Kesho yake ilikuwa asubuhi yenye mawingu kiasu cha kuvunja nguvu ya jua kali ambalo lilikuwa likitishia kutawala. Mmoja kati ya wale askari waliomchukua Waridi pale baa alikuwa tayari kawasili kazini kwake. Mkuu wake wa kazi alihitaji ripoti kamili ya "Kushambuliwa kwa yule msichana malaya" Akamtaka pia kujitahidi waliotenda tukio hilo watafutwe na kupatikaba haraka iwezekanavyo kwani mchezo wao wa kubaka wasichana si mzuri kimaadili hususan mchezo wa hatari.
Askari huyo akalazimika kumsubiri mwenzake kwa muda mrefu, hakutokea. Ikamshangaza. Kwa kuwa makazi yake hayakuwa mbali na kituo cha polisi cha Magomeni, askari huyo aliamua kumfuata nyumbani, Alimkuta! Lakini alimkuta katika hali ambayo haikuwa ya kawaida, Kwani haikuwa jambo la kawaida mtu aanze kuvaa suruali kabla haijafunika matako, aache kazi hiyo ba kuanza kuinamia sakafu hadi kichwa kigonge chini mfano wa mtu anayeswali. Na zaidi ya hayo mgeni aingie baada ya kupiga hodi mara kadhaa bila kuitikiwa, lakini akukute ukiendelea kuinama kimya kimya. Dakika mbili, tatu hadi tano.
"Bobi", askari huyo alimwita mwenzake kwa mshangao, akijiuliza huu ni mzaha wa aina gani, na umeanza lini! "Bobi", aliita tena askari huyo huku akimtazama tena kwa makini zaidi askari huyo. Ndipo alipoanza kuona povu lenye damu damu likimdondoka mwenzake mdomoni na puani. Akaruka nyuma, kisha akakusanya nguvu na kumsogelea ili amchunguze vizuri zaidi. Akayaona macho yake yalivyoduaa, akauona ulimi ulivyotoka na kutembea nje ya meno, akaona... Hofu ikamkumbuka ghafla. alikuwa akitazama maiti ya askari mwenzake. Hima akarudi kituo cha polisi kutoa taarifa.
Marehemu alipelekwa hosptali ambako daktari hakuchelewa kutoa taarifa kuhusu ugonjwa uliosababisha kifo hicho. "Ugonjwa wa moyo", daktari alidai. Kwamba alikutwa na ugonjwa huo ghafla wakati akivaa nguo zake, ikabainishwa kuwa kifo cha askari huyo kilitokana na shinikizo la damu.
Hakuna aliyeshuku kuwa asakri huyo amekufa kwa sumu ile, ya aina yake, ambayo aliigusa kutoka kwa Waridi, na kuifikisha sehemu iliyokusudiwa kufika, mwilini mwake, bila askari huyo kujua.
Sumu hiyo iliandawaliwa kwa ajili ya Joram Kiango peke yake
Wakati huo huo Joram Kiango alikuwa akipokea simu iliyopigwa ofisini mwake.
"Sauti yako i tamu mno masikioni sister, yaelekea nawe u kiumbe mzuri sana. Siwezi kuukataa kamwe mwaliko wa mtu mwenye sauti nzuri kama hiyo, Baada ya saa moja nadhani nitafika... Haya... Ahsante... Umesema wapi vile... Heh... Light Lodge?... Hapo siyo?. Nitafika baada ya saa moja...", akaweka simu chini na kuukunja uso wake akimtazama Neema Iddy, katibu wake ambaye pia alikuwa akumtazama.
"Nani?", Neema alihoji kwa shauku.
"Anajiita waridi".
"Waridi? Anataka nini?" Joram alipochelewa kujibu. Neema aliongeza. "Sikujua Joram kama nawe u mroho wa wanawake kiasi hicho. Sauti tu unaridhika na kuahidi kumfuata? Angalia Joram. Utaingia katika mtego. Una maadui wengi katika nchi hii".
"Nalijua hilo", Joram alisema. "Siendi kwa sababu ya sura wala sauti yake kama nilivyosema. Kilichonivutia ni maelezo yake. Anasema yeye ni yule msichana ambaye alipigwa pale baa ya Forest of Flowers. Anadai kuwa nia yake ni kunishukru pamoja na kunipa habari fulani ambayo inasisimua".
"Malaya kama yule! Hana habari yoyote. Anachotaka ni kukupata wewe tu".
"Hapana", Joram alimkatisha. Sauti yake ndiyo iliyonifanya nivutiwe hata kumwahidi kuwa nitakwenda. Inavyoonyesha kuna kitu zaidi ya anachosema. Nahitaji kujua ni nini. Zaidi ya sauti, nadhani utakumbuka kuwa jana binti huyo alilia sana akilitaja jina langu. Sijui alivyonijua".
"Ni mimi niliyekutaja kwanza".
"Ni kweli, lakini hiyo siyo sababu ya kumfanya aniite jina langu mara nyigi tena kwa ufasaha kiasi kile. Ni kama mtu aliyekuwa akinifahamu kitambo".
"Wewe si mtu unayefafamika Joram?".
"Pamoja na hilo", Joram aliongeza. "Ni wapi alikopata namba yangu ya simu? Tuseme kwenye vitabu vya simu. Kwa nini ahangaike kiasi hicho? Na kwa nini iwe mapema hivyo? Neema, huoni ni mwujiza huu? Jana tu alikuwa hoi. Leo anazungumza kwa uchangamfu kabisa na yuko logi badala ya hospitali! Huoni kama kuna jambo hapo? Yaonyesha kuwa ananitafuta. Yawezekana hata jana alikuwa akinihitaji mimi tu hakuwa majeruhi wala mgonjwa!" Akasita kidogo kabla hajaongeza kwa sauti ya chini akisema: Na atanipata. Kwa muda mrefu nimekuwa sina kazi ya kufanya".
Wakati huo Joram alikuwa wima akivuta droo hii na ile, akiweka hiki mifukoni na hiki kiunoni. Mara akaanza hatua za haraka kuelekea mlangoni.
"Yaani unakwenda Joram, mara hii!", Neema aliuliza kwa mshangao.
"Naam".
"Mapema namna hiyo? Si umemwambia baada ya saa moja?".
"Niliamua kumdanganya. Siamini kama yeye ananieleza ukweli mtupu, hivyo nami sioni ubaya wa kumweleza uongo kidogo. Nataka kufika mapema kidogo nione anachofanya".
"Lakini ujihadhari", Neema alimwambia wakati akivuka kizingiti cha mlango.
"Usijali Neema", Joram akamjibu bila kugeuka nyuma.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.