mwao. Kusudi langu kwako ni kukuomba uitangazie dunia kuwa nimefariki ghafla. Nadhani watafurahi na kuendeleza mipango yao. Ndipo nitakapofufuka na kuwashangaza kwa kuwatia mikononi.
Walijadiliana kwa muda ofisini. Kombora akawa ameafikiana kwa taabu sana na Joram. Nia ya Joram ilikuwa awaachie polisi kufanya kazi yao kwa makini. Lakini maelezo ya Joram yalimtua Inspekta Kombora hata akakubali japo kwa shingo upande. "Kumbuka ninavunja sheria zote za kushiriki katika uongo mkubwa kama huu. Hivyo. usiniangushe kwa kushindwa kutimiza ahadi yako ya kuwatia watu hawa mikononi mwa sheria", Inspekta Kombora alimwambia Joram.
"Wanifahamu vizuri Inspekta. nakuhakikishia kuwa Siwezi kushindwa kamwe", Joram alimjibu akiweka vyema ndevu zake za bandia na kuvaa miwani yake. Akautwaa mkongojo wake na kuiacha ofisi ya Inspekta Kombora kwa mwendo ambao ulimfanya Inspekta huyo ambaye hucheka kwa nadra sana aangue kicheko kipana.
Usiku huo taarifa ya habari ya Radio Tanzania Dar es Salaam ilibeba habari ambazo ziliwashitua wasikilizaji wengi kote nchini.
"...Joram Kiango yule mpelelezi mashuhuri wa kujitegemea amefariki ghafla akiwa nyumbani kwake kwa maladhi ambayo bado hayajathibitishwa. Madaktari wanaendelea na uchunguzi watatoa taarifa za kifo hicho hivi karibuni baada ya uchunguzi,,,"
Haikuwa habari njema hata kidogo. Wala hakuna aliyetarajia kuisikia. Kila aliyemfahamu Joram alitegemea kuwa kijana huyo angeuawa au kufa kwa risasi au madhara mengine kutoka kwa adui zake. Kufa kwa maradhi! haiwezekani!.
Taarifa za habari za sauti ya Kenya na Ujerumani ziliidaka habari hiyo haraka na kuitagaza kwa mapana zaidi... "Yule kijana machachari"... Walisema wakenya, "The Iron boy..." walimwita hivyo wajerumani... "Amefariki leo ghafla. Yawezekana na njama za wahujumu ambao walimuogopa sana kijana huyu kama moto".
Ndipo watu walipolazimika kuamini. Wengi walisikitishwa na kifo hiki. Wengine walitoa machozi. lakini Wachache walishangilia.